Kumi bora ya waandishi mahiri wa hadithi za Kiswahili

Feb 26, 2017
54
67
Miongoni mwa vipaji ambavyo Tanzania imetunukiwa, ni pamoja na orodha kubwa ya waandishi wa hadithi za Kiswahili. Waandishi wengi wamechomoza kwa uhodari na umahiri wao kila mmoja katika kona yake. Katika somasoma yangu nimeondokea kuwahusudu waandishi kama 30 hivi wanaofanya maajabu kupitia kalamu zao. Lakini, kwa kuchelea kuwakirihisha nafsi, nimeonelea niandike japo orodha fupi isiyozidi waandishi kumi tu, kila mmoja kwa sifaze matayasar.

1. SHAABAN ROBERT
Umahiri wake katika utunzi na uandishi wa mashairi na tendi kama vile; Mapenzi bora, Almasi za Afrika, Utubora mkulima, nk, ulipelekea akabandikwa lakabu ya "SHAHA WA MALENGA", yaani "mfalme/kinara wa washairi". Gwiji huyu alisifika barani Afrika kwa umahiri wake wa kutumia lugha fasaha yenye adabu na insafu, pamoja na zaida ya uwezo wake wa kuibua misamiati mipya iliyozidi kukitajirisha Kiswahili. Sheikh Shaaban Robert alikuwa ni mwanazuoni wa fasaha kubwa na hekima. Ukwasi wake wa maneno ulimfanya aweze kufupisha simulizi ndefu kwa kutumia maneno machache bila kuathiri mantiki (uwekevu maneno). Kipaji alicho kidhihirisha katika vitabu vyake kama ADILI NA NDUGUZE, MAISHA YANGU NA BAADA YA MIAKA HAMSINI, KUSADIKIKA, SIKU YA WATENZI WOTE, WASIFU WA SITI BINTI SAAD, nk, vilipelekea mzaliwa huyu wa Tanga kutumiwa na chama cha TANU katika harakati zake za kudai uhuru kama mhamasishaji, na baadaye kupewa heshima kubwa na utawala wa Kingereza, kwa kupewa tuzo ya uraia nchini Uingereza, yaani 'Member of the British Empire (MBE), pamoja na tuzo nyingine kama vile 'Margaret Memorial Prize for Writing'. Maneno hayatoshi kumzungumza bwana huyu aliyetawafu tangu mwaka wa 62.

2. MOHAMMED SAID ABDULLAH
Yamkini tangu kufariki kwake, hajapata tena kutokea mwandishi mwingine bingwa wa kuandika hadithi za kiuchunguzi zilizobuniwa kwa umahiri kama alivyofanya yeye. Mzee Mohammed kupitia mhusika wake mkuu katika vitabu vyake, aliyemwita Bwana MSA (ikiwa ni ufupisho wa majina yake mwenyewe, yaani, Mohammed Said Abdulla), aliuelimisha na kuuburudisha umma kwa namna alivyokuwa akiyaduhushi na kuyadunzi mambo mazito yaliyoshindikana kupatiwa ufumbuzi. Vitabu vyake kama vile Duniani kuna watu, Mzimu wa watu wa kale, Kisima cha Giningi, Siri ya sifuri, Mwana wa yungi hulewa, nk, vilimfanya mwandishi huyu wa Kizanzibar kujitwalia heshima kubwa barani Afrika. Kihistoria, hakuna aliyewahi kushika kitabu cha mzee huyu, na kukikacha bila ya kukimaliza.

3. BEN MTOBWA
Dunia kupitia Tanzania ilikuja kushuhudia kuibuka kwa wimbi kubwa la utunzi na uandishi wa riwaya za kijamii na kipelelezi kupitia kwa Ben Mtobwa, aliyeandika hadithi zake kwa kumtumia mhusika wake mkuu, Joram Kiango. Katika zamani hizo, waandishi wengi kama Elvis Musiba (Willy Gamba), Eddy Ganzel, Hammie Rajab, Faraj Katalambula, nk, waliokuwa wakiandika kwa namna iliyotaka kufanana, walijipatia umaarufu pamoja na heshima kubwa kupitia vitabu vyao kama vile Kikomo, Msako wa hayawani, Sanda ya jambazi, Simu ya kifo, nk. Kinachomfanya Ben Mtobwa aingie kwenye orodha hii kwa niaba yao, ni vitabu vyake vingi kutokukauka sokoni, kiasi cha kufanya vizazi hadi vizazi kuendelea kumsoma, tofauti na wenziye ambao miaka ya hivi karibuni wamepotea sokoni kwa kukosa usimamizi na uchapaji wa kazi zao.

4. BEKA MFAUME
Unaposikia vitabu bora kama Dhihaka, Mhanga wa Ikulu, Aya za shetani, Mwana Mji, Mwiba, nk, vikiongelewa kwa raghaba na kupigiwa mfano, basi fahamu kwamba, mtunzi na mwandishi aliyefanya kazi hizo zinazosifika kila pembe ya nchi hii, ni Beka Mfaume, au The Greatest kama anavyojiita mwenyewe. Ukibahatika kumsoma mzee huyu utagundua kwamba, ndani ya kichwa chake Mola amejaza ubongo uliohifadhi kipaji cha ajabu mno katika usimuliaji wa matukio pamoja na maarifa ya maisha ya kijamii.

5. HUSSEIN TUWA
Waswahili husema 'Mwana wa mhunzi asiposana huvukuza'. Tuwa ni mtoto wa msimulizi hodari na mwandishi pia, mama Sango Kipozi. Pengine ndiyo sababu za cheche zake kila uchao kuwasha moto katika wingu la uandishi wa riwaya.

Linapotajwa jina lake, Hussein Tuwa, kinachorindima vichwani mwa wengi ni ile sifa yake kubwa: BINGWA WA TAHARUKI. Na anapojiita bingwa wa Taharuki hatanii. Kwa wamsomao wanaelewa. Kama humjui, basi haraka katafute vitabu vyake kama MKIMBIZI, MFADHILI, MDUNGUAJI, WIMBO WA GAIDI, nk, ndipo utaelewa. Kila unaposoma sehemu ndogo tu ya visa vilivyomo katika vitabu vyake, basi utabaki roho juu huku ukitaka kujua mwishilizo wake kwa hamu na ghamu, mpaka utakapomaliza. Ufahamu wake mkubwa na maarifa aliyonayo kichwani, pengine kwa kupenda sana kujisomea au kusafiri sehemu nyingi duniani, kumemfanya awe na ufahamu pamoja ujuzi mkubwa wa kuyadadavua mambo magumu yanayojiri katika ulimwengu huu wa sasa, na kuyaweka katika vitabu vyake hata yakaeleweka kiurahisi.

6. PROF. E. KEZILAHABI
Pengine kwa sababu haandiki sana mitandaoni wala kwenye magazeti, ndiyo maana vijana wengi ambao hawakubahatika kupitia katika vyuo vya elimu za juu, ambako anafundisha, wanakuwa hawajamsoma vya kutosha. Umahiri wa Prof. Kezilahabi katika Kiswahili si tu ule wa kuzaliwa na kujifunza toka kwa wazee, kama ilivyo kwa akina Shaaban Robert na Mzee Mudhihir M. Mudhihir, bali yeye ni bingwa aliyesomea na kubobea katika lugha. Hivyo, lugha hiyo inapokutana na uanachuoni wake, huzalisha maandishi makali sana dhidi ya mambo ya msingi katika jamii hasa utawala mbovu, shida za watu katika jamii, nk. Utayasadiki niyanenayo kama utatafuta kazi zake chache tu; Rosa Mistika, Kaptula la Max, Kichwa maji, nk.

7. FADHY MTANGA
Huyu ni mwandishi kijana, mwenye upeo mkubwa juu ya mambo mbalimbali. Pamoja na kutoandika vitabu vingi sana, lakini vitabu vyake viwili tu vilivyotapakaa mtaani; FUNGATE na HUBA vimemtangaza na kumpambanua kama mwandishi mahiri sana. Fadhy ni msomaji hodari sana anayejibidiisha si tu kusoma vitabu, bali pia machapisho mbalimbali mitandaoni na kwingineko.

Amekuwa makini sana anapoandika hata sentensi moja tu, lazima atazingatia matumizi sahihi ya lugha na alama za uandishi kiasi cha ya kuyafanya maneno yake kuwa na ladha ndani ya ubongo wa msomaji hata kama ameamua tu kufanyiza stihizai. Fadhy ana uwezo wa kuchukua kisa cha kawaida kabisa, labda alichokishudia safarini au mtaani, lakini akakisimulia kwa ufundi mpaka ukajikuta hutamani kuishia njiani. Zaidi, mwandishi huyu ana ukwasi wa maneno ya Kiswahili, kiasi cha kumrahisishia kuandika sentensi fupi-fupi bila kumkirihi msomaji.

8. ERIC J. SHIGONGO
Unapoongelea waandishi waliopata kutamba na kusomwa zaidi magazetini, huna budi kumtaja mjasiriamali huyu mwenye historia ya kipekee. Shigongo ametoa mchango mkubwa mno kuhuisha utamaduni wa usomaji vitabu uliokwishaanza kupotea. Kwa kupitia vitabu vyake kama Siku za mwisho wa uhai wangu, Rais anampenda mke wangu, nk, Shigongo ameweza kujijengea heshima na ngome kubwa ya wasomaji wake. Zaidi, Shigongo amethubutu kuufanya uandishi wa vitabu kuwa biashara, hata ameweza kuwashawishi wengi kujikita huko.

9. MWANABALAGHA
Hapa hakuna haja ya kutoa maelezo marefu, kila mmoja anajua namna fanani huyu, aliye bingwa wa balagha katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati, anavyopambana na hali yake.

10. TAJA MWANDISHI WAKO
Hapa ili kuwapooza uchungu wale waliochukia kuona MwanaBalagha akishika nafasi ya tisa, tunaiacha nafasi hii wazi ili kila mmoja amtaje mwandishi wake bora kama hakutajwa orodhani.

Ahsante.
Maundu Mwingizi (MwanaBalagha)

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Ujue mie labda nina mtazamo tofauti

1) Asilimia kubwa ya watu wa mwambao wanajua kiswahili fasaha na hivyo kuwafanya wawe wa kipekee unaposoma kazi zao, tafuta waandishi hata wadogo tu ambao hawajukikani kabisa ila ni watu wa mwambao utabaini wanajua sana na si kwenye Hadithi tu bali hata nyimbo, sikiliza maneno ya taarabu na tunzi zao utabaini kujua kwao kiswahili fasaha kunawabeba sana tofauti na sisi wa maeneo mengine kama ya kwa kina mkuu wetu

2) Kuna vipaji vingi sana mitaani tena hata hawana shule kichwani wala utaalamu wa maneno ila ni wazuri sana wa kutunga Hadithi, kitu pekee ninachokifahamu kwa Shigongo hana kipaji kiiiiile cha kutishia amani ila amekua mjanja kuwatumia vipaji vya chini na kuwaweka katika himaya yake kama alivyo Diamond Platinumz hivyo kufanya watu wamuone mkali, mfano Shaluwa ni mkali tu ila yupo chini yake

3) Namba kumi hapo nipo mimi maana nikiangalia kazi nilizoandika na ambazo watu wamezisoma nimepata feedback nzuri sana kama Zafeera, Kitanzi cha upendo, Paka Mweusi, Mshumaa gizani, Monica, Daraja la Misukule, Binti wa ng'ambo na vinginevyo vingi tu vinanifanya niwe balaa katika utunzi wa Hadithi ila ndio hivyo "tatizo nyota"

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Dah umetumia kiswahili kimoja kitamu sana ambacho vijana wa sasa waliozoea kuandika Apo vipi wakimaanisha hapo vipi
Kabixa kabixa wakimaanisha kabisa kabisa Nyimbo ya roma wakimaanisha wimbo wa roma HUWEZI KUKUTA WAKIKITUMIA.

Hongera mwandishi wa mada hii.
 
Dah umetumia kiswahili kimoja kitamu sana ambacho vijana wa sasa waliozoea kuandika
Apo vipi wakimaanisha hapo vipi
Kabixa kabixa wakimaanisha kabisa kabisa
Nyimbo ya roma wakimaanisha wimbo wa roma
HUWEZI KUKUTA WAKIKITUMIA.
hongera mwandishi wa mada hii.
Pana mfumo wao wa kuandika
5=s
9=g
7=T
1=I
Mwanangu nilitaka kumuwamba makofi kwa upuuzi huo.
 
The bold hamjamuwekaa??mna wivu sana watu wa Jamii forum
Yule ni mtunzi au ni mkusanyaji wa makala mbalimbali na kuziweka ktk lugha ya kiswahili kwa mpangilio na mtiririko ulio tukuka?

Hapa tunazungumzia watunzi kasome kitabu cha ben r mtobwa.

Kiitwacho malaika wa shetani au tutarudi na roho zetu afu ukasome stori za vipepeo weusi uone utofauti.
 
Yule ni mtunzi au ni mkusanyaji wa makala mbalimbali na kuziweka ktk lugha ya kiswahili kwa mpangilio na mtiririko ulio tukuka?

Hapa tunazungumzia watunzi kasome kitabu cha ben r mtobwa
Kiitwacho malaika wa shetani au tutarudi na roho zetu afu ukasome stori za vipepeo weusi uone utofauti.
Mna wivuu wakati bold hakuna anaemfikia hapa JF na nje ya JF
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom