TAFAKARI YANGU KUHUSIANA NA PICHA YA MAUAJI YA MWANGOSI
Nikiwa nalengwa lengwa na machozi nimeiangalia na kuitafakari vizuri sana picha hiyo inayoonesha jinsi Mwangosi alivyotolewa uhai kikatilia sana. Mimi nimeiangalia na kuona kuna askari ambao walikuwa na uchu wa kumpiga na kuangamiza kabisa maisha ya Mwangosi na wale waliokuwa wanajaribu kuzuia wenzao asiendelee kushambuliwa na askari wenye uchu wa kutoa roho za watu. Mfano kuna askaari anayeonekana katikati akiwa ameshikwa kiunoni na Mwangosi huku Mwangosi mwenyewe akiwa ameshika kamera yake, anajaribu kwa kadiri awezavyo kuwazuia wenzake wasiendelee kumshambulia Mwangosi na ndio maana ilibidi Mwangosi ajishike kwake nafikiri wakati akianguka ili kujiokoa. Huyu askari anaonekana ameinua juu kirungu chake kama ishara ya kuwazuia wenzake wasiendelee kufanya unyama waliokuwa wakimfanyia Mwangosi. Kwakweli natamani kulijua jina la askari huyu pamoja na yeye mwenyewe. Alifanya jitihada za pekee lakini alishindwa kutokana na jinsi wauaji walivyokuwa na uchu na hasa huyu wa nyuma yake ambae ndio mlipuaji wa Mwangosi.
Mwingine anayeonekana kutaka kuzuia unyama huu ni huyo aliyeipa mgongo kamera. Huyu anaonekana kumzuia askari aliye kulia kwake ambaye anaonekana kwenda kwa kasi kumshambulia Mwangosi. Kuna huyo pia aliyevaa shati la kiraia akiwa na kofia nyeusi naye anaonekana kutaka kuzuia madhara zaidi.
Sasa askari watoa roho ni hao watatu wa upande wa kushoto au nyuma ya yule askari anayejitahidi kuzuia wenzake na ambaye ndiye ameshikwa kiunoni na marehemu Mwangosi. Hao ndio watoa roho wakuu wakiongozwa na huyo wa kushoto kabisa ambaye wakati huyo wa katikati anajitahidi kuzuia wenzake yeye akapata mwanya wa kufyatua kombora lake na kumtekeketeza kabisa mwanamwema Daud Mwangosi.
Huyo wa katikati ambaye ndiye anayeonekana kuwazuia wenzake huku Mwangosi akiwa amejishika kiunoni mwake anaonekana kama ni mtu aliyeona kuwa, kama ni kipigo alichokipata Mwangosi, basi kilikuwa kimetosha hivyo kuendelea zaidi ya hapo ingekuwa ni madhara makubwa ndio maana anajitahidi kuwazuia wenzake. Lakini kwa bahati mbaya alikuwa amezidiwa na askari waliokuwana uchu wa kumtoa roho Mwangosi.
Mimi binafi nawapongeza sana askari hao niliowaelezea kwa jinsi walivyojitahidi sana kuokoa maisha ya Mwangosi. Laana zote za duniani na mbinguni ziwaendee hao wengine wote waliohakikisha kuwa Mwangosi anafutika katika duniani hii kikatili kabisa, wa kwanza wao akiwa huyo Michael Kamuhanda na huyo mlipuaji wa bomu.
May the almighty God Rest In Peace the Innocent soul of Daud Mwangosi! AMEN!