MADIWANI na viongozi wa mitaa wanaotokana na Chama cha Mapinduzi (CCM), katika manispaa ya Iringa katika tukio la kushangaza, wamemkimbia Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, wakati wa operesheni usafi iliyoanza jana ndani ya manispaa hiyo.
Wakati watu mbalimbali wakijitokeza kushirikiana na mbunge huyo kufanya usafi katika kata ya Kitanzini, hakuna diwani wala kiongozi wa chama hicho aliyejitokeza kushiriki zoezi hilo, licha ya kuagizwa na kupewa taarifa kimaandishi.
Mbali na kumgomea, madiwani na viongozi hao, wanatuhumiwa kuwakataza baadhi ya wakazi wa mitaa hiyo kushiriki katika kampeni hiyo, kwa madai kwamba ingempatia sifa kubwa mbunge huyo anayetoka chama cha upinzani cha CHADEMA.
Viongozi wetu wa mitaa walipita na kutuonya tusiende kwa sababu kampeni hiyo imeitishwa na mbunge wa upinzani, badala yake tusubiri ile itakayotangazwa na CCM, alisema mkazi mmoja wa kata ya Kitanzini aliyeomba jina lake lisitajwe gazetini.
Madiwani hao hususan wa kata za Kitanzini na Mshindo, pamoja na kuendesha kampeni dhidi ya mbunge, kata zao ndizo zinazoongoza kwa kusheheni uchafu unaofikia takriban tani 100 katika mitaa ya Ubena, Madrasat na Mtunduruni.
Katika kampeni hiyo, ni madiwani wawili tu wa kata ya Mivinjeni, Frank Nyalusi na wa Viti Maalumu Suzan Mgonukulima, wote wa CHADEMA, walioshiriki kikamilifu katika tukio hilo.
Akizungumzia hali hiyo, Diwani wa Kata ya Mivinjeni Frank Nyalusi (CHADEMA) alionyesha masikitiko yake juu ya madiwani wenzake kutoshiriki zoezi la kuiweka manispaa katika hali ya usafi.
Baada ya kufika hapa nimesikitishwa sana kwa kuwa diwani wa kata hii tunayofanya usafi haonekani, wakati kata yake ndiyo yenye mlundikano mkubwa wa uchafu.
Kama yeye ni kiongozi wa eneo husika ameshindwa kuudhiti uchafu huu hadi mbunge kuingilia kati, hii ni aibu kwa Taifa.
Hii inaonyesha wazi kuwa viongozi wa CCM uwezo wao ni mdogo. Mahindi sasa hivi gunia moja ni sh 105,000, wanafunzi wa darasa la kwanza wanatakiwa kuchanga sh 75,000, badala ya wao kujadili mambo haya, wanaangalia mambo ya chama chao tu, alisema Nyalusi.
Diwani wa viti maalumu Suzan Mgonukulima ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Manispaa alisema, kama nchi itakuwa na viongozi kama wale waliosusia kampeni hiyo na kujenga moyo wa ushirikiano, hali ya nchi itafikia pabaya.
Akizungumza katika kampeni hiyo, Mchungaji Msigwa alisema siasa sio uadui na watu wanatakiwa kuwa marafiki katika suala zima la maendeleo ya nchi.
Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Kitanzini ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Jescar Msambatavanu, alisema asingeweza kushiriki kwa sababu alikuwa katika msiba huko Njombe.
Niko Njombe msibani tangu jana nimefiwa na bibi yangu, na sasa tunajiandaa kwenda kuzika, alisema Msambatavanu.
Naye Diwani wa Kata ya Mshindo Daudi Albert alipopigiwa simu mara tatu, ili aseme kilichomfanya ashindwe kushiriki, simu yake ilipokelewa na mwanamke aliyedai yupo Makambako.
source; Madiwani CCM wamkimbia mbunge wa CHADEMA
|
|