Mkazi wa Kijiji cha Lupande Kata ya Mawengi Wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe, Joseph Haule (25), amehukumiwa kifungo cha miezi 11 jela au kulipa faini ya Tsh. 300,000 baada ya kukiri kumtolea lugha ya matusi kwa maandishi Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ludewa (OCD) SSP Deogratius Masawe, hukumu hiyo imetolewa jana November 16,2021 katika Mahakama ya Mwanzo Mlangali, Ludewa.
Imeelezwa kuwa Mtuhumiwa huyo aliandika ujumbe wa matusi baada ya Mama Mkwe wake Berdeta Njelekela kutoa malalamiko ya kunyanyaswa kwa Mtoto wake ambaye ni Mke wa mtuhumiwa huyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika 12/11/2021 ukiongozwa na OCD huyo pamoja na wawakilishi wa dawati la jinsia kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Njombe.
Baada ya kutolewa malalamiko hayo ya unyanyasaji Masawe aliagiza Joseph na Mkewe Grace Lawrence wafike Kituo cha Polisi Mlangali ili waweze kusikilizwa migogoro yao ambapo katibu wa kitongoji Macarius Haule alifikisha barua ya wito lakini alijibiwa na Joseph kuwa hawezi kufika kufika kituoni hapo, Grace alifika kituoni huku akiwa na barua ya wito waliyopelekewa ambayo chini yake iliongezewa maandishi yenye matusi kutoka kwa Joseph akisisitiza kuwa haendi kituoni hapo na OCD hamfanyi chochote.
Grace alieleza kuwa ujumbe huo umeandikwa na Mume wake na kumkabidhi ili aifikishe kituoni huku akikiri kupata manyanyaso kutoka kwa Mume wake ambapo jeshi la polisi lilichukua hatua ya kumtafuta Mtuhumiwa na kufanikiwa kumkamata jana November 16,2021 na baada ya kukiri kosa akafikishwa Mahakamani.