Maisha ni fumbo, imeniuma sana

Maisha ni fumbo, imeniuma sana

OIL CHAFU

JF-Expert Member
Joined
Jun 8, 2012
Posts
996
Reaction score
776
Maisha ni fumbo tata ambalo huwezi kulifumbua, kitu pekee kinachoweza kutegua fumbo hilo ni muda.

Ilikuwa mwaka 1994, nilipoanza kidato cha kwanza, baba yangu ambaye ndiye tegemeo langu kunisomesha kwa asilimia 90 aliugua, aliparalayze, akafariki. Niliona dunia chungu, kwani baada ya pale maisha yangu ya shule siwezi kueleza isipokuwa Mungu tuu anajua. Kama ni kibarua kwenye mashamba ya watu nilifanya, mkaa nilichoma, biashara ya kuuza mboga, nyanya, matunda, nafaka nilifanya ili nipate ada lakini maisha yakawa magumu zaidi.

Mwaka 1995, siku moja nilimtembelea mzee mmoja ambaye yeye na mkewe walikuwa wafanyakazi wa serikali. Tulikuwa tunasali kanisa moja, hivyo tulifahamiana. Siku hiyo nilipowatembelea, nilikuwa nimeishiwa kabisa sikuwa hata na shilingi moja mfukoni. nilitembea umbali wa kilomita sita kufika kwao. Lengo langu ilikuwa niwaeleze tatizo langu ili wanisaidie walau 1,000/- ili ninunue mchicha wa Tsh. 20/-, mafuta ya sh. 50/- kalamu moja na daftari na sabuni. Kwa sh. 1,000 ingetosha bajet ya wiki nzima.

Nilipofika nyumbani, sikumkuta yule mzee, niliwakuta watoto. Baada ya muda mfupi mama akaja kutoka sokoni akiwa amebeba mizigo mingi sana, ameletwa na gari. Alipofika watoto walimpokea mama yao na kuanza kula vitu mbali mbali kama ndizi, embe na mengineyo. Jikoni binti alikuwa anapika chakula cha mchana na harufu tamu sana ya vitu kukaangwa ilikuwa iannifikia sebuleni. Nilikuwa na njaa sana kiasi kwamba mdomo ulikuwa umekauka.

Kwa nini naandika uzi huu? Endelea kusoma utanielewa.
Jitihada zangu zote za kuomba sh 1,000 ziligonga mwamba, mama alinijibu kuwa kama nimeshindwa shule nirudi kijijini kwetu nikalime. Watoto wakawa wananiangalia alafu wananicheka kwa jinsi nilivyovaa nguo ambazo haziendani na hadhi ya mjini. Miguu ilikuwa imejaa vumbi, viatu ni vya katambuga (matairi), jua lilikuwa kali nilitokwa jasho. Laiti ningepewa hata ndizi moja nikala au tonge moja la ugali lingenipa nguvu ya kurudi kwangu, niliambulia maji ya kunywa, tena baada ya kuomba.

Nikiwa njiani kurudi getoni kwangu, niliona kizungu zungu, jua lilikuwa kali, lakini mawazoni mwangu niliona giza likitanda mbele yangu. Niliona uchungu kwa nini wale vijana, tena wadogo kwangu wananicheka kwa sababu miguu yangu ina vumbi, nguo zangu hazina hadhi, chafu, hazijapigwa pasi.Nikamkumbuka baba yangu marehemu, sina baba nikalia machozi.

Nikiwa nakatiza mjini, sikutaka hata kumtazama mtu yeyote njiani, nilichojali ni kufika getoni kwangu. Mara nikasikia sauti ya mtu aliyeniita jina langu. Alikuwa jirani yetu kule kijijini. Alikuwa anafanya biashara kwenye mnada sehemu mbali mbali. Nikakumbuka kuwa kesho yake ni soko la mnada pale mjini, na yeye amekuja kuleta biashara zake.

Yule kaka aliniambia ndo kafika mjini na hajapata mahali pa kulala. Akaniomba kama kwangu kuna nafasi aje. Nikamwambia ndiyo kuna nafasi. Akanipa Tsh. 5,000 ili nikaandae chakula cha jioni. Nikamwacha mjini na mizunguko yake huku nikinunua nyama na mahitaji mengine. yeye alisema atakuja jioni. Sikuamini macho yangu kuwa siku ile nilinunua nyama, vitunguu, nyanya, mafuta, daftari, sabuni, na bado nikabakiwa na sh. 2,000. Kumbuka that was, 1995.

Miaka 19 baadaye.!!!!!!!
Nikiwa mkoa mwingine (takriban kilomita 1,000 kutoka kule nilikokuwa nasoma), nikiwa naendesha gari mjini, macho yangu yanagongana na kijana ambaye sura yake siyo ngeni kwangu, ila siwezi kumfahamu vizuri. Nikiwa nimempita kidogo, nikapunguza mwendo na kupaki gari pembeni. Nikashusha kioo cha gari na kumwita yule kijana ili nijue kama tunafahamiana. Kumbe ni mtoto wa yule mama aliyeniambia kuwa nikishindwa shule nirudi kijijini nikalime.

Kijana afya yake haikuwa nzuri sana, alikuwa amedhoofu. Katika kumwuliza, akaniambia mama yake alifariki kwa ugonjwa wa pressure na kisukari, mzee ameshastaafu. Pia yeye amemaliza chuo cha ualimu grade A, na amepangiwa mkoa ninaokaa, lakini vijijini. Anasema amesimamishwa mshahara wake yapata miezi mitatu kwa sababu ya kutoelewana na mkuu wa shule (mgogoro ulihusu suala la kuhama na kutaka kwenda shule). Alinisimulia mengi, lakini lingine ni kuwa familia yao iko kwenye wakati mgumu kwani kuna mgogoro wa mirathi baada ya mama kufariki, hata mzee hali yake ya kiuchumi ni mbaya sana.

Nilimwangalia kijana kwa kweli anatia huruma, wakati mwingine akiongea anatokwa na machozi. Namwona ni mtu aliyekata tamaa. Nashindwa kuamini kama ndio wale waliokuwa wakinicheka miaka 19 iliyopita. Aliniomba hela kama naweza kumsaidia walau nauli, japo sikuwa na hela wakati ule nilimpa 5,000. Siwezi kujua anawaza nini moyoni mwake anaponiona.

Jamani, usimdharau mtu kwa sababu ya unyonge wake leo, hujui kesho atakuwaje na pia wewe utakuwaje. Leo nimetokwa na machozi kwa kukumbuka mkasa huu.
 
If you make jokes with this thread, basi hujajua maana ya maisha. Iko siku na wengine watakujoke, wakati wewe uko serious. Sijaweka hata chembe ya joke kwenye huu uzi. Tatizo kuna watu humu hawajaexperience maisha kama haya. Usiombe yakukute.
 
Dah!..ama kweli wahenga walisema "hujafa hujaumbika"
~inauma sana...lakini kubwa zaidi kila mtu anasiku yake ya faraja...na simanzi..kila mwenye akili na utu na ajifunze kupitia kisa hiki.
 
Jaman hii story hasa kwa upande wa kukosa ada na kushindwa kusoma inahusu wengi sana mimi nikiwa mmjawapo, mtu unakuwa kama mjinga vile ni kwa sabb tu huna pa kushika kwa muda huo, omba uwe unausoma tu huu uzi na hayajakukuta kwani hata mimi machozi yamenitoka kwani nimekumbuka mbali sana.
 
Back
Top Bottom