Kumbukumbu : Uso kwa Uso na Simba.

Page 94

JF-Expert Member
Oct 22, 2015
5,204
15,198
Jana nilienda kanisani kutoa Shukrani, wakati natafakari juu ya mambo ambayo Mungu amenitendea kwa Ukuu wake nikakumbuka na Kisa hiki, Uso kwa Uso na Simba.

Wakati mwingine katika maisha, unaweza kutamani kupiga hatua fulani. Mfano, unaweza kutamani kuwa mtu fulani katika jamii. Lakini, unapokwisha kuwa mtu huyo huwa kuna changamoto kubwa sana ambayo pengine unaweza kuijutia nafasi hiyo.

July 200....
Ndiyo kwanza nilikuwa nimelitoka masomoni na kufika nyumbani. Kutokana ukweli kuwa jamii yetu ilikuwa ya Kifugaji, mwezi wa Saba huwa ni kipindi cha kuhama kwenda maeneo mengine kujitafutia malisho kwa ajili ya mifugo.

Sikuhitaji kuambiwa kuwa nahitajika kwenda kuwaangalia mifugo kwani natambua hilo ni jukumu la vijana katika jamii. Nilipumzika siku moja tu na keshokutwa baada ya kufika, nilianza safari kwenda uhamishoni walipo ng'ombe. Kutokana na umbali, nilitumia yapata siku mbili kufika. Nilifika siku moja baadae majira ya jioni.

Uhamishoni huku maarafu kama 'Ronjo', wanakuwepo askari wa jamii maarufu sana kama Morani na vijana wengine wadogo ambao bado hawajapitia jando. Wanawake ni nadra sana kuwepo. Huwa ni mkusanyiko wa boma mbalimbali. Niliwakuta wote wazima kabisa na buheri wa afya tele. Lakini, kuna jambo moja tu halikuwa sawa.

Simba alivamia na kuua ng'ombe wa boma lingine jana yake. Usiku huo huo nilipofika, aliwajeruhi wengine lakini hakuweza kuwaua. La, Haula!. Sasa ilitakiwa Simba auwawe. Hii ni ili kuepusha athari kubwa zaidi.

Hivyo usiku tulijikusanya Morani wa eneo hilo la Uhamishoni na kuazimia kwamba kesho asubuhi tukutane tuanze harakati za kumsaka Simba huyo na kummaliza. Ndugu zangu, sikia tu watu wanasema lakini Kiukweli usiku sikupata hata tone la Usingizi. Nawaza tu tukio lililopangwa kufanyika kesho yake. Kuua Simba.

Ijapokuwa nilishapambana na wanyama wengine kama fisi, Mbweha na Chatu, lakini hili la Simba hakika ilinitia hofu isiyo na kifani. Ikizingatiwa idadi yetu ilikuwa ndogo tu. Jumla, tulikuwa Morani 6 pekee na mzee mmoja ambaye kiitifaki hapaswi kwenda kwenye mapigano hayo. Acha kabisa Wakuu.

Masaa yalipita na asubuhi imewadia. Asubuhi ambayo jambo hili litatakiwa kutekelezwa. Tuliamka saa 12, Tuliwakamua ng'ombe kisha kupata maziwa kidogo na kuwafungulia wakapate majani maeneo ya karibu chini ya Uangalizi wa vijana wadogo. Karibia saa moja na dakika kadhaa tulijikusanya tukiwa saba.

Mzee akaanza kuzungumza. Simba lazima auwawe. Siyo siku nyingine, ni leo leo kabla jua halijazama. Kwanza alianza kwa kutukumbusha miiko ya Umorani;
1. Morani harudi nyuma. Mkishakubaliana jambo, hakuna kugeuza nyuma. Ni kusonga mbele tu. Morani husonga mbele daima.
2. Morani hakati tamaa. Pamoja na vikwazo atakavyokutana navyo lakini lazima afanikishe jambo aliloazimia.
3. Morani haogopi. Wewe ndiyo nguzo ya jamii nzima. Kuogopa kwako ni kuijaza hofu jamii yote. Pambana bila kuipa hofu nafasi katika mwili wako.
4. Morani hasaliti. Daima hutii kile anachoagizwa na wazee au kukubaliana na wenzake. Usiwasaliti wenzako. Usiwakimbie katika majanga.
5. Morani ni askari wa jamii nzima. Siyo kwa sababu wewe hujaguswa na janga ndivyo hivyo halikuhusu. Hapana, wana usemi wao kuwa likianza kwa yule linamaliza kwako. Kuokoa maisha ya yule ni kuokoa maisha yako.

Baada ya kuyazungumza na kutukumbusha yote, ni dhahiri kuwa hatukupaswa kupinga wazo lake zaidi ya kulitii ukizingatia kuwa simba alishaua ng'ombe mmoja na kuwajeruhi wengine kadhaa. Pengine tungeendelea tungeendelea kutulia angeleta madhara zaidi ikiwepo kuwavamia watoto.

Nitaendelea.
 
Kilichokuwa kinafata sasa ni matekelezo. Kuna matayarisho ya wali kabla ya kuanza safari. Kwanza hufanyika manuizi ambayo hupatikana Mkuu wa Kuwaongoza wengine. Pili kusafisha ngao pamoja na Kunoa mikuki na sime.

Mzee alifanya mambo mambo yake kisha akanielekeza kidole kuwa nyota yangu inaendana na siku hiyo hivyo ndiye ninapaswa kuwaongoza wenzangu. Roho karibia initoke. Kuwaongoza wenzangu kuua simba? Sikuwa na cha kuzungumza nilitulia kimya, sikutakiwa kujibu wala kukataa. Tukanoa sime na mikuki pamoja na kutayarisha ngao. Mwenzetu mmoja alikosa ngao, mimi ndiye niliyechukua ngao yake kutokana na kuwa Mkuu wa msafara. Kumbuka Simba lazima afe.

Kinachofanyika ni kuingia katikati ya Zizi la ng'ombe. Kisha kiongozi anawaongoza kutoka nje kwa mstari. Huku umebeba silaha zako zote. Tukatoka na kuanza kutembea muelekeo ambapo simba alijeruhi au kuua. Kuna manuizi hufanyika hivyo Simba hataenda mbali sana na alipofanya yake. Hao, tukaondoka. Kufika eneo hilo tukatawanyika sasa, ila hatukai mbali sana na kila mmoja wetu. Huwa tunapiga yowe ili Simba asikie na kujitokeza.

Tumezunguka na hatimaye tumemuona simba. Nilipomuona tu, nywele zilinisisimka kila kona ya mwili. Nilitamani nirudi nyuma kukimbia, nikakumbuka miiko ya Umorani. Nikasonga Mbele. Simba baadae akaanza kukimbia, hakuna kumuacha ni kumfukuzia tu. Akaenda akajiingiza kwenye kichaka fulani.

Tulipofika ni kuzunguka kile kichaka. Na sasa harakati za kumuua zinaanza. Lakini kuna sheria zake. Huwezi tu ukarusha Mkuki kiholela. Zifuatazo ni taratibu.
1. Kwanza usionyeshe hofu. Simba ana uwezo wa kumtambua mwenye hofu na hakika atapita na wewe kwanza. Utakuwa kitoweo chake siku hiyo.
2. Mikuki yote huwa juu, ikishikiliwa kwa mkono wa kulia au kushoto kutokana na mkono wenye uwezo nao. Hakikisha ngao umeishika kwa nguvu kuliko hata ulivyoshika Mkuki. Ili simba akikurukia umzibe nao.
3. Atakayeanza kurusha Mkuki ahakikishe anamchoma Simba kwenye Shingo na hakikisha hukosi target.
4. Mkuki wa kwanza ukirushwa, ndiyo ushara ya mapambano kuanza. Hivyo wengine mtafatia kwa kumchoma sehemu ambazo zitamkosesha nguvu.
5. Ukisharusha Mkuki, kwa speed ya ajabu uchomoe sime na uanze kumkatakata Simba kila mahali.

Hizo ndizo taratibu kuu ambazo lazima zifatwe katika kumuua Simba.

Nitarudi kuendelea.
 
Mimi Nina shida moja humu JF,hadithi kama hii nikija kuitafuta baadae siikuti,sijaelewa jinsi ya kutafuta thread za nyuma
 
SEHEMU YA 3
Wakati kila mmoja akiendelea kujitafakari kurusha Mkuki awe wa Kwanza, ghafla bin Haraka Simba alimrukia mwenzangu. Bahati nzuri au mbaya alikuwa na ngao. Lakini, kuna utaratibu pia. Ukiona Simba anakurukia Sogea hatua moja mbele au rudi hatua moja nyuma. Hii inakusaidia ili kum-push au kutokukuangukia kama zigo. Hii ni kumkosesha Simba balance. Ile incident sitaki kuikumbuka kabisa wakuu. Jamaa kwa ujasiri kabisa alipoona Simba anaruka, na yeye akapiga hatua moja mbele hivyo simba akasukumwa nyuma kidogo.

Sijui nilipata wapi ujasiri. Wakati Simba anaruka, nami ndipo niliporusha Mkuki wangu kwa nguvu ya ajabu. Nilijua hapa nimekwisha. Nilirusha Mkuki nikimkusudia shingoni lakini bahati mbaya kutokana na kujirusha kwake ilimpata tumboni. Ilimuingia haswa. Wenzangu nao walifatia. Simba alipigwa mikuki yote Sita.

Simba ana nguvu bhanah! Pamoja mikuki yote lakini bado alikuwa na nguvu. Alinyanyuka tena kumfata mwenzetu. Tukachomoa sime zetu zilizokuwa ndani ya ngao na kuanza kumkatakata maeneo mbalimbali. Inashauriwa sana kumkata miguu kwanza hasa kwenye catilages zinazounganisha unyayo (kwato) na mguu ili kumkosesha nguvu ya kutembea na kunyanyuka.

Simba alipomfata mwenzetu aligongwa na ngao na kusukumwa chini, sasa mkuki mmoja uligota chini kabisa. Simba alishindwa kunyanyuka. Ndipo akaanza kukatwa karibia kila pembe huku akinguruma kwa hasira na mhemuko.

Tulimuweza Simba. Hakuwa amekata roho lakini alipata maumivu yasiyomwezesha kumjeruhi mtu. Ningelikuwa na smart phone miaka hiyo, ningeliweza kuchukua selfie kabisa kabla hajalikata roho.

Nitaendelea.
 
SEHEMU YA NNE
Baada ya yote hayo, mikuki ilichomolewa na kummalizia kabisa mfalme huyu wa mwituni.
Nilijerujiwa mkono na sime katika harakati za kumkata Simba.

Baada ya yote hayo, Simba hukatwa Mkia pamoja na zile nywele zake kubwa. Wa kwanza kumtia Mkuki ndiye hupewa Mkia, kisha wa pili ndiye hupewa hizo nywele zake. Baada ya hapo Simba huzungushiwa majani fulani na kuachwa marehemu.

Safari ya kurudi nyumbani huanza. Hakika hakuna raha kama hiyo. Kukimbia kwa furaha na kuserebuka huku tukiimba nyimbo za kishujaa. Ni raha ya ajabu. Nilikuwa wa kwanza kumtia Mkuki. Nilikuwa Shujaa wa pambano. Pamoja na kuwa kiongozi wa msafara, nilikuwa pia shujaa wa kumtia Simba Mkuki. Ilinifurahisha sana. Mkia huo hufungwa kichwani, huku ukiitingisha kichwa. Inatia hamasa kuuzungusha na kuchezea.

Hali sasa ilikuwa shwari. Simba kamalizwa. Ni sherehe na burudani. Mwenye ng'ombe alifika jioni yake. Alufurahi sana. Alinizawadia ndama mmoja ambae hata hivyo baadae alikufa. Tulichinja mbuzi na kufurahi. Taarifa zilienea huko nyumbani maana huku tulikuwa uhamishoni porini kabisa. Nilitungiwa mpaka nyimbo za kunipongeza.

Hakuna siku ambayo nimeshindwa kuisahau. Huwa nikiikumbuka mwili wote unasisimka. Huwa najiuliza, ingekuwa vipi kama mimi ndiye niliyerukiwa na Simba? Ningeweza kweli kumrusha nyuma. Mungu ni mwema ndugu zangu.

Isingelikuwa taratibu kuwa wa kwanza kurusha Mkuki ndiye shujaa, hakika mwenzetu angelikuwa shujaa haswa......

Baada ya kukumbuka kisa hiki, nilitambua kuwa nina mengi sana ya Kumshukuru Mungu zaidi. Kaniepushia na kifo mkononi. Hakika yeye ni mwema.

This is my true Story. Ilinitokea katika Pori la Ngasurai huko wilayani Longido.. Sikukaa siku nyingi, nilirudi nyumbani na baadae kurudi shule.

====The End===
 
Back
Top Bottom