Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
LOWASSA NI TAASISI MADHUBUTI.
Nani alitegemea Wilbroad Slaa aliyeipenda CHADEMA kwa moyo wake kuacha siasa?
Nani alitegemea Lipumba kujiuzulu uenyekiti wa CUF?
Nani alitegemea Kungunge kujiunga upinzani?
Nani ayetegemea Sumaye kuwa kambi ya Lowassa?
Nani alitegemea CHADEMA na CUF kuacha siasa za MAANDAMANO?
Nani alitegemea CHADEMA kupata kura nyingi kiasi kile hata watu wafikiri CHADEMA ilishinda urais?
Nani alitegemea Magufuli kuwa rais wa Tanzania?
Nani alitegemea CCM kutumia nguvu kubwa katika uchaguz uliopita na kuufanya wa kufa na kupona?
Nani alitegemea Nabii Joshua kuja pekupeku Tanzania?
Nani alitegemea NabiiJoshua asingeuzulia kuapishwa kwa Magufuli ikiwa alithibitisha kuhudhuria na jina lake lilikuwako katika orodha ya wageni?
Nani alitegemea vyama ambavyo vilikuwa nje ya UKAWA vitikisike kama vihori kwenye mkondo wa bahari unaopigwa kaskaz au matlai?
Nani alitegemea Makonda kuwa mkuu wa wilaya na sasa mkuu wa mkoa?
Haya hayakutemegewa, na kwa vyovyote vile hakuna mtu aliyedhani japo kwa kuota, midhali yametokea ndio vema tukiri kuwa Lowassa hakuwa mtu bali taasisi. Taasisi ambayo iliamua kufanya kazi na UKAWA kama plani "C" baada ya plani "A" na "B" kufeli.
Taasisi ambayo ingeweza kutupeleka mbali katika kilele cha mafanikio kama ingetumiwa vizuri, ama kutuangamiza kabisa kama ingetumiwa vibaya.
Pamoja na hayo, kwa mambo yanayo endelea ndani ya serikali na CCM kwasasa, kwa vyovyote vile Magufuli naye alikuwa taasisi nyingine ilojificha na kuibuka kwa kutumia mwanya wa kushambuliwa Lowassa.
Unapo amka asubuhi uende kazini au shambani, unaipa kichogo nyumba yako huku ukitaraji ukirudi utaikuta kama ulivyo iacha, bi maana salama, lakini ukirudi na kukuta mambo yameharibika, utajilaumu kwa kusema laiti ningekuwako huenda mambo yasinge haribika, hapo sasa wakilaumu kisogo, kisogo ndio mchawi wako, naam, kisogo mchawi. Kwa minajili hiyo ndipo nikatunga shairi hili.
KISOGO MCHAWI?
1.
Natoa kingilambago, nisikizwe kilingeni,
Simtaki jini kago, maalim Subiani,
Namtaka Mwinyimbago, kibokoye Makatani,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
2.
Fundi kalia kibago, ufushe wako ubani,
Mpandishe Mwinyimbago, anipashe ya sirini,
Kichogo chake kigogo, aague kina nini,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
3.
Vile mchawi kichogo, imethibiti nadhani,
Kichogo huzua zogo, kwa jirani na nyumbani,
Lakini si cha mdogo, naomba zingatieni,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
4.
Akijitoa mdogo, hubaki poa kundini,
Tena hapeleki zogo, aendapo tambueni,
Kambare akina ngogo, hawastuki asilani,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
5.
Tena hafanyi mikogo, hauziki gazetini,
Aishi pale Kigogo, soko lake Buguruni,
Hawamjui wa dago, hata walio shambani,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
6.
Sasa katoka kigogo, ikazuka tafarani,
Wakubwa hata wadogo, wakafuata njiani,
Katangazwa si kidogo, luninga na redioni,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
7.
Kaondoka na mizigo, iliyo mwake kwapani,
Naeza kuita kago, isiyobebwa kichwani,
Kago limeleta zogo, alipolitua ndani,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
8.
Baadhi wakawa mbogo, hawamtaki mgeni,
Hasa mpenda mihogo, asiyetaka utani,
Akakusanya virago, akajitoa kundini,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
9.
Kigogo huyo kigogo, anatamba baharini,
Meli zimepata pigo, vihori viko shakani,
Hatari anayo chwago, nyangumi pia jodani,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
10.
Panda ewe Mwinyimbago, ili nipate yakini,
Ukiague kichogo, nikijue kina nini,
Kiasi kizue zogo, watu wakose amani,
Vipi iwe tafarani, alipowapa kisogo.
11.
Mkirika na mtogo, vimechomwa na ubani,
Kafurahi Mwinyimbago, ameshapanda rasini,
Ninawaacha kidogo, nimsikize lohani
Vipe iwe tafarani, alipowapa kisogo.
Dotto Chamchua Rangimoto(Njano5)
whatsapp/call 062284845394
Mzalendo.njano5@gmail.com
Morogoro Tanzania