UTPC
Journalists' Union
- Apr 17, 2026
- 45
- 30
Katika makala iliyopita, tulionyesha ukubwa wa tatizo la ugonjwa hatari wa Fungashada ya Migomba (BBTV) na madhara yake makubwa kwa wakulima na taifa kwa ujumla. Swali kubwa linalobaki bila majibu ni kwa nini ugonjwa huu usiokuwa na tiba wala chanjo unazidi kusambaa kwa kasi ya kutisha tangu ulipogunduliwa mkoani Kigoma mwaka 2020 na kuthibitishwa katika mikoa tisa. Katika sehemu hii ya pili ya uchunguzi wetu, tunafafanua chanzo cha kusambaa kwa ugonjwa huo.
Pia soma ~ Biashara Holela ya Miche ya Migomba Inavyowazamisha Wakulima
Uchunguzi uliofanywa katika Kata za Bigwa, Kauzeni, na Mzinga ndani ya Manispaa ya Morogoro, pamoja na Kata ya Mkuyuni katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, umebaini kuwa injini kuu ya kusambaa kwa ugonjwa huu ni biashara holela ya miche (machipukizi) ya migomba. Biashara hii inahamisha vimelea vya ugonjwa kutoka shamba moja lililoathirika hadi mashamba yaliyokuwa salama.
Vitovu vya biashara holela ya machipukizi
Maeneo yanayozunguka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kama vile Kata ya Boma na Mlimani, pamoja na Kata za Kauzeni na Mzinga, yamegeuka kuwa vitovu au soko huria la biashara holela ya machipukizi ya migomba. Vijana na wafanyabiashara binafsi wanajipenyeza kuchimba machipukizi haya moja kwa moja kutoka kwenye mashamba ya wakulima na kuyapeleka kwa wateja wanaohitaji kupanda.
Mathias Michel, mmoja wa vijana wanaojihusisha na biashara ya uuzaji wa miche ya migomba, anakiri bila kificho kuwa pamoja na kufanya biashara hiyo kwa muda mrefu, hana utaalamu wala mafunzo yoyote kuhusu ugonjwa wa Fungashada wala mbinu za usalama wa kilimo. Anategemea macho yake tu kutathmini ubora wa mche.
"Mteja akihitaji miche tunaenda kuichimba mashambani. Mimi naangalia tu kwa macho kama mche unaonekana mzuri. Sina utaalamu wa kujua kama una ugonjwa au hauna," anakiri Michel.
Kwa upande mwingine, Anna Simon, mkulima kutoka Kata ya Mkuyuni, anasema kuwa kukosekana kwa njia mbadala ya kupata mbegu rasmi na zilizothibitishwa kunawalazima wakulima kuendelea kuazimana au kununua miche kutoka kwa majirani zao kwa mazoea.
"Ukosefu wa mbegu bora zilizothibitishwa unawalazimu wakulima kuendelea kuazimana au kununua miche yenye virusi kutoka kwa majirani zao," analalamika Simon.
Mtazamo wa Wataalamu
Dkt. Beatrice Mwaipopo, mtafiti kutoka Idara ya Sayansi ya Mimea Vipando na Kilimo cha Bustani katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), anafafanua kuwa njia kuu inayochangia kusambaza ugonjwa wa BBTV kwa kasi ni usafirishaji wa miche yenye maambukizi kutoka shamba moja kwenda jingine.
"Shina moja lenye ugonjwa likitoa machipukizi 10 yakihamishwa yanaeneza ugonjwa huo mara kumi zaidi, maana shina moja lina uwezo wa kusambaza ugonjwa mara kumi. Wafanyabiashara hawa wanatumia macho tu kutathmini afya ya mche kama mgomba, jambo ambalo haliwawezeshi kubaini vimelea vya magonjwa, hivyo kuendelea kuhamisha virusi kutoka shamba hadi shamba jingine," anasema Dkt. Mwaipopo.
Ukimya wa TOSCI
Uchunguzi wa makala hii umebaini kuwa msingi mkubwa wa biashara hii holela ni kutosimamiwa na kutekelezwa kwa Kifungu cha 17(1-2) cha Sheria ya Mbegu ya Mwaka 2003 na marekebisho yake ya mwaka 2023. Vifungu hivi vimeweka utaratibu thabiti unaokataza mtu yeyote kujihusisha na biashara ya mbegu nchini bila kusajiliwa, au yeyote anayeagiza, kusafirisha, kuzalisha, kusambaza, au kuuza mbegu kulazimika kusajiliwa rasmi na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kabla ya kuanza shughuli hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa Chimagu, anakiri wazi kuwa hadi sasa hakuna mfanyabiashara yeyote wa mbegu za migomba aliyechukuliwa hatua za kisheria au kutozwa faini kwa kuuza miche isiyothibitishwa, jambo ambalo linawapa mwanya wafanyabiashara hao kuendelea kuvunja sheria bila hofu.
"Biashara ya mbegu au machipukizi ya migomba kwa miaka mingi imekuwa ikifanywa bila kufuata taratibu, lakini hata wakulima hawakuwa na utamaduni wa kununua rasmi, badala yake anaenda kwa mkulima mwenzake na kuchukua machipukizi na kupanda shambani kwake, hivyo tumeona kabla ya kuchukua hatua tuanze kwa kuwaelimisha," anajitetea Chimagu.
Kauli hii ya kuanza kwa elimu wakati janga likiteketeza maelfu ya ekari za wakulima inaonekana na wakulima kama kinga ya uzembe wa taasisi hiyo ya udhibiti.
Kukosekana kwa karantini
Hali inazidi kuwa mbaya kutokana na kutowekwa kwa kanda za karantini katika maeneo yaliyoathirika. Hamadi Mpeka, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bigwa Kisiwani, anasema kuwa kukosekana kwa karantini katika kata zilizoathirika na BBTV kunachangia kwa kiasi kikubwa kusambaa kwa ugonjwa huo.
"Kama hatua hiyo ingechukuliwa, ugonjwa wa fungashada ya migomba ungekuwa bado upo katika kata moja au ungekuwa umeshadhibitiwa. Sasa kuna hatari kubwa ya ugonjwa huu kusambaa mkoa mzima wa Morogoro," anaonya Mpeka.
Uchunguzi unaonesha kuwa hali hii inatokana na kutosimamiwa kwa Kifungu cha 45(3)(a) cha Sheria ya afya ya mimea ya mwaka 2020, ambayo inaipa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) uwezo wa kutangaza rasmi katika gazeti la serikali eneo lililoathirika au linaloshukiwa kuwa katika karantini (Quarantine Pest Area). Vilevile, Kifungu cha 45(4)(c) na Kifungu cha 46(6)(b) vya sheria hiyo vinatoa mamlaka kamili ya kuweka marufuku au vizuizi vya kusafirisha mimea na vifaa vyote vya uzalishaji kutoka maeneo yaliyoathirika.
Licha ya nguvu hii kubwa ya kisheria, Afisa Kilimo wa Manispaa ya Morogoro, Shabani Charles, anakiri kuwa sheria inawapa mamlaka hayo, lakini karantini haijawekwa kwa kuwa mkazo umewekwa kwenye kutoa elimu ili wakulima wenyewe wang'oe migomba iliyoathirika.
Wakati huo huo, Ally Kondo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Konga A, anasema kuwa baada ya ugonjwa kuingia eneo hilo mwaka 2021, wataalamu kutoka SUA walitoa mafunzo ya kutambua na kuteketeza migomba iliyoathirika, lakini zaidi ya asilimia 80 ya wakulima walishindwa kufanya hivyo kwa sababu migomba hiyo ndiyo ilikuwa chanzo chao kikuu cha chakula na kipato cha kila siku.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo Mkuu wa TPHPA, Hamad Lyimo, alipozungumza na wakulima Juni 27, 2025, mjini Morogoro kwenye semina ya kuwajengea uwezo wa kukabiliana na ugonjwa huo, alithibitisha kuwa tangu mwaka 2021 ugonjwa huo umeendelea kusambaa nchini na hadi mwaka 2024 ulikuwa umethibitishwa katika mikoa 8, ikiwemo Morogoro.
Ili kunusuru uchumi wa wakulima na kulinda usalama wa chakula nchini, ni wazi kuwa kauli mbiu na semina za kinadharia hazitoshi. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, TOSCI, na TPHPA lazima ziamke kutoka usingizini, zisimamie sheria kikamilifu kwa kuwawajibisha wauzaji wa miche holela, kutangaza karantini rasmi, na kutoa fidia au msaada wa mbegu mbadala ili kunusuru zao la ndizi lisiangamie kabisa.
ANDIKO LA: Farida Saidi Mangube, Morogoro
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.