Kwa nini Mlima Kilimanjaro uko Tanzania na si Kenya?

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
mihangwa.jpg


NASAHA ZA MIHANGWA

Joseph Mihangwa Toleo la 314 4 Sep 2013


314_kili.jpg



MPAKA wa Tanzania na Kenya ni wa ajabu na ni wa kushangaza pia. Tofauti na mipaka mingine ya nchi yetu upande wa Mashariki, Kusini na Magharibi, Mpaka huo wa Kaskazini umechorwa kwa mstari ulionyooka kana kwamba ulichorwa kwa msaada wa rula kuanzia Bahari ya Hindi, kuelekea Kaskazini hadi Ziwa Victoria.

Kwa jinsi ulivyoanza, mstari huo ulipaswa kwenda moja kwa moja Kaskazini Magharibi, na kuutupa nje Kaskazini Mlima Kilimanjaro uwe ndani ya Kenya, badala ya kuwa Tanzania ilivyo sasa. Lakini, pengine kwa sababu maalumu, mchoraji aliupaisha juu Kaskazini zaidi makusudi ulipokaribia Mlima huo, kisha ukapinda tena kuelekea Kaskazini Magharibi kwa unyoofu ule ule, kuhakikisha kwamba Mlima wote unakuwa ndani ya Tanzania badala ya Kenya; na kuendelea hadi Ziwa Victoria kwa kunyooka vivyo hivyo.

Kwa nini, nani kitu gani hasa kilimfanya mchoraji wa Mpaka huo kupindisha mstari huo kufanya Mlima Kilimanjaro uwe nchini Tanzania, badala ya kuwa nchini Kenya?


Mnyukano wa Wajerumani na Waingereza

Kuna dhana inayovuma kwamba, Malkia wa Uingereza, Victoria; alimpa zawadi mjukuu wake, mtawala (Emperor) wa Ujerumani, Wilhelm Mlima huo mwaka 1886, kwa sababu mjukuu huyo alipenda vitu vikubwa. Dhana hii si sahihi kwa sababu mwaka huo, Wilhelm hakuwa mtawala wa Ujerumani, bali Babu yake. Lakini jibu sahihi linatokana na Mataifa ya Ulaya kugombea Afrika (Scramble for Africa), mnyukano uliokamilishwa na Mkutano wa Berlin kwa mataifa hayo kukaa meza moja kuchora mipaka (partition) kuigawana Afrika.


Mnyukano huo ulishika kasi ya kutisha katikati ya miaka ya 1880, Uingereza ikiongoza na kufuatiwa na Ufaransa; huku Ujerumani nayo ikijikakamua kutoachwa nyuma katika kuwania makoloni.

Desemba 4, 1884, Sultani Mangungu wa Usagara (Msovelo) alisainishwa Mkataba wa “Urafiki” na Jasusi la Kijerumani, Karl Peters, bila kujua kwamba alikuwa anauza nchi yake kwa Wajerumani na kuitwa “Deutch –Ostafrika”, yaani “Afrika Mashariki ya Wadachi/Wajerumani” na kuimilikisha Kampuni ya Kijerumani iliyojulikana kama “German East African Company” (GEAC).

Februari 1885, Karl Peters aliomba ulinzi wa Kampuni yake kwa Kiongozi wa Ujerumani (Emperor), Bismarck, na kupewa barua ya kukubaliwa (Imperial Letter of Protection) kupata ulinzi wa maeneo (nchi) yote yaliyochukuliwa na GEAC upande wa Bara Magharibi mwa Dar es Salaam, na maeneo ya Uzigua, Ukaguru na Usambara ambako machifu 10 wa maeneo hayo walisaini Mikataba “kumuuzia” nchi zao bila kujua.

Ilichotaka GEAC ni kupata njia huru na Bandari kwenye Bahari ya Hindi, na hivyo kuzua mgongano na Sultani wa Zanzibar aliyeshikilia Pwani yote, kutoka Somalia upande wa Kaskazini hadi Rasi Delgado (Msumbiji) upande wa Kusini; na pia Bara yote iliyokuwa njia ya misafara ya Watumwa hadi Maziwa Makuu.

Na pale Sultani Sayyid Barghash alipoonesha jeuri ya kutokubali matakwa ya Wajerumani, Manowari ya kivita ya Kijerumani ilitia nanga Bandari ya Zanzibar na kuelekeza mitutu ya mizinga kwenye Kasri lake, naye akasalimu amri hima. Wakati huo Zanzibar ilikuwa chini ya usimamizi na ulinzi wa Uingereza (British Protectorate) kwa Mkataba maalumu.

Kuona hivyo, Februari 26, 1886, Waziri Mkuu wa Uingereza wa wakati huo, Lord Salisbury, aliingilia kati akiamini kwamba, haki za Zanzibar juu ya eneo lote la Pwani zilikuwa wazi, ingawa hakuwa na uhakika juu ya ukomo wake Kaskazini (Somalia?), lakini alifikiri umbali wa maili 60 ulimtosha Sultani. Alijua kuwa, himaya ya Sultani ilijumuisha pia Wilaya za Kilimanjaro na Uchagani; alisema: “Eneo lote la Wilaya ya Kilimanjaro kamwe haliwezi kuwa chini ya ulinzi wa bendera nyingine (mbali ya Sultani au Uingereza) bila kuathiri maslahi ya Uingereza”.



Wababe wote walikuwa na mikataba


Ni kwamba, Waingereza, Wajerumani na Sultani mwenyewe, wote walikuwa na mikataba waliyoingia na Machifu wa Kichaga kutambua himaya za wababe hao, kama tu alivyofanya Chifu Mangungu. Mmoja wa Mikataba ya Machifu hao 25 na Sultani, uliotiwa sahihi Mei 30, 1885, ulisomeka hivi:


“Sisi Masultani (machifu) wa Uchagani na Kilimanjaro, tunaapa mbele ya Jenerali Mathews na Askari wake na Wafuasi, kwamba, tunatambua kuwa (sisi) ni watawaliwa wa Mtukufu Sultani wa Zanzibar, na hivyo tunapeperusha bendera yake juu ya minara nchini mwetu kuthibitisha utii wetu kwake, na kuwa,tunamtambua kama mtawala/mfalme wetu”.


Mkataba huo wa pamoja ulitiwa sahihi (dolegumba) na Machifu Mandara wa Moshi, Kitungeti wa Kirua; Marealle wa Muranju (Marangu), Mitanuvi wa Mamba, Fumba wa Kilema, pamoja na Machifu wa Machame, Rombo, Taveta na wengineo.


Mandara alitia sahihi Mkataba mwingine kama huo na Mjerumani wa GEAC, Dakta Karl Juhlke, Juni 11, 1885, kumpa mamlaka yote na haki ya kuchukua na kutumia ardhi, kutoza kodi na ushuru, pamoja na kuanzisha utawala wake na Mahakama; kuvuna Mlima Kilimanjaro, Mito, Maziwa na Misitu yote.


Kubadilishana na haki hizo, Mandara alihakikishiwa ulinzi, yeye na mali zake, pamoja na elimu kwa watoto wake. Akitoa shukrani kwa Dakta Juhlke na GEAC, Mandara alisema: “Nawapenda sana Wajerumani kuliko mataifa mengine yote; zaidi kuliko Waingereza hasa, nani kwako pekee (wewe Juhlke) nitatoa nchi yangu”.


Hatimaye, baada ya kubaini kwamba alikuwa njia panda, Mandara alilalama akisema: “Sultani wa Zanzibar anataka nchi yangu; Wajerumani, vivyo hivyo nao wanataka nchi yangu; ninyi (Waingereza) mnataka nchi yangu pia! Aitakaye nchi yangu atakiona cha mtema kuni”. Hakutaja aina ya “cha mtema kuni” hicho.



Tume ya maridhiano yaundwa


Kutokana na kindumbwendumbwe hicho, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ziliunda Tume ya Maridhiano kubainisha mipaka kwa kuzingatia maeneo ya ushawishi wa nchi hizo kuepuka ugomvi, lakini Sultani hakushirikishwa.


Mijadala ndani ya Tume ilikuwa mikali, kila mshiriki akivutia upande wake. Mwakilishi wa Ujerumani alitaka kutumia Bandari ya Dar es Salaam iliyokuwa chini ya himaya ya Sultani, bila kutozwa kodi.


Pili, alitaka Sultani apunguziwe eneo la himaya upande wa Pwani ili abakie na urefu wa maili kumi tu; pia kwamba, madai ya Sultani huyo juu ya eneo la Kilimanjaro yasitambuliwe.


Tatu, Ujerumani ilitaka kampuni zote za Uingereza zilizokuwa eneo la Kilimanjaro ziondoke na zikubali kulipwa fidia ili Mjerumani ashike eneo lote hilo.


Kwa GEAC, Kilimanjaro lilikuwa jambo la kufa na kupona, na ilikuwa tayari kwa lolote kutoiachia; kama ambavyo tu Zanzibar ilivyokuwa muhimu kisiasa na kiuchumi kwa “Emperor” Bismarck wa Ujerumani kiasi kwamba, nchi hiyo ilikuwa na Ubalozi mdogo Visiwani humo tangu mwaka 1884 kuonesha umuhimu huo.


Uingereza na Ufaransa zilionesha kuunga mkono madai ya Sultani dhidi ya matakwa ya Ujerumani. Kwa kupewa ujasiri na msimamo wa nchi hizo, wakati mazungumzo yakiendelea, Sultani alituma kikosi chenye Askari 200, kikiongozwa na Jemedari wa Kiingereza, Jenerali Mathews, kwenda eneo la Kilimanjaro kusimika bendera nyekundu ya himaya yake. Wakati wakirejea, walipambana na Kikosi cha Wajerumani karibu na Taveta, kilichofika huko kwa madhumuni hayo hayo; mapigano yakazuka, lakini yakakoma sawia kwa maelekezo ya Tume ya Maridhiano iliyokuwa ikiendelea na kikao.

Wakati huo huo, Mwakilishi wa Uingereza, Sir Percy Anderson, alikuja na wazo la kati katika kutatua ugomvi wa Ujerumani na Uingereza kuhusu eneo la Kilimanjaro, la kuligawa sehemu mbili kuwapa Wajerumani nusu ya upande wa Kusini, na nusu ya Kaskazini wapewe Waingereza.

Pendekezo hilo lilipingwa vikali na Wajerumani kwa madai kwamba isingekuwa rahisi kuligawa hivyo eneo hilo lenye mlima na vilima, hivyo wakasisitiza wapewe eneo lote peke yao. Sir Percy alitupa hoja yake kutafuta suluhu mbadala.


Mombasa yatibua mambo


Ikazuka hoja kuhusu nani adhibiti Mombasa (bandari) ambayo ilikuwa chini ya himaya ya Sultani, lakini yenye kuwaniwa vikali na Uingereza na Ujerumani pia. Wajerumani walitaka wawe na Bandari Pwani ya eneo hilo na (iwe) njia fupi kuufikia Mlima Kilimanjaro kwa urahisi, na kwamba, Mombasa ulikidhi madhumuni haya kwavile ulikuwa katikati ya maeneo ambayo Ujerumani ilikuwa ikiwania upande wa Kaskazini na Kusini.

Waingereza hawakuwa tayari kupoteza Mombasa, kufa na kupona; kama ambavyo tu Wajerumani hawakuwa tayari kupoteza Kilimanjaro. Jemadari wa Kiingereza, Luteni Kanali Kitchner, tayari alikuwa ameshinikiza kukamatwa kwa Mombasa ili kiwe Kituo cha Manowari zakivita za Uingereza na ghala kuu la silaha katika bahari ya Hindi.

Nao wafanyabiashara na Wamissionari wa Kiingereza,walioweka vituo na Makao Mombasa, hawakutaka Serikali yao kuachia bandari hiyo pamoja na njia za biashara “kuangukia kwenye udhibiti wa Taifa shindani” kwani, kwa maoni ya Sir Percy, Uingereza ingekosabarabara ya uhakika hadi Ziwa Victoria “unakoanzia Mto Nile,na hivyo kuwa vigumu kuifikia Sudani ya Chini”. Kufikia hapo, mazungumzo yaligota na hali ya kutoaminiana kutawala.



Mpaka mpya: Taveta hadi Victoria


Ili kukidhi matarajio yake, Sir Percy aliwasilisha pendekezo la pili, la Mpaka unaoanzia Kusini mwa Mombasa kuelekea Taveta, kisha unapanda juu sehemu ya Kaskazini mwa Kilimanjaro (kuuingiza ndani mlima huo), na kuambaa hadi Mashariki mwa kingo za Ziwa
Victoria, kama unavyoonekana leo.


Kwa pendekezo hili la pili, Ujerumani iliamua kuachia Mombasa na kukubali kutia sahihi Mkataba wa makubaliano kwa kuridhika kwamba maeneo Kusini ya mpaka huo yaliyobakia mikononi mwake, yalikidhi kiu yake ya makoloni kufanya ijishughulishe kwa muda mrefu uliofuata.


Mkataba huo, uliofikiwa Novemba 1, 1886, ulielezea mpaka huo ifuatavyo: “Mstari wa Mpaka unaanzia kwenye mdomo wa Mto Wanga au Umbe,unakwenda moja kwa moja hadi Ziwa Jipe; unapita upande wa Mashariki mwa Ziwa na kupinda tena upande wa Kaskazini kabla ya kuvuka mto Rumi; kisha unachana katikati ya nchi ya Taveita (Taveta) na Uchagga; unaambaa chini ya kitako cha Mlima Kilimanjaro kwenda juu kuelekea Kaskazini; kisha unanyooka tena moja kwa moja na kutua upande wa Mashariki wa kingo za Ziwa Victoria Nyanza”.


Huo ndio ufafanuzi kwa maneno ya kidiplomasia, wa Mpaka kati ya Tanganyika (wakati huo ikiitwa Deutch – Ostafrika) na Kenya uliopo hadi leo. Chini ya makubaliano hayo, Ujerumani, kupitia Kampuni ya GEAC, ilijipatia Mlima Kilimanjaro na kupoteza Mombasa; na Waingereza kujipatia Mombasa na kupoteza Mlima Kilimanjaro.


Januari 1, 1891, maeneo yote ya GEAC yaliingizwa kwenye himaya ya Serikali ya Ujerumani kuruhusu uvamizi na uingiliaji kijeshi wa maeneo hayo,yakiwa tayari milki halali ya nchi hiyo.



Kutoka Deutch – Ostafrika hadi Tanganyika


Sultani wa Zanzibar kwa upande wake, alibakiziwa kipande cha urefu wa maili 10 tu za Pwani, ambacho miaka miwili baadaye, mwaka 1888, alikikodisha kwa Wajerumani kisha akapokonywa kwa nguvu mwaka huo huo na Wajerumani hao.


Wakati wa utawala wa Kijerumani, nchi yetu iliitwa “Deutch – Ostafrika”; na baada ya vita ya kwanza ya Dunia mwaka 1918, ambapo Waingereza walichukua nchi kutoka kwa Wajerumani, iliitwa “Tanganyika Territory”, jina lililopendekezwa na Mwingereza, Sir Cosmo Parkinson, kabla ya kuitwa kwa kifupi “Tanganyika” baada ya vita ya tatu ya Dunia, mwaka 1945.


Mipaka rasmi ya iliyokuwa “Deutch –Ostafrika” (Tanganyika), iliridhiwa Machi 22, 1921, kufuatia Mkataba wa amani uliofikiwa kati ya Uingereza na Ujerumani ambapo, kabla ya hapo, eneo lote la sasa la Kigoma na Biharamulo, lilikuwa chini ya Wabelgiji.


Kwa madhumuni ya mada hiini kwamba, Mlima Kilimanjaro upo Tanzania kwa sababu mji wa Mombasa uko Kenya, ikiwa ni matokeo ya minyukano ya mataifa mawili ya Kikoloni, Ujerumani na Uingereza. Na hilo hatuna nguvu nalo kwa kuwa historia sharti itawale.


Hapa tunapata fundisho pia; kwamba, Watawala wetu wa leo, wanaoingia Mikataba kimbumbumbu na kizembe na kina “Karl Peters” wa zama hizi,katika madini na ardhi, kama walivyofanya Chifu Mangungu wa Musovelo [Usagara] na Chifu Mandara wa Moshi; waelewe kwamba, wanatuweka rehani kwa wawekezaji hao chini ya ukoloni mpya, sisi na hatima yetu. Kwa sababu hii, tusishangae kuona siku mojatukivamiwa na wawekezaji hao, wakitumia majeshi ya nchi mama, pale tutakapoamka kutoka usingizini kudai ardhi rasilimali tunazoporwa. Huku ni kukaribisha historia kujirudia, kwa kilio na kusaga meno.






















- See more at: Raia Mwema | Gazeti la Tanzania lenye habari na makala mbalimbali
 
Hadi hii hoja kuingizwa JF;
Pia katika gazeti la Raia Mwema;
Kumetokea nini hadi kuhitajika ufafanuzi
Au ni kuwaweka sawa Watanganyika tu.
Mnaonaje na tukajua ni kwa nini Rwanda-Urundi zilitolewa Tanganyika,
Nini nafasi ya UK katika mgogoro wa Tanganyika na Malawi?

ni Uchokonozi tu.

Bazazi!
 
Mm mwenyewe nashangaa coz ni suala ambalo limekwa kwenye media na sijajua mantiki ya uwekaji wa hili suala au ndo kama ulivyosema kuwa kuna jambo linajadiliwa ama kuna ishu za kichochezi ambazo zinataka kuibuliwa kuhusiana na huu mlima!.
 
Uhuru kama kamuuwa mgombea mwenza Prof Saitoti wala hasiti kulalama mlima uwe wao, jamaa kwa tamaa ya utajiri sie
 
huu uzi kwanza ni mrefu sana, lakini hapo mwanzo tu pananifanya nijiulize maswali mengi sana....je umetumwa? , je wewe ni mkenya? au ndo wale wale mliozoeleka?
ngoja kinuke tu uone kama ICC watakuacha.
 
Hii inatufundisha kwamba si tu Chifu Mangungo wa Msovero aliyesaini mkataba asioujua bali wako wengine wa wakati huo (Chief Mandara, Kitungeti, Marealle) na pia wa wakati wetu sisi.
 
Kina Mangungo na Mandata waliingia mikataba kwa kufuatwa na wakoloni ilhali hawakuwa na elimu yoyote ile hata Sahihi waliweka kwa dole gumba. Sasa hivi imebadilika viongozi wenye elimu wao ndio wanaowafuata wawekezaji(wakoloni) na kuingia mikataba ya kipuuzi.
 
Back
Top Bottom