Lowasa Achoka Kuzushiwa
Novemba 27, 2010
WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ameeleza kushangazwa na mwenendo wa kisiasa wa siku za hivi karibuni ambao unaliingiza jina lake katika matukio makubwa ya kisiasa yanayotokea. Mbali ya kueleza mshangao wake huo, Lowassa alikwenda mbele zaidi na kusema alikuwa amefikia hatua ya kuchoshwa na aina ya siasa zinazomhusisha na mambo yasiyo na ukweli wowote.
"Nimechoka kukaa kimya kila mara zinapotengenezwa habari za uongo juu yangu. Imefika mahali sasa nimeamua kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale ambao kwa makusudi na kwa nia mbaya wanafinyanga uzushi dhidi yangu na wakati mwingine dhidi ya familia yangu," alisema Lowassa aliyezungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana.
Akitoa mfano ..................... [not relevant here]
Mbali ya hilo, Lowassa alisema, watu wasiomtakia mema, ambao hata hivyo hakuwataja, wamefikia hatua ya kuanza kuipaka matope hata familia yake katika mambo ambayo si ya kweli. Lowassa alikuwa akizungumzia habari zilizomhusisha mtoto wake Frederick Lowassa katika tuhuma za kuchunguzwa na taasisi za ndani ya nchi na zile za nchini Uingereza kwa madai ya kusafirisha fedha nje ya nchi katika mazingira yenye utata.
Habari hizo zilizoandikwa katika gazeti moja linalochapishwa mara moja kwa wiki, zilimhusisha Frederick na ununuzi wa nyumba yenye thamani ya pauni za Uingereza 475,000 (takriban shilingi bilioni moja) ambayo inatajwa katika maelezo ya awali iko mtaa wa Leinster Gardens, jijini London.
"Habari hizo zinazomhusu Frederick na ambazo zililitaja pia jina langu hazina ukweli wowote. Nimechoka kuzushiwa na kushambuliwa kwa mambo ambayo si ya kweli. Nimekuwa kimya na sasa wameanza kuichafua hata familia yangu.
"Nimewasiliana na Frederick mwenyewe ambaye amenihakikishia kuwa tayari ameshaanza kuchukua hatua za kulifikisha suala hilo mbele ya vyombo vya kimaadili na kisheria kama Baraza la Habari Tanzania (MCT) na mahakamani ili kulisafisha jina lake," alisema Lowassa. [Emphasis added]
Chanzo cha Habari: Tanzania Daima
Angalizo kwa waliokuwa wanamtetea Lowassa baada ya kuongea na TBC
Siku hizi inabidi kabla hujasema jambo ufanye uchunguzi wa kina na ufahamu cha kweli kipi na cha uwongo kipi, la sivyo unaweza jikuta katika matata mazito, hasa kama unafanya mambo kishabiki. Pia nimnukuu mdau mmoja kwenye blog moja: "kama kweli hii familia inasingiziwa, nadhani litakuwa ni jambo baya sana kutendewa, lakini kama wanatuambia wanasingiziwa na habari ni nyingine basi tukae na kutazama mchongo mzima unavyokwenda.."