Mbeya: RC Juma Homera amsafishia njia Dkt. Tulia 2025, asema watamlinda kwa mvua na jua

TikTok2020

JF-Expert Member
Oct 20, 2022
1,780
3,067
Dar es Salaam. Kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera inayoweza kutafsirika kama anamsafishia njia ya kuja kushinda ubunge Dk Tulia Ackson, imeibua mjadala unaoshinikiza marekebisho ya kuwabana watendaji wa Serikali kutumia madaraka yao kinyume na Katiba.

Dk Tulia ambaye ni Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini, alifanya ziara jimboni kwake Novemba 11 baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27, 2023 nchini Angola.

Alichosema Homera
Homera aliyeshiriki mapokezi ya Dk Tulia, alitoa kauli hiyo iliyozua mjadala kwa baadhi ya watu juzi katika viwanja vya Ruanda Nzovwe ambako ulifanyika mkutano wa mapokezi

Alisema hawako tayari kurejea kipindi cha miaka 10 iliyopita na watamlinda Dk Tulia kwa mvua na jua.
“Mbeya tuko vizuri na mimi ndiye mwenye Mkoa, nitahakikisha hakuna mtu atakayeleta uvunjifu wa amani 2025, Dk Tulia hakuna haja ya kuchukua fomu,” alisema.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi jana kufafanua kuhusu kauli hiyo, Homera alisema kauli yake aliitoa akiwa na kofia ya mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa huo.

“Mimi ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa, tuna uwezo wa kupambana mpaka akashinda kwa sababu ni mbunge wa CCM na mimi ni mwana CCM.

“Si uliona hata M-NEC (mjumbe wa Halmashauri Kuu)(Ndele Mwaselela) alizungumza pale? Kwa hiyo ni suala la sisi sote kuunganisha nguvu kuhakikisha kuwa anashinda uchaguzi wa 2025,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya baadhi ya vyama vya upinzani kuhusu wakuu wa mikoa kutumia nafasi zao kuwahujumu katika chaguzi, Homera alikanusha jambo hilo..

“Siwezi kuelekeza Jeshi la Polisi kwa sababu pale tunazungumzia siasa tu hatuzungumzii vyombo vya dola.
‘‘Vyombo vya dola mwenye mamlaka ni Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mimi sina mamlaka navyo,”alisema.

Juhudi za kuupata uongozi wa CCM kuzungumzia mchakato wa CCM kumpata mgombea wake kupitia kura za maoni, hazikufanikiwa baada ya uongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa, kukataa kuzungumzia suala hilo wala hata kutajwa gazetini.

Wakosoa kauli
Kauli hiyo imekosolewa na Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale akisema kauli hiyo isitiliwe maanani na wananchi wa Mbeya.

“Kauli hiyo haipendezi kwa kiongozi anayekaa kwenye ofisi za umma, kama anaamini atatumia njia ambazo sio sahihi CCM kupata ushindi, sisi kauli yetu ni kuwa uchaguzi hautafanyika nasisitiza uchaguzi hautafanyika,” alisema.

Alisema Chadema hawana ugomvi na Spika Tulia, bali kwa viongozi wa chama na Serikali kutokana na matamshi yao dhidi ya vyama vya upinzani kushiriki uchaguzi Mkuu 2025.

“Kama uchaguzi utakuwa wa demokrasia huru na Dk Tulia akapita, tunaahidi kama Chadema tutamuunga mkono kwa moyo mmoja katika kuleta maendeleo kwa jimbo la Mbeya Mjini na sio kauli za viongozi kutumia utashi wao binafsi,” alisema.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Profesa Abel Kinyondo alisema kauli hiyo inakumbusha umuhimu wa mapitio ya kikatiba ili kuondoa maeneo yanayoendelea kuimarisha mfumo wa chama kimoja kikatiba.

“Lakini hii kauli sio dalili nzuri kiuchumi, inajenga jamii ya vijana kuamini uchawa unalipa, vijana wengi watajielekeza huko wakiamini ni njia rahisi na hivyo kuathiri hata wanaojituma,” alisema Profesa Kinyondo.

Profesa Mohammed Bakari kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema kauli hiyo pia inatafsiri wazi CCM kujiimarisha katika dola.

“Kwa sasa ni jambo gumu kuitenganisha CCM na Dola kwa namna yoyote, watumishi wengi ni makada wa CCM sio wakuu wa mikoa tu, na ilifanyika hivyo kimakosa tangu mwaka 1992 tulipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi,hata uteuzi unazingatia sifa ya ukada,”alisema Profesa Bakari.

Aliongeza:“Matokeo yake watendaji wengi wazuri wanapoteuliwa wanalazimika kuyumbishwa uhuru wao na wanalazimika kuwa makada, kinachotakiwa ni kufanya marekebisho ya kikatiba.’’

Chanzo: Mwananchi

Cc.Erythrocyte 😄
 
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom