Ndege ya michezo ya angani aina ya Yakovlev Yak-55M yenye nambari ya usajili N55YA ilipata ajali mbaya na kupinduka juu chini katika Uwanja wa Ndege wa Quonset State Airport uliopo North Kingstown tarehe 10 Agosti 2024.
Ajali hiyo ilitokea baada ya ndege hiyo kupata hitilafu za kimitambo kwenye injini wakati ikipaa, jambo lililomlazimu rubani kurejea uwanjani hapo kwa dharura.
Wakati wa kutua rubani alipoteza udhibiti wa uelekeo na ndege ikatoka nje ya njia ya kuruka kabla ya kugeuka na kupinduka barabarani. Kwa bahati nzuri rubani alinusurika na majeraha madogo tu.
Ripoti ya mwisho ya uchunguzi kutoka Bodi ya Usalama wa Usafiri wa Anga ya Marekani (NTSB) imebainisha kuwa sababu kuu ya ajali hiyo ni ukosefu kamili wa uzoefu wa rubani katika urushaji wa ndege hiyo pamoja na uamuzi wake wa kutua kuelekea upande uliokuwa na upepo wa nyuma "tailwind" uliovuruga udhibiti.
Kwa mujibu wa NTSB siku ya ajali ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kabisa kwa rubani huyo kupaa na kurusha ndege hiyo ya Yak-55M baada ya kuinunua karibuni, na hakuwa amewahi kufanya mazoezi yoyote ya kupaa au kutua na chombo hicho.
Kumbukumbu za safari zake zilionyesha kuwa alikuwa na masaa 49.4 tu ya urubani katika maisha yake yote.
Pia hakuwa na uzoefu wowote uliorekodiwa wa kuendesha ndege zenye mfumo wa gurudumu la nyuma "Tailwheel" au maarufu kama "Aviator" ambazo zinajulikana kuwa na changamoto kubwa na zinahitaji mbinu maalum wakati wa kutua.
Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa rubani huyo alikuwa akifanya safari hiyo bila kuwa na leseni rasmi wala vyeti halali vya urubani vinavyomruhusu kisheria kurusha ndege hiyo.