Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke anayeishi Kijijini 15 Oktoba 2023

Dkt. Gwajima D

JF-Expert Member
Nov 28, 2015
543
3,575
Ndugu wana Jukwaa la JF; Wasaalam.

Tafadhali pokeeni taarifa kuhusu Siku ya Mwanamke anayeishi Kijijini 15 OKT, 2023. Kila mkoa utafanya kwa utaratibu wake ngazi zote za mamlaka yake. Sisi Wizara ya Jamii tutaungana na Mkoa wa Arusha, Kijiji cha Levelousi, Arumeru.

HISTORIA; Azimio la Umoja wa Mataifa Na. 62 la 18 Des, 2007. Tanzania ilianza kuadhimisha mwaka 2018 kwa lengo la kutambua jitihada na mchango wa wanawake wanaoishi vijijini kwenye maendeleo ya jamii.

SEKTA KUU ZINAZOGUSWA ZAIDI; uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuhakikisha usalama wa chakula cha Kaya na kuchangia ukuaji wa Uchumi wa Taifa.

BAADHI YA FAIDA ZA MAADHIMISHO; kuongeza mwitikio wa wanawake kushiriki katika shughuli za kiuchumi, kushiriki katika upangaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao; kujenga uelewa kuhusu fursa za uwezeshaji wa wanawake kiuchumi; kuhamasisha wanawake kuhusu fursa za kibiashara na matumizi ya zana na teknolojia sahihi na rahisi za uzalishaji zinazorahisisha kazi ili kuweza kumudu ushindani wa kibiashara sokoni. Pia, kutoa hamasa kwa wanawake na jamii kuhusu kukabiliana na umaskini wa kipato ili kuwa na uhakika wa chakula, lishe na malezi katika Kaya.

KAULIMBIU: “Wezesha Wanawake wanaoishi kijijini: Kwa uhakika wa Chakula, Lishe na Uendelevu wa Familia”

BAADHI YA UTEKELEZAJI WA SERIKALI ili kumuwezesha mwanamke anayeishi kijijini:

1. Kuwezesha wakulima ambao wengi wao ni wanawake wanaoishi vijijini kwa kuwapatia ruzuku kwenye mbolea kwa bei ya Sh. 73,468.00 badala ya Sh. 109,000 kwa mfuko wa kilo 50 kupitia Wakala waliopitishwa na Serikali kwa mwaka 2023. Aidha, Serikali Kupitia Mfuko wa Pembejeo wa Taifa imetoa mikopo ya Pembejeo za kilimo, mifugo na uvuvi.

2. Kuboresha kilimo cha biashara kwa kuondoa tozo, kodi na kufungua milango ya biashara nchi za nje. Zaidi ya Tozo 100 zimeondewa ili kupunguza gharama za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

3. Serikali inafanyia kazi kuboresha upatikanaji wa nishati mbadala kwa gharama nafuu ili kuchochea ustawi wa wanawake hususan vijijini, ikiwemo kuwawezesha kupata huduma na elimu kupitia vyombo vya habari juu ya masuala mbalimbali yanayowahusu na kuokoa afya dhidi ya athari ya nishati ya kuni ambayo ina athari.

4. Mikopo ya Sh bilioni 713.8 imetolewa ili kukuza ushiriki wa wananchi kwenye shughuli za kiuchumi Julai 2022 hadi Machi, 2023 ambayo imezalisha ajira 3,122,104 (wanawake ni 1,623,494 (52%) na wanaume 1,498,610 (48%). Mikopo hiyo imetolewa kwa wajasiriamali 2,203,838 (wanawake 1,234,149 (56%) na wanaume 969,689 (44%) katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi.

5. Kutungwa kwa Sheria ya Ardhi ya Kijiji Na. 5 (1999), Kifungu cha 20(1), kinachotoa nafasi kwa Wanawake kumiliki ambapo, kufikia 2021/22 jumla ya Hatimiliki za Kimila 1,171,884 zimetolewa kwa Wanawake 406,915 na Wanaume 764,969.

6. Kampeni ya ‘’Mtue Mama Ndoo Kichwani’’ imeimarisha upatikanaji maji na kufikia asilimia 77 ikiwa lengo ni kufikia 85% hivyo, kumwezesha mwanamke kuwa na muda wa kushiriki shughuli za kiuchumi

BAADHI YA SHUGHULI ZA MAADHIMISHO; mahojiano kupitia vyombo vya habari; maonesho ya kazi za wanawake na jitihada za wadau katika kuleta usawa wa kijinsia; makongamano na midahalo nk.

UJUMBE KWA JAMII; Wanawake ndio wanaokumbana na changamoto zaidi kutokana na mgawanyo wa majukumu katika familia; uwezo mdogo wa kipato; elimu na ujuzi duni; mila na desturi kandamizi; na pia changamoto za miundombinu isiyotosheleza vijijini.

Hivyo, Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anazingatia kipaumbele cha kuimarisha ustawi na maendeleo ya mwanamke anayeishi kijijini.

Nawasihi, jamii tujitokeze kuadhimisha kwenye maeneo yetu chini ya uongozi wa Wakuu wa Mikoa na Wilaya.

HITIMISHO; Nawatakia heri ya maadhimisho ya Siku ya Mwanamke wa Kijijini, 15 Okt, 2023.

Karibuni sana kwa mjadala ambao, huongeza kujenga fikra zetu na mshikamano wetu jamii.

JamiiYetuFahariYetu#

View attachment 2780685


IMG-20231012-WA0039.jpg
 
Unasemwa kuwa mwanamke wa kijijini ndiye anaongoza kwa kufanya kazi kwa muda mrefu. Wa pili mwanaume wa mjini, watatu mwanaume wa kijijini na mwisho mwanamke wa mjini. Hakika anahitaji maadhimisho yake.
 
Back
Top Bottom