singidadodoma
JF-Expert Member
- Nov 11, 2013
- 4,394
- 1,536
- Waziri wake aomba ulinzi, IGP afunguka
RAIS Dk. John Magufuli anapambana kufumua mfumo wa wauzaji wa dawa za kulevya nchini, maarufu kwa jina la wazungu wa unga, na kwa kuwa kazi hiyo ni ngumu na yenye hatari, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, amelazimika kuomba ulinzi maalumu.
Kwa mujibu wa waziri huyo, hali kwa sasa ni tofauti na ilivyokuwa awali. Anasema kinachoendelea sasa si kupokea orodha ya wauzaji wa dawa hizo haramu, bali kufumua mfumo wao na wakati waziri huyo akiweka hayo bayana, Raia Mwema, limeelezwa kuwapo kwa malalamiko dhidi ya baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi, wanaodaiwa kushirikiana na sehemu ya genge la wauza dawa za kulevya kudhoofisha kasi ya kikosi maalumu cha kupambana na dawa hizo.
Mara kwa mara, katika Serikali ya Awamu ya Nne, Rais Jakaya Kikwete amekaririwa akisema anayo orodha ya wauza dawa za kulevya na kuwaonya kusitisha shughuli zao hizo. Mbali na orodha ya wauza dawa za kulevya, Kikwete pia aliwahi kukaririwa akisema kuwa anayo orodha ya wala rushwa na wauzaji wa pembe za ndovu, lakini kwa sasa, Waziri Kitwanga anasema ‘wanatwanga’ kufumua mfumo wa wazungu wa unga, na si kuendelea kupokea orodha tu ya wauzaji hao.
Akizungumza na Raia Mwema jijini Dar es Salaam hivi karibuni kuhusu vita dhidi ya dawa za kulevya na hatma ya orodha ya majina ya wauzaji wa dawa hizo ambayo imekuwa ikatajwa kuwa mikononi mwa serikali tangu serikali ya awamu iliyopita, waziri huyo; “Nimeagiza wakuu wa upelelezi kote nchini waunde timu za kupambana na dawa za kulevya maana tumekamata nyingi sana na hiyo si nguvu ya soda, labda mimi nifukuzwe hapa (uwaziri). Nimeagiza watendaji wa polisi na uhamiaji pamoja na idara nyingine wanipatie taarifa Ijumaa ya kila wiki. Ninafahamu mtandao wote, ndio maana nilisema sihitaji orodha bali nahitaji kufanya kazi ili watu wanaofanya hizi biashara wafikishwe mahakamani.”
Katika kusisitiza kile anachokusudia kukieleza, Waziri Kitwanga alitoa mfano kwa gazeti hili akisema; “…mfano ni namna kikosi changu (dhidi ya dawa za kulevya) kilivyomtia nguvuni Daud Kanyau, anayedaiwa kujihusisha na biashara hizo.”
“Wewe mtu kama Kanyau alikuwa anakamatika? Ninachohitaji ni ulinzi. Kuwa ‘protected’. Mungu akikuhitaji kufa leo, utakufa saa hiyo hiyo lakini Mungu akihitaji kukutumia kwa ajili ya watu wake atakutumia hata kwenye vitabu vitakatifu imeandikwa,” alisema Kitwanga.
Alipoulizwa ikiwa mabadiliko ya ndani ya jeshi hilo yanahusiana na tuhuma zilizoorodheshwa kwa baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi, Kitwanga alisema kwa kifupi: “Ndiyo. Na tutaendelea si kusambaratisha mtandao tu wa dawa za kulevya, bali tutafanya mabadiliko kwa kila mmoja anayeonekana anashirikiana na wahalifu.”
“Tunapohamisha , watu wengine ni wazuri. Naomba isionekane wanaohamishwa ni kwa nia mbaya ni kwa nia njema ya kuleta ufanisi kwenye jeshi letu,” aliongeza kusema.
Wakati Waziri Kitwanga akijinasibu namna hiyo, baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi wamekuwa wakituhumiwa kushirikiana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Taarifa zilizolifikia Raia Mwema zinadai kwamba, baadhi ya maofisa hao wanadaiwa kushiriki kwa kulinda baadhi ya wahalifu.
Chanzo cha taarifa ndani ya kikosi cha kuzuia dawa za kulevya ambacho kwa sababu za wazi hatutakitaja gazetini, kimebainisha maeneo ambayo kumekuwa na udhaifu katika kukabili biashara hiyo haramu.
Chanzo hicho kinaeleza kuwa Wilaya ya Kinondoni, iliyoko Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo inayoongoza kwa dawa nyingi za kulevya kukamatwa, ambapo mwaka 2011/12 kilo 200 za heroin zilikamatwa. Februari 2011 zilikamatwa kilo 180 aina ya heroin eneo la Mbezi Jogoo jijini Dar es Salaam, Machi 11, 2011 kilo 81 za Cocaine, Septemba 2011, zilikamata kilo 97 za cocaine eneo la Kunduchi.
Aidha taarifa zaidi zinaeleza kuwa Oktoba 2014 zilikamatwa kilo 41 za heroin zikiwa kwenye majahazi katika Bahari ya Hindi na Oktoba 2014, kilo 35 zilikamatwa katika eneo la Ununio, Boko.
Chanzo hicho kiliongeza kusema kwamba miongoni mwa mitaa inayoongoza kwa biashara ya dawa za kulevya na kuwa na watumiaji wengi ni Ufipa na Wibu iliyoko Kinondoni, lakini hakuna jitihada zozote zilizofanywa na Jeshi la Polisi Kinondoni kuhakikisha vitendo hivyo vinakoma.
“Inakuwaje? Tuseme kwenye mitaa hiyo kama wanafanya tu biashara, uwezo polisi kukabiliana nao uko wapi? Lakini si Kinondoni tu uko pia Mkoa wa Tanga ambao Machi 2010 zilikamatwa kilo 95 za heroin na Desemba zilikamatwa kilo 62, Mkoa wa Lindi zikakamatwa kilo 2012 za heroin, hizi zinakamatwa na Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya,” kilisema chanzo hicho.
Raia Mwema lina taarifa kuwa baadhi ya wahusika wa biashara hiyo wameanza kutikisa kiberiti kupima uwezo wa wa Mkuu mpya wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Robert Boaz, ili kumuweka ‘sawa’. Aidha taarifa zaidi zinasema kuwa mkuu huyo ameanza kulalamikwa na wasaidizi wake kutokana na utendaji wake.
Akizungumza na Raia Mwema kuhusu shaka dhidi ya uongozi wake katika kitengo hicho, Boaz alisema: “Huwezi kujua majani yako strong (yana nguvu) kiasi gani kabla hujapika chai. Wajaribu waone kama niko mwepesi kama wanavyodhani.”
Akizungumzia baadhi ya maofisa wanaotuhumiwa kushiriki vitendo hivyo, Boaz alisema kwamba hawezi kukubali au kukataa kwa kuwa hao wanaotuhumiwa nao ni binadamu.
“Kimsingi siwezi kusema ndio au hapana, hao ni wanadamu wanaweza kutenda jambo kama hilo na sisi wajibu wetu ni kuchunguza lakini kama wana ushahidi wa aina fulani watuambie. Mimi napenda mtu mwenye akili timamu atambue kwamba jambo hili si jema halipaswi kutendwa,” alisema Boaz.
Akizungumzia tuhuma hizo kwa Askari wa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, ameliambia Raia Mwema kuwa tatizo la wasafirishaji na wauza dawa za kulevya ni kubwa linahitaji nguvu ya pamoja na rasilimali za kutosha.
“Ni tatizo kubwa linalohitaji resources (rasilimali) za kutosha pamoja na ushirikiano kutoka kwa vyanzo mbalimbali,” alisema IGP Mangu na kuongeza kuwa, kama kuna askari yeyote anayetuhumiwa kushiriki vitendo hivyo apatiwe taarifa na hatua zitachukuliwa dhidi yake bila kuangalia nyadhifa zao.
“Hili tatizo kubwa si kwa nchi yetu pekee bali ni dunia nzima. Lakini tunaendelea na operesheni mbalimbali,” alisema Mangu.
Akizungumzia changamoto zinazokabili baadhi ya wilaya zake za kipolisi kuhusu kukamata watumiaji na waingizaji wa dawa hizo, Mangu alisema: “Unajua sheria ya dawa za kulevya haizungumzi kama kulewa dawa hizo ni kosa. Kosa ni pale unapopatikana na dawa au kusafirisha. Kwa hiyo ndiyo changamoto tunayoendelea nayo.”
Raia Mwema