SoC03 Mabadiliko na Uwekezaji sekta ya Kilimo vizingatie mustakabali wa mwanamke katika kilimo

Stories of Change - 2023 Competition

Tonytz

Senior Member
Jul 18, 2022
159
1,142
UTANGULIZI.
kilimo ni shughuli inayojumuisha ufugaji na uzalishaji wa mazao. kilimo ni sekta muhimu sana katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania. Tunaweza kusema kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa Tanzania. Hii ni kutokana na ukweli kwamba asilimia kubwa(zaidi ya 90%) ya watanzania wanajishughulisha na kilimo kwa kuzalisha mazao mbalimbali na mifugo. Takwimu za shirika la chakula na kilimo (FAO) zinaonesha kuwa katika nchi zinazoendelea 43% ya nguvu kazi ya kilimo ni wanawake na pia wana mchango mkubwa katika uzalishaji wa chakula, ambapo wanazalisha chakula kwa 60%-80%. Taarifa ya UNDP (2023) inaonesha kuwa nchini Tanzania, 67% ya wafanyakazi wa kike wamejiajiri katika kilimo (nukuu kutoka TGNPTZ)

Katika kuboresha na kuendeleza kilimo nchini Tanzania, Wizara ya kilimo imekuwa ikiandaa na kutekeleza mipango mbalimbali yenye kulenga kuboresha sekta hii muhimu ya kilimo kwa Taifa na watu wake. Ili kuendeleza sekta kilimo, serikali kupitia wizara ya kilimo na kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo imeandaa programu za kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya kwanza na pili (ASDP I na ASDP II) ili kutekeleza mpango wa miaka kumi katika kuboresha sekta ya kilimo.

Screenshot_20230704-100816_1.jpg

Kielelezo namba 1. chanzo kutoka chapisho la ASDP II (2017)

Pamoja na juhudi za makusudi za kuleta maboresho kwenye sekta ya kilimo nchini, kuna mazingira ambayo hayampi mwanamke uhuru na ushiriki wa moja kwa moja katika uongozi na maamuzu kuhusu kilimo. Kwani, pamoja na umuhimu na mchango wao mkubwa katika kilimo na uzalishaji wa chakula, kundi hili la wanawake linakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile ukatili wa kijinsia na ushiriki duni katika uamuzi hasa unaohusu kilimo, mambo ambayo yanarudisha nyuma jitihada za wanawake katika sekta hii muhimu.

MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA KULINDA MUSTAKABALI WA MWANAMKE KWENYE SEKTA YA KILIMO.
Mustakabali wa mwanamke kwenye kilimo ni mada yenye mashiko na kuhitaji kuibua chachu ya kumpa mwanamke ushiriki wa moja kwa moja na maamuzi yanayohusu kilimo kwa mustakabali wa nchi yetu na wanajamii kwa ujumla. Ni muhimu mabadiliko na uwekezaji wa namna yoyote ile kwenye sekta ya kilimo kumpa mwanamke ushiriki na uongozi wa kufanya maamuzi na usimamizi, kwani wao ni chachu ya uzalishaji na kuleta maendeleo chanya kwa Taifa. Jamii nyingi za Tanzania zimekuwa na mitazamo hasi juu ya wanawake kwenye sekta ya kilimo kwa kumuona ni kiumbe duni na asiyepaswa kushirikishwa na kupewa uongozi wa kimaamuzi.
Sambamba na hayo, mwanamke amejikuta anaingia kwenye matatizo makubwa ikiwemo ukatili wa kingono na manyanyaso mengine kama vile kunyimwa umiliki katika ardhi. Hivyo ni muhimu kwa wizara za sekta ya kilimo na wadau wa kilimo kuona ni wakati sasa wa kumpa mwanamke uwezo na ushiriki katika mambo yote yanayohusu kilimo na maamuzi katika masuala ya kilimo. Hapa nitayajadili mambo kadhaa ambayo yataweza kuunda mustakabili wa mwanamke kwenye sekta ya kilimo.

Kwanza, kuhakikisha kuna kuwa na usawa wa kijinsia na uwezeshaji ndani ya sekta ya kilimo. Kwa miaka mingi mwanamke hakupewa kipaumbele kwenye kilimo wala hakupewa namna itayomwezesha ili kuendelez shughuli zake za kiuzalishaji katika kilimo. Ni wakati sasa kwa serikali kupitia wizara ya kilimo kwenye madaliko na uwekezaji wake kuhakiksha kunakuwa na uzingativu wa usawa na uwezeshaji. Kwa mfano, kuwapa wanawake fursa sawa ya kupata ardhi, rasilimali, mikopo na teknolojia. Serikali, mashirika na jamii yawapasa kubadilika kimitazamo juu ya mwanamke kwenye kilimo, na badala yake viongeze ushiriki wa kufanya kazi kwa pamoja ili kuondoa mila na desturi za kibaguzi kwa mwanamke na kutoa miongozo na sera saidizi zitakazomwezesha mwanamke kushiriki na kuongoza katika kilimo.

Pili, kuwekeza katika elimu na mafunzo ya wanawake katika kilimo. Kwa kuwapa wanawake fursa ya kupata elimu yenye tija, mafunzo ya ufundi stadi na huduma za ugani kunaweza kuongeza ujuzi na maarifa ya mwanamke kwenye kilimo. Sambamba na hayo, kutamwezesha mwanamke kuelewa namna ya kukabiliana na chgangamoto mbalimbali za kilimo zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Tatu, kuunda majukwaa ya mitandao ya mada za kilimo na programu za ushauri wa kilimo. Majukwaa na programu hizo zinaweza kuwapa wanawake usaidizi kwenye kilimo. Kwani mijadala na programu inaweza kukuza ubadilishanaji wa maarifa, kujenga mahusiano ya kitaaluma, na kuwawezesha wanawake kushinda vikwazo katika sekta hiyo na kufikia malengo yao.

Nne, kuwepo na sera zenye kumsaidia na kumtetea mwanamke kwenye kilimo. Serikali na watunga sera wana jukumu kubwa katika kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kwenye kilimo. Ni muhimu kutetea sera zinazozingatia jinsia na usawa, uwazi, utatuzi wa changamoto zinazowakabili wanawake kwenye kilimo. kwa mfano sera zinazowezesha upatikanaji wa haki za ardhi, mikopo, masoko na ulinzi wa kijamii. Pia sera zenye kuhimiza wanawake kwenye michakato ya kufanya maamuzi katika ngazi zote.

Tano, kuwasaidia wanawake katika kuongeza thamani ya mazao yao ya kilimo na kupata masoko, kwani hali hii huweza kuongeza kipato na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi. kwa mfano, kutoa mafunzo juu ya usindikaji wa chakula, ufungashaji, na viwango vya ubora kunaweza kuwawezesha wanawake kusonga mbele zaidi na kuingia kwenye ushindani wa masoko ya thamani ya juu. Hii inaenda sambamba na kuboreshwa kwa miundombinu ya soko, kupunguza vikwazo vya soko vinavyoegemea jinsia, na kukuza ujasiriamali wa wanawake kunaweza kufungua fursa mpya kwa wanawake katika sekta ya kilimo.

Sita, kuwekeza katika kilimo kinachozingatia hali ya hewa, kilimo mseto na kilimo cha umwagiliaji kunaweza kuwapa wanawake vyanzo mbadala vya mapato na kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kwani mabadiliko ya hali ya hewa kwa kiasi kikubwa humwathiri sana mwanamke katika uzalishaji wake.

Saba, kuwahimiza wanawake kufuata na kutumia teknolojia za kisasa za kilimo, kama vile kilimo cha usahihi, uchanganuzi wa data na mbinu za kuzingatia hali ya hewa. kuna wakati teknolojia hizo huwa ni gharama kupatikana, hivyo ni muhimu kuhakikisha teknolojia inapatikana na inapatikana kwa bei nafuu, na imeundwa kulingana na mahitaji maalumu ya wakulima wanawake.

Kwa kuhitimisha naweza kusema kuwa sasa umefika wakati wa kupinga mila potofu dhidi ya wanawake kwenye kilimo ili kuepuka mazingira yatakayomnyima mwanamke uwezo na ushiriki katika mapinduzi ya kilimo. zaidi naipongeza serikali kupitia wizara ya kilimo iliyo chini ya mheshimiwa waziri Bashe kwa hatua inazochukua zenye tija na nia ya kuboresha kilimo na kuleta usawa kwa wote katika ardhi na zana za uzalishaji.
 
Back
Top Bottom