Wadau, kwa wale waliosikiliza mahojiano kati ya Lowasa na Tido (ktk television ya taifa - TBC) na kusoma makala ya Lula ktk gazeti la Rai wiki hii wanaweza kukubaliana nami kuwa Tido Mhando anaanza kuidhalilisha hadhi aliyoipata baada ya kufanya kazi ktk shirika kubwa kama BBC. Najiuliza kwa mwanahabari aliyebobea kama Tido inakuwaje leo ashindwe kumhoji Lowasa maswali magumu kama yale aliyokuwa anawahoji viongozi wakubwa alipokuwa TBC? Yaani mahojiano yake na Lowasa huwezi hata kuyalinganisha na mtu wa kijiweni ambavyo angefanya kama angepewa fursa ya kumhoji Lowasa. Jamani, je ni kweli Tido ana njaa kiasi hicho kukubali kujidhalilisha ili awaoshe mafisadi? Si bora angepumzika tu nyumbani kuliko kukubali kuidhalilisha taaluma yake na sifa alizojipatia kwa muda mrefu baada ya kufanya kazi BBC. Ni kama vile alikuwa ameandaliwa maswali ya kumwuliza Lowasa. Na kama hii ndivyo ilivyo, kwa nini asikubali kubwaga manyanga kuliko kuchezewa hivyo??? Watanzania sijui tuna matatizo gani? Jamani Tido na wewe????
Naweka makala ya Lula hapa chini kwa wale ambao hamkufanikiwa kuisoma
Maswali ambayo Tido alishindwa kumuuliza Lowassa
Lula wa Ndali-Mwananzela
Julai 21, 2010
MAHOJIANO ya Mkurugenzi wa TBC Tido Mhando na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa ambayo yalirushwa Ijumaa iliyopita yameniacha na maswali mengi zaidi kuliko majibu.
Ilipodokezwa kuwa Lowassa angefanya mahojiano na TBC nilitarajia kuwa hatimaye baadhi ya maswali ambayo nimekuwa nikijuliza kwa miaka miwili karibu na nusu yatapatiwa majibu yake. Nasikitika kusema kuwa mahojiano yale yamerudisha maswali yangu kwa ari kubwa zaidi, nguvu kubwa zaidi na kasi kubwa zaidi.
Hata hivyo, kabla ya kuangalia maswali hayo ambayo yamenikamata kama sungura alivyonaswa kwenye sanamu iliyokuwa na ulimbo, nimeona niseme mambo machache kuhusu mahojiano yale ambayo nayo pia yamenifanya nijiulize kama TBC ni kampuni tanzu ya Lowassa au vipi?
Kwa nini TBC ilimhoji Lowassa?
Siku ile ya kuvunjwa Bunge nilitarajia watu watatu wangeweza kuhojiwa katika kuonyesha umuhimu wa siku yenyewe. Nilitarajia kuwa wangeweza kumhoji Spika wa Jamhuri ya Muungano, wangeweza kumhoji Waziri Mkuu na wangeweza kumhoji Kiongozi wa Upinzani na kubwa zaidi wangeweza kumhoji Rais. Sijaelewa kwa nini walimhoji Lowassa?
TBC itakuwa ina sababu yake na naweza kuhisi bila kutumia chembe nyingi za ubongo kuwa walimhoji Lowassa kwa sababu mahojiano yake ya kwanza na TVT na Tido huyo huyo yalionekana kama yalikatishwa hewani. Kwa hiyo, uamuzi ulichukuliwa kwa makusudi kabisa wa kuendelea pale walipoachia kwani ukichukua mahojiano hayo na kuyaweka sambamba utaona kuwa mahojiano ya wiki iliyopita yalikuwa ni mwendelezo na ukamilisho tu wa mahojiano yale ya miaka miwili iliyopita.
Lakini, hata hivyo, hili bado halijibu swali la kwa nini walimhoji Lowassa kwa sababu hakuwa na jambo lolote jipya la kusema zaidi ya kurudia utetezi wake ule ule wa 2008.
Serikali imelegalega baada ya Lowassa kuondoka?
Maswali ya awali ya Tido kwa Lowassa yalikuwa yanalenga kuwa Serikali imeyumbayumba na kulegalega baada ya Lowassa kuondoka.
Tido alipomuuliza Lowassa juu ya kupungua kwa msukumo katika masuala ya ujenzi wa shule za sekondari Lowassa akicheka kidogo alisema tu kuwa sijui msukumo umepungua kwa kiasi gani.
Kwa maneno mengine Tido na Lowassa walikuwa wanakubaliana kuwa msukumo wa utekelezaji umepungua, walichotofautiana ni kwa kiasi gani, kwani Tido alisema sana na Lowassa hakutaka kutumia neno hilo sana.
Hili ni muhimu kujua kwa sababu Lowassa alizungumza baada ya Waziri Mkuu wa sasa kuhojiwa. Sijui kwa nini Tido hakutaka kupata maelezo kutoka kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kujua kama msukumo umepungua au la. Kwa nini alimuuliza Lowassa?
Haya niyaache hayo wanajuana wenyewe. Hata hivyo, kuna maswali ambayo Tido alitakiwa kumuuliza Lowassa ili kuonyesha angalau chembe ya weledi. Hili ni muhimu hasa ukizingatia kuwa katika mazungumzo yao hayo Lowassa alituhumu kuwa waandishi hawana weledi na kujaribu kujenga hoja kuwa waandishi wakipata digrii basi kusajiliwa basi watakuwa ni waandishi wazuri. Kana kwamba wahasibu wote wenye CPA na waliosajiliwa ni waaminifu kwenye taaluma zao au mawakili wote ni waaminifu kwa viapo vyao! Kumbe mtu anaweza akawa na kabati la vyeti vya taaluma lakini akawa ni fisadi numero uno!
Sasa nilitarajia kuwa Tido angeweza kumuuliza maswali ambayo tumekuwa tukiyauliza kwa miaka miwili kila Lowassa anapozungumzia suala la kuonewa kwake na Kamati Teule ya Bunge. Nilitarajia Tido angeweza kumuuliza maswali ambayo majibu yake yangetupa mwanga kuelewa mawazo ya Lowassa hadi kujiuzulu yalikuwa ni ni hasa. Baadhi ya maswali hayo ni haya:
Lowassa alipata wapi madaraka ya kuingilia mchakato wa utoaji tenda kwenye taasisi ya Serikali, TANESCO? Na ni sheria gani iliyompa nguvu hiyo? Jibu lake la kuwa ilikuwa ni dharura halitoshi kwa sababu kama kweli kulikuwa na dharura ni Rais tu ndiye mwenye uwezo wa kutangaza hali ya dharura. Lowassa alipata wapi haki ya kutangaza hali ya dharura na kuchukua hatua za kusimamisha sheria mbalimbali?
Ni kwa nini hakujiridhisha yeye mwenyewe juu ya uwezo wa kampuni ya Richmond kuleta umeme badala ya kuwategemea watu wengine ukizingatia kuwa ni yeye ndiye aliyeunda kamati nje ya utaratibu wa kisheria wa zabuni?
Kwa nini hakujitetea mbele ya Bunge. Baada ya Lowassa kuomba nafasi ya kuzungumza kufuatia maneno makali ya Bunge siku moja kabla, nilitarajia kuwa hatimaye angeweza kujibu hoja mbalimbali za wabunge. Lakini aliposimama asubuhi ile Lowassa aliamua kubwaga manyanga chini. Hakujaribu hata kidogo kuelezea upande wake kwenye chombo sahihi ambacho kilipitisha uteuzi wake kwa kauli moja. Kwa nini hakujitetea?
Kwa nini hakuomba Bunge liahirishwe ili apate nafasi ya kujipanga kutoa majibu ya tuhuma mbalimbali. Waziri Mkuu ana kipaumbele bungeni. Baada ya madongo mengi kurushwa Lowassa angeweza kuomba Bunge liahirishwe kwa muda ili aandae majibu yake kwa Bunge. Kutokana na uzito wa hoja zile siwezi kuona jinsi gani Spika angeweza kumkatalia kumpa nafasi hiyo. Nina uhakika wa asilimia 100 kuwa endapo Lowassa angeomba muda wa kuandaa majibu angepewa. Kwa nini hakufanya hivyo?
Kwa nini anaamini kuwa hakupewa nafasi ya kujitetea wakati Kamati Teule haikutoa hukumu yoyote kwake? Hili ni muhimu kwangu kutaka kulielewa kwa sababu nina uhakika kuwa Lowassa anajua kuwa haki ya asili ya kujitetea inahusiana na hukumu na si tuhuma.
Mtu mtu akikamatwa na Polisi, ukishakusanywa ushahidi na kesi kupelekwa kwa mwendesha mashtaka hawezi kuinuka na kusema kuwa mbona hamkunihoji. Watu watamshangaa. Ila kama mahakama itapokea ushahidi huo na tuhuma hizo halafu kutoa hukumu dhidi ya mtu huyo bila ya kumpa nafasi ya kumsikiliza basi itakuwa imemnyima haki yake ya msingi ya asili, ile ya kusikilizwa.
Lakini Lowassa hakuhukumiwa na Kamati Teule kwani Kamati Teule kisheria haiwezi kupitisha hukumu yoyote bali inaweza kutoa mapendekezo kwa Bunge. Na sote tunajua kuwa Kamati Teule ilimpa nafasi Waziri Mkuu kujipima kutokana na uzito wa tuhuma hizo na kuchukua uamuzi unaofaa. Alikuwa na uwezo wa mambo mengi ya kuweza kufanya, kwa nini alichagua la kujiuzulu badala ya kujitetea?
Kama kweli Lowassa anaamini kuwa hakutendewa haki na Bunge kwa nini hakuleta hoja bungeni kama Mbunge anayeelewa wajibu wake na kutaka uchunguzi mpya ufanyike au kuwalazimisha Kamati Teule kuweka ushahidi wao dhidi yake hadharani ili kuona kama kweli alihusika na sakata la Richmond au la? Kinyume chake aliamua kuzungumza baada ya Bunge kuvunjwa? Haoni kwamba kwa kufanya hivyo ni kujionyesha kuwa hakuwa anajiamini mbele ya Bunge?
Pamoja na maswali hayo binafsi ningependa kujua kama TBC ina mpango wa kutoa nafasi kwa Spika au mjumbe yeyote wa iliyokuwa Kamati Teule kuweza na wenyewe kuelezea upande wao kwa mtindo ule ule uliofanywa kwa Lowassa?
Vinginevyo kama vile Lowassa alivyojiuzulu kwa kutumia madaraka yake vibaya (hata kama hakubali) naamin Tido Mhando naye ametumia nafasi yake ya Ukurugenzi wa TBC vibaya na kwa sababu hiyo natoa pendekezo na yeye afuate njia aliyoifuata Lowassa; ajiuzulu ampishe Mtanzania mwingine ambaye hataonekana kama anatumika kubeba viongozi au watendaji ambao wamefunikwa na wingu la tuhuma.