Geo C Starfish

New Member
Jul 17, 2021
4
6
Mwaka 1961, taifa letu pendwa la Tanganyika lilipata uhuru kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza na kuamua kuanza safari yake ya kujitegemea katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na hata kisiasa.

Ilipofika mwaka 1964 Taifa liliamua kuungana na taifa lingine lililokuwa huru la Zanzibar na kufanya uwepo wa taifa moja liitwalo Tanzania. Muungano huo ukajulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lengo la yote hayo lilikuwa ni kuongeza nguvu na umoja wa kuendeleza chachu ya mabadiliko ya kimaendeleo ambayo kila taifa lilikuwa nayo katika nyanja zote muhimu kama maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasi.

Mabadiliko ni hatua na hatua inapokuwa zaidi ya moja huwa ni safari. Hivyo Jamhuri hii ya Muungano iliamua kuanza safari hiyo kwa kuweka mipango mikakati inayoweza kurahisisha umbali na ugumu wa safari hiyo. Safari ya Maendeleo.

Viongozi wakuu wa Jamhuri hiyo walitambua kuwa hakuna safari inayoweza kuitwa safari kama hakuna mwanzo inapoanzia safari hiyo na mwisho inapoishia safari hiyo. Yaani ni kichaa pekee ndiye anaeweza kusafiri bila kujua anatoka wapi na anaelekea wapi. Ila kwa mtu yeyote mwenye akili timamu, safari yake huwa ni lazima iwe na mwanzo na iwe na mwisho. Na hata kama ikitokea msafiri anasafari zaidi ya moja, ni lazima kwanza akamilishe safari ya kwanza yenye mwanzo na mwisho kisha ndio aanze safari ya pili yenye mwanzo ambapo ni hapo alipoishi kwa safari ya kwanza na mwisho ambapo ni kule anakoelekea kwa safari ya pili.

Hivyo safari hiyo ya maendeleo wakaipa mwanzo kwa kuweka vipaombele vya safari ambavyo vikikamilika inakuwa ndio mwisho wa safari hiyo na baada ya hapo labda ndipo waanzishe safari nyingine ya pili. Vipaombele hivyo vilikuwa ni "kupambana dhidi ya UJINGA, kupambana dhidi ya MARADHI na kupambana dhidi ya UMASIKINI". Ni dhahili waliamua kuanzia hapo safari hiyo ya maendeleo sababu walijua fika kuwa taifa lilikuwa katika hali mbaya kiuchumi na ili uchumi ukue ilihitajika nguvu ya wananchi ambao kwa bahati mbaya kwa kipindi hicho walikuwa wanateseka dhidi ya maadui watatu ambao ni Ujinga, Maradhi na Umasikini.

Hivyo mikakati thabiti ilianzishwa ili kuwashinda maadui hao hatari walioweza kukwamisha safari hiyo ya maendeleo.

Mikakati ilikuwa ni kujenga shule kwa wingi na kuanzisha mifumo bora ya kielimu ili wananchi wasome na kuepuka ujinga, kujenga hospitali kwa wingi na kuanzisha mifumo bora ya afya ili wananchi waepukane na maradhi na pia kuanzisha mifumo mbalimbali ya uzalishaji hasa katika sekta ya kilimo na biashara ili kupambana na umasikini.

Tangu kipindi hicho mpaka sasa ni takribani zaidi ya miaka 50 imepita. Na kinachosikitisha ni kuwa taifa mpaka sasa bado halijafika mwisho wa safari hiyo na zaidi ya yote hata zile njia na mikakati thabiti iliyokuwa imewekwa ili kufanikisha safari hiyo imeanza kusahauliwa.

Swali ni; "Lini tutafika?"
"Lini tutakamilisha safari hii iliyoanza tangu miaka 50 iliyopita?"
Wananchi bado wanateseka na ujinga, japo sio kwa kiwango kikubwa kama zamani lakini bado tumeshindwa kufikia kiwango cha mabadiliko ya utandawazi wa kidunia katika kutatua mambo mbalimbali ya kimaendeleo.

Wananchi pia bado wanateseka na maradhi kila kukicha licha ya kuwa zimejengwa hospitali na zahanati na hata vifaa na wahudumu kuongezeka zaidi ya zamani lakini ongezeko la watu pia na mabadiliko ya tabia-nchi na utandawazi yamefanya tushindwe kabisa kufikia kiwango kinachoweza kutufanya tuimalize safari hiyo.

Umasikini nao ndio bado tatizo sugu ambalo limegeuka kuwa rafiki kwenye maisha yetu ya kila siku kwani ni kawaida sana kumsikia mwananchi wa Tanzania akijiita Masikini bila hata kusita wala kuogopa. Umasikini umekuwa ni sifa ya kujivunia ya Watanzania.

Mengi tuliyonayo bado ni "asante mkoloni", kuanzia mifumo ya uongozi, uwajibikaji mpaka miundombinu na vitendea kazi. Kwa kifupi ni kuwa, tumeshindwa vita na maadui hao watatu na hii yote imetokana na;
Kushindwa kuwa na viongozi wanaoheshimu na kuona umuhimu wa safari ya maendeleo iliyoanzishwa na waasisi wa taifa, iliyoanzia kwenye mapambano dhidi ya maadui hao watatu.

Kushindwa kuwa na mikakati endelevu ya kupambana na maadui hao ili tuweze kukamilisha safari yetu tuliyoianza miaka zaidi ya 50 iliyopita.

Kushindwa kuwa na viongozi ambao wanania thabiti ya kusafiri na wananchi katika safari ya maendeleo na wengi wao kubaki wakipambania maisha yao na familia zao.

Kushindwa kuwa na lugha moja ya maelewano juu ya tunapoelekea na kujikuta kila mmoja akiwa na uelekeo wake.

Kukosa mitazamo, fikra na macho ya kuona mbali ili mbele ya safari yetu tusikutane na vikwazo vya kutukwamisha.

Ni aibu kwa taifa kama letu lenye umri wa zaidi ya miaka 50, lenye ardhi kubwa na nzuri ya rutuba inayofaa kwa kilimo cha kila aina na lenye mifugo na wanyama wa kila aina kuwa miongoni mwa mataifa ambayo asilimia kubwa ya wananchi wake hawana uhakika wa chakula hata cha siku moja. Ni aibu kubwa.

Viongozi wetu wakuu wanatuambia kuwa wanapambana kujenga UCHUMI WA NCHI kwanza kabla ya kufanya mambo mengine lakini wanasahau kuwa uchumi unajengwa na wananchi tena wananchi wasio na ujinga, wasio na maradhi na pia wasio masikini wala wasio na fikra za kuukubari umasikini.

Ndio maana waasisi wa taifa hawakuanza moja kwa moja kuujenga Uchumi bila kuwaondoa maadui hawa watatu. Viongozi wetu wametupeleka kwenye safari ambayo hatujui tutafika lini sababu hatujui tumeianzia wapi na tunaenda kuishia wapi. Kwa sasa kila kiongozi anatuongoza kwa vipaombele vyake binafsi na muda wake wa uongozi unapoisha anaechukua nafasi ya kuongoza nae anakuja na vyake badala ya kuendeleza vya aliyemuachia kiti.

Hivyo kusababisha tubaki kama vichaa tusiojua wapi tunatoka na wapi tunaenda. Yani ni vurugu mechi, huyu anaanzisha hiki, yule akija anakitoa na kuleta hiki, mwingine akija anafuta yote na kuleta mengine. Ujenzi wa kiuchumi huwa haufanyiki wenyewe bila vichochezi.

Vichochezi hivyo vinapoimarishwa ndipo Uchumi huanza kukua na kuimarika taratibu bila nguvu kubwa. Vichochezi hivyo ni kama mifumo bora ya kuongoza taifa (uongozi), mifumo bora ya kisheria, mifumo bora ya uzalishaji mali na biashara na mifumo bora ya kuihudumia na kuilinda jamii na mali zake. Na yote hayo yanahitajika kuwa katika mwongozo mkuu wa taifa ambao ni KATIBA MAMA ya nchi iliyoimara.

Ifike mahali tukubali kuwa tumekosea njia na tukae chini kupanga mikakati yetu ya safari kwa ustadi na ubora utakaodumu vizazi na vizazi. Tukubari kuwa zama zimebadilika na mifumo ya uongozi ni lazima ibadilike.

Tukubali kuibadilisha taswira ya nchi kwa kuibadilisha au kuirekebisha KATIBA MAMA ya nchi yetu kwa maendeleo yetu ya pamoja na sio ya mtu mmoja mmoja.

Tukubali kufunga mikanda huku tukiweka tahadhari ya kutubana.

Tukubari kuwa na vipaombele ambavyo vitafatwa na kila kiongozi ajaye ili vifanyike na kumalizika kisha ndipo vianzishwe vingine kulingana na uhitaji wa wakati huo.

Nchi iongozwe kwa kutekeleza miongozo maalamu ya kudumu iliyopo katika maandishi yasiyodharaulika, yaani mipango mikakati ya taifa.

Hapo naamini tutafika mwisho wa safari yetu ya kwanza na tutaanza safari nyingine bila mashaka.

Mungu ibariki Tanzania.
 
Back
Top Bottom