MADA: Tatizo la Watoto kuchelewa kuongea. Ni kipi chanzo chake? Je, nawezaje kutatua tatizo hili?o hili

Justine Kakoko

Verified Member
Oct 5, 2018
32
125
Tatizo la watoto kuchelewa kuongea ni la miaka mingi sana lakini miaka ya hivi karibuni limeonekana kuongezeka kwa kasi sana siku hadi siku.

Kuchelewa kuongea ni moja kati ya matatizo ya mawasiliano ambayo huwakuta watoto: tatizo hili hujitokeza pale ambapo watoto hushindwa kuongea kuendana na hatua ya ukuaji walioifikia. Mtoto hushindwa kuongea au kuwaelewa watu wengine wakiongea. Aidha maendeleo ya lugha kwa mtoto husimama au huenda taratibu sana.

AINA ZA TATIZO LA KUCHELEWA KUONGEA KWA WATOTO

Zipo aina tatu za tatizo la kuchelewa kuongea kwa watoto. Aina ya kwanza ni ile ambayo mtoto hushindwa kusikiliza nini anaambiwa. Aina ya pili ni ile ambayo mtoto hushindwa kujieleza juu ya ni nini anataka. Aina ya tatu ni ile ambayo mtoto hushindwa kufanya vyote: yaani hushindwa kujielezea na kusikiliza wengine.

Kutokana na uzoefu wangu, aina ya tatu hujitokeza kwa watoto wengi zaidi, watoto wanaoshindwa kujieleza kwa kuongea pia hushindwa kujua nini wanaambiwa na watu wengine.

DALILI ZA TATIZO LA KUCHELEWA KUONGEA KWA WATOTO

Mtoto ambaye ana tatizo hili la kuchelewa kuongea mara zote huwa nyuma ya hatua zake za maendeleo na ukuaji. Ili mzazi/mlezi aweze kujua kama mtoto wake ana tatizo hili anaweza kuangalia kama mtoto wake ana dalili zifuatazo:-

Moja, Mtoto kushindwa kupiga kelele zisizo na mpangilio mpaka kufikia miezi 15. Kelele kama “Yaaa Yaaa”, “Daaa Daaa” au “Bluuuuu Bluuuu”

Mbili, Mtoto kushindwa kuongea mpaka kufikia miaka miwili. Kuongea neno moja moja au mawili ambayo yanaweza kumpa mzazi muelekeo juu ya nini mtoto anataka kusema. Kama vile “Mama tamu” “Mama acha” au “Baba Pira”

Tatu, Mtoto kutoweza kuzungumza sentensi fupi mpaka kufikia miaka mitatu. Sentensi kama vile “Naomba maji”, “Nataka kojoa”, “Naomba maziwa”, “Nataka mpira” au “Shikamoo Baba!”

Nne, Mtoto kuwa mzito kufuata maelekezo mpaka kufikia miaka mitatu. Mtoto kutoelewa nini anaambiwa na wenginine. Kwa mfano anaambiwa: “kaa chini” na anashindwa kujua nini anatakiwa kufanya na hata akifanya mara nyingi hufanya kinyume.

Tano, Matamshi ya maneno kuwa mabaya mpaka kufikia miaka mitatu. Kwa mfano, mpaka kufikia miaka mitatu mtoto anatamka neno, Shika-chika, Sasa – chacha au Mkate – Nkate.

Sita, mtoto kushindwa kuweka maneno katika sentensi mpaka kufikia miaka mitatu. Mtoto anaweza akawa anayajua maneno mengi lakini akawa anashindwa kuyaweka maneno katika sentensi moja akielezea kile anachokitaka hivyo huishia kulisema neno moja moja tu. Kwa mfano mtoto huishia kusema: “kula” akimaanisha anataka chakula, au “piga yule” akitaka kusema yule kampiga.


SABABU ZA TATIZO LA KUCHELEWA KUONGEA KWA WATOTO

Kutokana na uzoefu na tafiti zangu binafsi nimebaina ya kuwa zipo sababu nyingi za watoto kuwa na tatizo la kushindwa kuongea kwa wakati, kuendana na hatua na maendeleo ya ukuaji wao. Zifuatazo ni baadhi ya sababu:-

Moja, matatizo ya kusikia kwa watoto. Mtoto mwenye matatizo ya kusikia vizuri ni ngumu sana kuweza kuzungumza kwa wakati kama watoto wengine. Ni muhimu mzazi akiona mtoto wake anashindwa kufuata maelekezo na kuitumia lugha vizuri kuendana na umri wake afuatilie kama anaweza kuwa na tatizo lolote la kusikia ili aweze kupata msaada unaotakiwa mapema.

Mbili, Usonjii (Autism). Japo kuwa kuna baadhi ya watoto hawaathiriwi na autism katika maendeleo yao ya lugha lakini, kwa watoto wengi hupelekea kuchelewa kuongea. Angalau 70% ya watoto wenye Usonji huchelewa sana kuongea. Watoto wenye usonji huongea baada ya wataalamu kuwasaidia kujifunza na kutumia lugha kuendana na mahitaji yao. Ni ngumu kwa wao kuweza kujifunza kutumia lugha bila jitihada za wataalamu.

Tatu, mtoto kukosa watu wanaozungumza mara kwa mara karibu yake. Watoto huchukua lugha moja kwa moja kutoka kwa wazungumzaji wengine na ndiyo maana mtoto akiwekwa kwa watu wanaotumia lugha ya kiingereza atazungumza kiingereza, akiwekwa na wazungumzaji wa kiswahili atazungumza kiswahili n.k hivyo kwa mtoto kukosa watu karibu yake ambao huzungumza mara kwa mara humfanya ashindwe kuchukua lugha hali inayoweza kupelekea mtoto kuchelewa kuzungumza.

Nne, Wazazi kutokuwa na maarifa na hatua na maendeleo ya ukuaji wa mtoto. Sababu hii imekuwa ikipuuzwa sana na wataalamu kila wanapoelezea tatizo hili lakini binafsi nafikiri ni moja kati ya sababu kubwa kabisa. Wazazi wengi hawajui nini wafanye ili kuwapitisha watoto wao katika hatua mbalimbali za ukuaji pindi waoneshapo changamoto hali inayoweza kupelekea watoto kukwama katika matatizo bila usaidizi. Watoto wengi hushindwa kuongea mapema kwasababu wazazi wao hawana ufahamu na jinsi lugha kwa mtoto inavyojengeka na nini wafanye endapo kukitokea changamoto.

Tano, Mtoto kuzaliwa kabla ya muda wake (Njiti). Mtoto kuzaliwa kabla ya muda wake huweza kuleta matatizo mbalimbali likiwemo na hili la kushindwa kuongea mapema kwa mtoto. Kwani kuna baadhi ya viungo muhimu vya mwili wake vinakuwa havikumalizika kujiunda hivyo huendelea kujiunda taratibu mara baada ya kuzaliwa kwake.

Sita, Kumwacha mtoto atumie vifaa vya kielekroniki kama vile TV na simu kwa muda mrefu. Sababu hii pia haisemwi na wataalamu wengi, lakini nimeona ni moja kati ya sababu kubwa. Mtoto wa kuanzia miezi mpaka miaka mnne endapo ataachwa kwenye TV kwa muda mrefu yaana kwa zaidi ya saa moja kwa siku ni lazima itaingilia maendeleo ya ubongo. Ubongo ndiyo unafanya na kuratibu kila kitu kinachohusiana na maendeleo ya lugha kwa mtoto hivyo kwa maendeleo ya ubongo kuvamiwa na vifaa hivi vya kieletroniki vitu vingi vinavyotegemea maendeleo ya ubongo kuendelea pia husimama. Tutaliongelea hili kwa kina wakati mwingine kwani ni pana sana.

Saba, Mahusiano mabaya kati ya mtoto na mzazi/mlezi. Mtoto kuwa na mahusiano mabaya na mzazi/mlezi wake ni sababu nyingine ya mtoto kuchelewa kuongea. Mzazi/mlezi ambaye haoneshe mapenzi na ukaribu na mtoto wake au ambaye ni mkali kupitiliza kwa mtoto akiwa bado mdogo kabisa anaweza kupelekea mtoto kutotaka kuelezea hisia au mahitaji yake mapema hali inayoweza kupelekea mtoto akachelewa kuongea.

Nane, Familia kutumia lugha zaidi ya moja. Watoto wengi wanaokuwa katika familia inayotumia lugha zaidi ya moja huwa na tatizo la kuchelewa kuongea kwani watoto hulazimika kutumia nguvu ya ziada kutoa tafsiri ya baadhi ya maneno na kufananisha katika lugha zote mbili jambo ambalo huweza kuwachukua muda ukilinganisha na yule anayekua kwenye familia inayotumia lugha moja.

Tisa, Matatizo ya mdomo kama vile uzito wa ulimi. Mtoto mwenye ulimi mzito asipopewa tiba mapema tatizo hili ni lazima litamkuta kwani ulimi ni moja kati ya viungo muhimu sana kwenye uzungumzaji wa mtoto. Yapo mazoezi na jinsi ya kufanya ili mzazi aweze kulimaliza tatizo hili. Nitaligusia siku nyingine nikiwa naelezea juu ya jinsi ya kufanya ili kumaliza tatizo hili kwa watoto.

Kumi, Matatizo ya ubongo. Baadhi ya matatizo ya ubongo kama vile Majeraha kwenye ubongo yanaweza kuathiri misuli ambayo ni muhimu katika maendeleo ya lugha kwa watoto.

Hitimisho, Matatizo mengi ya maendeleo ya lugha na kuzungumza kwa watoto yanatibika kirahisi sana kama mzazi/mlezi atatafuta tiba mapema kabla ya mtoto kufikisha miaka mitano hivyo ni muhimu wazazi/walezi wakatambua mapema kuwa watoto wao wana tatizo hili na kutafuta tiba kutoka kwa wataalamu mapema.

Tuendelee kuwa pamoja nitaandika juu ya jinsi ya kupambana na tatizo hili wakati ujao. Ni rahisi tu, endapo mzazi/mlezi ukijitoa kwa moyo na kushirikiana na wataalamu.
 

Justine Kakoko

Verified Member
Oct 5, 2018
32
125
Kama anachelewa ila mwisho wa siku anaongea, sioni tatizo kivile.
Umeisoma makala yote? Mtoto anayechelewa kuongea huwa katika hatari ya kuwa nyuma katika kila kitu. Nimesaidia watoto wa namna hiyo, kama haujawahi kusaidia wala kuwa na mtoto wa namna hiyo unaweza usione uzito wa tatizo. Usipende kurukia hitimisho rahisi kwenye matatizo sensitive kama haya kwani kuna wazazi hawalali kisa matatizo kama haya.
 

Trubarg

JF-Expert Member
Jan 8, 2020
1,635
2,000
Hapo kwenye tv Ni vp mmana mtoto nahc watoto wengi hasa wa mjini huwa wanashinda kwenye tv
 

barafuyamoto

JF-Expert Member
Jul 26, 2014
29,770
2,000
Umeisoma makala yote? Mtoto anayechelewa kuongea huwa katika hatari ya kuwa nyuma katika kila kitu. Nimesaidia watoto wa namna hiyo, kama haujawahi kusaidia wala kuwa na mtoto wa namna hiyo unaweza usione uzito wa tatizo. Usipende kurukia hitimisho rahisi kwenye matatizo sensitive kama haya kwani kuna wazazi hawalali kisa matatizo kama haya.
Mbona umepaniki kiasi hiki? Hujiamini? Sijatukana, sijatumia maneno makali. Tatizo nini mkuu? Naona dalili za ulichelewa kuongea wewe mpaka unafika ukubwani. Sasa uzi wako una maana.
 

Justine Kakoko

Verified Member
Oct 5, 2018
32
125
Hapo kwenye tv Ni vp mmana mtoto nahc watoto wengi hasa wa mjini huwa wanashinda kwenye tv
TV inarudisha sana maendeleo ya ukuaji wa ubongo wa watoto. Nimefanya diagnosis kwa watoto wengi wenye tatizo hili, chanzo kwa wengi nimebaini ni TV. Nitaandika makala juu ya hili nikipata wasaa.
 

Justine Kakoko

Verified Member
Oct 5, 2018
32
125
Mbona umepaniki kiasi hiki? Hujiamini? Sijatukana, sijatumia maneno makali. Tatizo nini mkuu? Naona dalili za ulichelewa kuongea wewe mpaka unafika ukubwani. Sasa uzi wako una maana.
Sijapaniki, ni ngumu kupaniki kwa jambo dogo kiasi hicho. Nimeonesha msisitizo tu. Umeonesha mzaa kwenye jambo ambalo hauna uelewa nalo. Kuna wengine huwa hadi mabubu kwa kuchelewa kuongea tu, bila ya kutafutiwa tiba mapema.
 

Muuza simu used

JF-Expert Member
Aug 23, 2017
3,196
2,000
Nilitegemea mtoa mada utaweka na solution ya tatizo hili matokeo yake umekuwa sawa na wale wapiga ramli


Sent using IPhone X
 

Justine Kakoko

Verified Member
Oct 5, 2018
32
125
Nilitegemea mtoa mada utaweka na solution ya tatizo hili matokeo yake umekuwa sawa na wale wapiga ramli


Sent using IPhone X
Naandika mara kwa mara hapa. Nitaandika juu ya suluhisho muda ujao. Ninaenda kuedit hitimisho ili watu wajue kuwa nitaandika wakati ujao. Japo napendekeza utumie lugha nzuri, hakukuwa na haja ya kejeri. Tumia lugha nzuri muda ujao kama ipo kwenye sehemu ya maadili yako.
 

mtzedi

JF-Expert Member
Dec 13, 2011
3,668
2,000
Cha muhimu ni kucheza,kuimba na kuongea na mtoto. Pia ita watoto wengine wacheze nae chini ya uangalizi.
Nishaona mtoto wa miezi 10 anasema neno "baba", "mama" pia anaelewa ukimwambia lala,kula, piga makofi n.k.
Mtoto akiwa na utimamu wa afya ya mwili na akili akifika kuanzia miezi 7 cheza,imba naye.
 

petro matei

JF-Expert Member
May 11, 2014
623
1,000
Mtoto wangu wa miaka 4 na miezi 6 bado hajaongea mpaka leo ila kila kitu ukimtuma analeta na anakijua na pia hawezi kutulia kwa sehemu moja kwa mda. Je kwa mtoto kama huyu anahitaji msaada gani?

Kwa muda wote amekuwa akiudhuria mazoezi kwenye hospital Kadhaa na pia kuonana na doctor bingwa wengi.

Je, unaweza nisaidia au kunishauri hapo ?

Sent using Jamii Forums mobile app
 

Frank King

JF-Expert Member
Oct 7, 2012
1,311
2,000
petro matei,
Na mimi wakwangu Anamiaka hivyo hivyo,na tabia kama hizo hizo ulizozisema,,,kwakweli sijui tunafanyeje hapa.

Mtaalam ebu tupe namna tufanyeje wenda tukapata njia.
 

Ibofwee

JF-Expert Member
Apr 1, 2017
1,307
2,000
Mtoto wangu ana miaka mitatu na nusu lakin kupangilia sentens hayuko vizuri,ndio hao wanaosema nkate badala ya mkate, had vitoto vya miaka miwili vimemzidi

Ila kwny kuandika na kuhesabu anavikalisha vitoto vyote vya mtaani, yan anacatch haraka sana vitu akifundishwa

Kuna mwalimu huwa anajitolea kufundisha watoto hapa mtaan na amesema mtoto wangu ndo anaecatch vitu haraka sio wale wengine waliomzid kuongeaSent using Jamii Forums mobile app
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

Top Bottom