Asema atachanja mbunga kumnadi Slaa
Na Muhibu Said
Muasisi wa vyama vingi nchini na Mwenyekiti wa kwanza wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Mabere Marando, amejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku akisema amefikia uamuzi huo ili kuendeleza mageuzi na kuongeza nguvu za kukingoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.
Sababu nyingine ya uamuzi wake huo, amesema inatokana na kuhamasishwa na uamuzi wa Mbunge wa Karatu anayemaliza muda wake, Dk. Wilibrod Slaa, wa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia chama hicho mwaka huu.
Marando ambaye kitaaluma ni mwanasheria na Wakili wa Mahakama Kuu, alitangaza uamuzi wake huo katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam jana.
Hata hivyo, alisema uamuzi wake huo usichukuliwe kuwa una nia ya kutaka uongozi, kwani hana mpango wa kugombea nafasi yoyote ndani au nje ya chama hicho.
Maswali mengi yameulizwa. Nimeulizwa mimi kama nagombea nafasi yoyote au sigombei. Napenda kuwaarifu Watanzania kupitia kwenu kwamba, sigombei cheo chochote. Sigombei urais, sigombei ubunge wala sigombei uongozi katika chama, alisema.
Kwa msingi huo ndugu zangu, nimewaita hapa kuwaeleza kwamba, leo nimeamua kwamba nahama chama cha NCCR-Mageuzi na nitajiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema, alisema Marando.
Aliongeza: Sijapotea njia, kwa sababu Chadema ni wapiganaji, ni wapambanaji na upambanaji ndiko nyumbani kwangu.
Alisema amekuwa na msimamo wa dhati wa kutobadili mwelekeo wa kimageuzi katika nafsi yake, pia amekuwa na uvumilivu wa miaka 10 akitegemea kwamba, viongozi wake katika NCCR-Mageuzi, wangeweza kuinuka na kufanya kazi waliyodhamiria tangu awali ya kuongoza mageuzi nchini, bila mafanikio.
Nimeamua kubadili chama. Nimehamasishwa zaidi na uamuzi wa Dk. Wilibrod Slaa kugombea kiti cha urais kupitia chama cha Chadema, alisema Marando.
Aliongeza: Niliwahi kumuambia Dk. Slaa kwamba yeye binafsi kama akiamua kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa umakini wake ninaoufahamu, uwezo wake wa kujenga hoja bungeni na uongozi wake ambao umekifanya chama chake katika miaka yote hii kisiharibike kama chama chetu kilivyowahi kuharibika, nimeamini kwamba anaweza kuongoza na nimemuahidi kwamba akiniingiza katika timu yake ya kampeni kutafuta urais wa nchi hii, nitakata mbuga nchi nzima kumsaidia.
Alisema anaamini Dk. Slaa ataibuka mshindi na kwamba, asipofaulu, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ana uhakika atakuwa Rais nchini.
Marando alisema ana imani kwamba, wenzake waliopo na waliokuwa NCCR-Mageuzi, kuna wengi, ambao wanaheshimiana nao, hivyo akiwaomba wampe kura kwa niaba ya Chadema, ana uhakika watafanya hivyo.
Alisema pia anaamini akiwaomba wakipigie kura chama hicho nchi nzima, kwa heshima wanayopeana toka walivyoanzisha mageuzi mwaka 1990, watamuunga mkono.
Ni hawa watu ambao sasa nawanyooshea mkono nikiomba kwamba tufuatane, tujiunge na chama hiki, ambacho kweli kinaonyesha dhati ya kuendeleza mageuzi katika nchi yetu kwa nia ya kukiondoa Chama Cha Mapinduzi madarakani, alisema Marando na kuongeza:
Najua wengine watauliza hujarudisha kadi yangu ya NCCR-Mageuzi. Mimi nina kadi namba moja katika Chama cha NCCR-Mageuzi. Mimi ni mwanasheria. Jambo moja ambalo najua, ni kwamba ukiwa ni mwanachama wa CCM na uhame uende chama kingine, automatically (moja kwa moja) wewe ni mwanachama wa chama hicho kipya kisheria.
Hivyo, ninapohama na kujiunga na Chadema na kuchukua kadi mpya na kuilipia, nirudishe kadi yangu ya zamani au nisirudishe, mimi ni mwanachama wa chama kipya cha Chadema. Kadi moja namba moja ya chama chetu cha mageuzi, ni historia ya Mabere Marando, hatimaye siku moja hata wanangu watatoa kama baba yetu alikuwa ni mshiriki katika kuanzisha chama hiki, hii ndiyo kazi yake.
Marando alisema yeye na watu alioshirikiana nao katika kuanzisha mageuzi nchini, walikuwa na malengo makuu mawili; ikiwamo kuelimisha wananchi umuhimu wa demokrasia pana ya vyama vingi vya siasa na kuwahamasisha Watanzania kuanzisha vyama vingine vya siasa, badala ya CCM ili sera za vyama hivyo zieleweke kwa nia ya kukiondoa chama hicho madarakani.
Nasisitiza kwamba nafasi ya chama cha upinzani siyo kukosoa chama tawala wala kusahihisha chama tawala tu, kazi zao hazistahili kuishia hapo. Kazi za kukosoa na kusahihisha iwe ni kuelimisha umma na umma kutambua chama tawala hakifai na chama tawala kiondoke madarakani, alisema Marando.
Alisema mabadiliko nchini; kiuchumi na kisiasa yanayotamaniwa na Watanzania, hayataweza kupatikana bila kuiondoa CCM madarakani.
Marando alisema ili kuiondoa CCM madarakani, lazima vyama vingine vikue, vipate nguvu na wananchi wavielewe ili wavipigie kura katika Uchaguzi Mkuu.
Alisema binafsi mwaka 2000, baada ya chama chake cha zamani cha NCCR-Mageuzi kumuondoa Augustine Mrema katika uongozi, aliwania uenyekiti wa chama hicho, lakini akashindwa kupitia kura za kidemokrasia na kuamua kunyamaza.
Marando alisema wakati akiwa Mwenyekiti na baadaye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, alifanya kazi ya kutembea nchi nzima kueneza sera na kukisimika chama hicho, ikiwa ni pamoja na kufungua matawi ili kiweze kuenea na kuwa na uwezo wa kushinda uchaguzi na kuiondoa CCM madarakani.
Hata hivyo, alisema tangu alipoondoka kwenye uongozi wa NCCR-Mageuzi, alivumilia karibu miaka 10 akitegemea kwamba, wataweza kuendeleza kazi hizo alizozifanya katika uongozi, lakini hakuona dhamira njema ya kufanikisha mambo hayo.
Kutokana na hali hiyo, alisema akiwa mwanamageuzi asiyeyumba, alivumilia kuondoka NCCR-Mageuzi, lakini ameangalia muda mrefu jinsi ya kuchangia jitihada za kuhamasisha mageuzi nchini na kuwaelewesha Watanzania ili waweze kuungana kiasiasa kuiondoa CCM madarakani.
Alisema kwa miaka zaidi ya sita, Chadema imefanya kazi kubwa ya kutembea nchini, kuhamasisha umma na kuufanya umma uelewe umuhimu wa kuondoa CCM madarakani ili nchi iweze kupata mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Alizitaja kazi zilizofanywa na Chadema katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na Operesheni Sangara, ambayo viongozi wake wakuu walijitahidi na kufanikiwa kuzunguka kila kona ya nchi na kufanya kazi nzuri.
Pia, alisema wabunge wa Chadema walivyokuwa bungeni waliibua hoja nzito na nzuri, ambazo alisema zilidandiwa na baadhi ya wabunge wa CCM wakapata umaarufu.
Alisema hoja za wabunge hao wa Chadema walizozitoa bungeni, zimesaidia kuwaelewesha Watanzania jinsi wanavyoongozwa vibaya, wanavyoibiwa.
Kwa hiyo, kwa maoni yangu wameonyesha jitihada kubwa katika kuelekea azma, ambayo pia mimi ninayo, ambayo ni hatimaye kuondoa Chama Cha Mapinduzi katika madaraka, alisema Marando.
Alisema kutokana na hamasa ya kisiasa waliyokuwa wameiweka katika Jimbo la Rorya, alilowahi kuliwakilisha kupitia NCCR-Mageuzi, muda mrefu chama hicho kilikuwa na viongozi katika ngazi za vijiji, kata hadi matawini jimboni humo.
Hata hivyo, alisema katika miaka michache iliyopita baada ya Chadema kuanza kazi hiyo na kutokana na viongozi wa NCCR-Mageuzi waliokuwa hawafanyi kazi ya kuendeleza jitihada hizo, wanachama wengi wa NCCR-Mageuzi waligeuza matawi yao kuwa ya Chadema.
CHANZO: NIPASHE