Makapuku Forum

Rais wa Zamani wa Marekani Bill Clinton ametolewa Hospitali baada ya kulazwa kwa siku tano kufuatia kupata maambukizi kwenye kibofu cha mkojo.

Taarifa ya kituo cha matibabu cha UC Irvine imesema Clinton mwenye umri wa miaka 75 ameruhusiwa baada ya hali yake ya homa na chembe nyeupe za damu kurejea katika hali yake ya kawaida na kwamba amerejea nyumbani kwake mjini New York kukamilisha dozi yake ya dawa ya kukabiliana na bakteria mwilini.

Msemaji wa Rais huyo wa zamani katika kipindi cha 1993 hadi 2001, Angel Urena amesema alipelekwa Hospitali hiyo ya kusini mwa Los Angeles baada ya kupata maambukizi katika damu, yasiohusiana na Covid-19.

Gazeti la New York Times, lilimnukuu Msaidizi wa Rais huyo akisema Clinton alipata maambukizi katika kibofu cha mkojo na kusababisha maradhi yaitwayo Sepsis, maradhi ambayo yanawapata Wamarekani milioni 17 kwa mwaka kwa mjibu wa Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa na Kinga cha Marekani.
 
Taasisi ya Fally Ipupa (Fally Ipupa Foundation) na Doris Mollel Foundation zasaini makubaliano ya kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kusaidia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) katika Bara la Afrika.

Akizungumza kuhusu ushirikiano huu, Doris Mollel, Mwanzilishi wa Doris Mollel Foundation amesema ——— "Kuweza kuwafikia Watoto njiti Afrika ni ndoto tuliyokuwa nayo kwa muda mrefu sana, tunaamini ushirikiano huu na Fally Ipupa Foundation utakuwa ni mwanzo mzuri wa kuifikia ndoto hii, pia tunaendelea kuwashukuru sana Clouds Media Group kwa kuendelea ku-support Ajenda ya Mtoto Njiti kupitia vyombo vyao vya habari''

Kwa upande wake, Fally Ipupa ambaye pia ni Balozi wa UNICEF Congo amesema ——— "Hili ni jambo zuri sana, Mimi na Taasisi yangu tutashirikiana na Doris Mollel Foundation kuhakikisha Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati haswa wale wanaotoka katika familia duni wanapata mazingira bora"
 
"Nihimize katika kufanya kazi kwenu masuala ya nidhamu Longido hapa kulikuwa na Mkurugenzi mkorofi sana, hakukuwa na nidhamu ya kufanya kazi na ndio maana nikamtoa Longido nikampeleka kwingine akajifunze na hilo kumuhurumia tu ilikuwa nimuache kabisa"

"Kwahiyo niwahimize wote mnaofanya kazi katika ngazi ya Wilaya na hata ngazi za Mkoa kuheshimiana na nidhamu ya kazi, kila Mtu ana mamlaka yake muheshimiane nidhamu iwepo mfanye kazi kwa ushirikiano na maendeleo yatakuwepo"——— Rais Samia akiwa Longido leo
 
"Niliona bango linadai Mji wa Namanga, masuala haya yana vigezo vyake kwa sasa hivi Namanga bado haijakidhi vigezo lakini pia katika kudai Mji Mdogo fuateni hatua kwa hatua kila jambo lina taratibu zake"

"Lakini tukiitoa Namanga kuifanya Mji Mdogo mnaiua Longido, tusubirini tuongeze vyanzo vya mapato maendeleo yaonekane halafu tutafikiria hayo mambo baadaye lakini kwa sasa naomba mbaki kama mlivyo"——— Rais Samia akiwa Longido leo
 
Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) limetoa taarifa kwa Waislamu na Watanzania kwa ujumla kwamba Maulidi ya kuadhimisha mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W) Kitaifa yatasomwa usiku wa Jumatatu October 18,2021 katika Uwanja wa Kaitaba Bukoba Manispaa Mkoani Kagera na kufuatiwa na Baraza la Maulid litakalofanyika Jumanne Oct 19,2021 katika Uwanja huohuo wa Kaitaba.

Hivyo siku ya Jumanne October 19,2021 itakuwa ni siku ya mapumziko (Public Holiday), Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Ally Mbwana kwa niaba ya BAKWATA anawatakia sherehe njema za maadhimisho ya maulid na mapumziko mema.
 
Tanzania imetajwa kushika nafasi ya 77 kwenye orodha ya dunia ya Nchi ambazo passport zake zina nguvu zaidi huku namba 1 ikishikwa na Japan ambayo Passport yake ina nguvu ya kumuingiza mwenye nayo Nchi 192 duniani bila VISA au VISA wakati wa kuwasili.

Kwenye orodha hii Kenya imefungana na Tanzania kwenye namba 77 ambapo passport zao zina nguvu ya kuingia Nchi 72 bila VISA na kuziacha nyuma Nchi jirani kama Uganda ambayo imeshika namba 81 kwa kuingia Nchi 67 bila VISA, Rwanda namba 87 kwa kibali cha kuingia Nchi 61, Burundi namba 97 ikiwa na kibali cha kuingia Nchi 51, Congo DR namba 106 kwa kibali cha kuingia Nchi 42, Zambia namba 78 ikiwa na kibali cha kuingia Nchi 71.

Namba ya Tanzania ya mwaka 2021 ni ya juu tofauti na ile ya mwaka 2018 ambako ilikua na kibali cha kuingia Nchi 67 tu tofauti na Nchi 72 kwa mwaka 2021 kwa mujibu wa Mtandao wa Henley ambapo Mtanzania yeyote mwenye passport ya Tanzania anaweza kufika kwenye hizo Nchi bila kulipa VISA.
 
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, linamshikilia mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi Majengo, Manispaa ya Moshi, kwa tuhuma za kumshambulia mwanafunzi wa darasa la tano na kumsababishia majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Oktoba 15, 2021 shuleni hapo baada ya mwanafunzi huyo kushindwa kukamilisha kazi aliyokuwa amepewa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa akizungumza leo Jumatatu Oktoba 18, 2021 amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mwalimu huyo ambaye jina linahifadhiwa, wanamshikilia.

"Ni kweli tukio hilo lipo, mwalimu tayari tumemkamata tunamshikilia na tunaendelea kumuhoji, tunasubiri afisa ustawi wa jamii afike, ili mtoto aweze kuhojiwa,"amesema kamanda Maigwa.

Akizungumza mama wa mtoto huyo, Rose George amesema mtoto wake huyo ameshambuliwa vibaya kwa kupigwa ngumi, fimbo na mateke mwilini na mwalimu wake huyo baada ya kushindwa kumaliza kazi ya hisabati aliyokuwa amepewa.
 
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita wanaokabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi wakiingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha leo Oktoba 18, 2021 ambapo kesi hiyo inaendelea kwa ushahidi upande wa Jamhuri.
 
Simon Robert (43) mkazi wa Katunda Ibinzamata Manispaa ya Shinyanga, amenusurika kifo baada ya kuchomwa kisu tumboni na kichwani na mke wake, Amina Hamis (32) kutokana na ugomvi wa mapenzi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga George Kyando, akitoa taarifa ya tukio leo kwa vyombo vya habari, amesema limetokea saa 7 usiku wa kuamkia leo Oktoba 18.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi, ambapo wanandoa hao walianza kugombana baada ya kutuhumiana wao kwa wao ndipo mwanamke alipochukua kisu na kumchoma mwenzake kichwani na tumboni.

“Majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Rufani mkoani Shinyanga akipatiwa matibabu na hali yake ni mbaya sababu alichomwa kisu sehemu mbaya za kichwani na tumboni,” amesema Kyando.
 
Mti wa asili uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere umeshindwa kukatika na kubaki katikati ya barabara umekuwa kivutio kwa watalii kwa kutaka kuuona na kuushika kutokana na historia yake kutumiwa kufanya matambiko mbalimbali na jamii.

Mti huo aina ya Marula umekuwa kivutio kwa watu wanaofika kutembelea hifadhi hiyo ambapo mti huo unaelezwa kusaidia mahitaji ya wahusika.

Mti huo umelazimika kuachwa eneo hilo baada ya jitihada za kuukata kushindikana hivyo wajenzi wa barabara waliamua waweke barabara mbili pacha wakati wa upanuzi wa barabara ndani ya hifadhi hiyo ya Nyerere ikitokea Kijiji cha Mloka wilayani Rufiji Mkoani Pwani.

Ofisa Uhifadhi Mwandamizi, Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Seth Mihayo, akizungumzia mti huo alisema umekuwa kivutio kwa sababu wakati wa upanuzi huo wa barabara licha ya kutumia vifaa vya kisasa kama magreda ya kukata miti mikubwa mti huo ulishindikana kukatika na badala yake vifaa hivyo licha ya kuwa vya kisasa lakini viliishia kuharibika na mti kuendelea kubaki.
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiondoa Kitambaa kuzindua kiwanda cha nyama cha Eliya Food Overseas LTD kiliopo Eurendeke Longido Mkoani Arusha leo Oktoba 18, 2021.

Rais Samia yupo Mkoani Arusha akiendelea na ziara yake ya kikazi kutembelea, kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo ya Wananchi Mkoani Arusha, wa pili kulia Waziri wa Maji Jumaa Aweso, Mkuu wa Mkoa Arusha John Mongela, kushoto Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo.

 
Tathmini mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonyesha ni asilimia 14.2 tu sawa na mtu mmoja kati ya watu saba walioambukizwa Uviko-19 hugunduliwa barani Afrika.

Ripoti hiyo iliyotolewa Oktoba 14, imeeleza kuwa ili kubadili mwenendo huo na kuzuia maambukizi kusambaa, Ofisi ya Kanda (WHO ya Afrika) imetangaza mpango mpya wa kuongeza kasi ya upimaji Uviko-19 katika nchi nane.

Mpango huo unakusudia kufikia zaidi ya watu milioni 7 na vipimo vya haraka vya uchunguzi kwa mwaka ujao.

Uchambuzi wa WHO ulitumia kikokotoo cha Uviko-19 kilichotengenezwa na ‘Resolve to Save Lives’ ambayo inakadiria maambukizi kulingana na idadi ya visa na vifo na kiwango cha vifo vya maambukizi kilichowekwa kwa idadi ya watu.

Kikokotoo hicho kiligundua kuwa kufikia Oktoba 10, 2021 idadi ya jumla ya maambukizi ya Uviko-19 inakadiriwa kuwa milioni 59 barani Afrika, ambayo ni mara saba zaidi ya visa zaidi ya milioni 8 vilivyoripotiwa.
 
Kiwango cha ulaji wa mayai nchini kwa mtu mmoja kwa mwaka kimeshuka kutoka mayai 300 hadi mayai 106.

Kauli hiyo imetolewa jana Oktoba 17,2021 na Waziri wa kilimo, Profesa Adolf Mkenda wakati akifunga maadhimisho ya kilele cha siku ya chakula duniani iliyofanyika kitaifa mkoani Kilimanjaro

"Ulaji wa mayai nchini kwa mtu kwa mwaka ni mayai 106 ,kiwango hiki ni cha chini ukilinganisha na kiasi kinachopendekezwa ambacho ni mayai 300 kwa mtu kwa mwaka," amesema Profesa Mkenda.

Profesa Mkenda amesema walaji wa mayai ni wale wenye kipato cha juu na cha kati ambapo wengi wao ni waliopo maeneo ya mijini na vyuoni.

Amesema pamoja na kiwango ulaji wa mayai kuwa chini, uzalishaji wake umeongezeka kutoka bilioni 3.58 kwa mwaka 2019/20 hadi 4.5 kwa mwaka 2020/21 sawa na ongezeko la asilimia 26.
 
Machinga Jijini Dar es Salaam wameongezewa siku 12 kuanzia leo kuhama maeneo yasiyo rasmi ya kufanya biashara.

Kuondoka kwa wafanyabiashara hao mwisho ilikuwa iwe leo Oktoba 18,2021 baada ya kutolewa kwa siku 30 ambazo zilianza Septemba 18.

Nyongeza hiyo ya ya siku 12 imetolewa leo Jumatatu Oktoba 18, 2021 na Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wa Kariakoo kuhusiana na mpango huo wa kuwaondoa.
 
Polisi wilayani Nkasi mkoani Rukwa, inamshikilia mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Kennedy Fumpa (37) mkazi wa kitongoji cha Mabatini katika mji mdogo wa Namanyere kwa tuhuma za kuoa mwanafunzi wa darasa la tatu.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 11 na anasoma shule ya msigi Kipundukala iliyopo mjini humo.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mabatini, Godfrey Kalungwizi amesema jitihada za kumtafuta mwanafunzi hiyo zilianza baada ya kupata taarifa za utoro, ndipo walibaini kuwa ameolewa na mwanaume huyo.

Inadaiwa binti huyo aliozwa na bibi yake waliyekuwa wakiishi naye kwa gharama ya Sh400,000 lakini mwanaume huyo alipotoa Sh330,000 na kuongeza kitoweo aina ya Nguruwe chenye thamani ya Sh 70,000 na kukamilisha kiwango hicho cha fedha kilichohitajika kama mahari ya binti huyo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kipundukala, Josephat Laban amekiri kuwa binti huyo ni mwanafunzi wake wa darasa la tatu na alitoweka shuleni hapo kwa muda na kuhesabika kama mtoro, ambapo jitihada za kumtafuta zilikuwa zikiendelea bila mafanikio.
 
Nafikiri tangu msimu uliopita Simba ndio klabu yenye safu bora ya ulinzi kwenye mashindano ya vilabu Afrika...ubora huo unachagizwa sana na golikipa wao Manula (Aishi).

- Florent Ibenge, Kocha Mkuu RS Berkane.
 
Nililijua hili...
 
Dani Alves:
.
"Kila Mbrazil anayevaa jezi ya timu yake ya taifa basi anakuwa na uwezo mkubwa. Nje ya timu ya taifa nasikia watu wengi wakilalamika juu ya wachezaji wetu, mfano mzuri ni FRED. Lakini ukimtazama anapoichezea Brazil ni anaonyesha kuwa yeye ni bora kuliko viungo wote wa Manchester. Shida ni klabu au kocha, sio Fred. Mtazame akiichezea Brazil, ni mzuri zaidi kuliko wakati amevaa jez nyekundu. "
.
Mnakubaliana na Alves? tatizo ni Fred au klabu __!!
 
BIASHARA WAISHUKURU TFF, WAAPA KUPAMBANA KUFUZU
.
TFF imeamua kuahirisha mchezo huo wa Biashara dhidi ya Prisons uliokuwa upigwe kesho mjini Sumbawanga Rukwa, ili kuwapa nafasi wawakilishi hao kujipanga kwa safari ya kuwani mchezo wao wa Libya utkaopigwa wikiendi hii.
.
Meneja wa Biashara Frank Wabare amesema: ”Tunashukuru kwa mchezo huo kusogezwa mbele sasa tutapata muda wa kujifua kwaajili ya mechi dhidi ya Tripoli ugenini pia tutapa muda wa kushugulikia taratibu zote za safari kwa usahihi.”
.
“Kambi inaendelea hapa Dar na kila kitu kipo vizuri, tumepanga kusafiri Jumatano au Alhamisi kwa ndege ya kuunga kwani hakuna ya moja kwa moja hadi Libya, imani ya timu nzima ni kulinda ushindi wetu na kusonga mbele kwa hatua inayofuata ya michuano hiyo ya CAF, “ alisema.
.
Naye Kocha mkuu wa Biashara amesema; “Kuahirishwa kwa mchezo huo ni taarifa nzuri na imetufanya tuendelee kujinoa kwa ajili ya mechi ya Tripoli. Nimewaona wakicheza kwao, ni timu ngumu hivyo licha ya kwamba tuliifunga nyumbani, tutaenda kucheza kwa tahadhari kubwa ili tuweze kufuzu hatua inayofuata.”

…………………….
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…