Machozi ya Single Mama

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,885
MACHOZI YA SINGLE MOTHER.

Na. Robert Heriel.


Mlio wa kengele ya shule unasikika. Wanafunzi wanatoka madarasani mkuku mkuku kuwahi mstarini. Olaa! Wanafunzi wawili wanaanguka baada ya kupigana vikumbo wakiwa wanakimbia.

Waliokuwa nyuma yao wanawakanyaga lakini sio kwa makusudi bali ni kutokana na kushindwa kufunga breki za miguu yao.

Hatimaye Wanafunzi wanakaa mstari lakini wanafunzi wawili waliokanyagwa wanajikokota huku wakiwa nyang'anyang'a kwa kukanyagwa.

"Naona bado watu wanautani na Fuko Matata. Wananichokoa chokoa. Watanipata. Wewe kama hujalipa Ada ya shule, hujalipa pesa ya mlinzi, pita hapa mbele"
Anaweka Koti lake vizuri kisha anaendelea.

"Leo nitawachapa bakora. Ili mkiambiwa msije shule bila ada muelewe. Haya wote wasiolipa ada pita mbele"

Mwalimu Fuko Matata aliongea kwa vitisho sauti yake ikitoka kwa hasira. Mkono wake wa kulia alikuwa ameshika fimbo mbili alizozishikanisha pamoja.

Wanafunzi ambao hawajalipa ada walianza kutoka mbele.

"Wewe Starehe Hasara unafanya nini huko. Pita mbele. Wewe hata Ada ya mwaka jana hujamaliza. Nilikuambia usije shule kama huwezi lipa Ada. Haya pita mbele haraka"

Mwalimu Fuko Matata alibwatuka akimfuata Mwanafunzi aitwaye Starehe Hasara.
Alimlabua viboko vinne vya mgongo akimsindikiza alale chini. Kisha akamchapa bakora za moto sita za matako.

"Haya! Futika nisikuone hapa. Mwangalie na nguo zake chafu kama kichaa"

Mwalimu Fuko Matata aliongea akimpiga teke la kiuno Starehe Hasara.

Masikini Starehe Hasara aliondoka akichechemea kwa maumivu makali ya viboko. Mbali na maumivu ya viboko, pia maumivu ya kukanyagwa pale chini muwa wakiwa wanakimbia kuwahi mstarini.

Starehe Hasara alifika Nyumbani yapata majira ya saa tatu Asubuhi. Aliona jilo linafuka moshi akajua Mama yake atakuwa yupo jikoni.

Moja kwa moja akaingia jikoni. Hapo akamkuta Mama yake akiwa kainama akiwa anapuliza jiko la kuni la Mafiga matatu huku Moshi ukiwa umetanda jiko lote. Puuuu! Puuuu! Mama yake aliendelea kupuliza jiko ambalo halikutaka kuwaka. Kuni zilikuwa ni magunzi ya muhindi.

"Mama! Nimefukuzwa Ada shuleni"
Starehe Hasara aliongea na kumshtua Mama yake aliyekuwa hajamuona. Mama yake aliacha kupuliza kisha akamgeukia, akamtazama kwa huruma huku machozi ya moshi yakiwa yametotesha uso wake.

Uso wa mama yake Starehe Hasara ulitia simanzi. Ulikuwa na kila dalili ya shida na masumbuko ya dunia hii.

Alimkumbatia Mwanaye. Kisha akalia kwa nguvu zote.

"Twende shuleni nikaongee na Mwalimu wako"

Mama yake akaongea wakiachiana kukumbatiana.

"Mama! Mwalimu Fuko Matata hataki hata kukuona. Mimi sitaki kurudi shule. Acha tuu nisisome"

"Hapa mwanangu. Elimu ni ufunguo wa maisha. Bila ya kubembeleza ili upate ufunguo huo. Hutaweza kufungua mlango wa maisha yako"

"Nitauvunja mlango wa maisha yangu. Sio lazima ufunguo huo wa elimu"

Starehe Hasara aliongea bila kufikiri. Ni kama alikata tamaa. Mama yake akamsogelea usoni kisha akasema;

" Mlango wa maisha ukiuvunja utakudondokea utaanguka mwanangu. Mtaka cha Uvunguni Sharti Ainame"

Hapo wakatazamana. Starehe Hasara akaelewa Mama yake.

"Wewe kibwengo. Nilikuambiaje?"
Mwalimu Fuko Matata alifoka alipomuona Starehe Hasara karudi shuleni.

"Samahani Mwalimu. Nimekuja na Mama, yupo Ofisini kwa Mwalimu Mkuu"

"Sisi tumechoka na maneno yake ya ahadi hewa. Tunataka pesa"

Mwalimu Fuko Matata aliongea kisha akamuacha Starehe Hasara akiwa ametizama chini.

Kwa Upande wa ndani Ofisini.
"Nipo chini ya Miguu yako Mkuu. Tafadhali naomba umsaidie Mwanangu. Hilo ndilo tegemeo langu. Sina pesa ya kulipa Ada.

Naomba hata niwe mfanya usafi wa shule au mpishi ili niweze kumsomesha mwanangu. Mwalimu mkuu naomba usikie kilio changu"

Mama yake Starehe Hasara alilia akimuomba Mwalimu Mkuu akiwa kapiga magoti. Starehe Hasara alikuwa kwa nje akichungulia dirishani.

Hapo alimuona Mama yake akilia kwa uchungu mkali akiwa kapiga magoti. Starehe naye alijikuta machozi yakimtoka. Nini ameikosea dunia. Ni nini familia yake imefanya mpaka waishi kama wadudu. Loooh!

"Wewe Mama Starehe. Hukosi hadithi. Leo hivi kesho vile. Kwani Starehe hana Baba? eehe! Baba yake yupo wapi?"

Mwalimu mkuu aliongea kwa ukali. Akimtazama Mama Starehe.

"Wewe toka hapo dirishani"
Mwalimu mkuu alimfukuza Starehe pale dirishani. Kisha akamtazama Mama Starehe aliyekuwa pale chini amepiga magoti akilia.

"Alikuwa ni Mtu mwerevu sana. Alitambulika kwa unadhifu na utanashati wake. Lakini kilichonivuta kwake zaidi ni pesa zake. Alikuwa ni moja ya matajiri wakubwa katika ule mji. Kila mwanamke alitamani aolewe na yeye. Wapo walioenda kwa waganga kwa ajili yake. Wapo waliofunga na kuomba kanisani ili wampate. Pia wapo waliokuwa wakivaa kila aina ya urembo na kujichubua kisha hujipitisha katika ofisi yake ili awaone awaoe"

Hapo Mama Starehe Alimeza fumba la mate kisha akapangusa makamasi yaliyokuwa yanatoka puani. Akaendelea;

"Mimi nilikuwa kundi la tatu. Nilijipodoa nikapodoka. Nikajiremba nikarembeka. Nikajipaka nikapakika. Nikalivaa wigi likavalika. Mtoto huyo nikajipitisha kujaribu bahati yangu. Looh! Laiti ningejua kuwa haikuwa bahati bali nimkosi basi nisingesogeza hata kivuli changu. Lakini wanasema tamaa mbele mauti nyuma. Ndivyo ilivyokuwa. Nilijiingiza katika shimo la mauti bila mwenyewe kujua kwa tamaa ya pesa na maisha mazuri"

Hapo alitulia kwa kitambo kidogo kisha akamtazama Mwalimu mkuu. Naye alikuwa akimtazama. Kisha akaanza kulia. Mwalimu mkuu alibaki ameduwa. Hakutegemea kumuona mtu mzima kama Mama Starehe akilia kwa sauti kubwa kiasi kile.

"Nyamaza! Nyamaza basi"
"Mwalimu mkuu niache nilie tuu! Nimezoea kulia. Kulia ndio chaguo nililobakiwa nalo. Hivi Kama mwanangu amefukuzwa shule bado nisilie. Woyiii! woyi... woyiii!"

Hapo alizidisha kelele. Kisha akanyakaza kwa ghafla. Ofisi ikawa kimya ungedhani hapakuwa na mtu aliyekuwa analia.

Mwalimu mkuu akisaidiwa na picha ya Rais wa kwanza wa taifa na aliye madarakani wote walikuwa wamemtumbulia macho Mama Starehe.

"Nikafanya ujanja kujishikiza Mimba. Nilijua fika kuwa kwa kufanya vile ningekuwa nimeyapatia maisha. Nilijua hapo nitakuwa nimejihakikishia kuolewa naye. Pili, uhakika wa mtoto wangu. Looh! Kumbe nilikosea.
Kumbe hesabu ile ilikuwa ni kugawanya, mimi nikajumlisha"

Hapo akakohoa kisha akaendelea..

"Yule tajiri aliikataa mimba yangu. Akanitishia kuniua. Ati akanambia kuwa mimi ni Malaya tuu kamwe siwezi kumzalia mtoto. Kumbe nilichoweza ni kumstarehesha lakini sio kumpa mtoto. Nikajitutumua lakini niliishia kushindwa"
Kimya kwa kitambo kikatokea.

Kisha akaendelea.

" Tamaa mbele ndio iliniponza. Nilimuacha mwanaume wa kweli aliyenipenda. Lakini kwa umasikini wake sikumuona kitu. Yule anifaa kwa dhiki japo alinipa kidogo. Nikajihadaa na Mr. Hasara kwa sababu ya pesa zake. Leo haya ndio matokeo"
Anafuta machozi kisha anaendelea.

"Nadharaulika kwenye jamii. Mtaani watu wananisema. Kanisani nako usiseme. Kila kona nadharaulika. Ninafananishwa na kiwanja chenye mgogoro. Mimi sasa ni kiwanja jamani. Oneni hii ndio migogoro yenyewe. Sasa mimi ni kiwanja alafu mwanangu ndiye mgogoro. Mwanangu shuleni kageuka mgogoro. Mtaani mgogoro. Naumia mimi jamani. Natamani mimi ndio nikutwe na madhila haya na mtoto wangu abaki salama. Lakini Mpaka mwanangu anaumia"

Sasa alianza kuongea kwa polepole neno moja moja akisema;

"Nilikuwa na nyodo mimi. Nilikuwa mzuri mimi. Nilitaka wenye mipesa. Nao wenye mafedha walinitumia mimi. Wakaniachia mimba wakatoweka kama moshi wa Sigara. Nimebaki nalia. Soko langu limeshuka. Mtoto wangu anadhalilika. Loooh!"

Mama Starehe aliongea maneno yaliyougusa moyo wa Mwalimu mkuu kiasi cha kumtoa machozi. Mwalimu mkuu akajitolea kumsomesha Starehe Hasara.

Miaka kumi baadaye, Starehe Hasara alikuwa ni Mkurugenzi mkubwa katika kampuni la Mawasiliano.

Bila kutarajia, Baba yake Starehe aitwaye Hasara aliibuka kama Uyoga. Unajua kwa nini kama Uyoga. Ni kwa sababu Uyoga huibuka mara baada ya mvua. Uyoga hauibuki kwenye Ukame.

"Habari kijana, Naitwa Hasara. Mimi ni Baba yako"

Baba yake Starehe aliongea. Starehe alibaki mdomo wazi. Tokea azaliwe hakuwahi kumuona Baba yake isipokuwa kwenye picha. Leo live anakutana na Baba yake.

Jioni Starehe alimhadithia Mama yake kila kitu kuhusu ujuo wa Mr. Hasara. Mama alikasirika sana. Hakutaka kumsikia huyo mtu. Huenda alimchukia sana Mr. Hasara.

Aliamini kuwa Mt. Hasara ndiye shetani anayezungumziwa kwenye vitabu vya dini.

Siku zilipita pakawa hakuna maelewano baina ya Starehe na Mama yake. Starehe alitaka Mama yake amsamehe Baba yake, Mr. Hasara.

Jambo ambalo Mama hakuwa tayari nalo. Nikusema amesahau taabu aliyoipata kumlea Starehe, Angesahau jinsi alivyoimbwa mtandaoni, mitaani na kanisani kuwa single mother ni kiwanja chenye mgogoro.

Angesahau maneno ya Mr. Hasara kuwa yeye ni malaya kamwe hawezi kumzalia mtoto. Thubutu! Mambo hayo aliyakumbuka.

Starehe anakutea amekufa. Mama anadhulumiwa mali mahakamani na upande wa kiumeni.

Mwisho anazimia kisha kunakuwa na giza. Niite Taikon wa Fasihi.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
 
Back
Top Bottom