Mgogoro wa vita mashariki ya kati umeleta fursa na changamoto kwa mashirika ya ndege ya Kenya Airways (KQ) na Ethiopian Airlines (ET), kwani abiria na mizigo wanatafuta njia mbadala kutokana na kufungwa kwa viwanja vya ndege vya Ghuba.
Mashirika haya ya ndege ya Afrika, yanakutana na athari ya "Chungu-Tamu" kutokana na mgongano huo wa mataifa ya Ghuba.
Gharama za mafuta zimeanza kujitokeza kutokana na kuyumba kwa bei ya mafuta duniani, na kuathiri faida za mashirika ya ndege.
Ethiopian Airlines inatajwa kupoteza takriban dola milioni 137 kwa wiki moja kutokana na kusimamishwa kwa safari za ndege kuelekea vituo 10 vya Mashariki ya Kati, huku Kenya Airways ikifanya safari za kurejesha watu nyumbani kutoka Dubai.
Kwa upande mwingine Nairobi na Addis Ababa zimeweza kuwa vituo mbadala (Alternative Hubs) kwa abiria wanaosafiri kati ya Ulaya, Asia na Marekani kwa wakati huu wa kufungwa kwa anga mashariki ya kati.
Hii imeongeza mahitaji ya usafiri wa abiria na mizigo kwa mashirika haya mawili, na kuwafanya kuwa na nafasi nzuri ya kupata sehemu ya soko, na kukata makali ya hasara ya kusitisha safari kwenye vituo vyao vya mashariki ya kati.
Mfano, Kenya Airways imeongeza safari za ndege kwenda Paris, London, na Amsterdam kutokana na mahitaji makubwa ya wasafiri na mizigo lakini pia alikadhalika kwa shirika la ndege la Ethiopia.
Kwa mashirika mengine ya ndege kama RwandAir, Uganda Airlines, na Air Tanzania yana hatari ya kupoteza mapato kutokana na kusimamishwa mazima kwa safari za ndege kwenda Mashariki ya Kati.