SIKU moja baada ya Serikali kumkingia kifua Mbunge wa Bariadi Mashariki (CCM), Andrew Chenge ili asishtakiwe kwa rushwa katika mchakato wa ununuzi ya rada, Chadema imeweka hadharani kurasa 11 za ushahidi inaodai kuwa unaweza kumtia hatiani Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani wa Serikali kama atashtakiwa.Ushahidi huo uliotolewa jana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, ni ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Shirika la Upelelezi la Makosa Makubwa ya Jinai la Nchini Uingereza (SFO).
Kwa mujibu wa Dk Slaa, ukurasa wa tano wa ripoti hiyo, unaeleza jinsi Chenge alivyoshinikiza utekelezwaji wa mkataba huo na namna alivyofaidika kwa malipo ya kitita cha Dola 1.5 milioni kupitia akaunti ya Benki ya Barclays iliyoko katika kisiwa cha Jersey nchini Uingereza.
"Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kati ya mwaka 1995 na 2006. Katika kipindi hicho, BAE na SPS walikuwa wakifanya majadiliano ya ununuzi wa rada kwa ajili ya Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam na Chenge alihusika moja kwa moja katika mchakato huo hasa kushinikiza ununuzi huo," alisema Dk Slaa akinukuu waraka huo alioutoa pia kwa waandishi wa habari.
Aliendelea,"Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilitakiwa kutoa maoni na kuthibitisha malipo hayo na bila Chenge kukubali, kusingeweza kufanyika chochote."
Kinachofanywa sasa ni mpango wa makusudi wa Serikali ya CCM ambayo imeanza taratibu ya kuwasafisha watuhumiwa wa ufisadi kabla ya kufanyika kwa vikao vya chama hicho,alisema Dk Slaa.
Lissu: Chenge akishtakiwa hatoki
Kutoka Dodoma, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tindu Lissu amesema iwapo Watanzania wataamua kumshitaki Chenge, atatiwa hatiani mara moja kwa sababu ushahidi uliopo hawezi kuukabili.
Alisema kwamba anatambua wazi kuwa barua hiyo ya SFO, Serikali inayo.
"Barua hiyo mimi nimeipata kutoka huko serikalini, wao wanasema niwapelekee, siwezi kufanya upumbavu wa namna hiyo," alisema Lissu akisisitiza:
"Limeshindikana hapa bungeni kwa sababu Serikali inamkingia kifua. Sisi hatuna haja ya kuendelea kujisumbua. Sasa tumeamua tutaingia mitaani maana huko ndiko waliko walioumia kutokana na ufisadi huo," alisema Lissu.
"Lakini kwa hakika leo hii Chenge akifikishwa mahakamani ni kitanzi tu," alidai Lissu ambaye ana taaluma ya sheria akimanisha kuwa ushahidi wa SFO unaweza kumtia hatiani.
Kuhusu kuwepo kwa ushahidi unaotosheleza, Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema kuwa barua hiyo iliyoandikwa na SFO kwenda kwa Mwanasheria wa Serikali Machi 21, 2008, inaonyesha wazi jinsi fedha zilivyolipwa kwenye akaunti ya Chenge iliyopo katika kisiwa cha Jessy.
Alidai pia kuwa barua hiyo iliyosainiwa na Msimamizi wa Kesi za SFO, Mathew Cowie ilieleza jinsi sehemu ya fedha hizo zilivyotolewa na kupewa mtu mwingine anayefahamika kwa jina la Idriss Rashid.
Mbunge wa CCM achukizwa kauli ya Chikawe
Wakati Lissu akisema hayo, Ally Mohamed (Nkasi Kaskazini-CCM), alisema juzi hakupata usingizi kutokana na hasira alizopata baada ya kuchukizwa na kauli ya Chikawe kuwa Serikali haina ushahidi wa kumshtaki Chenge.
Wakati akifanya majumuisho wa bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mahusiano na Uratibu, Chikawe alisema uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru) unaonyesha hakuna Mtanzania aliyehusika na ufisadi wa ununuzi wa rada isipokuwa Waingereza watatu.
Source: Mwananchi