Kumbukumbu ya mapinduzi ya zanzibar 3 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kumbukumbu ya mapinduzi ya zanzibar 3

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by GHIBUU, Jan 3, 2012.

 1. GHIBUU

  GHIBUU JF-Expert Member

  #1
  Jan 3, 2012
  Joined: Jan 13, 2011
  Messages: 3,187
  Likes Received: 704
  Trophy Points: 280
  Wengi ya watanganyika hawajui history ya zanzibar na badala yake kuongea sana kwa jazba dhizi ya wazanzibari,nimewaletea histroy fupi juu ya zanzibar kabla ya mapinduzi 1964
  KUMBUKUMBU YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR 3
  Mahmia ya Muengereza
  Mahmia ni mfumo maalum wa ukoloni wa kijanja usio na sura ya kikoloni ya moja kwa moja lakini athari yake kwa raia haina tofauti na ukoloni wenyewe. Kwa mujibu wa sheria za kilimwengu za wakati huo nchi hiyo ya mahmia (protectorate) huwa haikutawaliwa bali imehifadhiwa au inalindwa mpaka pale itakapokuwa na uwezo wa kujitawala na kuendesha shughuli zake yenyewe. Mahmia hiyo huanzishwa kwa mkataba wa hiari kati ya dola kubwa na nchi dhaifu inayotaka kulindwa. Hata hivyo mkataba huo wa ulinzi huvunjwa pale nchi inayolindwa inapoona haina tena sababu ya kuhitaji ulinzi huo. Mtindo huo wa ulinzi unaonekana kuwa ni mfumo wa ujanja wa kikoloni kwani nchi nyingi zilishawishiwa na kushurutishwa na madola makubwa kuingia katika mikataba ya ulinzi bila ya hiari zao. Nchi inayolindwa hua chini ya utawala na utiifu wa dola inayotoa ulinzi. Uhusiano kati ya nchi inayolindwa na nchi nyengine hufanywa na dola inayotoa ulinzi kwa kufuata sera zake. Raia wa nchi inayolindwa hulazimika kufuata sheria za nchi inayotoa ulinzi. Mambo yote muhimu yanayoashiria kujitawala wenyewe ndani ya nchi kama ulinzi, uraia, utumishi, uhamiaji, uhusiano wa kimataifa na mambo mengine yote huratibiwa na huendeshwa na dola inayotoa ulinzi. Halkadhalika dola inayotoa ulinzi hufanya kigugumizi au hupinga kuuvunja mkataba huo wa ulinzi na hivyo kuendelea kuikalia nchi inayoilinda hadi muda inayotaka yenyewe. Raia hulazimika kufanya harakati za kudai uhuru wao kutoka kwa walinzi wao ikiwa sio tofauti na wale wanaodai uhuru kutoka kwa wakoloni wao. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa za wakati huo pia wakati nchi inayolindwa inapokabidhiwa uhuru wake hakuna kitendo cha kushusha bendera ya dola iliyokuwa ikitoa ulinzi kwani nchi hiyo haikupata uhuru kutoka katika utawala wa kimabavu bali ni wa hiari.

  Katika mwaka wa 1890 ndani ya ufalme wa Seyyid Ali Bin Said, Zanzibar iliingizwa chini ya ukoloni wa Muengereza kwa ujanja wa mahmia, yaani Mahmiya ya Uengereza au British protectorate kwa lugha ya kiingereza. Malengo ya nje ya mahmia hii ilikuwa ni kuilinda nchi ya Zanzibar mpaka pale itakapokuwa na uwezo kiusalama na kitaalamu wa kujitawala yenyewe. Mahmiya ya Uengereza Zanzibar ilioanzishwa kwa mkataba usio wa hiari na wa kushurutishwa na dola ya Uengereza ulitiwa saini kati ya Sayyid Ali Bin Said, akiwa mfalme wa Zanzibar na Queen Victoria, akiwa malkia wa Uengereza, tarehe 14 Juni 1890. Kinyume na inavyodaiwa na baadhi ya wanahistoria kwamba Sayyid Ali aliitelekeza Zanzibar kwa waengereza kwa hiari yake na kwa masilahi yake. Kuanzia hapa ndipo waengereza wakajimilikisha kwa nguvu visiwa vya Unguja na Pemba. Hapa ifahamike kwamba kipindi hichi Zanzibar inaingia chini ya himaya ya Muengereza Sultani (ambaye ukoo wake unatokea Oman) amekuwa akitawala Zanzibar vizazi kwa vizazi kama mtawala wa kijadi. Hivyo basi Muengereza kupitia mahmia hiyo alimtawala Sultani, yeye mwenyewe na raia zake kwa ujumla. Kufuatia kuanzishwa kwa mahmiya ya Uingereza, Mfalme alilazimishwa kubaki mfalme bandia wa kikatiba (ya ukoloni) aliyechaguliwa na kuwekwa juu ya kiti cha ufalme na hata ikibidi kuondolewa na waengereza wenyewe. Pia mfalme alipokea mshahara wake kutoka kwa wakoloni hao. Baadhi ya wafalme walijaribu kupingana na ubabe huu wa waengereza lakini hawakuweza kufanikiwa kwani Muengereza alikuwa na nguvu kubwa za kijeshi na alifanikiwa kuzuia majaribio yote ya uasi.
  Moja ya matukio muhimu yanayokumbukwa zaidi yanayoonesha utawala wa mabavu na ubabe wa wakoloni wa kiengereza dhidi ya wafalme wa Zanzibar na raia zao ni matokeo ya “vita vya Alhamisi” (Anglo-Zanzibar war). Vita hivi vilipiganwa siku ya Alhamisi ya tarehe 27 Ogasti 1896. Vita hivi vimeipatia Zanzibar umaarufu mkubwa wa kihistoria duniani. Vita hivi vinatambuliwa kama vita vifupi zaidi duniani ambavyo vilidumu kwa muda wa dakika 40 (kuanzia saa 9:00 asubuni mpaka saa 9:40 asubuhi siku hiyo hiyo) tu. Sababu ya vita hivyo ni kutokana na waengereza kushurutisha ufalme kwenda kwa Seyyid Barghash badala ya kaka yake mkubwa Seyyid Khalid ambaye ndiye hasa aliyekuwa na haki ya kurithi ufalme kwa wakati huo. Hii ni kwa sababu Seyyid Khalid alikuwa na mitazamo isiyozingatia na inayopingana vikali na masilahi ya wakoloni hao wa kiengereza wakati mitazamo ya Seyyid Barghash ilikuwa inakubalika na wakoloni. Seyyid Khalid kwa maana hiyo alikuwa ni kama pachikizo la waengereza. Hivyo basi waengereza hawakuwa tayari kumkabidhi Seyyid Khalid ufalme.
  Vita vilizuka pale Barghash alipoamua kujitangazia ufalme mara tu baada ya kifo cha Ami yao Seyyid Hamad Bin Thuwein. Wakati bendera inapepea nusu mlingoti kuashiria msiba wa nchi kutokana na kifo cha Seyyid Hamad Bin Thuwein, Seyyid Khalid aliipandisha bendera na kujitangaza kuwa yeye ndie mfalme mpya baada ya kifo cha ami yao. Wakati anafanya hayo alikuwa tayari ameshatayarisha kikosi cha askari ili kukabiliana na Muengereza pindipo atajaribu kumtoa madarakani. Seyyid Khalid alipewa siku tatu na Muengereza kutoka katika kiti cha ufalme vyenginevyo atapigwa vita. Siku tatu hizo ziliiisha siku ya Alhamisi tarehe 27 Ogasti 1896 saa 3:00 asubuhi bila ya kukiachia kiti cha ufalme. Ilipotimia saa 3:00 asubuhi meli ya kijeshi ya Muengereza iliwasili Zanzibar na kukaa baharini kando kidogo na Beit Ajaib (Jumba la kifalme) na kuanza kushambulia. Pamoja na kufanikiwa kumtoa Seyyid Khalid madarakani, mashambulizi hayo yaliuwa askari wengi wa mfalme, raia wa kawaida waliokuwa katika shughuli za upagazi bandarini pamoja na kuishambulia na kuiangamiza kabisa nyumba ya Beit el Hukmu iliyokuwa jirani na Beit el Ajaib. Beit el Ajaib nayo ilishambuliwa na kubomolewa upande wa kushoto na kuuangamiza kabisa mnara wa Beit el Ajaib ambao hapo mwanzo ulikuwa pembeni ya jumba hilo. Baada ya marekebisho ya Beit el Ajaib mnara huo ukawekwa mbele ukigandanishwa na jengo kama unavyoonekana hadi leo. Waengereza walikuwa ndio walio na haki na mamlaka ya maamuzi yote muhimu ya nchi, halkadhalika kuyahodhi masoko na njia zote za uchumi na biashara. Kwa misingi hiyo basi mkoloni huyu Muengereza aliweza kuyadhibiti na kuyaingiza mapato yote ya nchi mifukoni mwake hususan yale yatokanayo na mazao maarufu ya biashara kama karafuu na mbata.
  Waengereza ndio walianzisha na kutilia maji mivutano ya kibaguzi na migawanyiko ya kikabila iliyopelekea uchonganishi mkubwa miongoni mwa raia wenyewe kwa wenyewe, na halkadhalika chuki baina ya raia na aila ya kifalme. Kabla ya kufika kwa muengereza mivutano na migawanyiko ya kikabila haikuwepo kabisa Zanzibar (Amrit 1986). Kabla ya ujio wa waengereza Zanzibar ilikuwa ikishuhudia migawanyiko ya kitabaka pekee. Ukabila na urangi ulianzishwa na waengereza pale walipowaundia wazanzibari vyama vilivyojengeka kwa misingi ya kikabila mwanzoni mwanzoni mwa karne ya 20.
  Sheria ya kikoloni wa Uengereza hapa Zanzibar ilimtaka kila raia ahakikishe amejitambulisha kupitia jumuiya ya kabila lake katika jumuiya nyingi za kikabila zisizopungua 23 zilizokuwepo Zanzibar. Kwa mfano jumuiya ya waarabu ilikuwa maalum kwa watu wanaonasibika asili zao kutokea Oman, jumuiya ya washirazi ilikuwa ni ya watu weusi wenye asili za kishirazi (kiiran), jumuiya ya waafrika ilikuwa ni ya watu wenye asili zao kutokea bara, jumuiya ya wahindi ilikuwa ni ya watu wenye asili za kihindi nk. Hii ni staili na sera ya ukoloni wa muingereza ya wagawe uwatawale. Hata hao waarabu wenyewe waligawanyika tena kwani wale waarabu walionasibika kutokea Yemen ya kusini walikuwa na jumuiya yao mbali iliyoitwa jumuiya ya washihiri. Makabila yalikuwa yakipambana kupitia jumuiya zao za kikabila hali iliyoathiri utaratibu mzima wa kiuchumi na kijamii na baadae sura ya ukabila ikahamia katika harakati za siasa zilizoanzia miaka ya 1950.
  Taasisi hizo za kikabila ndizo zilizowafundisha watu kubaguana na kuwaletea migogoro mingi huku yote hayo yakichochewa na kutiliwa mafuta ya mafundisho ya umishini dhidi ya uwarabu ambao ulifahamika kama uislamu (Armit 1986). Mkoloni wa kiengereza aliubadilisha mfumo wa utawala wa Zanzibar kwa mujibu wa atakavyo yeye wakati huo huo akimridhisha kwa khiana mfalme aliyekuwepo. Mnamo mwaka 1891, Muengereza alifanikiwa kumshawishi Sultani kuanzisha utawala wa kikatiba (ya kikoloni) na ndipo General Sir Lord Mathews alipoteuliwa kama waziri wa kwanza, His Highness first minister wa Sultani. Waziri huyu wa kwanza alimsaidia Sultani katika uwendeshaji wa serikali kuhusu shughuli za kila siku na mambo ya ndani ya nchi. Pia Uengereza ilikuwa na balozi wake anaemwakilisha malkia wa Uengereza aliyekuwa akijulikana kama His Majesty Agent Consul-General. Huyu alishughulikia mambo yote ya nje ya Zanzibar. Hivyo basi Muengereza kwa kutumia vyeo hivyo viwili aliitawala kikamilifu Zanzibar. Katika mwaka 1914 Muengereza alikifuta cheo cha waziri wa kwanza na cheo cha balozi wa kiingereza Zanzibar na badala yake kuanzisha cheo kimoja kipya kilichojulikana kama Mwakilishi mkaazi wa kiingereza, British resident. British resident alikuwa akifanya kazi chini ya usimamizi wa kamishna mkuu, High commissioner. Mabadiliko haya yalitokana na pale Uengereza ilipoamua kuhamisha mambo yote ya Zanzibar kutoka katika afisi ya mambo ya nje, Foreign office kwenda katika afisi ya makoloni Colonial office.
  Katika mwaka huo huo wa 1914 Muengereza alimshauri Sultani aanzishe baraza la mahmia (Protectorate council) lililoongozwa na Sultani na usaidizi wa Mwakilishi mkaazi muengereza. Wajumbe wengine a baraza hilo walikuwa ni Katibu wa serikali, Mwanasheria mkuu na Mweka hazina. Wajumbe wengine waliteuliwa kutoka nje ya serikali kwa misingi ya kikabila ambao waliteuliwa na Mwakilishi mkaazi Muengereza na kuridhiwa na Kamishna mkuu. Wajumbe hawa ni mzungu mmoja, mwarabu mmoja na wahindi wawili. Baraza hili lilikuwa na kazi ya kumshauri Sultani. Katika mwaka 1924 cheo cha Kamishna Mkuu kikafutwa na kubakishwa cheo cha Mwakilishi Mkaazi.
  Ilipofika mwaka 1926 sheria ya kuundwa kwa mabaraza mawili: Baraza la kiutendaji (Executive Council, Kwa kifupi EXCO au Majlis Tanfidh) na Baraza la kutunga sheria (Legislative Council, kwa kifupi LEGCO au Majlis Tashrii) yaliundwa na Muengereza. Mabaraza haya hayakuwa na uwakilishi wa wananchi kwani wajumbe wake wengi walikuwa ni maafisa wa serikali. Katika LEGCO mambo yalikuwa afadhali kidogo kwani kulikuwa na wajumbe sita ambao Sultani alipewa ruhusa ya kuwateua kwa idhini ya Mwakilishi Mkaazi. Wajumbe hawa sita waliteuliwa kwa misingi ya kikabila ambapo waarabu na wahindi ndio wakipata kipaumbele. Mwafrika wa mwanzo, kuingia kwenye LEGCO aliteuliwa mwaka 1946.
  Mabadiliko mengine yalifanywa na Muengereza katika mwaka 1956 ambapo mabaraza matatu yalitambuliwa badala ya mawili. Mabaraza haya ni yale mawili ya mwanzo (EXCO na LEGCO) pamoja na baraza jipya la Ushauri (Privy Council au Kwa kifupi PRIVCO) ambalo lilipewa kazi ya kumshauri Sultani katika majukumu yake ya kikatiba. Baraza la kutunga sheria hapa lilikuwa na wajumbe 13 ambao ni maafisa wa serikali na wajumbe 12 walitoka nje ya serikali. Mpaka kufika mwaka wa 1952 wajumbe wasiokuwa wa serikali wakipatikana kwa uteuzi. Ilipofika mwaka 1952 Jumuiya ya waarabu (Arab Association) chini ya Sheikh Ali Muhsin ilisimama kudai uchaguzi wa wajumbe wa LEGCO Baada ya uteuzi. Serikali ya Uengereza hata hivyo haikulikubali ombi hilo. Jambo la kushangaza ni kuwa jumuiya ya waafrika (African Association) iliunga mkono uwamuzi wa waengereza la wajumbe wa LEGCO kuendelea kuteuliwa. Hii bila shaka ilikuwa ni kwa sababu wengi wa wanachama wa jumuiya ya waafrika wenye asili ya bara walikuwa hawajapatiwa uraia wa Zanzibar. Hata hivyo baadhi ya waafrika waliokuwa raia kamili walipingana na uwamuzi wa jumuiya yao ya African Association kuhusu suala hilo. Baada ya vuta nikuvute za mda mrefu baina ya wakoloni na Arab Association mwisho serikali ilikubali madai ya uchaguzi badala ya uteuzi. Wajumbe wasiotoka katika serikali walipatikana kwa uteuzi (wajumbe 6) na kwa uchaguzi (wajumbe sita).
  Mahmia ya muengereza ilidumu hadi mwaka 1963 ambapo Zanzibar ilipewa uhuru wake rasmi ikitokana na makucha ya Muengereza. Katika mwaka 1963, Kenya ambayo hapo mwanzo hata haikuwepo katika ramani ya Afrika ikaanza pirika pirika za kuudai mwambao wa Kenya ikiwemo Mombasa iwe Sehemu yake. Ilipofika tarehe 8 Oktoba 1963, Duncan, katibu wa baraza la mawaziri la Kenya, Seyyid Jamshid bin Abdalla, mfalme wa Zanzibar, Jomo Kenyatta, rais wa Kenya na Sheikh Moh’d Shamte, waziri mkuu wa Zanzibar, walitiliana saini kwa masharti maalum mkataba wa kuuuwachia mwambao wa Kenya uliokuwa sehemu ya Zanzibar kuwa sehemu ya Kenya. Baadhi ya masharti ya mkataba huo ni kupewa uhuru wakaazi hao wa mwambao ambao asilimia kubwa ni waislamu kuishi kwa mujibu wa utamaduni wao wa kiislamu bila ya kubugudhiwa.
  Chimbuko la harakati za kudai uhuru
  Kama kuna enzi ngumu sana katika historia ya Zanzibar basi inaweza kuwa ni nyakati za kutafuta uhuru zilizoitwa kama zama za siasa. Hapo miaka ya 1950, Zanzibar kama ilivyokuwa kwa nchi nyingi za kiafrika zilizotawaliwa, iliingia katika harakati za kudai uhuru wake dhidi ya ukoloni. Harakati hizi zilikuwa ni za kuitoa Zanzibar katika makucha ya Muengereza ambae alivimiliki kwa mabavu visiwa vya Unguja na Pemba kwa muda wa miaka 73 kwa ujanja na kisingizio cha kuihami. Mfumo wa ushindani wa vyama vingi vya siasa alizozifundisha mkoloni Muengereza ndizo zilizoongoza harakati hizo za kuelekea uhuru wa Zanzibar. Harakati za siasa za kudai uhuru wa Zanzibar zilitawaliwa na vugu vugu kali la ukabila, uasili na urangi. Kama ilivyokwisha kuelezwa hapo kabla kwamba hadi kufikia hapa wazanzibari walikuwa wanaijuwa vyema kuicheza ngoma yao ya ukabila waliofundishwa na wakoloni wao waengereza.

  Hivyo basi ilikuwa si rahisi hata kidogo kwa watu waliopikwa vyema kwa falsafa ya kutetea masilahi ya kabila kuweza kuepuka kuchanganya ukabila katika siasa. Vyama vilivyoshiriki siasa zile za kuelekea uhuru wa Zanzibar ni ZNP, ASP, ZPPP na Umma party. Mwenendo mzima wa siasa hizo ulitawaliwa na misingi ya ukabila na hivyo itakuwa ni uongo kusema kuwa kipo chama katika hivyo kilichoweza kuwepuka ukabila. Ijapokuwa vipo vyama kati ya hivyo ambavyo vilijinasibu na ukabila kwa asilimia mia (100%) na kujipachika majina ya kikabila kama vile ASP, pia vipo vyama ambavyo vilijaribu kutupilia mbali falsafa za ukabila na kuwaunganisha wazanzibari wote katika harakati zake za siasa lakini ilishindikana kwa kuwa wingu la ukabila lilikuwa limeshatanda na lilikuwa likipigiwa ngoma na kuchezwa takriban na kila mzanzibari kwa kila kundi kuliona kundi jengine kama adui.
  Chimbuko la harakati za siasa za Zanzibar za kujikomboa kutokana na unyanyasaji wa muengereza unaweza kuhusishwa na vita vya ng’ombe vya mwaka wa 1954. Vita hivi vya ng’ombe ndivyo vilivyowaletea wazanzibari muamko wa kujikusanya na kujiundia umoja wa kutetea masilahi yao dhidi ya wakoloni. Sababu ya vita vya ng’ombe ni pale serikali ya kikoloni ilipozua mpango wa kuwachanja ng’ombe wote dhidi ya maradhi ya sotoka ambayo yalikuwa yakiathiri miguu na midomo. Ghafla habari hizo za kuchanjwa ng’ombe zikazagaa Zanzibar nzima kwamba wakoloni hawakuwa na lengo la kuwachanja ng’ombe dhidi ya maradhi yoyote bali lengo lao lilikuwa ni kuwaua. Kipindi hichi bei za bidhaa za kilimo zilikuwa juu hali iliyosababishwa na vita vya Korea. Kwa hivyo habari za kuuliwa ng’ombe ilikuwa ni tishio kubwa kwa wakulima kwalni ilikuwa ni kuhatarisha ubora wa maisha yao (Armit Wilson1986).
  Mara tu baada ya tukio hili la uchokozi wa wakoloni wa kiengereza, wakulima waliamua kujikusanya na kuanzisha umoja wa wakulima uliokuwa na harakati za kivitendo. Mapambano mengi baina ya wakulima na waengereza yalizuka. Wakati vuguvugu liliporipuka waengereza walikuwa wakitumia njia za mabavu kulizima na hatimae kuwauwa wakulima na viongozi wao kutiwa mbaroni. Mara moja wakulima waliwahi kulivamia gereza na kufanya fujo kubwa hadi kufanikiwa kuwakomboa viongozi wao. Tukio hili liliwapelekea waengereza kutumia mabavu zaidi na kuwatia tena mbaroni viongozi hao wa wakulima. Miongoni mwa viongozi hawa waliokuwa mashuhuri na maarufu hawa wafuatao
  1. Maalim Zaidi
  2. Bwana Miraji Shaalab na
  3. Bwana Haji Hussein

  Baada ya muda vuguvugu jipya lenye muelekeo wa kisiasa likazuka. Vuguvugu hili lilikuwa na lengo la kupambana na ukandamizaji wa waengereza. Viongozi wale wa wakulima wakaamua kuanzisha chama kilichoitwa “Chama cha umoja wa raia wa Sultani”. Chama hichi kiliitwa hivi kwa kuwa uraia wa Sultani haukuwa kitu cha ajabu. Ukoo wa sultani ulikuwa umeshapoteza uarabu wake wa asili na kuwa waswahili baada ya miaka mingi ya michanganyiko ya damu. Hivyo wakulima hawakumzingatia Sultani kama ni mgeni au mkoloni wao bali walimchukulia yeye na aila yake kuwa ndio wao mwenyewe. Hii ndio maana wakaona fahari kujitambulisha chama chao kwa jina la raia wa Sultani. Wengi walikiunga mkono chama hicho isipokuwa mabwanyenye wa mijini. Wao waliukubali umoja huo wa kitaifa lakini hawakukubaliana na kujinasibu chama hicho na uraia wa Sultani. Kutokana na upinzani wa mabwanyenye wa mijini kuhusiana na jina la chama hicho kuhusishwa na uraia wa Sultani. Hivyo basi jina jipya likapendekezwa na kukubaliwa liwe Chama cha kitaifa cha Zanzibar (Zanzibar Nationalist Party-ZNP). Kama kuna chama cha kujinasibu na wakulima hasa ni hichi maana chimbuko lake ni kutetea masilahi ya wakulima (Armit 1986).
  Ukabila na ugozi katika harakati za kudai uhuru
  Ukabila na ugozi sio katika wasifu wa kimaumbile wa mwanadamu bali ni nyenzo za kijamii zitumikazo kwa ajili ya kufikia malengo ya kisiasa hususan katika jamii za watu wenye migawanyiko mikubwa ya kijamii. Nembo za “Uafrika” dhidi ya “Uarabu” na “Ubara” dhidi ya “Uzanzibari” zilitumika kama ndio utambulisho wa kizalendo wa kizanzibari katika harakati hizo za siasa za kudai uhuru. Ukabila na ugozi kama asemavyo mtaalamu wa sayansi za siasa, Martin Doornbos, sio nyenzo za kutoa tafsiri ya chochote ndani ya mjengeko wa jamii za wanadamu lakini maneno hayo yenyewe ndio yanayohitaji kutolewa tafsiri. Ukabila na ugozi hujengwa pale patokeapo vita vya madaraka baina ya makundi na matabaka yaliomo katika jamii. Suala la kuunasibisha utambulisho wa kizalendo na ukabila, ugozi na urangi inaonekana ni la kutegemea mazingira ya kisiasa na ya kijamii katika jamii husika na kwa wakati maalum.

  Inaonyesha wazi kwamba, baadhi ya mazingira ya kijamii hayawezi kutumia utambulisho wa kizalendo kwa misingi ya ukabila au ugozi. Kwa mfano jamii nyingi za Afrika ambazo zina mivutano mikali na isiyokwisha ya ukabila katika nchi kama vile Congo, Ruanda, Burundi Uganda na Kenya, nchi zote hizi watu wake takriban wote wana ngozi nyeusi na makabila ya kibantu. Hawa wao wote wanajitambua kama ni wazalendo katika nchi zao bali makabila hugombania kutofunikwa na makabila wenzake. Hata hivyo zipo jamii zinazoona ni fahari zaidi kuupima utambulisho wao wa kizalendo kwa kuzingatia makabila yao na rangi za ngozi zao. Hii hutokea pale jamii moja inapoona ipo haja ya kuitenga jamii nyengine kwa hisia ya “ugeni” na “uwenyeji/uzawa”. Lengo kubwa ni kuweka msingi wa tofauti baina ya jamii mbali mbali kwa lengo la kuzitenga baadhi ya jamii hususan kiutawala. Pia wapo wataalamu wa sayansi jamii ambao huupima utambulisho wa kizalendo kwa kuangalia historia ya watu hao, utamaduni wao na athari yao kiujumla katika jamii kubwa waliomo. Hii ina maana kuutambua utambulisho wake wa kizalendo kundi la jamii halina budi kujiuliza swali “sisi tulikua nani na tulitokana na nani hapo kabla?”, “iko wapi athari ya asili yetu katika jamii kubwa tulioko?”.
  Zanzibar ilikuwa na kambi mbili kuu katika harakati za kisiasa za kudai uhuru zilizoutafsiri utambulisho wao wa kizalendo kwa misingi tofauti. Kambi ya kwanza ni ile iliyotumia misingi ya ukabila na ugozi na kuwatambua wazanzibari kama sehemu ya waafrika, wenye ngozi nyeusi, wenye asili ya makabila na utamaduni wa kibantu na kinyume chake wale wote wasiokuwa na sifa ya uafrika ni wageni katika Zanzibar. Kambi ya pili ni ile ambayo haikujali sana rangi au aina ya ngozi za watu walizonazo. Kambi hii ilizingatia zaidi historia refu na pana ya wahenga wao. Hapa kilichoangaliwa ni ipi katika jamii iliyopo ina mizizi mirefu na mipana katika Zanzibar? Pia ilizingatia ni nani katika waliopo ndio waliotoa athari kubwa katika utamaduni wa wazanzibari? Iliangalia lugha za wazanzibari, lahaja na lafudhi zao, imani zao na ustaarabu wao kiujumla. Wafuasi wa kambi hii waligundua kuwa washirazi na waarabu ndio watu walio na mizizi mirefu na mipana ndani ya Zanzibar. Halkadhalika utamaduni wao, ikiwemo lugha zao, lahaja zao, lafudhi zao, na imani zao katika dini ndio mambo makuu yanayopamba ustaarabu wa wazanzibari. Hata hivyo kambi hii haikuwatenga waafrika wenye asili za kibantu alimradi tu nao wanayo mizizi mirefu na mipana ndani ya ardhi ya Zanzibar.
  Kuanzishwa na muelekeo wa siasa za ZNP (Jogoo)
  Chama cha mwanzo cha siasa kuundwa kwa lengo la kupigania uhuru kilikuwa ni Zanzibar Nationalist Party (ZNP), yaani chama cha kiraia, au kwa kiarabu Hizbul-wattan, kwa maana hiyo hiyo ya chama cha kiraia. Chama hichi kiliundwa katika mwaka wa 1955 kufuatia kumalizika vuguvugu la vita vya ng’ome. Miongoni mwa waanzilishi na wafuasi wa mwanzo wa ZNP walikuwa hawa wafuatao.
  1) Bwana Vuai Kitoweo
  2) Bwana Ramadhani Khamis
  3) Bwana Haji Hussein
  4) Bwana Othman Sudi
  5) Maalim Makusudi
  6) Maalim Wazir bin Maalim
  7) Sheikh Mahmoud Kombo
  [​IMG] Bwana Miraji Shaalab
  9) Sheikh Rashid Hamad
  10) Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani
  11) Bwana Amani Thani n.k

  Katika makala yake ya Tanganyika and Zanzibar Union, Profesa Haroub Othman ameandika kwamba Chama hichi kiliongozwa na sera za utaifa (uzalendo) na jitihada za kuwaunganyisha wazanzibari wote katika harakati za kudai uhuru dhidi ya mkoloni Muengereza. Hivyo basi wananchi wa makabila na asili tofauti, yaani washirazi, waafrika, waarabu, wahindi, wakomoro, washihiri na wengine wengi walijitokeza kukiunga mkono chama hicho.
  Chama hichi kilijaribu sana kutaka kulibadilisha wingu la ukabila lililokuwa limetanda hapo kabla kuelekea katika wingu la uzalendo. Hata hivyo chama hichi kilibatizwa jina la “chama cha waarabu” kwa kua kiliungwa mkono na waarabu takriban wote wa Zanzibar chini ya ushawishi mkubwa wa Sheikh Ali Muhsin Barwani, mwanazuoni wa dini ya kiislami ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Arab Association. Sheikh Ali Muhsin ni mtu aliyeheshimiwa sana na waarabu wenzake na wazanzibari wengine kutokana na misimamo yake ya kidini na siasa kali alizokuanazo dhidi ya wakoloni wa kiengereza tangu kabla ya vyama vya siasa kuundwa. Sheikh Ali Muhsin hakuwa tayari kuuona u-Tanganyika unajipenyeza ndani ya Zanzibar, kwa kuwa ni utamaduni na ustaarabu tofauti na uzanzibari. Yeye mwenyewe bila shaka aliona kufanya hivyo itakuwa ni kulinda utamaduni na ustaarabu wa wazanzibari uliojengeka kwa misingi ya dini ya kiislamu kutokana na kumezwa au kuathiriwa na utamaduni wa watanganyika. Picha hiyo hapo juu ikionesha mkutano wa hadhara wa ZNP bila shaka itausuta ule usemi kwamba chama hicho kilikuwa ni cha waarabu kwa kuwa hakuna sura ya kizanzibari iliyokosekana katika picha hiyo.

  Chama cha ZNP hakikuzaliwa na jumuiya yoyote ya kikabila wala mawazo ya ukabila katika zile jumuiya zilizokuwepo hapo kabla. Waliounda chama hichi ni watu waliotokea jumuiya mbali mbali za kikabila na za kiraia waliofahamu kuwa kwa kulinda makabila kamwe Zanzibar haiwezi kujikomboa. Ndipo watu hao wa makabila mbali mbali, wakulima, wasomi nk walipokutana na kuunda chama cha ZNP kwa lengo la kukusanya nguvu za kizalendo kuikomboa Zanzibar. Hapa ieleweke kuwa kiongozi wa Jumuiya ya waarabu, Sheikh Ali Muhsin hakuwepo Zanzibar wakati chama hichi kinaundwa. Wakati huo chama cha ZNP kinaasisiwa Sheikh Ali Muhsin alikuweko London kwa Malkia, kuyawasilisha madai ya jumuiya ya waarabu ya kuhimiza uhuru wa Zanzibar. Habari za kuundwa chama cha ZNP, Sheikh Ali Muhsin alizipata baada ya kurejea Zanzibar. Chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kiliundwa na Washirazi na Waafrika wa Kiembe Samaki na baadaye wakaungwa mkono na wajumbe wa Arab Association. Hatua hiyo ndiyo inayotumiwa kukivalisha chama hicho sura ya kikabila. Ushahidi mzuri ni katika uchaguzi mkuu wa mwisho kabla ya Mapinduzi wa Julai 1963, ZNP na ZPPP walipata kura 46% wakati Waarabu katika visiwa walikuwa asilimia 16% tu. Jambo la kuzingatia hapa ni kwamba waarabu, wote kwa ujumla wao walikiunga mkono chama hichi kutokana na kuwa chama chengine kikuu mpinzani wa ZNP, yaani ASP kilikuwa wazi wazi kikiwakataa watu wasio na asili za kiafrika na kishirazi. Hivyo basi watu wa makabila mengine kama vile waarabu, wahindi na wakomoro walikiona sio chao na walikiona ZNP ndio chama chao.
  ZNP ilijaribu kuyawakilisha makundi yote ya kijamii ndani ya chama. Japo kuwa ZNP ilihakikisha ina wasomi wa kutosha lakini pia ilitambua kuwa inahitaji kuungwa mkono na watu wa kawaida kama vile wakulima. Hivyo basi watu wasiokuwa wasomi nao wakakiunga mkono chama hichi na hata kushika nafasi za juu kama vile Bwana Vuai Kitoweo, mshirazi wa kimakunduchi ambae alishikilia uwenyekiti wa chama hichi. Chama hichi kiliwatambua wazanzibari kuwa ni raia wote wenye mizizi mirefu ndani ya Zanzibar bila ya kujali asili na rangi zao. Chama hichi kilipendelea utaratibu wa serikali ya kidemokraisia inayoongozwa na waziri mkuu na muendelezo wa ufalme wa kijadi usio na madaraka kama vile Uengereza.
  ZNP na harakati za kudai uhuru
  Hatua nyengine muhimu katika harakati za siasa za ZNP ilikuwa ni uondoshwaji wa uwakilishi uliojengwa kwa misingi ya ukabila. ZNP iling’ang’ania na kudai kwa wakoloni haki ya kila mtu mzima kupiga kura jambo ambalo lilipingwa vikali na wakoloni kwa kuwa lilihatarisha utawala wao. Pamoja na hili ZNP ilianza kupiga makelele kudai uhuru wa Zanzibar kuharakishwa ikiwa ni pamoja na kutumiwa kwa katiba mpya ambayo italazimisha na kuharakisha uhuru wa Zanzibar. Harakati za kudai uhuru za ZNP zilianzia katika Jumuiya ya waarabu. Baada ya kuchoshwa na uchaguzi wa wajumbe wa baraza la kutunga sheria kwa misingi ya ukabila Jumuiya ya waarabu waliamua kufanya mgomo kuyasusia mabaraza yote ya serikali. Mara tu baada ya kumalizika kwa mgomo huo Sheikh Ali Muhsin alitumwa na Jumuiya ya waarabu kusafiri kwenda Ulaya kuwasilisha madai ya Jumuiya hiyo ya mabadiliko ya katiba ili kuruhusu uchaguzi wa “mtu mmoja kura moja” pamoja na kuharakishwa kwa uhuru wa Zanzibar. Katika ziara hiyo Sheikh Ali Muhsin alipata nafasi ya kuzungumza na wakuu wa serikali ya Uengereza na wakuu wa vyama vya siasa na kuwasilisha madai yake. Mara tu baada ya kurejea Zanzibar aliwakuta wazanzibari wa jumuiya mbali mbali za kikabila wameshajikusanya na kunda chama cha siasa cha ZNP.

  Matokeo ya ziara ya Sheikh Ali Muhsin yalikuwa na matunda mazuri kwa Zanzibar. Katika mwaka 1956, serikali ya Uengereza ilimtuma mjumbe wake maalum Mr. Coutts kwenda Zanzibar kufanya uchunguzi juu ya madai hayo yaliyowasilishwa na Sheikh Ali Muhsin. Mara baada ya kuwasili, Mr. Cuotts alipokewa kwa shangwe na maandamano makubwa ya ZNP. Waandamananji walipiga kelele na walibeba mabango yaliokuwa na ujumbe wa kudai “kura moja kwa mtu mmoja”, kuharakishwa kwa uhuru wa Zanzibar, na kuondolewa kwa ubaguzi wa rangi na asili. Mr. Coutts alirejea Uengereza na kuwasilisha ripoti yake kwa Malkia. Baada ya muda serikali ya Uengereza ilileta ujumbe maalum kwa balozi wake aliyekuwepo Zanzibar kuwa madai ya ZNP ya “kura moja mtu mmoja” yamekubaliwa lakini suala hilo litaanzia na viti sita tu, viti vyengine sita vitaendelea kupatikana kwa utaratibu ule ule wa uteuzi. ZNP haikufurahishwa na uwamuzi huo ingawa nafuu ndogo ilipatikana na hivyo basi iliendelea na juhudi zake.
  Baada ya kelele nyingi za ZNP za kudai katiba mpya na uhuru wa Zanzibar serikali ya Uengereza ilimtuma mjumbe mwengine mwaka 1960 ili kuja kuangalia kama kweli Zanzibar imefikia hatua ya kupewa uhuru wake. Mjumbe huyu alikuwa ni Sir Hilary Blood. ZNP kama ilivyo kawaida yao walifanya maandamano makubwa kuonyesha hisia zao na madai yao kwa Sir Hilary Blood. Mara hii walibeba mabango yaliyoandikwa “UHURU 1960” wakimaanisha wanataka uhuru wa Zanzibar si zaidi ya mwaka wa 1960. Sir Hilary Blood alipofika Zanzibar alivikuta vyama vitatu vya ZNP, ASP na ZPPP. Vyama vyote hivi vya siasa pamoja na vyama vya kijamii walisoma risala zao kwa Mjumbe huyo wakiwasilisha madai yao. Sehemu ya risala ya ZNP ilikuwa hivi:
  “……….Si wakati tena sasa wa kuhoji kama tunayo haki ya kujitawala wenyewe au hatuna uwezo wa kufanya hivyo. Siku za kufanya hivyo zimeshapita leo hii hakuna tena kambi mbili juu ya suala hili (la kujitawala wenyewe). “…………baraza la kutunga sheria lazima lichaguliwe na wananchi na serikali iundwe upya kuruhusu mfumo wa wizara. “…………kwa namna yeyote mtakuwa hamfanikiwi wajibu wenu ila ni kuwaudhi wananchi wa Zanzibar pindipo mkilazimisha jambo lolote lisilokuwa uhuru kamili wa Zanzibar”.

  Kuanzishwa na Muelekeo wa siasa za ASP (Kisima)
  Katika mwaka wa 1957, miaka miwili baada ya kuundwa kwa ZNP, Chama cha Afro – Shirazi kiliundwa. Chama hichi kilizaliwa na muungano wa jumuiya mbili za kikabila, African Association (yaani jumuiya ya kutetea masilahi ya wazanzibari weusi wa asili ya kiafrika) na Shirazi Association (yaani jumuiya ya kutetea masilahi ya wazanzibari weusi wa asili ya kishirazi) kupitia ushawishi wa ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa kikoloni (Isaa 1999).

  African Association (AA) ilikuwa tawi dogo la Tanganyika African Association (TAA) ambayo iligeuka na kuwa TANU katika mwaka wa 1954. Kama walivyokuwa wazazi wake, ASP nayo ikaibukia na siasa hizo hizo za kukunwa na kutetea masilahi ya makundi fulani tu ya wazanzibari na kupuuza mengine. Kwa lugha nyengine chama hichi kiliridhika na kutosheka kuwawakilisha wazanzibari wenye asili ya kishirazi na kibantu peke yao. Baadhi ya waasisi wa chama hicho ni hawa wafuatao.
  1) Sheikh Abeid Amani Karume
  2) Sheikh Thabit Kombo Jecha
  3) Sheikh Moh’d Shamte Hamad
  4) Sheikh Ameir Tajo
  5) Bwana Abdalla Amur Suleiman n.k

  Katika kujitafutia uimara wa kisiasa na umaarufu Chama cha ASP kiliifumania itikadi ya ugozi kuwa ndio itakayowahamasisha watu walio wengi na kukikubali (Burges 2009:56). Bila shaka kutumia sera za ukabila za kupigania masilahi ya watu weusi walio wengi ulikuwa ni sera muhimu kwa wanasiasa wa ASP na turufu kubwa ya kutafuta uungwaji mkono wa wazanzibari walio wengi ambao ni wa asili za kishirazi na kiafrika. Hii ndio sababu ASP ilijifaidia umma mkubwa nyuma yake kuliko chama chengine chochote. Chama cha ASP kiliwatambua wazanzibari kuwa ni wale raia wote wenye ngozi nyeusi na wenye asili ya kiafrika. Chama hichi kilipendelea utaratibu wa serikali ya kijamhuri yenye kuongozwa na raisi ufuatwe baada ya uhuru na mfumo wa kifalme ukomeshwe.
  ASP na harakati za kudai uhuru
  Kuhusu katiba mpya na uhuru wa Zanzibar, chama cha Afro-Shirazi kilikuwa na utata mwingi. Wakati lengo kuu la harakati hizo ni kuharakisha uhuru wa Zanzibar, ASP ilionekana kutokuwa wazi juu ya msimamo wake kuhusu uhuru. Wakati vyama vyengine vilikuwa vikipigania kuharakishwa kwa uhuru, ASP ilipendelea zaidi kucheleweshwa kwa uhuru huo. ASP ilitowa matakwa na msimamo wake waziwazi mbele ya kamati ya uchunguzi iliyokuwa chini ya bwana Hilary Blood kwamba hakuna haja ya mabadiliko yoyote ya kikatiba kwa kuwa nchi ya Zanzibar kwa wakati huo haikuwa tayari kujitawala na kujiendesha yenyewe. Hivyo basi kwa mtazamo wa kizalendo Karume alikuwa kibaraka mdogo wa wakoloni kwa kuwakilisha mawazo yanayolingana na yale ya wakoloni. Hivyo basi wakoloni walifurahia sana sera na misimamo ya ASP ya kupalilia ucheleweshwaji wa uhuru wa Zanzibar. Madai ya ASP kwa Sir Hilary Blood yalikuwa ni kama yalivyo katika sehemu ya risala ya chama hicho hapo chini.
  “………Chama cha ASP kinashauri na kuwamini kwamba baraza la kutunga sheria lisiwe na zaidi ya viti 25 ambapo katika hivyo viti vitatu vitengwe kwa ajili ya maafisa wa serikali (wakoloni). Vilivyobaki ndio vipigiwe kura ya “mtu mmoja kura moja”. “…………..Maafisa wenyewe wa serikali wawe ni waziri wa sheria, waziri wa fedha na waziri wa ulinzi na mambo ya nje”. Maafisa wa serikali kwa mujibu wa katiba ya kikoloni walikuwa na wakoloni waengereza wenyewe.

  Maamuzi ya Sir Hilary Blood baada ya hapo hayakutofautiana sana na mapendekezo ya ASP kwani Sir Hilary Blood aliamua viti 22 vitapigiwa kura na nane vitatengwa kwa ajili ya uteuzi wa maafisa wa serikali. Kwa usaliti huu wa wazanzibari mbele ya wakoloni ZNP iliamua kumshitaki Karume lakini katika jambo hili ilikuwa ni sawa na kesi ya nyani kumpelekea tumbili na hivyo Karume alishinda kesi hiyo. Harakati za siasa za ASP kuelekea Uchaguzi wa kwanza zilipambwa na kampeni ya uchaguzi iliyojulikana kama “Uhuru zuia”. Wakati wanasiasa wanacheza ngoma yao ya siasa za kudai uhuru, Karume yeye anacheza ngoma ya jinsi gani madaraka ya nchi baada ya uhuru hayatawashirikisha waarabu na magoa. Raisi wa Ghana, nchi ya mwanzo kupata uhuru barani Afrika, Dr Kwame Nkrumah aliitisha mkutano wa vyama vyote vya siasa vinavyopigania uhuru Afrika, All Africa conference, mwaka 1958. Kwa upande wa Zanzibar, chama cha Afro-shirazi kiliwakilishwa na mzee Abeid Amani Karume, na chama cha Zanzibar Nationalist party kiliwakilishwa na Sheikh Ali Muhsin. Msimamo wa ASP kuhusu uhuru ulikuwa mbaya na wa kikoloni kiasi ambacho ujumbe wa ASP ilibidi kuondolewa mkutanoni lakini ujumbe wa TANU ukiongozwa na mwalimu Julius Nyerere ukakiokoa chama cha ASP kwa madai kwamba walikuwa wachanga na hawana uzoefu wa siasa.(wapi?).
  Katika kitabu chake, Bwana Maulid Mshangama anasema hivyo hivyo katika mkutano wa shirikisho la vyama vya kupigania uhuru Afrika mashariki na kati PAFMECA, uliyofanyika Mwanza mwaka huo huo wa 1958 kiongozi wa ASP alikataa kabisa kabisa kutia saini mkataba wa uhuru (Freedom charter) uliotayarishwa na Dr Kiano wa Kenya. TANU kwa mara nyengine ikawaokoa ASP kwa madai kwamba sio lazima kila mjumbe wa mkutano atie saini bali saini ya Mwenyekiti wa PAFMECA Bwana Francis Khamis wa Kenya ilikuwa inatosha. Hivyo basi inajuzu kusema kwamba chama cha ASP kiliundwa si kwa lengo la kupigania maendeleo na ukombozi wa wazanzibari bali kulinda hisia kali za ukabila na urangi jambo lililorahisisha masilahi ya wakoloni kwa kuendelea kuitafuna Zanzibar (Armit 1988.page). Kwa watu wengi waliokuwa wasomi ubeberu wa waengereza lilikuwa jambo baya zaidi kwao kuliko jambo jengine lolote. Hivyo basi dhambi ya kuunga mkono ukoloni ilikifanya chama cha ASP kudhoofika na kujikuta hakina msimamo wake mwenyewe wa kisiasa, hatimae kilipoteza hadhi yake kwa kujiparatisha kwa wakoloni. Sera kubwa za ASP ilikuwa ni kupinga kila sera na wazo la ZNP. Shabaha ya harakati za ASP ilielekezwa dhidi ya ZNP zaidi kuliko dhidi ya ukoloni wa waengereza uliokuwepo. ASP ilimudu hata kupingana na wazo na msimamo wa ZNP dhidi ya ujenzi wa kituo cha upelelezi cha kunasia habari (tracking station) cha wamarekani kilichokuwepo Zanzibar wakati wa ukoloni (Armit 1986).
  Fitna ya TANU katika harakati za kudai uhuru Zanzibar
  Chama cha ASP kina chimbuko lake muhimu kutoka Tanganyika. Kama ilivyokwisha kuelezwa hapo nyuma kuwa African Association (AA) ilikuwa ni tawi dogo la Tanganyika African Association (TAA) iliyoasisiwa na Nyerere ambayo iligeuka na kuwa TANU katika mwaka wa 1954. ASP ilikuwa na ofisi yake ndogo huko Dar es Salaam. Viongozi wa ASP hawakuweza kusafiri hadi wapatiwe hati za kusafiria kutoka katika ofisi ya chama iliyoko Dar es Salaam. Nyakati za chaguzi za Zanzibar na kampeni katika harakati za kuelekea uhuru Bibi Titi Mohammed na Bwana Ali Mwinyi Tambwe ambao wote ni watanganyika walikuwa wakipanda katika majukwaa ya siasa wazi wazi kwa kukiunga mkono na kukipigia debe chama cha ASP na kuvibomoa vyama vyengine vilivyopigania uhuru kwa itikadi za uzawa na unasaba (Thani 1995). Watoto wa wazee wa ASP kama vile rais mstaafu wa awabu ya tano wa Zanzibar Dr. Salmin Amour walikuwa wakichukuliwa na TANU na kupatiwa elimu huko Tanganyika.

  TANU ilikipa kila aina ya msaada chama hichi cha ASP ili kufanikisha siasa zake (Thani 1995). Katika makala yake ya Tanganyika and Zanzibar Union, Profesa Haroub Othman ameandika kuwa suala la TANU kujitokeza kukibeba chama cha ASP ndilo lililopelekea kuzuka kwa malumbano makali baina ya ASP na ZNP na kila mmoja kumuona mwenzake adui zaidi kuliko wakoloni waliokuwepo. Baada ya kuwa na shabaha moja ya mapambano dhidi ya ukoloni mapambano yalielekezwa dhidi ya vyama hivi vyenyewe kwa vyenyewe. Katika malumbano hayo ZNP ikidai ASP ikiunda serikali baada ya uhuru itaiuza na kuikabidhi Zanzibar kwa watanganyika na kuuhujumu uislamu. ASP kwa upande wake ilikuwa ikijibu malumbano hayo kwa kusema kwamba pindipo ZNP itaunda serikali baada ya uhuru itaurudisha utumwa na wazanzibari watakuwa vijakazi na watwana wa waarabu. Halkadhalika ASP ikiwataja viongozi wa ZNP kuwa vijukuu vya Sultani waliochachamaa kuhakikisha utawala wa kisultani juu ya watu weusi unaendelezwa Zanzibar.
  Ijapokuwa vyama vya ZNP na ASP vilitofautiana sana sera na itikadi zao, hapo mwanzoni vilionyesha mashirikiano ya hapa na pale katika harakati za kudai uhuru. Kitu kinachojidhihirisha wazi ni kwamba mashirikiano ya vyama hivyo yalikuwa yakififia kadri chama cha TANU kilivyokuwa kikijipenyeza katika siasa za Zanzibar. Tena kikijipenyeza kwa staili ya kupendelea na kuunga mkono upande mmoja (ASP) na huku ikihujumu upande mwengine (ZNP). TANU ilikuwa ikidai kwamba Zanzibar ni ya waafrika na sio ya waarabu kwa hivyo wazanzibari hawana budi kuunga mkono chama cha ASP ambacho ndicho kinachopigania masilahi ya watu weusi, waafrika wanyonge. Hili lilikuwa bila shaka ni kuyabomoa malengo ya kuanzishwa kwa umoja wa mashirikiano ya kupigania uhuru wa waafrika wa mashariki na kati (PAFMECA). PAFMECA iliundwa kwa lengo la kuweka mikakati ya kuunganisha nguvu za pamoja za vyama vya siasa vya kupigania uhuru. Si hayo tu TANU ilitoa mchango wake mkubwa chini ya Nyerere katika kufanikisha mapinduzi ya 1964.
  Kama itakavyoelezwa huko mbele kulifanyika mazungumzo ya mwanzo ya katiba ya uhuru wa Zanzibar huko Lancaster House mwaka 1962. Mazungumzo yalikuwa ni kati ya serikali ya ZNP/ZPPP na chama cha upinzani, ASP. Pamoja na mambo mengine katika mkutano huo kulipangwa kujadiliwa tarehe ya kutolewa kwa uhuru wa Zanzibar. ASP lakini kama kawaida yake haikuwa tayari kuuona uhuru unapatikana wakati serikali imo mikononi mwa ZNP/ZPPP. Hivyo basi ASP walikataa kuzungumza chochote katika mkutano huo na kusisitiza kuwa hapatakuwa na mazungumzo yoyote mpaka hapo uchaguzi mwengine utakapofanyika. Hata hivyo baada ya ZNP/ZPPP kushindwa jitihada ya kuwashawishi ASP wakubali kufanya mazungumzo hayo kwa maneno matupu ndipo walipoamua kuwaahidi kuwashirikisha katika serikali yao kwa kuwapa wizara tatu kati ya wizara nane pamoja na kura ya “veto”. Hivyo basi baada ya kukabidhiwa madaraka hayo ASP itakuwa si chama cha upinzani tena bali ni sehemu ya serikali, yaani ZNP/ZPPP/ASP. Kwa ahadi hiyo Karume alifurahi na kuwaambia ZNP/ZPPP wawape muda ili wakalitafakari suala hilo wakiwa peke yao. Baada ya hapo, Karume aliwasiliana na Nyerere kwa njia ya simu ili kusikiliza ushauri wake kuhusiana na ahadi hiyo waliopewa na ZNP/ZPPP. Kwa kuwa Nyerere hakupenda kuona ZNP/ZPPP wanaongoza serikali ya uhuru ya Zanzibar, aliwashauri ASP waikatae ahadi hiyo waliopewa na ZNP/ZPPP mara moja. Wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa makao makuu ya ASP Kisiwandui baada ya kufanikiwa kwa mapinduzi ya 1964, Sheikh Thabit Kombo alitoboa siri hii kwa kusema “Tunamshukuru Mwalimu Nyerere kwa kutuvua mtego waliotaka kutunasa mahizbu wakati wa mkutano wa mwanzo wa katiba huko Uengereza. Mahizbu walitaka kutufanyia ujanja wa kutaka tuungane pamoja katika kuendesha serikali. Na katika kutaka kutimiza ujanja wao, walikiri kutupa wizara tatu katika serikali yao. Lakini Mzee Karume kabla ya kusema lolote alizungumza na Mwalimu (Nyerere) kwa simu kumtaka shauri lake juu ya suala hili. Mwalimu alimwambia Mzee Karume asikubali kufuata shauri hilo la Hizbu kwani huo ni ujanja tu wa kutaka pasiwepo na upinzani. Mkitaka shauri yangu kataeni. Ndipo Mzee alipokataa.
  Nyerere alikuwa ni mtu muhimu sana katika mipango na utekelezaji wa siasa za ASP na mikakati ya kuvihujumu vyama vya ZNP/ZPPP. Kama itakavyoelezwa huko mbele mkono wa Nyerere ulikuwa wa aina yake na wenye umuhimu maalum katika kuyapanga, kuyaandaa na kuyatekeleza mapinduzi ya 1964. Alishiriki mipango ya awali ya mazungumzo kati yake na makomred na viongozi wa ASP waliodhamiria kufanya mapinduzi hayo. Nyerere alitowa mchango mkubwa wa silaha na mamia ya askari wa serikali yake katika kusaidia kufanikisha mapinduzi ya 1964. Ijapokwa katika hotuba zake wakati wa uhai wake aliwahi kutamka mara kwa mara kutohusika kwake na vurumai za Zanzibar za kabla ya mapinduzi na mapinduzi yenyewe lakini uhalisia wa mambo ni kinyume na matamshi yake hayo. Nyrere alikuwa mchezaji mkubwa na muhimu (significant role player) katika kuiunga mkono na kuiwezesha kambi ya ASP katika mapambano yake dhidi ya ZNP/ZPPP na hivyo basi hawezi kuachwa kuhusishwa na mafamikio na lawama juu ya yale yalioambatana na enzi hiyo kwa Zanzibar. Harith Ghassany anamnukuu Mzee Mohammed Omar ambae pia alijulikana kama Mzee Mkwawa kwa kuhusiana na Chief Mkwawa akibainisha kwa kina suala hili anadai lengo lao kubwa la kushirikiana na ASP ni kurudisha heshima ya waafrika wenzao. Mzee Mkwawa anasema:
  “Madhumuni yetu ni kutafuta historia yetu ya Kiafrika matokeo yalotokea baina ya Visiwani [Zanzibar] na Tanganyika. Mwaka wa 1960 kwenye mwezi wa tisa [Septemba] kama hivi, walitolewa vijana wawili kati ya Zuberi Mtemvu na Chipaka, kuja eneo la Wete, Pemba, kuja kufanya kampeni. Hawa walichukuliwa na chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kuja kufanya kampeni ili kuonekana chama cha TANU kibaya. Zuberi Mtemvu alisema mnachokifata si chama cha haki, mnafikiri ule msikiti mkubwa ulojengwa Tanga msikiti, lakini si msikiti ule wanasali Waislamu na Wakristo. Kwa hivyo kama mnafuata TANU mmepotea ndugu zetuni, wa visiwani. Nyinyi ni Washirazi, waumini, leo mnaweza kuungana na chama dhaifu kama TANU ambapo kiongozi wao hana maadili ya Kiislamu. Kwa hivyo nyinyi ule sio msikiti na kama yupo ambaye anaweza kuhakikisha kuwa ule ni msikiti kwa hivyo ajitokeze. Kwa hivyo mimi nikaona nijitokeze. Nikasema mimi nauwelewa sana, nawaelewa watu walokuwa wameshuhudia kuwa ule ni msikiti wakaukubali. Wa kwanza ni Sultan mwenyewe Abdalla bin Khalifa ni mmoja aloalikwa kuufunguwa huo msikiti. Msikiti mkuu wa Ijumaa wa Tanga. Kwa hivyo mimi nikaeleza Seyyid Abdalla alikuwepo, Sheikh Abdalla Saleh Farsi alikuwepo, Kabaka kutoka Uganda alikuwepo. Naskitika kusikia ati ule si msikiti. Kwa hivyo kama siku hiyo ndipo niliposema kama ni hivyo watu hawa watatu walitanassar wakafata dini ya Kikristo. Kwa sababu wamemfata kiongozi wa TANU wa Kikristo. Kwa hivyo hapo niliona uchungu. Nikakata kadi ya Afro-Shirazi si ku hiyo nikawa mwanachama rasmi. Kwa hivyo hata shughuli zangu, mimi nilikuwa ni mjenzi…kama sub-contractor nikichukuwa majumba kujengesha, nilinyimwa. Nilinyanganywa kabisa shughuli zote. Nikafutiwa. Sasa kwa Zuberi kusema hivyo alikuwa kanunuliwa. Akaona awafurahishe mabwana lakini ana hakika kuwa yeye Zuberi ule ni msikiti. Lakini kwa sababu ya mambo ya kampeni ilibidi azungumze hivyo apate haja yake. Baada ya hapo mkutano ukafungwa, watu wakarudi, na mimi nikawekwa kituoni Wete, nikahojiwa umetuharibia kampeni yetu wewe, hufai. Nikaandikwa. Nikatiwa katika Tanganyika Standard ili nisafirishwe, wakati niliishi katika hapo mahala si chini ya miaka kumi na tano niko hapo. Hapo Pemba. Kwa hivyo nilipokuwa nimenyimwa kula kitu, hata nikenda dukani kutaka kitu japo kipo naambiwa hakipo. Nikawa nadhilika, nikatafuta mashuwa, nikapanda nikarejea Tanga. Ile kurejea Tanga nikafika ndani ya mikono ya serikali, nikahojiwa, nikakamatwa immigration paspoti sina, wakati ule mkubwa wa immigration wa kwanza alikuwa Alkabeza wa Mkoa wa Tanga. Myamwezi huyu. Kwa bahati asubuhi nikawachiwa nikaja zangu nyumbani. Kufika nyumbani si nikakaa kiasi ya wiki moja ya mapumziko, nikafatwa na Mkuu wa Mkoa pamoja na wazee wa TANU, nikachukuliwa ofisini, kwa Mkuu wa Mkoa, marehemu Bwana Jumanne Abdalla. Akanambia “tulikuwa tunataka mtu anaweza kuijuwa Unguja na Pemba vizuri kwa hivyo tumefurahi kukuona wewe.” Kwa hivyo mzazi wangu akanambia “utatumikia”. Kwa vile unaelewa utatumika kwenda, lolote la kule la kulielewa tukalipata sisi hapa. Kwa hivyo alikuwa mzee wangu hasa alonizaa mwenyewe, Mzee Omari, na jamaa yangu Mwalimu Mlimhere, na wengineo, kina Abdalla Rashid Sembe, kina Kisenge, waziri huyu alikuwa. Kwa hivyo nilishughulika nikaambiwa nirejee Unguja. Kwa hivyo nikakubali kutumika. Nikaambiwa utakwenda Unguja pamoja na vitu vetu, kama barua hivi, security inaweza kujuwa hizi siri, kwa sababu security ina vyombo vya mivuke, barua inachanuka wenyewe, ikasomwa halafu ikarudishwa ikafika mahala. Tunazungumzia mwaka 62. Kwa hivyo nikaanza kushughulika kwenda kule nikapeleka barua kule kama kutambulisha huyu kuwa ndiye atakayekuwa anawasiliana. Na nilifika ofisi Kijangwani. Na nikapokewa vizuri sana na waheshimiwa kina Aboud Jumbe, kina Saleh Saadalla, wengi tu.Barua zinatoka huku. Na mwenzetu, mkuu wetu wa safari alikuwa ni Master Oscar Kambona, ambaye alinichaguwa mimi na marehemu Issa Mtambo. Lakini ilikuwa lazma tukutane kule [Zanzibar]. Kwa hivyo mimi nikaambiwa nikutane na Issa na naweza mpa maelezo yangu niliyoyagunduwa mimi kule ayapeleke moja kwa moja kwa Oscar. Hata ndipo nliporudi tena ndo tukaanza kampeni ya kuona katika uchunguzi wetu kuiona hali ya Unguja na Pemba kwenye uchaguzi umeingiliana na Sultani kauvalia njuga. Kwa hivyo tulipata ari tukaona lazima tutetee Uafrika. Itabidi mimi nijitolee hali mali, kwa hivyo nikarudi Tanga nikawaambia hali ya huko ni ngumu kwa sababu Ufalme umeingilia kati. Hili suala ni gumu. Sasa lazma haya yetu tuchukuwe ziada. Kukaa kuendelea kiasi ya miezi miwili, uchaguzi karibu karibu, ZNP wakaanza kuchukuwa watu kujaza majimbo kutoka Kenya kuwatia Zanzibar. Kwa hivyo tukashtuka na sisi tukaanza kuomba misaada Tanganyika kupata watu wa kuweza kuwachukuwa na kuweza kupiga kura. Kwa hivyo tukaweza kuchukuwa watu kutoka Tanga, vijiji vyote vya Tanga, wanaojuwa lugha, lafidhi nzuri ya Kiswahili inofanana na Unguja. Kwa hivyo tukafanya hivyo. Tukachukuwa wake, waume, vijana, wavulana wanojiweza. Kwa hivyo tukapeleka Pemba na Unguja. Vijiji vya Mkoa wa Pwani wote. Mikoa ya pwani na walokuwa lugha zao mbaya tulikuwa tukishawatia Unguja tunawatia chuoni mule ndani ya nyumba tunamowaweka. Na tulikuwa tunatumia kuwapa kila mtu mwana wa Afro-Shirazi kumpa watu watano alale nao, kumi, na wanafundishwa Kiswahili safi, na kijezo kilokuwa cha madhumuni, kilikuwa ni kijezo cha kuweza kutaja “halwa”, kutaja “binzari”, “tangawizi”. Kwa hivyo walikuwa wana uhakika hawa watu wa Unguja, kuwa watu wa bara hawawezi kutamka Kiswahili kama hicho. Kwa hivyo, tulifuzu katika watu tulokwenda nao wakaweza kutumia lugha vizuri, walipita. Ilikuwa sentensi yako kabla hukiingia katika kuandika kutaka kwenda kupewa cheti, tiket ya kwenda kuvoti unaambiwa “taja suala hili, hii nini, inaitwa nini?” Majina yameandikwa. Hii taja, hii ni halwa, tangawizi, binzari. Kwa hivyo walipita. Kwa sababu tuliwafundisha si chini ya miezi mitano, sita. Tumo ndani ya kuwafundisha lugha ile mpaka wakaelewa kuwaita watu kwa lafidhi za Kiunguja, japo wengine walikuwa wakijikwara, lakini ilikuwa si rahisi kumtambuwa. Kwa hivyo tulifuzu, tukaanza kuingia. Tukakaa kitako. Sasa kabla ya kura, tulipoona kuwa sasa vipi tutapata wanachama wengi katika upande wa Pemba, ikabidi tuwalishe yamini kwa sababu wote Pemba walijihisi ni Hizbul Watan (ZNP). Wote. Kwa hivyo pamoja na ZPPP, wakijifanya wao ni Washirazi, si Waafrika.2 Kwa hivyo sasa mtu alipokuwa akitaka aingie chama, tukifanya kampeni aingie cha Afro-Shirazi, tunampiga kampeni, tunampa msahafu, aape “Wallahi Billahi Tallahi mimi nitaipigia kura Afro-Shirazi hapo kama kuna sadaka ya kumhangaisha tunampatia. Na awe ana wazimu akiiunga mkono Hizbu. Awe akili zake si timamu.” Wengine walitupigia, wengine waliona haiwezekani. Kwa hivyo tulifaulu sana, hata vijiji vilokuwa vigumu, kijiji kimoja cha Ole na Kangagani, kilikuwa kigumu sana, kwa hivyo nilikwenda mimi pale nikaitwa “Tindo.” Nikaipauwa, nikajenga shule ya pale. Pale nilifanya vituko vangu, pesa ya pale yote nikaiwacha pale. Nikawanunulia wanawake pale nguo. Nikaweza kupata wanachama pale na ilikuwa hakuna, kwa hivyo tukamwita Mzee hayati Karume, akaweza kuingia Kangagani na kufanya mkutano mkuu. Tukaipata Ole. Baada kufanya hivyo wakajuwa ni mimi nilofanya hivyo, hakuna alofanya isipokuwa yule fundi aloletwa. Kwa hivyo ikabidi mimi nitoke, nikaja kijiji cha Ole, Dodo. Pale usiku wa saa saba, nikatoka ili kufanya kampeni zangu, nikakamatwa kijiji cha Macho Mane, njia ya kwenda uwanja wa kutua ndege Vitongoji. Nikakamatwa hapo. Nikakamatwa na gari la Mohamed [Ahmed] Nassor Mazrui, ndo lilikuwa ni gari lake, na vijana kina Mtendeni, kina…wengi tu, kina Mkomi, kina Hatibu. Nikakamatwa, nikarudishwa Ole usiku huohuo. Nikatiwa kula rangi, nikapigiwa beni, nikaitwa “Kitimbakwiri cha Tanganyika”. Kwa hivyo nikakokotwa, nikapigwa sana, na nikatiwa pilipili lakini kwa bahati nzuri kulikuwa na Inspekta wa Kingazija, aitwa, kama Khamisi hivi, kile kifupi, pamoja na chini yake Master Benecto. Pilipili nilipakwa mwilini. Kwa hivyo, kupelekwa Ole, nyumbani kwa candidate [mgombea] mwenyewe anayesimamia uchaguzi, yule ndiye atakayechaguliwa, Sheikh Rashid Hamadi. Wakaanza kupiga kelele wakamwita kwa jina lao la kichama “Ya Zaim!” Wakapiga kelele “Hayyen na Mkashkash!” Kwa hivyo tumekikamata hichi kitimbakwiri. Mimi nikatamka, nikamwambia “nakusikitia Sheikh Rashid hujapata kutawala unaanza kuuwa. Ukitawala utakuwaje? Wewe unaamrisha kikundi hiki kinikamate na kunitesa.” Kabla ya hapo, baada kumaliza hapo, wakaingia yule Inspekta pamoja na wa chini yake, Master Benecto, wakamwambia “unafahamu suala, kitendo kinopita kisheria unawezekana kuwa kesho usisimame kwenye uchaguzi? Kwa hivyo hichi kitendo kiondoke.” Kwa hivyo Sheikh Rashid akatowa amri palepale “mwachilieni! Mimi wala sikuwatuma nyie. Mmejifanyia kwa hamasa zenu na ari zenu za siasa tu, lakini mimi siwezi kuamrisha kitendo kama hicho cha haramu.” Kwa hivyo nikaachiwa, nikarudi, nikapelekwa hospitali Chake Chake, nikahudumiwa na kijana, huyu alikuwa ni dresser msaidizi wa daktari, anaitwa Hassan Al Maardhi, wa Mtambwe kwao. Kwa bahati palikuwa na daktari mmoja wa Kiarabu, Dr Mahfudh, kwa hivyo alisaidia sana, nashkuru. Nikatiwa malhamu, nikatoka malengelenge, majimaji kwa lile joto la pilipili, na mpaka leo mbavu, hivi nnavozungumza hapa, mpaka leo mbavu huwa zanibana bana, kwa sababu zisizokuwa za kawaida—pilipili. Kwa hivyo nikaachiwa. Kuwachiwa, sasa mimi wakanitia moto zaidi. Hapo nikapamba moto. Nikachukuwa hatua kubwa sana ya kuigombania Afro-Shirazi kuliko hapo. Ndipo nilipoweza kuja huku, nikarudi Tanganyika, nikaanza kuchukuwa watu kwenda fanya kampeni, nawaorganise [nawapanga] watu…nikisha waorganise nawachukuwa nawapakia ndani ya magari, watu wa town [mjini] pale, na branch [tawi] yangu ilikuwa ni ile ya chama cha Wazungu, Magiriki, barabara ya kumi na nne. Kwa hivyo nikashirikiana na Chama cha Wafanyakazi [Tanganyika Federation of Labor] kiongozi, Bwana Victor Mkello. Kaweza kunikusanyia watu kufanya kampeni na kuweza kupata watu nikawa napakia hapa nenda nao kutoka [barabara ya] kumi na nne Head Quarters [makao makuu] nenda nao moja kwa moja napita njia ya Pangani, kijiji cha Kipumbwi. Nilikuwa nikipakia ndani ya mabasi yanoelekea njia ile ya Pangani na kutoka mashamba ya mkonge. Mabasi kutoka Tanga yalikuwa ni gari ya Abdalla Saidi, marehemu sasa, magari yakina Hashu Sleman, mabasi ndo yalokuwa wakati huo yapo. Na magari mengini yoyote, yoyote yale, yanoelekea njia hiyo walikuwa watu wanarukia. Hata magari ya mizigo. Sio lazima basi. Kwa hivyo nikatia watu kwenda kuandikisha na kuwarudisha na kuwapeleka tena, kutegemea chaguzi…………….” (Ghassany 2010).
  Kuanzishwa na muelekeo wa siasa za ZPPP (Nduaro)
  Mwishoni mwa mwaka wa 1959, chama chengine cha siasa kilichojulikana kama Zanzibar and Pemba people’s party (ZPPP) kiliundwa. Chama kilianzishwa na washirazi waliouasi uongozi wa Karume ndani ya ASP (Burgess 2009:69). Waasisi wa chama hichi ni baadhi ya viongozi waliokihama chama cha ASP baada ya kukerwa na viongozi wenzao. Viongozi hawa waliojitenga waliiona ASP inawajali zaidi na kuwaheshimu waafrika na kuwadharau washirazi. Kuanzia hapa washirazi walianza kujitambua kuwa udugu wao ni bora zaidi kwa waarabu wa Zanzibar kuliko wabantu kutoka bara (Burgess 2009:69). Kwa mujibu wa washirazi na chama chao cha ZPPP, kuwatambua waarabu kama ndugu zao ndio njia pekee ya kuunusuru mustakbali wa utamaduni na ustaarabu wa wazanzibari na dini yao ya kiislamu. Kinyume chake, kuunga mkono ushawishi wa Nyrere na utanganyika uliokuwemo ndani ya ASP ni hatari dhidi ya utamaduni wa wazanzibari na dini yao. Chama hichi kiliunga mkono utaratibu wa serikali ya kidemokrasia chini ya waziri mkuu na mwendelezo wa kuwa na mfalme wa kijadi usio na mamlaka ufuatwe baada ya uhuru. ZPPP kama ZNP walimtambua mfalme wa Zanzibar kama mzalendo mwenzao atokanae na aila yao. Katika kitabu chake cha “Kwaheri ukoloni kwaheri uhuru, Zanzibar na mapinduzi ya Afrabia”, Harith Ghassany anamnukuu Mzee Mohammed Omar ambae pia anajulikana kama Mzee Mkwawa kwa kuhusiana na Chief Mkwawa. Mzee Mkwawa anatoa sababu ya ZPPP kuwakana ASP kwa itikadi ya uzawa:

  “………..Tukapata viti va kutosha. Ikawa viti vilivotuangusha ni viti va Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP), viti sita. Tukasema, tutafanikisha. Tukamfata mwenzetu Mohamed Shamte, tukamvika buibui, tukaja naye YASU, mpaka kwa mkwewe Othman Sharifu. Akatujibu kuwa “hata mkinipa utume sitaweza kuwa pamoja na nyinyi.” Maneno hayo aliyasema nyumbani kwa mkwewe, Othman Sharifu. Na juhudi hizo zote alizifanya Othman Sharifu. Kumchukuwa mkwewe, akashirikana na wenzake kina Mdungi Usi, kina Saleh Saadalla. Karume akajitolea kuwa uongozi wote nitakupa wewe, mimi niwe chini yako, au niwache kamwe, niwe mtu wa kawaida lakini serikali iongozwe na Waafrika. Shamte akakataa. “Hata mkanipa utume,” nasema tena. Shamte alisema sitaki tu kuungana na watwana kama nyie………..”(Gassany 2010).
  Asili ya chama hichi ni pale mpasuko ndani ya ASP ulipozuka. Mpasuka huu ulizuka pale Sheikh Ameir Tajo alipopeleka madai kwa Waengereza kwamba Zanzibar haijawa tayari kupata uhuru baada ya uchaguzi wa 1957 kwa kuwa viongozi wengi wa chama chao cha ASP kilichoshinda uchaguzi hawakuwa na uwezo wa kuendesha serikali. ASP walipogundua kwamba Sheikh Ameir Tajo ndie aliyepeleka habari hizo kwa Waengereza, wakaamua kumfukuza katika chama. Sio kufukuzwa tu katika chama lakini mwanazuoni huyo maarufu wa Zanzibar wa dini ya kiislamu alitukanwa matusi makubwa na wafuasi wa ASP jambo ambalo lilichukuliwa kuwa ni kumdhalilisha yeye na kuudhalilisha uislamu. Huo ndio ukawa mwanzo wa mgawanyiko ndani ya ASP. Baada ya kufukuzwa Sheikh Ameir Tajo katika ASP, viongozi wawili wa ASP Sheikh Moh’d Shamte na Sheikh Ali Sharif wakaamua kumuunga mkono Sheikh Ameir Tajo na hivyo na wao kuihama ASP. Waasisi wa chama cha ZPPP ni wakiwemo hawa wafuatao.
  1) Sheikh Ameir Tajo
  2) Sheikh Moh’d Shamte
  3) Sheikh Ali Sharif
  4) Bwana Abdalla Amour Suleiman nk


  Baadae Bwana Ali Sharif na Bwana Abdalla Amour walirejea tena katika ASP. Misingi na itikadi za chama hichi zililingana na itikadi na misingi ya chama cha ZNP jambo lililokuwa chachu ya vyama vya ZNP na ZPPP kuungana pamoja na kuwa na mashirikiano ya kisiasa dhidi ya ASP.
  Umma party
  Mara tu baada ya kumalizika uchaguzi wa Juni 1961, Wakati huo huo, ulizuka mtafaruku na migongano ndani ya chama cha ZNP juu ya mwelekeo wa Zanzibar kuhusu itikadi na sera za uchumi za kufuata baada Uhuru. Mtafaruku huo ulikuwa kati ya viongozi wake wakuu Sheikh Ali Muhsin, aliyekuwa na kundi kubwa la wafuasi, na Bwana Abdulrahman Mohamed Babu, Katibu Mkuu wa chama na mwenye kundi dogo la wafuasi. Wakati Sheikh Ali Muhsin alitetea sera na siasa za mrengo wa kulia na utii kwa Sultani, Babu kwa upande wake alikuwa muumini mkubwa wa itikadi za Karl Marx, mbinu za ukomunisti wa kichina na chuki kwa ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo. Wafuasi hao wa Babu katika itikadi yao ya ukomyunisti walijulikana kama makomred. Makomred ni watu waliounga mkono ukomyunisti kwa moyo wao wote na kuufanya kuwa sehemu ya imani yao. Kama walivyokuwa viongozi wao wa juu ulimwenguni Karl Marx na Lenin makomred pia hawakuamini Mungu wala kuwepo kwake. Walifahamu dini ni utaratibu wa kuijengea jamii nidhamu, woga na utii ili kurahisinya unyonyaji unaofanywa na mabepari. Makomred waliamini kwamba kuwepo kwa makundi mawili katika jamii, lile la matajiri na lile la masikini sio jaala ya Mwenyezi Mungu bali ni unyonyaji na unyang’anyi wa watu wachache kujitajirishi kupitia mfumo wa kibepari na wengi ambao ndio wanaonyonywa kubakia masikini. Hivyo basi makomred waliamini dini ni chombo kilicholetwa na mabepari ili kuwajengea wale wanaonyonywa imani kwamba umasikini wao na utajiri wa wenzao si matokeo ya jitihada zao bali majaala ya Mungu yasioepukika. Kutokana na kukosa itikadi madhubuti ya kidini makomred walikuwa na utamaduni wa kukosa heshima na nidhamu. Hawakuwa na huruma wala ubinadamu.

  Wakati ASP ikijishughulisha zaidi za kupeleka wafuasi wake nje ya nchi kusomea fani mbali mbali za kitaalamu ZNP wao kwa ushawishi wa Babu walipeleka wafuasi wao kuchukua mafunzo ya kivita. Akiwa katibu wa ZNP Babu alipeleka wafuasi wake Cuba na China kwa mafunzo ya kijeshi na mbinu za kivita vya msituni, na ambao siku chache tu kabla ya Mapinduzi ndio kwanza walikuwa wanarejea Zanzibar kutoka mafunzoni. Hii ni katika mipango ya awali ya Babu ya kufanikisha mapinduzi ya Zanzibar pindipo jitihada za kidemokrasia zitakapomuia vigumu. Wote waliopata mafunzo ya kijeshi walikuwa ni makomred wafuasi wa Babu waliokuwa na utiifu mkubwa kwake na siasa yake ya ukomyunisti wakati Sheikh Ali Muhsin kwa bahati mbaya hakujua malengo hayo ya Babu ya baadae.
  Baada ya ZNP kuzifahamu itikati na siasa za makomred hawakupenda tena kushirikiana nao. Visingizio hivi na vile alivitoa Babu kasikitia ulalamishi ndani ya ZNP baada ya kukataliwa ombi lake kutaka lazima watu wake (makomred) wasimamishwe wagombea katika majimbo ambayo ZNP ilikuwa na uhakika wa kushinda. Baada ya kukataliwa ombi lake hilo akakihama chama hicho yeye na wenzake wawili wanaounda makomred top three. Mara tu akatangaza kuunda chama chake, Umma party. Ktika mkutano wa hadhara mara tu baada ya kuundwa kwa umma partry, maelfu ya watu walikusanyika wakiwa na hamu ya kumsikiliza Babu. Babu aliupamba mkutano huo kwa kumpiga mabomu ya kisiasa Ali Muhsin kwa kusema: “Alaamatu-lmunaafiq thalaatha, Idhaa waaada akhlafa, waidhaa hadatha kadhaba waidhaa utumina khaana” Akiimaanisha “Alama za mnafiki ni tatu, akitoa ahadi hwenda kinyume, akizungumza husema uongo na anapoaminiwa hufanya hiana” Hadithi hii ya Mtume katika dini ya kiislamu ilikuwa ni kifungulio cha hotuba ya Babu akimkejeli Ali Muhsin kwa kuvunja mkataba wa makubaliano yao wakati akiwa ndani ya ZNP.
  Hapo tena ZNP wakawaandama makomred na kuwaanika hadharani kwamba hawana dini, ni walevi, ni wazinifu, wanakula mchana katika mwezi wa Ramadhani, wanabadilishana wake zao, hawaamini Mungu na hivyo ni tishio kubwa dhidi ya uislamu. Katika kitabu cha maisha yake cha Burgess, Komred Ali Sultan Bin Issa anadai kwamba wafuasi wa ZNP waliagizwa kuwahujumu umma party kwa kuwalenga mawe kila wanapokuwa katika mikutano yao ya hadhara au wanapopita mitaani. Umma Party kiliungwa mkono na kilipigiwa upatu pia na Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (FPTU na ZPFL ), Umoja wa Waandishi wa habari, wamiliki wa vyombo vya habari na Wanaharakati wa siasa za mrengo wa kushoto ndani ya ASP.
  Chama cha umma au Umma party kiliasisiwa na Bwana Abdulrahman Babu, mkongwe wa siasa Zanzibar. Aliunda Umma party akishirikiana na makomredi wenzake baada ya siasa zake kushindikana wakati akiwa ndani ya ZNP. Babu ni mwanasiasa mkongwe mwenye asili ya kingazija aliyekuwa akiishi Vikokotoni Unguja, architect makini na aliyebobebea kwa siasa za kikomunisti. Zipo tetesi kuwa ndiye aliemfundisha na kumuambukiza Mwalimu Nyerere sisa za kijamaa. Hii ni kwa kuwa Mwalimu nyerere alisomeshwa na mabepari wa kiingereza, huko London, hivyo utaalamu wa ujamaa hakuwa nao. Babu sio tu alikuwa mwanasiasa, lakini pia mtu msomi aliyebobea, mwandishi mashuhuri wa vitabu na mwanamapinduzi ya 1964. Kwa muda wa miaka isiyopungua arobaini (40) Babu alikuwa yumo ndani ya harakati za siasa.

  Kiukweli Babu hakuwa na msimamo wowote wa kichama. Msimamo wake wa kichama ulikuwa ni wa kujifichia tu. Hii ndiyo maana aliweka mbele mafunzo ya kivita kwa wafuasi wake kabla ya chochote. Ndio sababu pia akaona kheri kujitoa katika ZNP kuliko kupotezeza nguvu na ushawishi wake katika chama hicho. Wakati watu wanacheza ngoma yao ya siasa za vyama vingi waliofundishwa na Muengereza, Babu yeye alikuwa anatafuta njia ya kupenyea ili aipeleke nchi kwenye siasa zake za kikomyunisti. Mambo ya vyama hata hayakuwemo kichwani mwake. Sheikh Karume aliwahi kumpachika Babu jina la kupanga na kumwita “tumbili” kwa tabia zake za kurukia chama hichi na kile. Babu naye alikuwa mtu muhimu katika siasa zile za kuelekea katika Zanzibar huru (Issa 1999). Kama Babu hakuwa katika waliokuwa mbele katika mipango ya mapinduzi ya 1964, basi pia hawi wa nyuma katika kuyaandaa, kuyasifu, kuyaunga mkono, kuyatekeleza na kuyalinda kwa nguvu zake zote.
  Yote hayo kwa Babu yalikuwa na lengo moja tu, yaani njia ya kupenyea ili kufanikiwa kuigeuza Zanzibar kutoka katika mfumo wa kibepari wa Muengereza na Sultani na kuipeleka katika mfumo wa kijamaa wa misingi ya ukomyunisti. Babu alikuwa kiongozi mkuu wa makomred wa Zanzibar waliounga mkono ukomyunisti. Pia alikuwa mtu aliyekuwa na ushawishi juu itikadi ya kikomyunisti katika Afrika ya mashariki na Afrika kwa jumla. Wamarekani hawakuwacha kumjengea shaka kubwa Babu kwamba angeyatumia mapinduzi ya Zanzibar na Kuifanya Zanzibar kuwa “African Cuba” yaani chimbuko la harakati za mapinduzi ya kikomyunisti Afrika Mashariki na Afrika yote kiujumla. Kwani kwa Marekani hatima ya hili ni kuuvuruga na kuudoofisha mfumo mzima wa kibepari ambao ndio kwanza ulikuwa unaenea taratibu Afrika na duniani kwa ujumla.
  Chaguzi kuelekea uhuru wa 1963
  Safari ya Zanzibar kuelekea kwenye uhuru ilikuwa na misukosuko mingi. Katika safari hiyo ya kuelekea uhuru, makundi mbali mbali ya wazalendo waliruhusiwa kufanya siasa za ushindani ili kutafuta nguvu za kukubalika na wananchi na hivyo kukabidhiwa uhuru. Ushindani huo ni kwa kupitia chaguzi zilizovishindanisha vyama vya siasa vya kupigania uhuru vilivyokuwa na sera na itikadi tofauti. Tofauti na Tanganyika ambako kulikuwa na chama cha TANU kilichoungwa mkono na watanganyika karibu wote, vyama viwili vikuu vya siasa vya Zanzibar, ZNP na ASP vilikuwa na wafuasi na nguvu sawa (Othman 1996) jambo ambalo lilizua mivutano na migogoro mingi kila baada ya uchaguzi. Mkoloni Muengereza ndie aliyeretibu na kusimamia chaguzi zote zilizofanyika kwa kutumia utaratibu na mfumo wa chaguzi za nchi ya Uengereza. Mfumo wa uchaguzi ulikuwa wa mshindi kuchukua kila kitu (winner takes all) ijapokuwa chama kilichoshinda kinaweza kukishirikisha chama chengine katika kuunda serikali. Ushindi ulipatikana pindipo chama kitashinda viti vingi katika viti vyote vilivyoshindaniwa. Hadi kufikia uhuru palifanyika chaguzi nne (4). Uchaguzi wa kwanza ni uchaguzi wa mwaka 1957, wa pili ni wa Januari 1961, wa tatu ni wa June 1961 na wa nne ni wa Julai 1963.

  Uchaguzi wa kwanza
  Uchaguzi wa kwanza ni ule wa 1957 ambapo chama cha ASP kilishinda viti vitano (5) kati ya sita vilivyoshindaniwa. Kimoja kati ya hivyo sita kilichukuliwa na chama cha Muslim association ambacho kilikuwa na ngome yake katika mji mkongwe. Hapa ndipo ASP ilipolalamika kwa nini waingereza waliwnyima haki ya kuunda serikali. Inasemekana chimbuko la suala hili la ASP kunyimwa hakiya kuunda serikali na waingereza ni pale Sheikh Ameir Tajo alipopeleka madai kwamba ASP haijawa tayari kupata uhuru na kuendesha nchi baada ya uchaguzi wa 1957. Sababu kubwa ya Sheikh Ameir Tajo na wenzako kufiia maamuzi hayo ni pale walipobaini kwamba chama kilipata bahati mbaya ya kukosa wasomi miongoni mwa waasisi na viongozi wake. Hili la kukosa wasomi kwa akina Tajo lilikuwa muhimu sana kwani chama hakikuweza hata kumiliki katiba yake wakati ZNP wakiwa na wasomi wa kutosha walikuwa na katiba inayoongoza chama chao (Burgess 2009). ASP walipogundua kwamba Sheikh Ameir Tajo ndie aliyepeleka habari hizo, wakamfukuza kwenye chama. Huo ndio ukawa mwanzo wa mgawanyiko ndani ya ASP.

  Jadweli no 3: Matokeo ya uchaguzi wa kwanza mwaka 1957
  CHAMA KURA VITI
  1. Afro-shrazi party (ASP) 23940 5
  2. Zanziabar Nationalist Party (ZNP) 8604 -
  3.. Muslim Association 6612 1
  Jumla ya kura halali 39156 6
  Chanzo: Ripoti ya Mbita

  Uchaguzi wa pili Januari 1961
  Uchaguzi wa pili ulikuwa Januari 1961 uchaguzi ambao vyama vya ZNP na ZPPP viliamua kushirikiana. Matokeo ya uchaguzi huo yaliupatia umoja wa ZNP/ZPPP ushindi wa viti kumi na mbili (12). Kwa kuwa kiti kimoja kiligoma kuunga mkono umoja huo, basi vikabaki viti kumi na moja (11). Kile kiti kimoja kiliiunga mkono ASP. Kwa upande wake ASP ilijinyakulia viti kumi (10), na kufanya idadi ya viti vyake kuwa kumi na moja. Hapa ndipo iliposhindikana kupata mshindi wa kuweza kuunda serikali na uchaguzi kupaswa kurudiwa tena katika mwezi wa juni 1961.

  Jadweli 4: Uwiano wa idadi ya kura na viti kwa vyama vya ASP, ZNZ na ZPPP kati ya Unguja na Pemba katika uchaguzi wa Januari 1961
  JANUARI 1961
  Zanzibar (Unguja) Pemba Jumla kuu
  (ASP) 27,495 9,203 36,698

  (ZNP) 15,555 17,169 32,724
  (ZPPP) 1,946 13,595 15,541
  Jumla 44,996 39,967 84,963 44
  Chanzo: Africa elections Data base

  Uchaguzi wa tatu June 1961
  Katika uchaguzi huu wa Juni 1961 zilizuka fujo kubwa na umwagikaji wa damu. Kwa umaarufu fujo hizi zilijulikana kwa jina la vita vya Juni. Fujo hilo lilipelekea watu sitini na nane (68) kufariki na wengine kwa mamia kuumia vibaya. Kati ya 68 waliokufa, 65 walikuwa ni wa asili ya kiarabu na watatu (3) walikuwa wa asili ya kiafrika (Okello, 1967). Tukio hili la June 1961 lilitowa dalili kubwa kwa matokeo ya Januari 1964. Sababu za fujo hizo ni pale watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa ASP ambapo inasemekana wengi wao ni wageni walioletwa Zanzibar kwa njia za magendo kutokea Tanganyika kuja kupiga kura. Pia watu hao waliwashambulia kwa mawe wafuasi wa ZNP/ZPPP wakati wakiwa njiani wanaelekea katika upigaji kura. Katika kitabu chake cha “Kwaheri ukoloni kwaheri uhuru, Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia”, Harith Ghassany anamnukuu Mzee Mohammed Omar ambae pia alijulikana kama Mzee Mkwawa kwa kuhusiana na Chief Mkwawa. Mzee Mkwawa anasema:

  “Kwa hivyo nikashirikiana na Chama cha Wafanyakazi [Tanganyika Federation of Labor] kiongozi, Bwana Victor Mkello. Kaweza kunikusanyia watu kufanya kampeni na kuweza kupata watu nikawa napakia hapa nenda nao kutoka [barabara ya] kumi na nne Head Quarters [makao makuu] nenda nao moja kwa moja napita njia ya Pangani, kijiji cha Kipumbwi. Nilikuwa nikipakia ndani ya mabasi yanoelekea njia ile ya Pangani na kutoka mashamba ya mkonge. Mabasi kutoka Tanga yalikuwa ni gari ya Abdalla Saidi, marehemu sasa, magari yakina Hashu Sleman, mabasi ndo yalokuwa wakati huo yapo. Na magari mengini yoyote, yoyote yale, yanoelekea njia hiyo walikuwa watu wanarukia. Hata magari ya mizigo. Sio lazima basi. Kwa hivyo nikatia watu kwenda kuandikisha na kuwarudisha na kuwapeleka tena, kutegemea chaguzi. Tulifanikiwa, na kuwatia watu kama walivofanikiwa wao Hizbu. Kwa bahati tukafuzu. Tukapata viti va kutosha” (Ghassany 2010).
  Vitendo vya fujo vya watu hao viliendelea mpaka ndani ya majumba kwa watu kupigwa, kuibiwa mali zao na kuuliwa. Udadisi unaonyesha kwamba watu wengi waliuliwa wakiwa majumbani mwao na sio njiani au katika foleni za kura ambako ndiko fujo zilikoanzia. Jambo hili linathibitisha kwamba fujo hizi ziliambatana na chuki za ukabila. Matokeo ya uchaguzi huu wa Juni 1961 yalikuwa hivi: ASP walipata viti 10 na umoja wa ZNP/ZPPP walipata viti kumi na tatu (13).
  ZNP/ZPPP waunda Serikali ya madaraka ya ndani
  Kufuatia matokeo ya uchaguzi huo wa tatu ndipo umoja wa ZNP/ZPPP ukapewa uwezo wa kisheria wa kuunda serikali ya madaraka ya ndani (Responsible Government). Serikali hii pia iliitwa kwa jina la serikali ya mshikizo. Serikali hiyo ilikuwa na mamlaka ya kuendesha baadhi ya mambo Fulani tu ya ndani ya nchi na mambo muhimu yote yaliendelea kuwa chini ya wakoloni waengereza. Serikali hii iliundwa na wakoloni ili kupunguza shauku na hamasa za ZNP/ZPPP za kupatikana uhuru na kuchukua madaraka jambo ambalo lilikuwa linakwamishwa kutokana na mizozo ya chaguzi. Hivyo basi waengereza walifahamu kwamba kwa kufanya hivyo kungeliwapa subira ya uchaguzi mwengine wa mwisho. Serikali hiyo ya madaraka ya ndani iliundwa tarehe 24 Januari 1963 na kudumu hadi tarehe 10 Disemba 1963 siku ambayo serikali mpya ya uhuru ilipatikana.

  Serikali ya madaraka ya ndani, kutoka kushoto: Sheikh Ameir Tajo, Ali Muhsin,
  Miraj Shaalab, Vuai Kiteweo, Sheikh Moh’d Shamte, na Seyyid Abdalla bin Khalifa

  Mkutano wa mwanzo wa katiba ya uhuru
  Sultani alitawala Zanzibar bila ya katiba iliyo rasmi. Hii inathibitisha kwamba utawala wa kisultani ulikuwa ni muendelezo wa utawala wa kienyeji uliokuwa ukirithiwa kwa zaidi ya karne mbili. Zanzibar ilipokuwa chini ya ukoloni wa muingereza ilikuwa ikiongozwa na katika ya kikoloni wa muingereza iliyo rasmi. Huu ndio mfumo wa utawala wa kikoloni ulivyokuwa duniani kote. Mara tu baada ya wimbi la vurumai la harakati za uchaguzi wa Juni kutulia, vidonda kupoa, misiba kusahaulika na hofu kutulia, mkutano wa mazungumzo ya katiba ya uhuru yalifanywa huko Lancaster House London. Mazungumzo hayo ya katiba yalichukuwa muda wa wiki mbili (2) kuanzia tarehe 19 Machi hadi tarehe 6 Aprili 1962. Kipindi hichi ni kile cha miaka miwili kutokea Juni 1961 hadi Julai 1963. Mkutano ulifanyika na vyama vyote vilivyoshiriki katika harakati za kupigania uhuru vilishiriki mazungumzo hayo ya katiba. Mazungumzo yalikwisha bila ya mafanikio yoyote.
  Matokeo ya Juni Uchaguzi wa 1961 (angalia jadweli no 52) yaliyowapa ushindi ZNP/ZPPP ndio yaliyotumika kama kigezo cha kuitishwa kwa mkutano wa Katiba mjini London ili kupitisha katiba ya Zanzibar huru. Babu alihudhuria mkutano huo kinyemela baada ya kunyang’anywa na Serikali hati yake ya kusafiria lakini akapewa hati nyingine na Serikali ya Tanganyika. ASP walikataa kufanya mazungumzo yoyote na serikali ya ZNP/ZPPP. ASP walitaka mazungumzo hayo yasifanyike hadi hapo uchaguzi mwengine utapoitishwa. ZNP/ZPPP walijaribu kwanza kwa maneno matupu kuwashawishi ASP wakubali kufanya mazungumzo lakini ilishindikana. Baada ya kushindiikana maneno matupu ndipo ZNP/ZPPP walipowaahidi kuwashirikisha ASP katika serikali kwa kuwapa wizara tatu na kura ya “veto” (casting vote). Kwa maana hiyo sasa kutakuwa na serikali ya mseto ikihusisha vyama vyote vitatu, yaani ZNP/ZPPP na ASP. Kwa kuwa wazo hilo halikuwa baya Karume aliomba muda wakalitafakari vyema na chama chake na kuahidi kutoa maamuzi baadae.
  Lakini hata hivyo, ASP walikataa pendekezo hilo baada ya kushauriana na Nyerere na hivyo kusisitiza kwamba hakuna mazungumzo yoyote baina yao hadi hapo uchaguzi mwingine utakapofanyika kabla ya uhuru. Hivyo basi muafaka haukufikiwa na Mkutano ukavunjika.. Baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya London, Serikali ya Uengereza ilimtuma mjumbe wake, Duncan Sandy, Zanzibar kujaribu kwa mara ya mwisho kutatua tatizo hilo la kikatiba kwa njia ya serikali ya mseto. Sandy aliwakutanisha viongozi wa pande zote mbili lakini hakuna maridhiano yaliyofikiwa. Serikali ya Uengereza iliamua iundwe serikali ya ndani ya mshikizo (transitional government) Juni 1963, na kufuatiwa na uchaguzi mwingine wiki mbili (2) baadae.
  Uchaguzi wa mwisho Julai 1963 (mpata mpatae mkosa ujingawe)
  Kulipangwa kufanywa uchaguzi mwengine ambao ndio uwe wa mwisho kuelekea uhuru kamili wa Zanzibar. Uchaguzi huu ndio ule wa Julai 1963. Ilipofika Julai 1963 uchaguzi huu ukafanyika. Matokeo ya uchaguzi huu yakawa hivi: ASP ilijipatia viti 13 (Unguja 11 na Pemba 2), ZNP ilijipatia viti 12 (Unguja 6 Pemba 6) jambo ambalo linaashiria kwamba ZNP ilijipatia ushabiki sawa kati ya Pemba na Unguja. ZPPP kwa upande wake ilijipatia viti 6 (vyote kutoka Pemba). Hivyo basi muungano wa ZNP/ZPPP ukajikusanyia jumla ya viti 18 dhidi ya viti 16 vya ASP. Kwa matokeo hayo muungano wa vyama vya ZNP/ZPPP ukapewa ruhusa ya kuunda serikali ya uhuru ya Zanzibar.

  Jadweli 5: Uwiano wa idadi ya kura na viti kwa vyama vya ASP na ZNZ /ZPPP kati ya Unguja na Pemba katika uchaguzi wa Julai 1963
  JULAI 1963
  Unguja Pemba Jumla kuu
  (ASP) 53,232 33,853 87,085

  (ZNP/ZPPP) 31,144 42,415 73,559
  Juml 84,376 76,268 160,644
  Chanzo: Africa elections Data base

  ZNP/ZPPP waunda serikali ya uhuru
  Baada ya vuta nikuvute nyingi katika harakati hizo za ushindani wa kisiasa, muungano wa vyama vya ZNP na ZPPP, wakaibuka washindi. Kufuatia ushindi huo waengereza wakawapa ruhusa ZNP na ZPPP kuunda serikali ya uhuru. Serikali hiyo ya uhuru ilikuwa na muundo wa Waziri mkuu kama mkuu wa serikali na mfalme asiye na mamlaka yoyote. ZNP na ZPPP waliigiza mfumo huu kutoka kwa wakoloni wao, waengereza. Sheikh Moh’d Shamte Hamad, mpemba wa Chambani, aliyekuwa Rais wa ZPPP akachaguliwa na umoja wa ZNP/ZPPP kuwa waziri mkuu wa serikali hiyo na mfalme Jamshid Bin Abdalla kuendelea kubaki na heshma ya kiti chake cha ufalme bila ya mamalaka ya juu ya kuendesha serikali. Serikali hiyo ilikuwa na viongozi wafuatao.

  1. Seyyid Jamshid Bin Abdalaa (Mfalme) – Muunguja
  2. Sheikh Moh’d Shamte (Waziri mkuu) – Mpemba
  3. Sheikh Rashid Hamadi – Mpemba
  4. Dr Idarus Baalawy – Mpemba
  5. Sheikh Abadhar Juma – Mpemba
  6. Sheikh Maulid Mshangama – Mpemba
  7. Sheikh Omar Hamad -Mpemba
  8. Sheikh Ali Muhsin – Muunguja
  9. Bwana Juma Alley – Muunguja
  10. Bwana Ibuni Saleh – Muunguja
  11. Sheikh Ameir Tajo – Muunguja
  12. Bwana Amirali Abdul-Rasul – Muunguja

  Hii ndio enzi pekee katika historia ya Zanzibar kabla ya maridhiano ya wazanzibari ambapo watu wenye asili ya kisiwa cha Pemba waliweza kushika madaraka ya juu ya serikali kwa asilimia 50 kwa 50 na wenzao wa kisiwa cha Unguja.
  Mkutano wa pili wa katiba ya uhuru
  Mara tu baada ya uchaguzi wa mwisho kumalizika na serikali kuundwa, Uengereza ilizitaka pande mbili, upande wa serikali (ZNP/ZPPP) na upande wa upinzani, ASP kukutana Lancaster House nchini Uengereza kwa ajili ya mazungumzo ya Katiba ya uhuru wa Zanzibar. Ili kuweka matayarisho mazuri ya mkutano huo wa katiba, balozi wa Uengerza wa Zanzibar, Sir Gorge Mooring aliitisha mkutano uliozihusisha pande zote mbili hapo hapo Zanzibar. Mkutano huo wa matayarisho ulimalizika kwa mafanikio makubwa. Pande hizo mbili za mazungumzo zikawasili Uengereza na kushiriki mazungumzo ya Katiba ya uhuru na kuweza kukubaliana takriban vifungu vyote vya mazungumzo bila hitilafu yoyote. Baada ya mkutano kufanikiwa pande zote mbili zilirejea Zanzibar.

  Uhuru wa Zanzibar wa 1963
  Tarehe 10 Disemba 1963 Zanzibar ilipewa rasmi uhuru wake kutoka katika utawala wa kiarabu na udhibiti wa walinzi wao wa kiengereza. Hakukuwa na tukio la kushusha bendera ya Muengereza kwa kuwa Zanzibar haikuwa koloni bali ni Mahmia. Badala yake bendera ya rangi nyekundu tupu ya Sultani ndiyo iliyoteremshwa na bendera ya Zanzibar huru yenye karafuu mbili katikati ikapandishwa. Uhuru huo ulikabidhiwa kwa serikali ya umoja wa ZNP/ZPPP. Wananchi walioupokea uhuru kwa mikono miwili wakiwa ni kutoka kambi ya ZNP/ZPPP waliushereheka katika kila kona ya nchi mijini na mashamba. Tafrija mbali mbali zikafanywa Unguja na Pemba kusherehekea uhuru wa 1963. Hata hivyo ni nusu tu ya wazanzibari ndiyo walioupokea uhuru huo kwa moyo mkunjufu na kuusherehekea. Pamoja na roho za wafuasi wa ASP kujikunja kufuatia uhuru huo, Karume alitoa agizo kwa wafuasi wake wa ASP nao kusherehekea uhuru huo. Karume aliwahi kutoa hotuba ya kuupokea uhuru huo kama inavyosomeka hapo chini.

  “Leo mwezi 10 Disemba, 1963, ZANZIBAR imekuwa Huru. Hii leo sisi watu wa visiwa hivi tumepata haki ya kuchukuwa mahala petu kuwa ni Dola sawa na nyengine katika umoja wa Nchi za Dola za Commonwealth. Kwa uchache, kuwa mwanachama katika umoja huo, kuna maana kwamba nchi hii ni huru chini ya mpango wa Sirikali ambayo msingi wake umejengwa juu ya kuendelea kwa ridhaa ya wananchi.
  Ili kufikilia matarajio yetu hayo tunayo moja katika Katiba zenye msingi madhubuti iliyohusika na shuruti za haki za binadamu, haki za mambo ya siasa na uhuru wa dola yoyote nyengine. Ni wajibu wa watu wote wa dola yetu mpya, kila mmoja katika sisi bila ya kujali fikra zetu za siasa au madaraka yetu kusaidia kweli kweli Katiba yetu iweze kufanya kazi. Pamoja na manufaa, haki na uhuru ambayo yote hayo yamepatikana baada ya nchi kuwa huru.
  Tulioyapata leo mwezi 10 Disemba ni mipango ya mwanzo tu ya kuweza kufanya juhudi kwa ukamilifu dhidi ya maadui zetu nao ni ujinga, umasikini na maradhi na kuweza kuleta imani penye khofu na shaka na kuleta masikilizano mahala ambapo hata hivi sasa adawa ipo, na kuleta mapenzi mahala ambapo pana chuki, ili dola yetu mpya ichomoze katika neema, umoja na furaha.
  Kwa hivyo katika hii siku ya leo na tumwombe Mwenye Enzi Mungu Mtukufu Subhaanahu wa Taáala, atuweke tuifanye na tuitimilize kazi kubwa ya kujenga taifa letu ili dola yetu mpya ya ZANZIBAR ipate baraka ya matunda mema ya kazi zetu. Uhuru na Umoja, Uhuru na Kazi!”
  Wafuasi wa ASP wakiwa hawana furaha waliusherehekea uhuru huo huku wakimtuhumu kiongozi wao Karume kwa usaliti kutokana na kuutambua uhuru huo. Pamoja na kushereheka huko, nusu hii ya pili ya wazanzibari wakiwa ni wafuasi wa kambi ya ASP waliubeza, waliudharau na walikataa kabisa kuutanbua uhuru huo na kuuita uhuru wa bandia. Hata hivyo sio sahihi kuuita uhuru wa bandia kwani bila uhuru huo hakuna sheria inayotambua kuondoka kwa utawala wa kiingereza Zanzibar na ni hivyo hivyo bila ya uhuru huo mapinduzi yaliyofuatia baada siku chache baada ya uhuru hayawezi kufanyika wala kutambulika. Kama mapinduzi hayakupindua dola huru ya Zanzibar basi bila shaka yameipindua dola ya malkia wa Uengereza iliyokuwa na dhamana ya ulinzi kisheria kwa nchi ya Zanzibar.
  Kuanzia hapo Zanzibar ilitambuliwa rasmi kuwa ni nchi huru barani Afrika ambayo imejikomboa kutokana na makucha na ubeberu wa Uengereza na utawala wa kisultani. Bila ya kuchelewa serikali ya uhuru ya Zanzibar chini ya Sheikh Moh’d Shamte na Sultani iliomba uanachama katika umoja wa mataifa (UNO) ili itambuliwe kuwa miongoni mwa nchi huru ulimwenguni. Ombi hilo lilikubaliwa na umoja wa mataifa na hivyo basi Zanzibar ikakabidhiwa kiti chake katika umoja wa huo wa mataifa huru duniani. Sheikh Moh’d Shamte alitoa hutuba ya kusisimua katika mkutano huo wa kuitambua Zanzibar kama nchi huru na mwanachma mpya wa UNO.
  Hotuba ya Sheikh Moh’d Shamte katika kutoa salamu za uhuru katika mkutano wa umoja wa mataifa huko New York.
  Mh Rais! (wa UNO), ni heshima na furaha kubwa kwangu kuwepo hapa nikiiwakilisha Zanzibar wakati huu ombi la Zanzibar la kujiunga na Umoja wa mataifa likiwa limekubaliwa na mkutano mkuu. Uingiaji wa Zanzibar katika Jumuiya hii kubwa kwa mujibu wa akili yangu una umuhimu sana, hii ni kwa sababu imetoa changamoto kuwa hakuna nchi ndogo na dhaifu ambayo haiwezi kuwakilishwa katika jumuiya hii kwa fursa na nafasi sawa na yale mataifa makubwa ulimwenguni. Wako watu wanaoliona hili sio sawa. Lakini mimi nalizingatia hili kama ni uimara wa jumuiya hii na ni jambo litakaloitia hamu na kuishajihisha Zanzibar kutumia fursa na uwezo wake katika kutekeleza malengo ya kuanzishwa kwa Umoja wa mataifa.

  Napenda kufikisha shukurani za nchi yangu kwa marafiki zetu dunia nzima ambao wamefanya mengi katika kuunga mkono juhudi na mapambano yetu ya kuelekea uhuru, kwa kamati ya mapambano dhidi ya ukoloni ambayo imetowa mchango wa kutosha katika kuhimiza uhuru wetu, na kwa jumuiya hii ambayo tunajivunia kama ni mafanikio makubwa. Kwa wote hao bado tunaendelea kutegemea kila aina ya msaada na uungwaji mkono katika kuwaletea maendeleo watu wetu ili nasi tuweze kutoa mchango wetu katika utatuzi wa matatizo ya kilimwengu. Napenda pia kutuma shukrani zangu kwa waheshimiwa wote katika baraza la usalama na mkutano mkuu wa umoja wa mataifa ambao wametoa michango yao katka mapambano yetu na mafanikio yetu. Kwa wote wale waliotudhamini hadi kukubaliwa ombi letu na kwa waheshimiwa wote waliotupigia kura ili kupewa uanachama, sina budi kuwambia: ahsanteni.
  Mh. Rais. Matatizo ya kisiasa ndiyo yanayotawala vichwa vya habari duniani, lakini kiujumla haijulikani kwa mfano maradhi ya malaria imeweza kuwa vita kubwa kuliko vyovyote, sasa yameshatokomezwa kabisa Zanzibar, kwa mashirikiano na jitihada za WHO, UNICEF na serkali na watu wa Zanzibar. Pia ilikuwa haifahamiki kuwa pole pole lakini kwa ufanisi tunajaribu kwa msaada wa ILO na FAO kupunguza kasi ya ukosefu wa ajira. Ziko njia nyingi ambazo nchi na jumuiya za kimataifa zimeshirikiana na sisi katika kutatua matatizo yetu. Wote hao tunawapa shukurani zetu.
  Ssa ni kwamba nguvu za watu wetu ni kubwa kutokana na kurudi kwa ufahari wa nchi yetu na utaifa wetu ambao tunautarajia kwa ari tukitegemea msaada kutoka kila mahali. Zanzibar ni miongoni mwa mataifa madogo kwa idadi ya watu na ukubwa kukubaliwa uwanachama katika umoja wa mataifa. Hii ni kama kujitoa muhanga kwa Zanzibar, muhanga ambao bila shaka hauna maana muhimu kwa mataifa tajiri, lakini ni muhanga ulio na umuhimu mkubwa kwa nchi yetu yenye vyanzo finyu. Tunafuraha kujitoa muhanga huu katika jumuiya hii. Ikiwa sisi si matajiri kwa wingi, kwa mipaka, au kwa utajiri basi hatujihesabu kama masikini wa thamani katika maisha yetu ambayo ndio muhimu, na ni kwa hili ndio tunaamini tutakuwa na mchango wetu japo dhaifu katika shughuli za mkutano mkuu wa jumuiya hii.
  Tuna historia ndefu ya heshima na ustaarabu nyuma yetu. Kama vile walivyo watu wengi ulimwenguni, mizizi yetu inatokana na vyanzo vingi, zaidi kutoka Afrika, lakini pia kutoka Arabuni, ustaarabu wa Kiasia, kipasia, kihindi na sehemu nyingine. Wazungu katika safari zao za uchunguzi walikutia kila aina ya ukarimu na neema katika mwambao wetu. Watu wa asili nyingi tofauti walipaona Zanzibar ni pahala pazuri pakupumzikia na kutulia ambapo mipango ya uvumbuzi na na maendeleo ya Afrika ya kati na mashariki ilifanywa. Bila shaka ni kutokana na mizizi hii ilijengeka kwa makarne, kwa kuchanganya tamaduni mbali mbali, na kutufanya kuwa watu wa kujivunia hadhi ya nchi yetu kwa ustaarabu na urafiki. Hata hivyo tukiwa katika ulimwengu huu wa kisasa hatukusudii kuyaendekeza yaliyopita, na hii ndio itikadi tutakayoifuata kujenga mustakbali wetu.
  Serikali huru ya Zanzibar ni serikali ya kifalme inayooongozwa na katiba iliyo chini ya misingi ya uhuru na demokrasia, ambayo inaongozwa na waziri mkuu pamoja na baraza la mawaziri walioteuliwa, wenye majukumu na wanaohojiwa na wajumbe wa mkutano mkuu, wajumbe ambao huchaguliwa na wananchi wote walio na haki ya kuchagua. Haki za msingi za binadamu zenye misingi ya uhuru na demokrasia na uhifadhi wa raia kutokana na ubaguzi ndio manbo yalizingatiwa katika katiba ya Zanzibar. Malengo yetu makuu ni amani na maendeleo hapa nyumbani na duniani kote kiujumla. Lengo kuu ni kusaidia kujenga mazingira ya kisiasa katika ulimwengu ambao maadui wakuu wa mwanadamu, yaani njaa, ujinga na maradhi yatazingatiwa na hivyo rasilimali na wakati hautopotezwa bure. Sera kuu ya Zanzibar ni ukarimu bila ya ubaguzi wan chi yeyote kwa misingi ya rangi, dini, utamaduni au itikadi. Zanzibar huru inaunga mkono harakati zote za amani kwa misingi ya ushirikiano wa kimataifa. Katika kupata uhuru wake Zanzibar imechagua kubakia kama mwanachama wa jumuiya ya madola na inafuraha kutoa mchango wake katika uhusiano wake mwema unaoendelea baina ya Zanzibar na Uingereza.Tunaamini kuwa jumuiya ya madola ni nchi nyingi zenye usawa na uhuru sawa na utaifa sawa na watu wa tamaduni mbali mbali ambao kwa hiari zao na kwa misingi ya kidemokrasia wameungana wakiwa na madhumuni ya kuendeleza amani, mashirikiano, na maendeleo kwa pamoja.
  Ni lengo la Zanzibar pia kuendeleza mafungamano yaliyopo baina yake na Afrika pamoja na nchi za mashariki. Mwishoni tunaunga mkono misingi ya Azimio la Bandung la mwaka 1955 na sera ya umoja wan chi huru za Afrika ulioanzishwa Adis Ababa mwaka huu. Zanzibar ina urafiki wa karibu na nchi nyengine za Afrika mashariki na lengo letu kuu kuuendeleza uhusiano huu na mashirikiano ndani au nje ya shirikisho la Afrika ya mashariki. Kwa hili ninafuraha sana kuona Kenya ambayo ina mafungamano na urafiki mkubwa na Zanzibar nayo imealikwa ktika ghafla hii ya leo. Katika kipindi hichi cha cha leo cha kujivunia katika historia yetu, naomba niruhusiwe ninukuu maneno yafuatayo ya Shakespeare “We are two lions littered in one day”
  Mheshimiwa, katika kukabidhi ombi letu la uanachama nimetayarisha Azimio la dhati la pamoja na lile lililofanywa na mataifa mengine yaliofika hapa leo, kwamba kwa niaba ya serikali yangu nakubali majukumu na wajibu wote uliomo katika sera ya umoja wa mataifa na naahidi kutekeleza wajibu na majukumu yote. Azimio hili ni la dhati la moyoni na la ukweli kwangu, na namuomba Mungu iwe hivyo, na kwa hivyo Zanzibar italiheshimu azimio hili kwa moyo wote.
  Ahsante sana Mheshimiwa Rais!

  ASP baada ya uhuru
  Kambi ya ASP haikuupokea kwa moyo mkunjufu ushindi wa ZNP/ZPPP, uhuru wa Zanzibar na serikali mpya ya uhuru. Hii ni kutokana na sababu nyingi. Mosi, ASP hawakuupendelea mfumo wa uchaguzi wa ushindi wa idadi ya viti ambao ulilazimishwa kufuatwa na Muengereza. Hii ni kwa sababu mfumo huo ulipuuza maamuzi ya wengi na kuyazingatia maamuzi ya wachache. Mfumo huo ulimpa ushindi aliyeweza kuibuka na viti vingi hata kama idadi ya wananchi waliomuunga mkono ilikuwa ndogo. Kinyume chake, mfumo huo ulimnyima ushindi aliyepata viti kidogo hata kama aliongoza kwa wingi wa uungwaji mkono wa wananchi. ASP ijapokuwa ilipata asilimia 54.2 ya kura zote zilizopigwa lakini ilijipatia idadi ya viti 13 tu na hivyo kwa mujibu wa mfumo huo wa uchaguzi ilikosa uhalali wa kuunda serikali. Kinyume chake muungano wa ZNP/ZPPP japokuwa walipata asilimia 45.8 tu ya kura zote zilizopigwa lakini walijinyakulia idadi ya viti 18 kuishinda ASP na hivyo kwa mujibu wa mfumo wa uchaguzi ZNP/ZPPP walikuwa na uhalali wa kuunda serikali. Pili, ASP haikuwa ikilikubali hata kidogo suala la kuendelea kwa utaratibu wa ufalme wa kiarabu Zanzibar jambo ambalo lilipewa baraka zote na kuwa katika sera za ZNP/ZPPP. ZNP/ZPPP hawakuona ubaya wowote kuendelea na ufalme huo walioutambua kuwa ni aila halisi ya kizanzibari na kwa kuwa haukuwa tena na madaraka yoyote.
  Hata hivyo mara baada ya ushindi wa ZNP/ZPPP na serikali kuundwa viongozi wa ASP walijaribu kuanzisha mazungumzo na ZNP/ZPPP wakiomba iundwe serikali ya mseto na pia kuangalia uwezekano wa kugawana kwa usawa nafasi za baraza la mawaziri. Jambo hili linathibitisha kwamba ASP mwisho wa siku walikubaliana na ushindi huo wa ZNP/ZPPP ila hawakuwa tayari kundi hilo kubwa la wazanzibari kupuuzwa katika serikali mpya ya uhuru. Hivyo basi inaonyesha wazi kwamba mwanzoni ASP walikuwa tayari kumaliza mizozo ya siasa bila ya fujo kwa kutumia njia za kidiplomasia na ustaarabu wa kisiasa. Ombi hilo la kuwashirikisha ASP katika serikali ya uhuru lakini lilikataliwa vikali na ZNP/ZPPP kwa madai kwamba nafasi kama hiyo ilitolewa kwenye Mkutano wa Katiba wa kwanza London, lakini ASP kwa wakati huo walikataa kwa kutii ushauri wa Nyerere. Kwa kauli ambayo haikutarajiwa, Waziri Mkuu Shamte alijibu kwa kejeli ya kisiasa kwamba “siasa si kugawana mateka” na akamshauri Karume avunje ASP na wanachama wake wajiunge na ZPPP.
  Baada ya hapo ndani ya ASP mambo hayakuwa shwari na ndipo kambi mbili ziliibuka. Kambi hizi zilitofautiana na kupingana vikali kuhusu mtazamo na maana ya uhuru, ushindi wa ZNP/ZPPP na uhalali wao wa kuunda Serikali, huku viongozi hao wa ASP wakilaumiana kila mmoja kwa chama chao kushindwa. Kundi la kwanza bila shaka likiongozwa na Karume lilitaka ASP ifuatilie kwa nguvu na kwa gharama zozote kuhakikisha kwamba inaundwa serikali ya mseto ikishirikisha vyama vya ZNP, ZPPP, na ASP kama njia pekee ya muafaka wa kisiasa Zanzibar. Kundi la pili la viongozi wa ASP bila shaka likiongozwa na Abdalla Kassim Hanga lilitaka kuwapo kwa upinzani wa nguvu na wa wazi wazi dhidi ya Serikali kwa kushirikiana na makomred wa umma party, na kwa kutumia mipango na mbinu za chini kwa chini kuihujumu Serikali na kuitoa madarakani kwa nguvu.

  Makomred baada ya uhuru
  Mara tu baada ya ZNP/ZPPP kuingia madarakani chama cha Umma kilipigwa marufuku. Makomred waliudhika mno na kwa hivyo walijipanga kulipiza kisasi chao. Hili linaweza kuwa kosa kubwa sana walilolifanya ZNP/ZPPP kwa kuwa mpaka wakati huo uhuru unapatikana sio ZNP, ZPPP wala ASP bali ni makomred wa Umma party peke yao ndio waliokuwa wamebobea katika mbinu za kijeshi na kivita. Katika kulipiza kisasi chao makomred waliungana chini kwa chini na kwa mikono miwili na viongozi wa Afroshirazi Youth League waliounga mkono ukomyunisti. Hivyo basi umoja wa makomred na ASP ukaundwa uliokuwa na lengo la kuijumu na kuipindua serikali ya ZNP/ZPPP. Katika kitabu cha Race Revolution and the struggle for the Human Rights in Zanzibar, Komred Ali sultan Bin Issa anasema kwamba:
  “Wakati ZNP walipokipiga marufuku chama cha umma, ASP walikuwa wameshajua wao zamu yao [ZNP] ilikuwa inakuja baadae. Kuna msemo wa Kiswahili unasema ukimuona mwenzio anyolewa wewe tia maji. Serikali [ya ZNP] ilituanza sisi kutupiga marufuku kwa kuwa ilikuwa ikituogopa kuliko ASP ijapokuwa sisi tulikuwa wachache. Hawakuaweza kuwamini kwamba ASP walikuwa na uwezo wa kuwafanya lolote lile lakini ukweli ni kwamba viongozi wa Youth League [ya ASP] hasa ndio walioyapanga mapinduzi” (Burgess 2009).
   
Loading...