Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,073
- 15,350
Mwenendo wa Uhuru wa Vyombo vya Habari Tanzania unatisha
Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) unalaani mwenendo unaoendelea wa baadhi ya viongozi wa serikali, taasisi za umma na vyombo vya usalama kudhoofisha uhuru wa wanahabari na vyombo vya habari nchini.
Katika kipindi cha miezi minne iliyopita, jumla ya matukio manane (8) ya madhila dhidi ya waandishi wa habari na vyombo vya habari yamejitokeza katika mikoa ya Dar es Salaam, Manyara, Mbeya na Mwanza.
Katika matukio haya waandishi wa habari wanane (8) walikamatwa na jeshi la polisi, kuwekwa ndani na baadhi kunyang'anywa vifaa vyao vya kazi na mmoja kupewa saa 24 kujieleza kuhusu matamshi yake aliyoyatoa katika mahojiano na chombo kimoja cha habari. Pia katika matukio haya chombo kimoja cha habari kimefungiwa kwa siku 90. Waandishi hawa waliachiwa kwa dhamana baada ya msaada wa kisheria uliotolewa na washirika wa CoRI.
Mpaka sasa jumla ya matukio 55 ya madhila yamerekodiwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Madhila hayo ni dhidi ya waandishi wa habari, vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa na yaliripotiwa mwishoni mwa mwaka 2025. Wakati kipindi hiki cha kati ya Januari hadi Aprili kuna rekodi ya madhila manane, kipindi kama hiki mwaka jana kuriripotiwa madhila tisa (9).
Mwenendo wa Hali ya Uhuru wa Vyombo vya Habari 2026
Wakati Tasnia ya Habari ikiwa katika maandalizi ya kusherehekea Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari hapo Mei 3, 2026 mwenendo huu usiotofautiana sana na mwaka jana unaashiria kuendelea kwa mazingira magumu kwa wanahabari nchini.
Katika vyumba vya habari, wanahabari na vyombo vya habari bado wanakumbana na shinikizo la kisheria na kiutendaji, hali inayochochea kujidhibiti (self-censorship) na kudhoofisha uhuru wa kuripoti masuala ya msingi ya kitaifa.
Madhara kwa Ujenzi wa Demokrasia
CoRI inasisitiza kuwa mwenendo huu una madhara makubwa kwa maendeleo ya demokrasia nchini, ikiwa ni pamoja na kudhoofisha uwajibikaji, kupunguza upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati, kukuza hofu na kujidhibiti kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari, kudhoofisha michakato huru ya kisiasa na utawala bora.
Itakumbukwa kwamba kwa mujibu wa ripoti ya Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF) Tanzania iliendelea kupanda katika viwango va Kimataifa vya Uhuru wa Habari, ambapo ilikuwa nchi ya 95 kati ya nchi 180 kwa mwaka 2025 na ya 97 kwa mwaka 2024. Kwa kuendelea kutokea matukio haya kunaleta taswira hasi kwa taifa na kudhoofisha jitihada zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali katika kuhamasisha uhuru wa habari na wa kujieleza.
CoRI inaamini kuwa uhuru wa vyombo vya habari ni nguzo muhimu ya uwazi, ushiriki wa wananchi, na utawala wa sheria katika jamii yoyote ya kidemokrasia.
CoRI inatoa wito kwa:
1. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha ulinzi wa wanahabari na kuheshimu kikamilifu uhuru wa vyombo vya habari.
2. Vyombo vya dola kuacha vitendo vya vitisho, unyanyasaji na kuingilia kazi za wanahabari.
3. Mamlaka za udhibiti kuhakikisha sheria na kanuni zinatumika kwa haki bila kuathiri uhuru wa kujieleza.
4. Wadau wa habari na umma kuendelea kutetea haki ya kupata taarifa kama msingi wa demokrasia.
Mwisho, CoRI inaamini kuwa bila uhuru wa vyombo vya habari, hakuna demokrasia imara. Hivyo, ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha kuwa mazingira salama na huru kwa vyombo vya habari yanakuwepo ili kulinda haki za wananchi na mustakabali wa taifa.
April 28, 2026
Kwa Umoja Wetu, CoRI,