Magazetini
JF-Expert Member
- Aug 16, 2014
- 593
- 1,713
BEI ya rejareja ya mahindi kwa mikoa ya Rukwa na Katavi imeporomoka kwa kasi kubwa kufuatia wakulima kuvuna kiasi kikubwa cha zao hilo ambalo sasa limekosa soko la uhakika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, wakulima hao wamedai gunia la mahindi lenye uzito wa kilo 100 kwa sasa linauzwa kati ya Sh 18,000 na Sh 20,000 tofauti na bei ya msimu uliopita ya Sh 45,000.
Imeelezwa kuwa wakulima walikuwa wakitegemea kuuza kwa wingi mahindi yao kwa Wakala wa Taifa wa Chakula (NFRA), Kanda ya Sumbawanga mkoani Rukwa lakini amepangiwa kununua tani 35,000 za mahindi katika msimu huu wa uuzaji wa mahindi ambao umeanza.
Mmoja wa wakulima maarufu wa zao hilo wilayani Mpanda, William Mbogo alisema msimu huu wa kilimo amevuna zaidi ya gunia 200 za mahindi lakini yamekosa soko.
"Sisi wakulima katika mikoa hii ya Rukwa na Katavi tumehamasika na kulima mahindi kwa wingi kwa kufuata kanuni bora za kilimo hivyo kuvuna ziada kubwa ya zao hili lakini cha kusikitisha yametudodea hatuna soko la uhakika," alisema.
Wengi wa wakulima wa mikoa hiyo wanalilia soko la uhakika la mahindi wakisema yanawadodea kutokana na nchi jirani, Zambia, pia kuvuna ziada kubwa ya mahindi.
Mkulima mwingine wa wilayani Nkasi, Credo Nkanga alisema wamekata tamaa kulima mahindi kutokana na kukosa soko la uhakika.
"Sasa hivi ukitoka na kutaka kununua mahindi wakulima watakuchangamkia kwa kukuuzia kwa Sh 18,000 kwa gunia la ujazo wa kilo 100 kwa kukosa soko la uhakika hakika kwetu sisi wakulima wadogo ni majanga," alisema Nkanga.
Mwenyekiti wa Matai Agriculture and Marketing Cooperative Society Ltd (MAMCOS), Kaprikoni Kayumbi anapendekeza bei ya ununuzi kwa msimu ujao wa mahindi iwe kati wa Sh 750 na 800 kwa kilo kupitia NFRA kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji.
"Soko tunalolitegemea kwa sasa ni NFRA lakini bei yake bado haikidhi hivyo tunaiomba Serikali kupitia wakala wake huyu tumuuzie mahindi kwa bei ya ushindani," alisema.
Kwa mujibu wa Meneja wa NFRA, Kanda ya Sumbawanga, Amos Mtafya katika msimu huu wa ununuzi wa mahindi mikoa ya Rukwa na Katavi imepangiwa kununua tani 40,000 pekee za mahindi ambazo ni sawa na asilimia 10 ya ziada ya tani 359,785 zilizovunwa msimu huu wa kilimo mkoani Rukwa pekee.
CHANZO: Habari Leo