Chadema wasakamwa, wadaiwa wahaini
Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko; Tarehe: 4th March 2011 @ 07:36 Imesomwa na watu: 1160; Jumla ya maoni: 2
WANASIASA na taasisi mbalimbali nchini wamepinga maandamano yanayoendeshwa na Chadema kuhamasisha wananchi kuipinga Serikali na kuiondoa madarakani kuwa ni uhaini na inapaswa kushitakiwa.
Aidha, wamemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, kuangalia uwezekano wa kukisimamisha au kukifuta chama hicho kwa usalama wa Taifa na kudai kuwa maandamano hayo ni chanzo cha vurugu na kuvunjika kwa amani, ambazo ni dalili zinazopaswa kuchukuliwa hatua za kiusalama haraka ili Taifa lisiingie katika machafuko ya kisiasa.
Katika siku za karibuni Chadema imekuwa ikifanya maandamano na mikutano ya hadhara kwa lengo la kupinga ufisadi serikalini, hali ngumu ya maisha inayotokana na kupanda kwa bei ya vyakula, malipo kwa Kampuni ya Dowans na tatizo la umeme.
Wakizungumza na wanahabari Dar es Salaam jana, Wanaharakati wa Haki za Watu Wenye Ulemavu nchini, walisema kinachofanywa hivi sasa na vyama vya siasa na wanasiasa kuzunguka nchini kuhamasisha wananchi wakubali kuondoa Serikali halali madarakani, kinaweza kusababisha madhara makubwa.
Walipongeza hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wiki iliyopita na kupinga maandamano yanayoendelea katika mikoa tofauti na kusema madhara hayo waathirika wake ni jamii ya watu wenye ulemavu.
Msemaji wa wanaharakati hao, Abubakar Rakesh, alisema wanampongeza Rais kwa kuona kwamba amani ya Watanzania ambayo ni tunu inaanza kutoweka kwa kusema kwake na kuwaondoa hofu Watanzania, imeonesha jinsi anavyowajali wananchi wake.
"Uzoefu na ushahidi unatuonesha, kwamba nchi nyingi duniani zilizokabiliwa na migogoro na uvunjifu wa amani, wahanga wakubwa wa kupoteza maisha ni watu wa jamii ya walemavu, hivyo tunamwomba Rais aendelee kukemea lakini pia asiyumbe katika kulinda amani ya nchi yetu," alisema Rakesh.
Walimtaka Rais Kikwete pamoja na kuendelea kukemea hali hiyo, lakini pia asiyumbe katika kulinda amani ya nchi na kuhakikisha kuwa Katiba iliyopo inaheshimiwa na kila mmoja, kwani Katiba ya nchi si ya chama.
Katibu wa Kamati ya Amani Umoja na Mshikamano wa Kitaifa (UPF), Risasi Mwaulanga, alisema wanachofanya Chadema ni uhaini wa wazi, kwani umma utakapokasirika utapata hamasa na kugomea sera ya chama tawala na kuacha kushiriki shughuli za maendeleo.
"Vyombo vya usalama vinatakiwa kuchukua hatua dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema na Katibu Mkuu wake wakamatwe na kufunguliwa mashitaka ya uhaini, ikiwa ni pamoja na Bunge kutoa onyo kwa wabunge wake na Msajili kuangalia vifungu vya Katiba kuona uwezekano wa kukisimamisha au kukifuta chama hicho," alisema Mwaulanga.
Pia aliwataka wananchi kupuuza mikutano yao ya hadhara bila kujali itikadi, kujenga ushawishi wa kutengwa na taasisi mbalimbali hadi watakaporekebisha mustakabali wa siasa zao za uchochezi nchini .
Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema, alisema maandamano hayo yanahamasisha wananchi kuiga mifano ya nchi za Kaskazini mwa Afrika, ambazo chanzo cha maandamano na hatimaye vifo yametokana na vyama vya upinzani.
"Maandamano hayawezi kutuondolea matatizo tuliyonayo, bali yatasababisha maafa makubwa yasiyoweza kulipika, kama ilivyotokea kwenye nchi nyingine duniani, ni wazi tunaweza kuiondoa Serikali iliyoko madarakani kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria kwa ridhaa ya wananchi kwa kura zao," alisema Mrema.
Aliwasihi wapinzani wenzake kuwa kwa kutumia njia sahihi wana uwezo wa kuingia madarakani, ndiyo maana walipata asilimia 40 ya kura za urais na wana wabunge na madiwani.
"Wapinzani tuko bungeni, kwenye halmashauri za miji, serikali za vijiji na vitongoji, kwa nini tusitumie fursa hizo? Baada ya uchaguzi siasa zihamie bungeni na kwenye mabaraza ya halmashauri na miji na si kuishia maandamano na mikutano tu," alisema Mrema.
Alisema wapinzani wana wenyeviti katika kamati mbalimbali za Bunge, hivyo wanaweza kupambana na ufisadi na wakishindwa ni uzembe wao, kwani hawana kikwazo, aliwataka kukamata mafisadi na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria kwani ufisadi hauwezi kuondolewa kwa maandamano.
"Kwa mfano mimi nilishakabidhiwa vitabu vya ukaguzi kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali vinavyoonesha kwenye halmashauri za miji kuna ubadhirifu wa kutisha, kuliko hata ubadhirifu unaodaiwa kufanywa na Dowans," alisisitiza Mrema.
Aliwataka Watanzania wasidanganywe na kufananisha Tanzania na nchi nyingine kama Libya na Misri, kwani matatizo hayafanani na nchini tatizo ni umasikini, hali ngumu ya maisha, umeme na ufisadi, wakati nchi hizo zingine, matatizo yao ni mfumo mbaya wa kiutawala tofauti Tanzania.
Jumla Maoni (2) Maoni Nashukuru sana kwa mpinzani wa kweli na mwenye busara Mh. Agustino Mrema kwa kuliona hili linalofanywa na wanasiasa wa Chama cha Chadema na kuwapa Watanzania wenzake tahadhari kubwa, Ndugu zangu, Mh. Slaa na Mh. Mbowe, hivi ni kweli mnawapenda Watanzania wenzenu kwa kuwashawishi hayo mnayoyafanya? Nina Imani kwa ukomavu wenu wa kisiasa mnaelewa wazi athari kubwa na mbaya iliyo mbele kwa hayo mnayoyatazamia. Sie sote ni Watanzania na wazalendo wa kweli wa nchi yetu, nawashauri msitumie mikutano yenu kuwashawishi Watanzania kuichukia serikali ilikuwa madarakani kwa ridhaa ya Watanzania wengi. Nawatakia mzee Slaa na Father Mbowe, siasa njema na zenye mabadiriko kimtazamo. Maoni Nimegundua kuwa wananchi wengi wa Tanzania hatuelewi vitu gani ambavyo tukivifanya vinavyoweza kutuletea maendeleo nchini,kwa umbumbu huu watanzania wengi wanadanywa kwamba maandamano tena ya jasba kwamba huleta maendeleo bila kujua kuwa maandamano ya watu wenye hasira na jazba huzaa uvunjifu wa amani ambayo ndio kitovu kikuu cha nchi kupata maendeleo,ukitaka kujua ukweli huu angalia nchi ambazo zimekumbwa na mizozo ya kivita kwa muda mrefu jinsi walivyo na hali ngumu ya maisha.Ni hatari nchi kuingia katika machafuko kwani kila kitu husimama ,hakuna shule,hakuna cha huduma za afya,uzalihsaji mali mashambani na viwandani ,hakuna kinachotoka wala kuingia nchini kwa ajili ya kuinua uchumi badala yake hata kile kidogo kilichopo hutumika na serikali katika kukabiliana na hali mbaya ya hatari inayokuwepo ya machafuko.Watanzania wengi tumezaliwa nchi ikiwa na amani sasa tumelewa na amani hiyo kiasi kwamba tunatamani machafuko nchini,eeh Mungu tuokoe na balaa hii ya machafuko Tanzania ,tujalie kuwa kuwa na amani siku zote ipitayo akili na fahamu zetu ili tuendelee kufurahia mema na baraka na neema tele tuliyopewa na MOLA MUUMBA WETU AMINA.