Mahakama za dini zijadiliwe kwa kina | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mahakama za dini zijadiliwe kwa kina

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Paschal Matubi, Sep 15, 2008.

 1. P

  Paschal Matubi Member

  #1
  Sep 15, 2008
  Joined: Sep 15, 2008
  Messages: 92
  Likes Received: 31
  Trophy Points: 25
  WAKATI mijadala kuhusu kuanzishwa kwa mahakama za kidini, unaoongozwa na mjadala wa kuundwa kwa Mahakama ya kadhi, inapamba moto, nadhani ni wakati muafaka wa kukaa chini na kutafakari kwa kina na kuyasoma kwa makini mawazo yote yanayowasilishwa.

  Kwa njia hiyo tutajikuta tumefika mahala tunajua mahitaji ya wengi katika jambo hili. Baada ya hapo kitakachobaki ni kutathmini uwezo wa kufanyia kazi yaliyopendekezwa. Naamini wataalamu wa uchumi, sheria na wengine watatusaidia kwa hilo la mwisho.

  Wasiwasi wangu ni kutokuwa na uhakika na idadi ya wanaoelewa vizuri miundo ya mahakama za madhehebu yetu.

  Ingawa kinachozungumziwa kwa undani ya Mahakama ya Kadhi, lakini tufahamu kuwa kimsingi kinachojadiliwa hapa ni mahakama za kidini.

  Kwa kuwa mimi napata nafasi kusoma sheria za dhehebu langu (Kanisa Katoliki). Leo ni nafasi yangu kueleza ninachokiona ndani ya sheria hizo.

  Lengo ni kuwasilisha maelezo ya muundo wa mahakama za kanisa langu, ili tunapotamka Mahakama ya dini tutarajie nini kutoka kwa Wakatoliki.

  Kueleza muundo sidhani kuwa ni kitendo cha kujiunga na moja ya kambi zilizogawanyika wakati wa mjadala.

  Hata nikihofu kutogawanyika haitasaidia maana sina uwezo wa kujadili lolote zaidi ya ukatoliki. Hivyo mengi ninayoeleza ni ya ukatoliki.

  Mahakama ni neno la Kiswahili linaloeleweka kama chombo cha kusimamia haki. Kuelewa mahakama za Kanisa Katoliki ni vizuri kudadisi kwanza muundo wa utawala wa kanisa hilo.

  Pia ni muhimu kujua baadhi ya sheria zinatumika katika kanisa hilo.

  Nahofu mazoea yanaweza kufanya utawala wa kanisa na tawala za nchi kama yetu, ambayo huongozwa kwa kutenganisha mihimili mitatu ya mamlaka, kuanza kuchanganya mambo.

  Kanisa Katoliki ni tofauti. Ni kawaida kukuta mtawala ndiye anatunga sheria au kushiriki vikao vya kutunga sheria na vilevile aweza kuwa ni jaji au yumo katika jopo la majaji (tribunal) wa kesi.

  Kanisa lina sheria nyingi. Hapa yatosha kutambulisha zile zijulikanazo kwa jina la Canon Laws.

  Hizi zimeorodheshwa kwa namba kuanzia ya kwanza hadi ya 1752. Sheria hizi zaweza kupatikana kwenye maduka ya vitabu na maktaba za Kanisa Katoliki.

  Imekuwa ni juhudi ya Kanisa kutafsiri sheria hizi kwa lugha ya Kiswahili kama ilivyotokea mwaka 1995 kwenye matoleo ya gazeti la Kiongozi.

  Muhtasari wa muundo wa kanisa duniani umeelezwa kuanzia Can. 330 hadi Can. 571. Kuhusu muundo huo, humu yatasimuliwa machache.

  Iwapo tutapiga hatua kuhitaji mengi ya kitaalamu basi Kanisa limesheheni wataalamu waliobobea kwenye sheria za Kanisa.

  Kanisa Katoliki linaongozwa na Papa, akiwa na makao yake kwenye nchi iitwayo Vatican City.

  Papa ndiye mkuu wa Kanisa Katoliki hapa duniani (Can. 331 na Can. 335). Anaendesha kanisa kwa kupitia chombo kiitwacho Roman Curia kinachoelezwa kwenye Can. 360.

  Kuona zaidi muundo wa uongozi wa Kanisa Katoliki duniani, yapaswa kupitia Can. 330 hadi Can. 563.

  Sheria hizi zina maelezo kuhusu Papa (Can. 330-335), Kadinali (Can. 349-359), Askofu (Can. 375-430), Askofu wa kanda (Can. 435-438), Parokia (Can. 515-552), Baraza la Maaskofu (Can. 447-459), Balozi wa Papa (Can. 362-367), Mikutano ya maaskofu au sinodi (Can. 342-348) na mengineyo.

  Zipo sheria zingine hutolewa na gazeti la Vatican (The official gazette of the Holy See), linalojulikana kama Acta Apostolicae Sedis (AAS). AAS huchapishwa kwa lugha ya Kilatini, ambalo ni jambo la kawaida ndani ya Vatican na hutoka mara 12 kwa mwaka.

  Katika Kanisani Katoliki haujatajwa wadhifa unaotumia neno Mkuu kwamba mamlaka yake yanaathiri Tanzania nzima. Zipo taasisi neno hili liko hivyo. Huko tunakuta nyadhifa kama, Waziri Mkuu, Jaji Mkuu, Mnadhimu MKkuu, Mdhibiti Mkuu.

  Sina ufahamu mzuri atajwapo Askofu Mkuu wa nje ya ukatoliki kwamba Ukuu ule unaenea mpaka wapi.

  Hivyo na kwa ndugu zetu Waislam anapotajwa Sheikh Mkuu au Kadhi Mkuu. Nina ujuzi tu na mazingira ya dhehebu langu. Natumaini uhakika kwingine unapatikana kwa waumini wa madhehebu hayo.

  Hata hivyo, ndani ya Ukatoliki kuna wadhifa wa Askofu Mkuu (Archbishop).

  Ni yule aliyepewa mamlaka au kazi fulani. Kazi hiyo yaweza kuwa kuongoza Jimbo lenye hadhi ya Jimbo Kuu (Archdiocese) au idara (taasisi) mojawapo ya kanisa.

  Hapa nchini wapo sita ambapo watano wanaongoza majimbo yenye hadhi ya Jimbo Kuu ambayo ni Mwanza, Tabora, Songea, Arusha na Dar es Salaam na mmoja ni Balozi wa Vatican hapa nchini.

  Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza ni Mhashamu Anthony Mayala wakati Muadhama Polycarp Kadinali Pengo yeye ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

  Askofu Mkuu Joseph Chenoz ndiye balozi wa Vatican hapa nchini. Nje ya Tanzania twaweza kumtaja Askofu Mkuu Celestino Migliore yeye ni mwakilishi wa Vatican katika Umoja wa Mataifa.

  Masuala yaliyoorodheshwa kwenye Can. 435-438 ni aina ya majukumu mengine ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu.

  Wakati anatimiza hayo hujulikana kama Metropolitan au Askofu wa Kanda (Tafsiri yangu).

  Eneo la mamlaka haya huitwa Ecclesiastical province) au Kanda (Tafsiri yangu). Majimbo yaliyo ndani ya kanda hii huitwa suffragan dioceses.

  Jumla yako 15 na matatu kati ya hayo ni Zanzibar, Musoma na Tunduru-Masasi. Kwa jina jingine huitwa suffragan Bishop.

  Hata hivyo, Can. 435(3) inatueleza kuwa huyu Askofu wa Kanda (Metropolitan) hana mamlaka ya utawala katika majimbo yale (suffragan dioceses).

  Urefu wa maelezo ya Askofu Mkuu ni kuepuka utata unaoweza kujitokeza kwa kujaribu kufananisha kilichomo kwenye dhehebu moja na jingine.

  Tunapojadili jambo hili ni vizuri kuondoa aina zote za utata.

  Ni vizuri kuendelea kujua neno Askofu (Bishop) ndani ya Kanisa Katoliki. Wako wa aina tofauti na majukumu yao hutofautiana wakati mwingine.

  Wanaelezwa kuanzia Can. 375 hadi Can. 430. Wengi nchini ni wale wenye madaraka ya kuongoza majimbo na wanaitwa Askofu wa Jimbo Can. 376.

  Wote wale 15 wa zile suffragan dioceses na wale watano wa Majimbo Makuu wako katika kundi hili. Sheria zinazoeleza usawa wao ni Can. 381-402.

  Mfano wote wana haki ya kuwa na Askofu Msaidizi (Auxilliary Bishop) kama ilivyo sasa kwa Jimbo Kuu la Dae es Salaam Can. 403(1).

  Ilitokea hivyo kwa Jimbo la Rulenge kwa Askofu Msaidizi Hayati Askofu Christopher Mwoleka (1969) na kwa Jimbo la Bukoba kwa Askofu Msaidizi Placidus Gervasius Nkalanga (1961-1969).

  Tuone sasa madaraka ya Maaskofu majimboni mwao kwenye maeneo ya utawala (executive), kutunga sheria (legislative) na kutoa hukumu (judicial).

  Ninanukuu Can. 391(1): ..It is for the diocesan Bishop to govern the particular Church entrusted to him with legislative, executive and judicial power according to the norm of the law.

  Pia ninanukuu Can. 391(2): .. The Bishop exercises legislative power himself. He exercises executive power either personally or through Vicars general or episcopal Vicars, in accordance with the law.

  He exercises judicial power either personally or through a judicial Vicar and judges according to the norm of the law.

  Ifuatayo ni tafsiri yangu kwa hizi mbili. Ya kwanza inaeleza madaraka yake Askofu ndani ya jimbo lake.

  Madaraka hayo ni kutunga sheria, kutawala na kuhukumu kwa kufuata taratibu za sheria.

  Inayofuata ni jinsi anavyotimiza madaraka hayo ama yeye mwenyewe au kutumia wasaidizi wake na kama ni hukumu basi yeye mwenyewe au kutumia majaji wanaotambuliwa na sheria za kanisa.

  Sheria inaeleza jinsi Askofu wa jimbo huyu kuwa ni jaji wa kwanza wa mahakama ya kanisa kama inavyoeleza Can.

  1419 (1). Ukisoma Can. 1421(1). Waweza kuridhika kuwa Askofu wa jimbo anatakiwa aweke majaji ambao wamepitia madaraja kama upadre.

  Pia Baraza la Maaskofu linaweza kuruhusu mkatoliki wa kawaida (laity) kuwa mmoja wa majaji - Can. 1421(2).

  Hata hivyo, majaji wanatakiwa wathibitike kuwa na elimu nzuri ya sheria za kanisa Can. 1421(3).

  Hadi hapa tumeona ngazi ya awali ya Mahakama ya kanisa ambayo ni kwa jimboni kwa Askofu (suffragan Bishop). Ni muhimu kujua kuwa kwa ruhusa toka Vatican maaskofu kadhaa wanaweza kukubaliana kuwa ngazi hii ifanyike sehemu moja kama inavyoelezwa kwenye Can. 1423 (1).

  Zaidi kuhusu ngazi hiyo ni vyema kupitia Can. 1419-1437.

  Baada ya hapo Can. 1628 inaruhusu rufani kwenda ngazi ya juu ambayo hapa ni The tribunal of second instance au ngazi ya pili (Tafsiri yangu). Ngazi hii inaelezwa kwenye Can. 1438-1441.

  Baada ya ngazi ya pil bado rufani yawezekana (Can. 1628). Rufani baada ya hapa inabidi ipelekwe Vatican Can. 1442-1445.

  Ni muhimu kusisitiza kuwa Papa ndiye Jaji Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani kama inavyoelezwa kwenye Can. 1442.

  Zaidi ya hapo, hakuna rufani kama inavyosisitizwa kwenye Can. 333(3).

  Hata hivyo, adhabu na mwenendo wa mahakama za kanisa ni somo refu.

  Hapa inatosha kueleza adhabu nyingi zinapatikana Can. 1311-1399.

  Wakati mwenendo wa Mahakama ya Kanisa unapatikana kwenye Can. 1400-1752.

  Sikueleza mtiririko unaoanzia Parokiani ambako ni kanisa lenye linaloongozwa na Padri mwenye wadhifa wa Paroko.

  Mashauri ya huko yanalenga kusuluhisha zaidi na hivyo ni jambo la kawaida kusikia Baraza la Usuluhishi kwa ngazi hii.

  Iwapo usuluhishi haukuwa wa mafanikio basi shauri ndipo linapata nguvu ya kuwasilishwa kwenye ile ngazi ya kwanza ya mahakama.

  Hayo ndiyo maelezo kidogo kuhusu Muundo wa Mahakama ndani ya kanisa Katoliki. Maoni yangu ni kwamba mjadala uliopo uende sambamba na kuanza kuelimishana undani wa Mahakama hizi za dini.

  Tukifanya hivyo tumepiga hatua kwenye safari ya kujiridhisha kwamba tunajua tunalolijadili.

  Mimi ni mmoja wa waumini wa kawaida na si mtaalamu wa sheria za Kanisa. Itakapobidi wataalamu wajitokeze ili kujibu zaidi maswali yanayojitokeza.

  Kwa mfano; Je, ni nani tumpe wajibu wa kuhudumia maaskofu wote nchini kama majaji wa mwanzo wa Mahakama za Kanisa letu? Je, uwezo ni upi? Je walipwe mishahara kwa kiwango gani? Na ni nani mwenye wajibu wa makazi yao? Tuzidi kujiuliza.

  Tumeona mahitaji ya utaalamu wa sheria za Kanisa.

  Je, ni nani tumkabidhi jukumu la kusomesha wataalamu wa kanisa katika vyuo na viwango vinavyokubalika na Kanisa Katoliki?

  Tumeona kuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Kanisa Katoliki ni Papa (Can. 1442). Tunapofikiria kukidhi mahitaji ya wakuu wa mahakama hizo basi ndani ya ukatoliki tumfikirie huyo.

  Hivyo tujipange kukidhi mahitaji yake na wenzake mahakama za madhehebu mengine popote walipo duniani.

  Ni dhahiri kwamba kuwauliza mahitaji yao ni sehemu ya mchakato wa kuunda mahakama hizo.

  Vatican City ni nchi inayojitegemea (Sovereign State), ikiongozwa na ni Papa huyo huyo.

  Mahakama za dini zikiingizwa ndani ya katiba basi majaji wake pia wanaingia kwenye katiba hiyo.

  Papa kama jaji mkuu wa wakatoliki anakuwa ameingia ndani ya katiba. Kiongozi wa Jamhuri ya Vatican City anakuwa ameingia ndani ya katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

  Maoni yangu, kujiandaa kukubali mahakama hizo ni kujiandaa kukubali matokeo yake kama haya.

  Kwamba ndani ya katiba yetu tunajikuta tunataja marais zaidi ya wale wanaoongoza nchi yetu.

  Je, nani awajibike kwa suala la ulinzi wa majaji na hadi Jaji Mkuu wa mahakama za dini?

  Tumeandaa ulinzi gani kwa majaji wakuu ambao baadhi ni wakuu wa nchi duniani kama alivyo Papa?

  Je, ni nani achukue jukumu la usafiri wa majaji wakuu, achilia mbali majaji wengine? Je, tuna uwezo wa kukidhi mahitaji ya usafiri kwa Jaji Mkuu wa Kanisa Katoliki na wengine wa aina hiyo?

  Je, tunafikiri vipi haja ya kuwa na warsha, semina kwa majaji kubadilishana mawazo. Kwamba vikiitishwa basi dunia ishuhudie Papa akiongeza safari za kuja Tanzania kukutana na majaji wenzake wa mahakama za dini. Hatuwezi kutegemea kwamba atatuma mwakilishi siku zote.

  Source (Tanzania Daima):
  Makala -Mahakama za dini zijadiliwe kwa kina
   
Loading...