Mabadiliko ya Katiba hayaepukiki

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,072
1,250
M. M. Mwanakijiji

Ukiondoa maneno kama “uchakachuaji” na “tume ya uchaguzi” maneno ambayo yatakuwa yanajirudia rudia tena na kuanza kukera watu yatakuwa ni “Katiba Mpya”. Hakuna wakati ambapo hoja ya “Katiba Mpya” inarudi kwa nguvu zaidi kuliko wakati huu unaofuatia uchaguzi kwani kwa upande mmoja haja ya kuwa na Katiba hiyo mpya imemulikwa kama taa kubwa ya usiku na kila mtu anaanza kuona.
Hata hivyo nina uhakika mkubwa kuwa kwa wale wasiojua Katiba au ambao hawajawahi kukaa chini na kuisoma Katiba ya nchi yao wanaweza wasijue mambo fulani fulani ambayo hayaingii akilini na kwa pamoja yake yanapaza sauti kuita “tunahitaji Katiba Mpya”.

Katika ukorofi wangu na uchokozi wa hoja naomba nidokeze kidogo juu ya mambo yafuatayo ili kuonesha kuwa Katiba yetu ilivyo sasa ina vipengele vya ajabu ambavyo haviwezi kuondoka kwa kuombea au kupuuzia bali kwa kukaa chini na kuvifungia kazi kuviondoa aidha kwa mabadiliko makubwa ya katiba au kwa kuamua kuandika upya Katiba yetu. Naomba nitaje mambo machache ambayo mengine nimeyajadili kwa kina kwenye mtandao wa Jamiiforums.com.

1. Rais Kikwete angekuwa mgombea pekee wa Urais bado angepigiwa kura na Watanzania wote?

Sijui kama unajua kwamba kama vyama vingine vyote visingesimamisha wagombea wa Urais kama kina Slaa na Lipumba na kumuacha mgombea wa CCM Dr. Kikwete bado Watanzania wangempigia kura kama tulivyofanya wakati wa chama kimoja?

Kwamba baada ya CCM kupata mgombea wake wa Urais na vyama vingine kwa sababu moja au nyingine kushindwa kusimamisha wagombea Tume ya Uchaguzi isingemtangaza Kikwete kuwa ni “Rais” bali ingeliweka jina lake kwenye karatasi za kura na wapiga kura wangetakiwa kupiga kura ya “Ndiyo” au “Hapana”?

Kama ulikuwa hujui basi habari ndiyo hiyo. Katiba yetu na sheria yetu ya uchaguzi inaweka utaratibu wazi kuwa endapo mgombea wa Urais atakuwa ni mmoja tu bado atapigiwa kura na wapiga kura kwa mtindo wa “ndiyo” au “hapana”. Yaani hawezi kuwa Rais kwa kupitishwa tu na chama chake kuwa mgombea?

Kama tungekuwa na utaratibu wa Rais akikosa wapinzani basi anakuwa ni Rais bila haja ya kupigiwa kura unafikiri ni kiasi gani kingetumika kushawishi wagombea wengine wasijitokeze au kurudisha fomu ili mgombea wa chama kimoja abakie peke yake na kisha atangazwe kuwa ni Rais bila kuwapa wananchi nafasi ya kumkubali au kumkataa?

2. Wagombea wasio na wapinzani wanatangazwa ni wabunge bila kupigiwa kura yoyote?

Katiba hiyo hiyo inayosema kuwa mgombea wa Urais ambaye hana mpinzani bado atapigiwa kura ya “ndiyo” au “hapana” inanyima fursa hiyo kwa majimbo ambayo wagombea wake wamejikuta hawana wapinzani? Katika majimbo hayo sheria hiyo ya ajabu inasema ati kwa vile mtu hana mpinzani hadi siku ya mwisho ya kurudisha fomu basi mgombea huyo pekee “ataonekana kuwa amechaguliwa”.

Yaani, kura za maoni za watu wa chama kimoja zinahesabikuwa kuwa ni kuchaguliwa na watu wote! Wamarekani wanasema “go figure” - nenda ukafikirie! Hii ina maana gani? Mgombea wa Ubunge au chama chake kinaweza kujitahidi kuzuia wagombea wengine wasiingie kwenye kinyang’anyiro kwa sababu wanajua dakika ya mwisho wakikosekana wagombea wengine basi mtu wao atakuwa amepita “bila kupingwa”.

Ukiwauliza amepita vipi bila kupingwa wakati hakuna mwananchi hata mmoja aliyepewa nafasi ya kupinga kwenye sanduku la kura wanasema “ndiyo sheria ilivyo”. Mfano mzuri ni Jimbo la Nyamagana. Mgombea wake baada ya kukosa mpinzani alijua tayari kapita “bila kupingwa” lakini aliporudishwa yule mgombea wa chama kingine mgombea wa chama tawala akaangushwa na wananchi waliopewa nafasi ya kupinga!

Je, majimbo mengine ambayo wananchi wake hawakupewa nafasi ya kumchagua Mbunge wake na badala yake kupewa mbunge kwa mtindo wa “kupita bila kupingwa” haki yao ya kuchagua mbunge wao itatetewa na nani?

3. Je umewahi kujiuliza ni nani anamuapisha Spika na kwanini?

Sote tunajua kuwa Rais huapa mbele ya Jaji Mkuu ndivyo katiba inavyotaka na Jaji Mkuu huapa mbele ya Rais. Lakini Spika wa Jamhuri ya Muungano anaapa mbele ya Katibu wa Bunge. Rais wa Muungano na hata yule wa Zanzibar wote wanaapishwa na Majaji wakuu na Majaji Wakuu nao wanaapishwa na Marais. Lakini linapokuja suala la Spika anaapa mbele ya Katibu wa Bunge kwa nini?

Yumkini ni kweli kuwa Spika wa Bunge si mkuu wa Mhimili kama ilivyo kwa Rais na Jaji Mkuu? Wenye hoja hii wanatudokeza (kama wengi tulivyosikia kufuatia sakata la wabunge wa CHADEMA kutoka Bungeni) kuwa “Rais ni sehemu ya Bunge kwa mujibu wa Katiba”.

Kama hili ni kweli Spika anaweza vipi kuwa mkuu wa Mhimili wa Bunge wakati Mhimili huo unamhusisha Rais ambaye ni Mkuu wa Mhimili mwingine? Kama Rais ni sehemu ya Bunge kama Katiba inavyosema basi Spika hawezi kinadharia kuwa Mkuu wa Bunge kwani atakuwa ni Mkuu wa Rais ambaye ni Mkuu wa Utendaji.

Sasa, kama Spika si Mkuu wa Bunge na ni msimamizi wa mikutano ya Bunge tu na mijadala ya Bunge kama baadhi ya watu wanavyofikiri basi Bunge letu bado halijawa mhimili unaojitegemea nje ya Mhimili wa Urais. Kwa maneno mengine, kwa kadiri ya kwamba Rais ni sehemu ya Bunge basi Bunge SIYO mhimili wa mwingine wa serikali. Labda tuliweke hivi; kama Katiba ingesema Mahakama ina sehemu mbili na sehemu yake mojawapo ni Rais tunaweza kusema kuwa Mahakama hiyo itakuwa ni huru kutoka madaraka ya Rais? Hili linaonekana katika kuapishwa kwa sababu kama Wakuu wa Mihimili ya Mahakama na Utendaji wanaapa kwa nguvu iliyosawa nao (Jaji Mkuu kwa Rais, na Rais kwa Jaji Mkuu) kwanini Spika ambaye kimsingi ukifikiria anawajibu mkubwa tofauti kabisa na wa Rais na Jaji Mkuu aapishwe na Katibu tu wa Bunge ambaye yeye mwenyewe ni mtumishi tu.

Lakini labda cha kutukoroga zaidi ni kuwa Kanuni za Bunge (25:2) zinatuambia kuwa “Mbunge yeyote aliyechaguliwa kuwa Spika kabla ya kushika madaraka yake, ataapa Kiapo cha Spika mbele ya Bunge. Lakini endapo atachaguliwa Spika ambaye siyo Mbunge, basi ataapa Kiapo cha uaminifu kwanza kabla ya kuapa Kiapo cha Spika.”

Kumbe utaratibu wa Bunge wenyewe hausemi kama Katibu ndiyo asimame kushuhudia kuapishwa kwa Spika (labda kama kuna mabadiliko ya kanuni hiyo). Kwa maneno mengine mama Anna Makinda alipochaguliwa kuwa Spika alitakiwa kusimama mbele ya wabunge na kuapa yeye mwenyewe.

Hili nalo lingetuletea matatizo kwanini Rais aapishwwe mbele ya Jaji Mkuu na asingesimama na kuapa tu mbele ya Watanzania? Au kwanini Jaji Mkuu aape mbele ya Rais badala ya kuapa tu mbele ya Watanzania?

4. Je unajua mgombea anayehisi kuonewa kwenye Ubunge au Udiwani anaweza kwenda mahakamani lakini wa urais hawezi?

Nadhani hili hapa sasa hivi kila mtu anajua. Kuwa kama mtu ni mgombea wa udiwani au Ubunge anayehisi kutotendewa haki katika kuhesabu kura au kutangazwa mshindi anaweza kwenda mahakamani na kudai haki yake na ushindi wa aliyeshinda unaweza kutenguliwa?

Hili linajulikana siyo kinadharia bali kihistoria kwani tumeshawahi kuwa na wabunge ambao Ubunge wao ulitenguliwa baada ya ushahidi kuonekana haukuwa wa haki. Kuanzia mwaka 1995 katika mfumo wa vyama vingi tuna wabunge waliopoteza viti vyao baada ya mahakama kuona kuwa hawakuingia madarakani kihalali.

Lakini cha kushangaza ni kuwa Katiba hiyo hiyo inayotambua “haki” za waliodhulumiwa katika Ubunge na Udiwani kudai mahakamani inakataza waliodhulumiwa katika Urais kuhoji mahakamani au kwenye “chombo kingine chochote”. Kwa maneno mengine, hata mgombea wa Urais akiingia kwa mbinde na kwa upinde na akatangazwa kuwa ni Rais huku kuhesabu kura kwake kukiwa na matatizo au kutangaza matokeo kukawa kwa matatizo lakini akishatangazwa hakuna namna yoyote ya kupinga na kuwa utaratibu umeweekwa kuwa akitangazwa tu basi ndani ya siku saba lazima aapishwe na hivyo kuondoa uwezekano wowote wa mtu kuandaa kesi yoyote ya kupinga ushindi huo.

Hapa mtu mwenye uwezo wa kufikiria atajiuliza kama aliyedhulumiwa Ubunge na Udiwani anaweza kupinga na akashinda mahakamani kwanini aliyegombea Urais hawekewi utaratibu wa kulalamika ushindi wa aliyetangazwa na kupewa nafasi ya kuleta ushahidi wake mahakamani?

Kwenye nchi inayodai kuwa inataka kujenga jamii yenye “haki” hivi hawa wanaoonekana kudhulumiwa kwenye kura za Urais walalamike wapi? Ndio maana binafsi nachukulia kitendo cha Wabunge wa CHADEMA kutoka ukumbini kuwa ni kitendo kidogo sana wala hakihitaji watu kuruka roho zao wala kumuudhi rais bali kukubali tu kuwa ndio njia pekee ya wao kuonesha malalamiko yao.

Sielewi kwanini watu wengine wamekwazika kiasi cha wengine kuanza kumfikiria Rais wa Tanzania kama “baba” yao! Jamani hii ni demokrasia na wakati mwingine demokrasia inakera na kuudhi.

Tujifunze kuvumilia demokrasia na gharama yake. CHADEMA wangeweza kumzomea, wangeweza kupiga kelele, wangeweza kujilaza ukumbini pale, au wangeweza kusimama nje na mabango pale Bungeni yenye maneno ya kila namna lakini wakaamua kutoka nje kwa heshima, bila kunyosha vidole, bila kumtukana mtu na kilichonifurahisha ni kuwa wabunge wa CCM wakazomea na kuguna wengine lakini hakuna mtu anayeona kitendo chao ni cha kukosa heshima kwa wabunge wenzao.

Lakini walichofanya ni kuinuka na kutoka ukumbini na kama Waziri Mkuu alivyosema yawezekana wabunge hao walikuwa wanaangalia hotuba ya Rais kwenye runinga. Kama hilo ni kweli, kwa nini watu wengine wamekwazika kiasi cha wengine kukasirika kabisa!

Wabunge hao wamefanya walichofanya kutuma ujumbe wao juu ya ubovu wa tume ya uchaguzi na tatizo la Kikatiba, watu wanazungumzia suala la Katiba na nilitegemea viongozi wa serikali badala ya kuanza kupiga mikwara wangesema tu kuwa wako tayari kusikiliza manung’uniko ya CHADEMA na jambo hilo lingeisha. Kwa sababu hakuna kitendo cha kumkataa kumtambua Rais au kukataa kutambua matokeo ya Urais ambacho kinabadiliki kuwa Kikwete ni Rais.

Hivyo, tuangalie suala hili kuwa ni la kidemokrasia na binafsi sitashtuka huko mbeleni wabunge wengine wakitoka wakiona hawajaridhishwa na jambo fulani.

Tunataka demokrasia, tuwe tayari kuishi nayo! Isiwe ni demokrasia ya kwenda kupiga kura tu lakini bila kujali matokeo yake!

5. Je unajua Waziri Mkuu akijiuzulu au kufa Baraza la Mawaziri nalo linavunjika japo yeye hakuliunda?

Mojawapo ya maajabu ya mfumo wetu ni kuwa Baraza la Mawaziri linaundwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu. Mawaziri hao hata hivyo hawali kiapo chochote mbele ya Waziri Mkuu isipokuwa wanaapa kwa Rais.

Kwa maneno mengine mawaziri wote na manaibu wao kihaki kabisa wako chini ya Rais na si chini ya Waziri Mkuu japo kiutendaji wanaweza kupokea maagizo toka kwa Waziri Mkuu. Lakini Waziri Mkuu hawezi kumfukuza Waziri au Naibu Waziri hata mmoja.

Lakini cha kushangaza ni kuwa Waziri Mkuu akijiuzulu na baraza la mawaziri linavunjika na vile vile Waziri Mkuu akifa baraza la Mawaziri nalo linavunjika.

Lakini kwanini linavunjika wakati yeye hakuliunda. Nchi nyingine baada ya Waziri Mkuu kuteuliwa na Rais na kuapishwa yeye ndiyo aidha anunda baraza la mawaziri au anapendekeza majina ya baraza la mawaziri kwa Rais ambaye anaweza kuyakubali.

Katika mifumo hiyo ni wazi kuwa Waziri Mkuu na baraza lake nalo ni kwishnei.

Lakini katika mfumo wetu Waziri wetu mkuu haundi wala kupendekeza baraza la mawaziri sasa kwanini livunjike kama Waziri Mkuu ndiye mwenye makosa?

Kuwakumbusha vizuri ni kuwa Waziri Mkuu Lowassa alipojiuzulu na kukubaliwa basi baraza la Mawaziri lisingeweza kuendelea kuwepo.

Ndio maana tuliwasahihisha wale waliotangaza kuwa “Rais kavunja baraza la Mawaziri kufuatia kujiuzulu kwa Lowassa”. Ukweli ni kuwa Rais hakuvunja baraza lile bali lilivunjika automatically baada ya kukubaliwa kujiuzulu kwa Lowassa.

Je ulijua na hilo?

Kwa ufupi ni maswali hayo machache naomba tuyafikirie na tujiulize kama kweli tunahitaji Katiba mpya au la. Yapo na maswali mwengine vile vile ambayo tunaweza kujiuliza. Yapo maswali yanayohusu Zanzibar na viongozi wake na yapo maswali yanayohusu masuala ya dini na imani na Katiba yetu.

Yapo maswali yanayohusu mamlaka mbalimbali ya Rais na viongozi wengine na yapo maswali yanayohusu Bunge na wabunge. Tukianza kuyauliza yote hapa wengine tunaweza kuitwa “wachochezi, wasaliti na wanaotaka kuligawa taifa letu”. Lakini, ni mwanadamu ambaye hataki kutumia ubongo wake kufikiri?

Kama hatia basi itakuwa ni hii ya kuwafanya watu wafikiri hatia ambayo tunasema tunaikubali. Tutaendelea kuwafanya watu wetu wafikiri nje ya kawaida. Kwani tayari mapambano ya kifikra tuliyoyaasisi miaka mitano iliyopita yanasimama kama ushahidi wa mwamko mpya wa taifa.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom