Kuzima intaneti ni kuminya haki za binadamu

Simon Martha Mkina

Investigative Journalist
Sep 5, 2020
20
107
Na Simon Mkina

MARA zote serikali zenye kuongozwa na watawala dhalimu duniani, huzima mtandao wa intaneti kwa madai makubwa matano; kuimarisha usalama wa taifa, kulinda uchaguzi, kuepusha vurugu, kuzuia udanganyifu kwenye mitihani na kukwamisha kusambaa kwa taarifa za uzushi.

Hata hivyo, madai yote haya hutolewa kwa sababu ya woga wa serikali hizo dhidi ya nguvu ya umma, kwani wananchi wanapogundua kudanganywa, serikali iliyoko madarakani uhofia uhai wake, hivyo njia rahisi ya kudhibiti nguvu hiyo ni kuwanyima mawasiliano na taarifa.

Ifahamike kuwa, katika dunia ya sasa, serikali dhalimu huogopa zaidi umma wenye kuwasiliana na kuwa na sauti moja yenye nguvu. Serikali nyingi hazitaki umma wenye taarifa sahihi; zinapenda watu wake wapate taarifa ‘zilizochujwa’ ama zisizokuwa sahihi na ‘nusu-nusu.’

Madai haya ya serikali hizo zinazoongozwa kiimla, yamezoeleka, hasa katika nchi za Pakistan, Indonesia, Iran, Iraq, Jordan, Kazakhstan na Myanmar.

Takwimu za Shirika la Access Now lenye makao yake makuu New York, Marekani linaeleza katika taarifa zake za hivi karibuni - kwamba mwaka 2019 na 2020, ulikuwa mbaya zaidi duniani baada ya nchi 78 kuzima mtandao wa intaneti kwa madai yaliyoainishwa hapa.

internet shutdown.PNG


Inaelezwa pia kwamba mwaka uliofuata wa 2021, India iliongoza dunia kwa kuzima mtandao wa intaneti mara nyingi zaidi kuliko nchi yoyote. Nchi hiyo inayotajwa kuwa bingwa wa teknolojia, ilizima mtandao huo mara 106, kati ya 182 – iliyoripotiwa kutoka nchi 81.

Kwa mara ya kwanza, Tanzania ikaonekana katika taarifa hiyo ya miaka miwili – 2019 na 2022, ingawa nchi hiyo ilizima mtandao huo na kukaa kimya. Serikali haikutoa madai yoyote kama nchi zingine zinavyofanya. Iliamua kuminya mawasiliano hayo kimyakimya.

Taarifa zinaeleza kuwa kuzimwa kwa mtandao huo nchini Tanzania kulitokana na sababu ya hofu, wakati nchi ikijiandaa na uchaguzi wake mkuu wa mwaka 2020, ambapo nguvu ya upinzani ilionekana kuimarika – tena ikikomazwa na matumizi makubwa ya mtandao wa mawasiliano na upashaji habari.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) wa wakati ule, James Kulaba, alikataa kuweka wazi sababu za kuzimwa kwa mtandao huo.

“TCRA haipo kwa ajili ya kuzuia watu kupata habari na kuwasiliana, bali kutoa fursa kwao kuwa na mtandao wenye uhakika wa intaneti na kuwa chanzo cha kuwaletea maendeleo,” alisema injinia huyo.

Pamoja na kushindwa kukubali kwamba mtandao wa intaneti ulizimwa mara kadhaa, lakini alikiri kwamba “endapo ilitokea hali hiyo, basi huenda mitambo ilikuwa katika matengenezo kwa muda.”

Intaneti ni haki, ni maisha

Kuzimwa mwa mtandao wa intaneti kwa Tanzania kulileta taharuki, siyo kwa viongozi na wanachama wa vyama vya siasa, kama iliyoelezwa na wachambuzi, bali kuna idadi kubwa ya wananchi ambao walikiri “kuvurugwa kwa maisha” yao.

Wananchi waliohojiwa walidai kuzimwa kwa intaneti kuliathiri mtitiriko wa shughuli zao za kuingiza kipato kila siku, kwani sehemu kubwa ilitegemea kuwepo kwa mawasiliano hayo.

Magayane John (29), msimamizi wa duka la huduma ya intaneti anayefanya shughuli zake eneo la Mwenge, Dar es Salaam, anakiri kwamba kuzimwa kwa mtandao wa intaneti kulimfanya akose mapato kwa siku nzima.

Anasema mapato yake ya Sh. 40,000 hadi 50,000 kwa siku, yalikosekana, hivyo kuharibu mtiririko wa kipato katika biashara yake. Katika duka hilo, Magayane ana kompyuta 12.

“Licha ya mimi kukosa kipato, lakini wateja wangu, walikosa huduma muhimu, kwani wapo wanaosoma vyuo, wafanyabiashara na watu wa kada mbalimbali wanaotegemea intaneti kufanya shughuli zako,” anaongeza Magayane.

Dkt. Lenny Kasoga, mtaalamu wa uchumi na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (mstaafu) anaeleza hasara za kuzimwa kwa mtandao wa intaneti ni kubwa zaidi katika dunia ya sasa yenye kutegemea mtandao huo kwa mawasiliano.

Anasema serikali zinazozima mtandao wa intaneti, hazina sababu za maana kufanya hivyo, bali ni kuogopa nguvu ya umma kwa “matendo maovu dhidi yao,” na kwamba ni uonevu tu wa watawala wasiowajibika ipasavyo.

“Ukiangalia kwa umakini, unagundua kuwa madai yote yanayotolewa na watawala kufungia intaneti, ni upuuzi tu, hakuna sababu ya kufanya hivyo; iwe wakati wa uchaguzi au wakati wa amani au kipindi chochote kile,” anaongeza.

Mchumi huyo anasema biashara nyingi za kuagiza na kuuza bidhaa, zinategemea zaidi mawasiliano ya intaneti, yanapozimwa, tafsiri yake ni kuzidisha umasikini kwa wananchi.

Fatuma Karume, wakili wa mahakama kuu na mwanaharakati wa haki za binadamu, akizungumzia kadhia ya kuzimwa kwa intaneti Tanzania anasema; “ule ulikuwa uhuni wa watawala na kuminya demokrasia.”

Wakili huyo anasema kuzuia intaneti kunaweza kuelezwa kwa maneno machache kwamba –“ni udikteta,” kwani unazuia haki ya msingi ya binadamu, ambayo ni kuwasiliana, kuwa na uhuru wa kujieleza bila kuingiliwa.

“Kuzimwa kwa mtandao kunatumiwa na mataifa dhalimu kuzuia upinzani na kupokonya haki za kuwasiliana - mara nyingi hutumiwa wakati wa vipindi muhimu kama vile uchaguzi au maandamano, lakini kimsingi, wanaoumia ni wengi hata wasiopenda kujihusisha na siasa – ni kinyume cha haki za binadamu,” anasema.

Je, mtu anaweza kuishtaki serikali kwa kufunga intaneti? Fatuma anasema “ndiyo.” Serikali inaweza kushtakiwa mahakamani kwa kuzima intaneti.

internet shutdown2.PNGKatibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, anasema kilichofanywa na serikali wakati ule kilikuwa na dalili mbaya ya uendeshaji wa nchi yenye kujali haki za binadamu.

“Hakukuwa na sababu ya kuzuia watu kuwasiliana na wengine kuendelea na shughuli zao zinazotegemea uwepo wa intaneti ili kufanya kazi na biashara, wengi walikwama kipindi kile na watu walipoteza kipato – haikuwa sahihi hata kidogo,” anasema.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa, Lameck Kishimbo anasema kufungwa kwa mtandao wa intaneti hakuathiri wanasiasa pekee, kama serikali nyingi zinavyodhani, lakini ni hakika kwamba huathiri zaidi uchumi wa wafanyabiashara wanaotegemea intaneti.

Lameck ambaye alikuwa mwaka wa pili wakati mtandao wa intaneti unazimwa, akisomea shahada ya kwanza ya sayansi ya kompyuta, anasema wanafunzi wote hutegemea zaidi mtandao huo kupata vitabu na maarifa mengine, unapozimwa, kwa sababu zozote zile, huathiri mwenendo wa masomo yao. Anashauri serikali ya sasa “kuacha hata fikra za kuzima mtandao wa intaneti.”

Je, VPN inasaidia?

Wakati mtandao wa intaneti unazimwa mwaka 2020, Watanzania walihamasishana zaidi kujiunga na mfumo unaoweza ‘kupiga chenga’ zuio la matumizi ya intaneti kwenye simu.

Mfumo huo, maarufu kwa jina la VPN, ulihimizwa zaidi na watu wengi wakiwamo wa wanaharakati na wataalamu wa mtandao wa intaneti. Mmoja wao ni mwanaharakati Maria Sarungi ambaye ‘alijitolea’ kuelimisha wananchi njia ya kukwepa zuio la kupata intaneti.

Akitumia zaidi mtandao wa Twitter, Maria alifundisha namna ya kupakua VPN anuai, huku akieleza manufaa yake, siyo wakati wa kufungwa kwa intaneti tu, bali pia husaidia ‘usalama’ wakati wa kutumia intaneti.

Mtaalamu wa mawasiliano ya intaneti kutoka kampuni ya Microx Solutions ya Jiji la Mwanza, Amrsan Shah anaeleza kwamba VPN ni mfumo wenye uwezo wa kukwepa njia za kufungia mawasiliano ya intaneti kwa kuwa haiingii wala kupitia kwa ‘wakala.’

“Ni vigumu sana kuzuia intaneti kwa watu wanaotumia mfumo wa VPN na huenda ndiyo njia sahihi na salama kwa wakati wote kunapokuwa na zuio la matumizi ya intaneti katika nchi yoyote,” anaongeza.

Peggy Hicks, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano, Taratibu Maalum na Haki ya Maendeleo, katika Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) anasema - "ukiona serikali zinahangaika kufunga mtandao wa intaneti, anza kutambua kwamba haki za binadamu ziko shakani.

Makala haya ni sehemu ya mpango maalum wa kukuza ujuzi kwa vyombo vya habari unaoendeshwa na Wakfu wa Thomson Reuters. Yaliyoandikwa humu siyo dhamana ya Wakfu.
 

WALOLA VUNZYA

JF-Expert Member
Nov 20, 2020
2,132
1,651
Taifa lilipitia kipindi kigumu,na mtaka yote kwa pupa hukosa yote,Magufuri alikosa uhai,urais na heshima ya kibabe kwa sababu tu ya ujinga.
 
3 Reactions
Reply
Top Bottom