Tanzania Daima
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaendesha nchi kibabe bila kuheshimu uhuru wa mahakama.
Akihutubia mkutano wa hadhara juzi katika viwanja vya Kiwalani, Dar es Salaam, baada ya kuwashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kuwachagua Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kupitia CUF, Profesa alisema CCM imeshindwa kuonyesha demokrasia kwa vile imekuwa ikiingilia mambo mengi ya kisheria.
Lipumba alisema Mahakama Kuu iliamua kuwepo na mgombea binafsi lakini kutokana na uoga CCM imekataa kwa vile inahofia kupoteza madaraka.
Kama kungekuwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) huru na yenye haki hata chaguzi ndogo sita zilizowahi kufanyika ilitakiwa mgombea binafsi aruhusiwa kugombea! alisema Lipumba.
Kuhusu suala la ufisadi, alisema anashangazwa na jinsi wabunge wachache waliojiita wapambanaji walivyoshindwa kumaliza suala la kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond hadi Bunge kuamua kufunga mjadala huo.
Kuhusu sakata la rada, Profesa Lipumba alisema aliyekuwa Waziri wa Miundombinu Andrew Chenge ndiye anayehusika lakini katika hali ya kushangaza ameendelea kushika madaraka ndani ya CCM badala ya kufikishwa mahakamani.