Simulizi zinasema kuwa kuna watu waliwahi kupachezea na kuzindika mambo yao mahali hapo. Ndiyo maana kuna mambo ambayo ukifanya kinyume, yanakurudia mwenyewe kwa namna mbaya sana.
Usiku giza linapoingia na watu wanapoenda kulala, mizimu huamka na yale maroho huanza kazi zake. Kuna simulizi pia za watu kupelekewa moto vibaya sana. Haya yalitokea zaidi kipindi kile kabla ya yule wa mwisho kuondoka. Wanasema kipindi hicho hakukuwa na kulala kabisa.
Hata hivyo, location yenyewe inaweza kuwa tatizo kubwa. Pale ni kama madhabahu takatifu; ukikipapasa vibaya kidogo tu au kukinajisi, basi vile viumbe vikichoka kukaa kwenye maji makuu huja pale ufukweni kwao kubarizi.
Hiyo midude, wanasema haina mzaha, hasa kuanzia saa saba mpaka saa tisa. Ni kama eneo lote linachukuliwa kwa muda fulani hakuna kutoka, ila kuingia ni ruksa.
Niliwahi kuishi nyumba ya aina hiyo huko Tanga. Wenyeji waliniambia, “Hapo pazito, usipaone kama kawaida. Hakikisha hupachafui kiroho. Na siku ukienda kuchafuka nje, hakikisha unajitakasa kabla ya kuingia ndani.”
Siku moja ya weekend nikapita chocho moja lenye mitungi na mikasi. Nikajifurahisha nafsi mpaka karibu siku inapinduka ndipo nikarudi nyumbani. Bahati mbaya nikajisahau kujitakasa.
Nikaingia ndani, nikatia komeo, nikajilaza fofofooo foool!
Saa nane usiku nikastuka ghafla. Nikakuta chumba chote kimejaa mwanga. Nikacheki taa—haikuwa imewashwa. Nikadhani labda ni wenge la mitungi tu. Kabla sijakaa sawa, ule mwanga ukapotea, nami nikahisi wazi kabisa kuwa pale chumbani (sio kitandani) sikuwa peke yangu.
Vituko vilivyoendelea kuanzia hapo mpaka alfajiri, kabla ya adhana ya kwanza, sitakaa nisahau kamwe.
Hapa palipo sasa pamechafuliwa na kunajisiwa vibaya sana. Si mahali pasafi tena, wala hapana utukufu. Yale madude tayari yamefanya hapo kuwa kiwanja chao cha kudumu, na mizimu imeruhusu. Hivyo ni mahali hapakaliki, hapalaliki!
Falme mbili haziwezi kukaa pamoja—ufalme wa nuru na ufalme wa giza lazima zipigane. Ukivaa joho jeupe nje lakini ndani umejaa uvundo, lazima usande.
Wapangaji waliotangulia walitumia damu kubwa kwa uchache na kwa uangalifu mkubwa, ndiyo maana walivumiliwa kwa kiasi fulani. Lakini washauri wabaya na vipotoshi waliodai itumike damu kubwa kwa wingi wameharibu kila kitu kabisa.
Sasa miungurumo, miito, vilio na taswira za wenye damu zao zinawaandama kila wanapokanyaga pale. Panatisha sana, na kuogopesha kupita kiasi.
Ukimuona baba ameondoka kwenye nyumba yake, hata kama ni ya kupanga, akaenda kuishi uswazi kwenye nyumba ndogo—wakati mwingine usimkejeli. Muonee huruma. Ana mambo mazito na magumu moyoni.
Good morning, Tanganyika!