Herbalist Dr MziziMkavu
Platinum Member
- Feb 3, 2009
- 43,114
- 34,955
Moja ya madaraja yaliyogeuzwa dampo jijini Dar es Salaam.
UNAWEZA usiamini lakini huu ndiyo ukweli wenyewe kwamba madaraja mengi ambayo yapo jijini Dar es Salaam yaliyojengwa kwa gharama kubwa hivi sasa yamegeuzwa madampo ya takataka na yamo hatarini.
Uchunguzi wa Fumuafumua wiki hii umegundua kuwa madaraja hayo yanatumika kama sehemu za kutupia takataka na wananchi wanafanya vitendo hivyo mchana kweupe.
Madaraja kama la Jangwani, Riverside, Malindi, Mtoni Relini, Tandale, kwa kuyataja machache, yameathirika na uharibifu huo wa mazingira na kuna hatari ya kubomolewa na maji pindi mvua zikianza kunyesha.
Uchunguzi umebaini kwamba kutupwa kwa takataka katika madaraja hayo ndiyo chanzo cha mafuriko kwani wakati wa mvua maji hushindwa kutiririka na matokeo yake kujaa darajani na kusambaa sehemu za makazi ya watu.
Hapa Tandale hilo ni tatizo kubwa sana, licha ya Mto Ngombe kufukuliwa, baadhi ya wananchi wanatupa taka na baada ya kipindi kifupi takataka zitajaa na mvua zikija, tutegemee mafuriko, alisema mwananchi mmoja aliyejitambulisha kuwa anaitwa Said Idd, mkazi wa eneo hilo.
Hata hivyo, uchunguzi umeonesha kuwa wengi wa wanaotupa takataka ni vijana waliojiajiri kuzoa takataka mitaani kwa ujira wa shilingi 2,000 hadi shilingi 3,000 kwa kiroba na wanapozichukua majumbani, humwaga kwenye madaraja.
Tatizo ni manispaa zimeshindwa kuhakikisha usafiri wa magari ya takatakata unakuwepo mitaani ndiyo maana uchafu huzolewa na vijana nao kuchafua mazingira kando ya madaraja, alisema mkazi mwingine wa Mwenge kijijini.
Hivi karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Teresia Huviza, aliwashukia viongozi wa Jiji la Dar es Salaam kuwa ndiyo chanzo cha kukithiri uchafu jijini kwa kuwa hawazoi takataka inavyopasa.
Hata hivyo, Meya wa jiji hilo, Dk. Didas Masaburi ameibuka na kusema tuhuma hizo haziwahusu.
Dk. Masaburi alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, alipozungumza na waandishi wa habari katika kikao cha kufunga mwaka 2012.
Alisema kauli ya waziri huyo inaonekana kujichanganya, kwani kazi ya kuliweka jiji hilo katika hali ya usafi si ya jiji bali wahusika wakuu ni halmashauri na kazi kubwa ya mamlaka ya jiji ni kusimamia hali ya usafi wa dampo lililoko Pugu Kinyamwezi.
Hizo lawama wanapaswa wazielekeze kwenye halmashauri kutokana na wenyewe kushindwa kupeleka taka na sio sisi jiji, kama wenyewe hawatuletei taka dampo nani alaumiwe? alisema.
Dk. Masaburi alieleza kustaajabishwa na utaratibu unaotumiwa na baadhi ya mawaziri kwa kuzishambulia halmashauri kuwa zinafuga uozo wa uchafuzi wa mazingira, ambapo hata huko kwenye ofisi za wizara zao upo uchafu.
Natoa wito kwa Serikali Kuu kubadili utaratibu wake kwa kuzitengea fedha za kutosha halmashauri hizo na kuzifikisha kwa wakati, lengo likiwa ni kwenda sambamba na sheria ya mazingira ya mwaka 2004. Vyanzo ya mapato wakati mwingine vinaweza kuwa chanzo cha halmashuri hizo kushindwa kusimamia sheria hiyo ya utunzaji wa mazingira, alisema.