Makala: Zitto Kupanda au kushuka | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Makala: Zitto Kupanda au kushuka

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by SubiriJibu, Sep 2, 2009.

 1. S

  SubiriJibu JF-Expert Member

  #1
  Sep 2, 2009
  Joined: Jun 26, 2009
  Messages: 1,124
  Likes Received: 776
  Trophy Points: 280
  ___________________________
  Soma RAIA MWEMA ya leo:

  Inapatikana hapa
  ___________________________

  NILIIPOKEA vizuri taarifa ya uamuzi wa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe (Mb) kuchukua fomu ya kugombea uenyekiti wa chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika leo Jumtano.

  Nilimwuunga mkono Zitto kwa moyo wangu wote, kumpongeza, na kumwombea dua apambane vyema na Mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe katika kinyang’anyilo hicho. Najua si mimi peke yangu, bali na Watanzania wengine kadhaa walifurahia uamuzi huo adimu wa Zitto; ingawa wapo pia waliouona kama usio sawa sawa.

  Binafsi nilimuunga mkono Zitto kwa sababu kuu nne. Kwanza, nilijua kwamba uamuzi wake ungeleta msisimko mkubwa katika siasa za Tanzania kwa mwaka huu, msisimko wenye mwelekeo tofauti na msisimko wa muda mrefu katika siasa za Tanzania kwa kipindi cha miaka miwili sasa.

  Kwa miaka kama miwili sasa, siasa za Tanzania zimekuwa na msisimko mmoja tu – Ufisadi, na ndani ya huo, makundi ndani ya CCM na kusumbuka kwa Serikali ya Rais Kikwete kupambana nao.

  Kwa maoni yangu, sio jambo jema sana kwa siasa za nchi kuegemea agenda moja tu kwa muda mrefu sana. Upepo wa kisiasa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi, lakini lazima uvume kwa muda na kisha kupisha mawimbi mapya!

  Madhara ya agenda moja kuvuma kwa muda mrefu sana bila kupitwa na wakati, ni pamoja na kujenga usugu kwa yule anayeelemewa na agenda hiyo, kuwafanya wengine wajisahau katika mapungufu waliyonayo kwa kuwa hayaguswi kwa muda mrefu; maana taifa lote linakuwa linang’ang’ana tu na udhaifu wa aina nyingine isiyowagusa wao kwa wakati huo, na kisha kujenga viwango vikubwa vya visasi miongoni mwa jamii.

  Siamini kwamba CHADEMA na vyama vingine vya upinzani ni vitakatifu. Nina uhakika vinayo mapungufu na mengine tunayajua. CCM ina mapungufu mengi, tena yanaonekana kwa uwazi zaidi kwa sababu ya ukubwa wa chama, na ‘u-kioo’ wa chama kwa vile ndicho kina serikali.

  Yanapotokea mashambulizi ya kukisakama CCM, kwa maoni yangu, inakisaidia kujirekebisha (iwe kwa kupenda au kwa kulazimika), na kujiweka katika nafasi bora zaidi kisiasa. Siyachukii hata kidogo mashambulizi ya kisiasa.

  Lakini kusukwasukwa kisiasa kunakoikabili CCM ni muhimu kuvikabili pia na vyama vingine vya kisiasa vya upinzani; hata kama ni kwa kiwango pungufu.

  Nasema hivi kwa sababu chama kinachojitahidi kama CHADEMA, ni chama ambacho kinaweza wakati wowote kuwa mbadala wa CCM na kukamata dola.

  Ni kwa maana hiyo hatuwezi kujivunia kukiacha chama hiki ambacho wakati wowote kinaweza kuiongoza nchi yetu bila kupata changamoto za kukumbushwa mapungufu yake, kusukwa sukwa japo kidogo ili kijiweke bora zaidi kisiasa.

  Maana; ieleweke wazi kwamba mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Chama kikiwa na mapungufu kikiwa kwenye kambi ya upinzani kikabembelezwa mapungufu yake yasiguswe, kikishashika dola itakuwa vigumu zaidi kukibana kwa mapungufu yale.

  Kwa mfano, pale ambapo chama kinatuhumiwa kwa ukabila au ukanda kikiwa bado kiko kambi ya upinzani, yafaa kibanwe sana na kikikaidi umma ukiadhibu kwa udhaifu huo kabla hakijatwa dola ili kikitwaa dola kiwe kinajua wazi kwamba kinaweza kupoteza dola ikiwa kitaendekeza ukabila.

  Yatupasa kukumbuka kwamba Watanzania hatujawahi kushuhudia chama tawala kikinyang’anywa dola kwenye uchaguzi. Hivyo hatujajua umuhimu wa kukiandaa chama pinzani kuwa chama tawala makini kwa mahitaji ya wananchi, na siyo tu kwa ilani na sera zilizoandikwa kwenye makaratasi na chama chenyewe.

  Sasa kwa kuwa udhaifu wa chama huweza kukabiliwa vizuri zaidi kutoka ndani kuliko nje, ilikuwa muhimu sana kwa CHADEMA kupita kwenye uchaguzi wenye ushindani mkubwa wa mitazamo ili wao wenyewe wakosoane sera na mielekeo yao.

  Wote tumeshuhudia kwamba wakati wabunge wa upinzani wakiongozwa na DK. Slaa na Mh. Zitto wakiishambulia Serikali ya CCM kwa ufisadi, chama hiki tawala hakikuweweseka kwa kiwango kikubwa kama kilivyokuja kuweweseka juzi baada ya wabunge wa CCM wenyewe wakiongozwa na kina Mh. Anne Kilango, Spika Sitta, Dk. Mwakyembe, nk.

  Ni kwa sababu vita ya kutoka ndani huwa makini na yenye mashiko zaidi kuliko ya kutoka nje!

  Sababu ya pili ya kumuunga mkono Zitto Kabwe ilikuwa imani yangu kwamba Zitto ni mpinzani bora zaidi nchini kwa sababu rekodi zake zinamweka kama mtu pekee ndani ya kambi ya upinzani ambaye siasa zake za upinzani hazina agenda ya siri zaidi ya ile moja ya kuitafutia Tanzania serikali mbadala wa serikali ya chama kilicho madarakani.

  Maana tumekuwa tukiwashuhudia wapinzani ambao ishara zinaonyesha, tetesi zinaaminisha, na hata uchunguzi unasisitiza kwamba kuibadili CCM madarakani ni agenda ya juu tu, lakini agenda kamili ndani ni ama utajiri, biashara, utukufu, au kitu kingine kifananacho na hivyo.

  Sababu ya tatu ya kumuunga mkono Zitto ilikuwa tamaa yangu ya kuishuhudia CHADEMA ikitekeleza kwa vitendo kile ambacho imekuwa ikikikemea sana dhidi ya CCM; nacho ni kwamba CCM imekuwa na utamaduni wa kuvumiliana na kusulubiana kwenye kinyang’anyilo cha ugombea urais ili aliye madarakani kwa miaka mitano ya kwanza aachiwe kumalizia kipindi cha pili; na kwamba rais wa nchi atokanaye na CCM asipingwe inapofika wakati wa kugombea uenyekiti wa chama.

  CHADEMA wamekuwa wakiuponda sana utaratibu huu kwamba ni wa kizamani, unaokandamiza demokrasia, na unaoinyima CCM na nchi nafasi ya kupata viongozi bora.

  Hili nalikumbuka zaidi miezi kadhaa iliyopita, viongozi kadhaa wastaafu wa CCM wakiongozwa na Mzee Pancras Ndejembi walipowashauri wana CCM wasijitokeze kuchukua fomu kumkabili Rais Kikwete mwaka 2010. CHADEMA waliwapinga na kuwazomea sana wazee hawa.

  Makada wawili maarufu wa CHADEMA wanaotekeleza ukada wao kwa njia ya uandishi, kaka zangu Absaloom Kibanda na Ansbert Ngurumo waliandika makala nzito gazetini kuwashambulia wazee wale na CCM yao; huku wakijitahidi kuuonyesha umma ‘uhafidhina’ wa CCM.

  Ndiyo maana niliposikia Zitto kachukua fomu kupambana na Mwenyekiti wake Mbowe, nikajua sasa CHADEMA wamepata nafasi ya kutuonesha kwa vitendo kile walichokuwa wanakikemea kwa maandishi na matamshi.

  Nilisubiri kwa hamu kuwasoma tena kina Kibanda na Ngurumo, na wengine wakimtia moyo Zitto na kuwakemea wote ambao wangemwambia Zitto amekosea kumkabili mwenyekiti wake!

  Sababu ya nne ilikuwa hamu yangu ya kuiona CHADEMA, kwa mara ya kwanza, ikipokezana kijiti cha uenyekiti kwa mtu ambaye hana uhusiano wa zaidi ya ule wa kisiasa na mwenyekiti aliyemtangulia. Mtu ambaye hana undugu wa kifamili, wala wa ukwe wala historia ya kufanya kazi pamoja Benki Kuu miaka ya nyuma, na mwenyekiti aliyemtangulia!

  Faida ya jambo hili ni mwanya wa chachu ya mawazo yenye mtiririko tofauti na yenye uzoefu tofauti, na hata yenye makuzi tofauti na mtangulizi wake. Hii ni muhimu kwa ukuaji wa chama na upana wa vionjo vya kisiasa.

  Tofauti na Mh. Hamad Rashid aliyenukuliwa akisema alitarajia Zitto asingefika mbali na nia yake, mimi niliamini sana Zitto angegangamala na kumkabili Mbowe kikweli kweli.

  Lakini sivyo ilivyotokea; kwani dakika za mwisho Zitto alijitoa kugombea akisingizia ushauri kutoka kwa wazee wa CHADEMA!
  Hiyo ni mara yangu ya kwanza kumuona Zitto akikosa msimamo na kuweweseka kimaamuzi. Niliamini Zitto asingesikiliza kelele za chura, angeendelea kuyanywa maji mpaka akate kiu yake.

  Nilitambua uwezekano wa Zitto kushinda au kushindwa kwenye uchaguzi, lakini nilitamani ashindwe kwa idadi ya kura na siyo kwa ‘ushauri wa wazee’.

  Nafsi yangu ilianza kupigwa bumbuwazi niliposoma makala ya kaka Kibanda akimtisha Zitto kwamba uamuzi wa kumkabili Mbowe ni anguko lake mwenyewe. Nikajua kaka Kibanda kapitiwa tu akasahau kwamba kwa kuandika hivyo anaikana tahariri yake mwenyewe aliyopata kuiandika dhidi ya kina mzee Ndejembi!

  Nilishangaa zaidi kuona kaka Ngurumo naye anaipigilia zaidi msumalr ‘Demokrasia ya CHADEMA’ kwa kumponda rafiki yake wa karibu Zitto, na kumuunga mkono Kibanda!

  Ndipo kilipoibuka kitu ambacho majigambo ya siku zote ya CHADEMA yalinifanya nisitarajie kukiona kikiibukia CHADEMA. Kwamba demokrasia ya chama na mwanachama ikatelekezwa kwa njia ya ‘ushauri wa wazee’.

  Wazee wale wale waliokianzisha chama na kukiwekea katiba inayompa mtu uhuru wa kugombea uongozi bila uhuru wake kuathiriwa na msukumo toka ndani au nje ya chama!

  Hivi ikitokea leo Mwalimu Nyerere akafufuka akawakusanya wazee wenzake kina Kawawa alioasisi nao taifa hili; Wakawaweka kikao CHADEMA na kuwapa ‘ushauri wa wazee’ kwamba kwa kuwa ni chama chenye umri mdogo sana kuliko CCM, basi, wasiwe na haraka kugombea dola (urais) wala ubunge, waiachie kwanza CCM nafasi na wao watapewa dola wakati wao ukifika; watakubali?

  Watamwelewa Mwalimu akiwashauri kwamba wasiipinge CCM ili kuzuia mpasuko wa nchi? Maana ni kweli CHADEMA kuipinga CCM kunasababisha sasa hivi nchi iwe ya moto. Kama wazee hawa wanaona changamoto ambazo CHADEMA inaipa CCM ni muhimu, kwa nini waone ni makosa Zitto kumpa Mbowe changamoto?

  Tutakosea tukipata mashaka kwamba huenda hapa wazee walikuwa wanalinda tu heshima ya ‘mkwe’, na siyo maslahi ya chama?

  Nilisononeka zaidi nilipomwona, kwa mara ya kwanza, Zitto akizungumza na waandishi wa habari huku akijiumauma. Sikuwahi kumwona akiwa katika unyonge huo. Ni pale alipokuwa anakiri kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti kwa kuheshimu ‘ushauri wa wazee’ badala ya nguvu ya demokrasia.

  Alijitetea kwamba amefanya hivyo baada ya wazee kumwabia kwamba kugombea kwake kunaweza kukisambaratisha chama.

  Hiki ni kichekesho. Ina maana Zitto hana akili za kutosha wala upeo wa kuona jambo lipi linaweza kusambaratisha chama na lipi haliwezi kusambaratisha chama, mpaka aambiwe na wazee?

  Ina maana Zitto hajimudu kichwani, hana uwezo wa kupima uzito wa mambo, ndiyo maana akaaamua jambo baya bila kujua, mpaka alipoambiwa na wazee ndipo akajua?

  Sasa wa nini huyu kuwa mbunge na mwakilishi wa watu kwenye jimbo ambalo namo kuna wazee? Si awapishe wazee; maana yeye hana busara ila wao? Wa nini huyu siku nyingine kupigiwa kura kuongoza watu wenye uwezo wa kuona mema na mabaya wakati yeye hawezi kuona mema na mabaya mpaka aambiwe na wazee?

  Ingemwachia Zitto heshima kutochukua kabisa fomu ya kugombea kuliko kuchukua fomu kwa jeuri ya demokrasia na kisha kujiondoa kwa jeuri ya ‘ushauri wa wazee’.

  Amesahau kwamba yeye ni tofauti na mwana CHADEMA mwingine yeyote. Zitto ni alama ya CHADEMA na nguzo ya upinzani nchini. Uamuzi wowote wa kijasiri unaofanywa naye lazima unawagusa wengi nchini na kuvuta zaidi mshikamano wa mapambano ya kuiendeleza nchi.

  Lakini uamuzi wowote wa kilegelege kama huu wa ‘ushauri wa wazee’ unawaponda wengi mioyo na kuwakatisha tamaa. Uamuzi wa ‘ushauri wa wazee’ aliochukua Zitto umetia doa rekodi ya demokrasia ya CHADEMA.

  Maana; kama Zitto amekiri kwa kinywa chake mwenyewe kwamba wazee wamemwambia akigombea uenyekiti chama kitasambaratika, ina maana wanajua na yeye ameeleweshwa, kwamba demokrasia ikiheshimiwa ndani ya CHADEMA chama kitasambaratika.

  Hii ndiyo kusema kwamba CHADEMA inasamabaratishwa na demokrasia na kuimarishwa na ‘ushauri wa wazee’.

  Kwa kuwa Zitto ametamka kauli ya aibu kwamba amekataa ‘rushwa’ ya wazee kwamba atoe jina lake kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti ili apewe ukatibu mkuu, ina maana amekiri kwamba kuna rushwa ndani ya CHADEMA, na kwamba huenda hata Mbowe ametetewa na wazee kwa sababu wana maslahi fulani binafsi na uongozi wake. Basi tusimsikie Zitto akipokea cheo chochote kingine ndani ya CHADEMA; maana kakiri mwenyewe kwamba amekataa cheo kama mbadala wa fomu yake ya kugombea. Akipewa akapokea tutajua ‘changa’ tayari.

  Vyovyote vile baada ya kuyumba katika suala lile la Dowans na ukigeugeu huu aliouonyesha katika uchaguzi huo wa CHADEMA, chati ya umaarufu wa Zitto haiwezi kubakia vilevile ilivyokuwa mwaka jana au juzi.

  Nimalizie kwa kumuasa Mh. Zitto kutokosea tena na kufanya maamuzi legevu kiasi hicho. Huenda jamii isimhukumu sana kwa kosa la leo; maana ni la pili tu baada ya lile la kusisitiza TANESCO inunue mitambo chakavu ya kampuni inayotuhumiwa kwa ufisadi ulioitikisa sana nchi. Lakini akiendelea hivi na akafanya kosa la tatu, huo utakuwa ndiyo mwisho wake kisiasa!
   
 2. M

  Mwafrika JF-Expert Member

  #2
  Sep 2, 2009
  Joined: Nov 20, 2006
  Messages: 5,490
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 0
  Naona mwandishi kasahau kosa lingine la Zitto - kujiunga kwenye kamati ya madini ya Kikwete. Kamati ambayo ilikula pesa tu na haikufanya chochote kuzuia uuzwaji wa mali na ardhi ya watanzania kwa Barick.
   
Loading...