Mafisadi wanatumia fedha za wizi kujisafisha- Mengi

mmaroroi

JF-Expert Member
May 8, 2008
2,960
544
Mafisadi wanatumia fedha za wizi kujisafisha- Mengi

2009-01-07 12:51:00
Na John Ngunge


Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, ameonya kuhusu tabia ya baadhi ya mafisadi kutumia fedha za umma walizoiba ya kuanzisha vyombo vya habari kwa nia ya kuwachafua watu wengine ili kuvuruga juhudi za kupambana na ufisadi nchini.

Alisema tabia hiyo inaweza kuvuruga jamii ishindwe kuunga mkono juhudi za kupambana na mafisadi kwa sababu ya kulishwa habari potofu zenye nia ya kusafisha waovu na kuchafua watu wengine.

Mengi alisema hayo katika mazungumzo na Balozi wa Ujerumani nchini, Guido Herz, Kamishna wa Sera ya Haki za Binadamu na Misaada ya Kibinadamu wa Ujerumani, Gunter Nooke na Ofisa wa Ubalozi huo anayeshughulikia masuala ya Kenya, Tanzania na Uganda, Raff Heinkele, walipotembelea vyombo vya habari vya IPP jana.

Mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa kampuni ya The Guardian Ltd jijini Dar es Salaam jana, na kuwashirikisha Mkurugenzi Mtendaji wa The Guadian Ltd, Kiondo Mshana; Mkurugenzi Mtendaji wa Radio One/ITV, Joyce Mhavile na Mkurugenzi wa Uhariri, Sakina Datoo.

Viongozi wengine waandamizi wa vyombo vya habari vya IPP waliohudhuria ni Naibu Mhariri Mtendaji wa The Guardian Ltd, Bernard Mapalala; Mhariri Mtendaji wa The Guardian on Sunday, Richard Mgamba; Mhariri Mtendaji wa Nipashe, Jesse Kwayu;, Mhariri Mtendaji wa Nipashe Jumapili, Flora Wingia na Mhariri Mtendaji wa Lete Raha, Edmund Msangi.

Mengi alisema vyombo vya habari nchini tofauti na vile vilivyopo nchi za magharibi, havina ajenda ya pamoja ya kitaifa.

``Vyombo vya habari ni lazima viwe na ajenda ya pamoja ya kitaifa katika kupiga vita ufisadi...nina hofu kuhusu suala hilo baada ya kuona baadhi ya magazeti yakirudisha nyuma juhudi zilizopo za kupiga vita ufisadi,`` alisema.

Aliongeza wakati vita dhidi ya ufisadi ikiendelea, baadhi ya magazeti yameanza kurudisha nyuma juhudi hizo, na kwamba hali hiyo ikiendelea inaweza kuleta vurugu kubwa katika jamii.

Alisema kwa mfano, hivi karibuni baadhi ya magazeti yamekuwa yakitaka Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, avuliwe kinga ili afikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili, lakini baadhi ya watu na magazeti wamekuwa wakipinga hatua hiyo.

Alisema baadhi ya vyombo hivyo, vimekwishaanza kuandika kwamba hakuna sababu za kumchunguza Rais Mstaafu Mkapa na hata kumuondolea kinga ili afikishwe mahakamani, kwa madai kwamba hatua hiyo inatakiwa ifanywe kwa marais wote waliotangulia.

Maelezo ya Mengi yalikuja baada ya Kamishna Nooke kutaka kusikia maoni mbalimbali ya wahariri kuhusu masuala kadhaa yanayohusu haki za binadamu nchini.

Aidha alisema, kumekuwa na vitendo vya rushwa katika baadhi ya vyombo vya habari, ambapo baadhi hupewa fedha ili kusafisa watuhumiwa kwa kuwatetea dhidi ya tuhuma zinazowakabili.

Hata hivyo, alisema baadhi ya magazeti bado yanajitoa kimasomaso kuandika habari za ufisadi.

Akitoa maoni yake, Mgamba alisema utendaji wa vyombo vya habari kwa sasa umekuwa madhubutu katika kuibua vitendo vingi vya kifisadi tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

``Sasa unaweza kuona nguvu ya vyombo vya habari katika kupiga vita rushwa tofauti na miaka 10 iliyopita...na hatua ambayo serikali inachukua dhidi ya watuhumiwa,``alisema.

Sakina alisema pamoja na kuwapo kwa uhuru wa habari nchini bado kuna baadhi ya viongozi wa serikali wanatishia uhuru wa habari na kutoa mfano wa kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi kama kielelezo cha kufinywa kwa uhuru huo.

Pia alisema gazeti la Tanzania Daima nalo limeandikiwa barua ya kutishwa kama ilivyokuwa MwanaHalisi.

Kwa upande wake, Balozi Herz, alitaka kujua masuala ya ukabila na udini yanavyoripotiwa katika vyombo vya habari nchini kwa kuwa hajasoma popote kama mambo hayo yapo.

Akizungumzia suala hilo, Kwayu alisema wahariri na Watanzania kwa ujumla wanaheshimu kabila la kila mtu na dini yake.

Alisema hali hiyo inatokana na misingi mizuri iliyowekwa na Rais wa kwanza, Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere ya kupiga vita ukabila na udini.

``Hatuchukulii suala la ukabila na udini kuwa ni mambo makini sana...na hivyo, hatutoi kipaumbele katika kuendekeza mambo hayo,`` alisema.

Hata hivyo, Kamishna Nooke alisema kujua iwapo mauaji ya albino yanawiana na suala la ukabila.

Kwa upande wake, Mapalala, alisema mauaji hayo hayana uhusiano wo wote na ukabila au udini, badala yake yanahusiana na vitendo vya kishirikina.

Lakini Mengi alisema mauaji ya albino hufanywa na watu matajiri ambao wanawatumia watu fukara kuendesha mauaji hayo.

``Suala la mauaji ya albino, hususan katika sekta ya madini, kuna imani kwamba mmoja akipata kiungo cha albino atapata madini kwa wingi zaidi,`` alisema.

Alisema imani kama hiyo ni ya zamani kwani hapo awali baadhi walikuwa wakiwaua watoto na kuwatolea kafara kwa lengo la kupata madini mengi, na kwa sasa wanawatumia albino kama njia ya kupata utajiri.

Alisema watu wanaotafuta utajiri kwa kushirikiana na watu wenye imani za kishirikiana ndio wanafanya vita dhidi yao kuwa ngumu.

Hata hivyo, alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kazi nzuri aliyoianza ya kupambana na watu wanaojihusisha na mauaji ya albino na akataka hatua kali zichukuliwe dhidi yao.

Akizungumzia uhuru wa habari, Mengi alisema juhudi za kupigania uhuru wa habari bado zinaendelea.

Mapema, Balozi Herz na ujumbe wake walitembelea kituo cha Radio One na ITV na kampuni ya uchapishaji magazeti ya The Guardian Ltd.

SOURCE: Nipashe
 
Back
Top Bottom