Liverpool na laana ya ubingwa wa EPL

Aug 23, 2019
22
19
Nilipata kuandika ....
LIVERPOOL
NA LAANA YA UBINGWA WA EPL
NA
NIHZRATH NTANI JNR.
Ni Jumamosi moja jioni. Naam! ni jioni ile ya Jumamosi ya April 28, 1990. Historia ninayoizungumzia hivi leo ni ya miaka 29 iliyopita. Mwanaume mmoja mwenye umri kati ya miaka 45 hadi 55 ,akionekana mwenye akili timamu.
Macho yake yalikuwa yakiitazama milingoti miwili lilipo lango la Liverpool.
Ni katikati ya milingoti hii miwili. Pande la mtu kweli kweli, mwanaume mwingine angali akiwa amesimama mahala hapo.
Hapa ni dimbani Anfield. Mwanaume huyu aliyesimama kati kati ya milingoti hii miwili ni Bruce Grobbelaar. Huyu ni golikipa wa Liverpool jioni hii. Siku moja historia kuhusu Bruce Grobbelaar nitaandika .
Macho ya mwanaume huyu mwenye umri unaokadiriwa kati ya miaka 45 hadi 55 yalikuwa yameganda kumtazama Bruce Grobbelaar jioni hii.
Magoli mawili kutoka kwa Ian Rush na John Barnes dhidi ya Queens Park Rangers yaliihakikishia klabu ya Liverpool kutwaa ubingwa wa Ligi daraja la kwanza ya Uingereza( Sasa inatambulika kuwa ni Ligi kuu ya Uingereza) Huo ulikuwa ubingwa wao wa 18. Furaha iliyoje.
Ni katikati ya sherehe, mwanaume yule akamfata Bruce Grobbelaar na kumwambia ;
"Liverpool haitaweza kutwaa tena taji la ligi kuu ya Uingereza"
Bruce akayasikia maneno haya yakipenya katikati ya ngoma ya masikio yake. Mwishowe akayapuuza.
Mwaka mmoja baadae yaani 1991. Bruce Grobbelaar akakutana tena na mtu huyu usiku mmoja ndani ya klabu ya starehe ya Carven iliyoko katika mtaa wa Mathew jijini Liverpool.
Ajabu ilioje! Kauli ya mtu yule ikawa ni ile ile kuwa ; Liverpool haitoweza kutwaa tena taji la EPL.
Mtu huyu kwanini anayasema maneno haya? Kwahiyo; Ameipa laana Liverpool. Je Jambo lipi baya amefanyiwa mtu huyu na Liverpool?. Kwanini aipe laana Liverpool?.
Je ni nani mtu huyu? Ni mtu mmoja asiyejulikana na hakuna anayejua jina lake hadi hivi leo. Huzuni ilioje!
IMEPITA MIAKA 28 SASA
Kila kitu kimebadilika katika historia ya soka la Uingereza. Wakati Liverpool ina mataji 18 ya ligi kuu ya Uingereza. Manchester United ilikuwa na mataji saba pekee miaka 28 iliyopita.
Huku klabu iliyokuwa inamfuatia Liverpool kutwaa mara nyingi ubingwa wa EPL ilikuwa ni Arsenal. Wakiwa wamefanya hivyo mara tisa kabla ya mwaka 1990.
Miaka 29 baadae. Historia imebadilika katika soka nchini Uingereza. Mashabiki wengi wa soka wenye umri chini ya miaka 30 bado wangali wakiitazama klabu ya Liverpool kama klabu inayopambwa mno.
Huku ikijivunia zaidi historia kuliko uhalisia wake. Wanayo haki ya kusema hayo.
Wakati huu nchini Uingereza ni Manchester United ndio klabu inayohesabika kuwa yenye mafanikio makubwa kuliko klabu yoyote.
Katika miaka 28 ya Liverpool ya kushindwa kuleta taji la EPL, Anfield. Manchester United wamefanya hivyo mara 13 na kuwa jumla ya mataji 20 ya EPL.
Ni katika kipindi hicho. Tumeshuhudia vilabu vya Chelsea, Arsenal na Manchester City mbali na Manchester United zikitwaa ubingwa wa EPL zaidi ya mara mbili kila mmoja. Huku kukiwa hakuna ubingwa kwa Liverpool. Inasikitisha.
KWANINI BRUCE GROBBELAAR ANAAMINI LIVERPOOL INA LAANA NA UBINGWA WA EPL?
Angali bado na kumbukumbu za mtu yule hadi hivi leo. Bado angali anaisikia kauli ile. Wakati ule aliyachukulia maneno yale kwa namna ya mzaha na kisha akayapuuza. Miaka 28 baadae ,Bruce anayaamini maneno yale. Bruce anakubali kabisa kuwa kuna Laana Liverpool. Kwanini anaamini jambo hili?
Ndani ya miaka 28 iliyopita. Liverpool ilikaribia kutwaa taji hili la EPL mara mbili na mara zote iliishia kulitazama taji likienda kwa wapinzani wao kiajabu kabisa. Ni wakati gani walikaribia kutwaa taji hili?
Ni msimu wa 2008/2009 chini ya mhispania Rafa Benitez, Liverpool ilikosa taji katika mechi chache za mwisho.
Ila kichekesho zaidi ulikuwa ni msimu wa 2013/2014. Ulikuwa ni kama maajabu ya soka yakitimia. Imani ya kuwa na laana ikaonekana hapa.
Baada ya kulikosa taji katika msimu wa 2008/2009. Matumaini ya liverpool kutwaa taji la EPL yakarejea tena msimu huu chini ya kocha Brendan Rogers.
Ni msimu huu, ndoto ya Ubingwa iliyeyuka mithili ya mtu anayezama majini huku nyote mkishuhudia.
Zikiwa zimebakia mechi tatu tu ligi kumalizika msimu huo. Liverpool ilikuwa kileleni kwa tofauti ya alama tano dhidi ya Manchester City.
Baada ya mechi tatu kumalizika. Liverpool wakaishia nafasi ya pili huku mashabiki wengi wa soka wakipigwa na butwaa wasiamini kilichotokea.
Ni kitendo hiki kikaipa uzito kauli ya mwanaume yule kuwa Liverpool imelaaniwa. Kwanini usiamini katika moja ya maajabu ya kushangaza ?
Jambo lingine ni kuwa; Kwa miaka 15 iliyopita. Klabu yoyote inabakia kuwa kileleni mwa ligi katika kipindi cha krismasi na mwaka mpya mwishowe inakuja kuwa Bingwa wa nchi hiyo.
Hadithi na historia hiyo huenda huwa ni tofauti inapokuja kuhusu klabu ya Liverpool. Wamefanya hivyo mara mbili na mara zote haikuweza kutwaa taji hilo.
JURGEN KLOPP ATAWEZA KUVUNJA LAANA HII?
Sote tunatazama mbio zao kwa umakini mkubwa. Mpaka muda huu Liverpool wangali kileleni kwa tofauti ya alama mbili tu huku akiwa mbele ,mchezo mmoja dhidi ya mpinzani wake Manchester City.
Kimahesabu ni ngumu kwa Liverpool kutwaa Ubingwa ila katika soka lolote linaweza kutokea. Sala za mashabiki wa Liverpool kwa wakati huu ni kuiombea Manchester City ipoteze pointi.
Kwenye karatasi Manchester City amebakiza mechi ngumu kuliko Liverpool. Katika mechi sita zilizobakia za liverpool.
Wamebakiza dhidi ya Southmpton, Chelsea, Cardiff, Huddersfield, Newcastle United na mwisho Wolverhmpton.
Huku wapinzani wao Manchester City wakibakisha mechi saba dhidi ya Cardiff, Crystal Palace, Tottenham, Manchester United, Burnley, Leicester City na mwisho ni dhidi ya Brighton.
Manchester City inaonekana ana mechi ngumu zaidi kuliko Liverpool lakini je Liverpool inaweza kufuta laana hiyo? Mashabiki wengi wa Liverpool wangali na hamu ya kuiona klabu yao ikitwaa ubingwa wa EPL kuliko ule wa Ulaya.
Kama liverpool ikishindwa kutwaa Ubingwa wa EPL msimu huu bila shaka, laana hii ingalipo.Tusubiri



CREDIT : Nihzrath Ntani Jrr
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom