Kufuta falsafa - Afrika tunatengenezwa mataahira

EP cosmetics

JF-Expert Member
Oct 18, 2015
2,469
3,840
(Sehemu ya Kwanza)

UTANGULIZI
Andiko langu hili limelipanga katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza inahusu nadharia tete zangu kuhusiana na mdororo wa elimu na mmomonyoko wa maadili katika nchi za Kiafrika na kati ya watu weusi tuishio barani Afrika kwa ujumla. Sehemu ya pili inahusu mkasa unaotazamiwa wa kufutwa kwa somo la Falsafa katika taasisi zetu za elimu.

Kama nitakayosema si kweli basi ni nadharia zangu tete. Kama mambo hayo hayapo sasa basi labda yanakuja. Bila shaka, kila mzazi na mwanadamu anayejali na anayetazama vizuri maendeleo ya dunia, anafuatilia maendeleo ya watoto, vijana na Waafrika kwa ujumla.

Swali lake la maana ni “Kuna nini?” Kuna nini kwani kuna nini? Hili ni swali linaloendesha mbio mioyo ya wazazi na walezi wengi wenye kujali. Wasiojali wanatazama mambo haya kama watazamaji waliojihudhurisha kushuhudia mechi fulani ya mpira wa miguu. Kifupi, kuna ishara nyingi za kuporomoka viwango vya elimu barani mwetu.

I. KUTENGENEZEKA MATAAHIRA
Sikilizeni king’ora changu. Tunatengenezeka mataahira. Miaka 100 ijayo Afrika itajaa mazombi, mataahira wasioweza kujua jema/zuri wala ubaya. Natoa mifano mine kushadidia neno hilo. Mifano yangu nimeichapua kutoka sehemu nne nyeti: ofisi ya maamuzi, darasani, kwenye umma na kanisani. Ofisi ya Maamuzi
Vyombo vya juu vya elimu vinashinikiza kuondoa somo la Falsafa katika mfumo wa elimu. Kuna shida. Yaani watu wenye PhD wanataka somo la Falsafa liondolewe vyuoni sijui likishaondolewa “PhD” itamaanisha nini tena. Hisia zangu ni kwamba watu hao wenye vyeti vilivyoandikwa “PhD” hawajui hata maana ya “Ph” katika “PhD” walizopata. Inatisha. Je, si ishara ya mdororo wa elimu huo?

Darasani Kuna wanafunzi hata wa shahada wasiojua mambo ya msingi. Inasikitisha maana elimu ya Chuo Kikuu ndiyo elimu ya juu kuliko ya sekondari. Kama juu kunavuja, chini kumelowaje? Wanasema Waswahili, “Ukiona kilemba kimechafuka, usiulize makubasi!” Nina ushahidi. Nimeshuhudia mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya ualimu katika historia asiyejua historia ya nchi yake, Tanzania. Aliombwa azitaje tawala tatu zilizotokana na utawala wa Mbwambo wa Upare akaandika eti ni Afrika ya Kusini, Burkina Faso na Palestina. Hii maana yake hata Jiografia ya Tanzania hajui. Sasa mtu kama huyu atawafundisha nini watoto? Mwalimu wa historia asiyejua historia ya nchi yake mwenyewe atafundisha nini?

Kwenye Umma Nina ushahidi watoto wetu kuzidi kuwa wazito madarasani zaidi na zaidi. Lakini kusudi eti waonekane wamefaulu ufaulu wa juu, alama A imeshushwa ianzie 75%. Pamoja na kushushwa hivyo “maksi”, baadhi ya wanafunzi wanamaliza masomo pasipo kujua kuandika wala kuhesabu.

Hapa usiseme wanaomaliza masomo pasipo kujua kuandika vizuri pamoja na kushindwa kushika masomo wanayofundishwa. Hali ni mbaya mintarafu matumizi ya alama za uandishi, uandikaji maneno na matumizi ya aina za maneno, hususani nomino, vivumishi na vitenzi. Kwa mtu anayejua kanuni za lugha inakera sana vijana wanapoamua kujionesha kuwamo katika lugha za kigeni kama Kiingereza wakisema “Kiswanglish.” Hapo utasikia au utasoma vitu kama “kudefence”, “kuperfomance”, “kuleft” n.k. Yaani wanachukua nomino au vitenzi vilivyo katika muda uliopita kutengenezea vitenzi vya wakati uliopo jambo ambalo ni sawa na kujenga maneno kama “kumlo”, “kuchakula”, “kumasomo”, “kulikwenda” n.k.

Si haya tu, mdororo wa elimu unaakisiwa kwa nguvu mitandaoni kwa vijana wengi kushindwa kujibu hoja na badala yake kujibu kwa litania za matusi. Mtu anaandika kitu, anakuja mtu anamtukana tu.
Kanisani Baadhi ya viongozi na walimu wa dini waliotarajiwa kuwa wajuzi kusudi wafundishe kweli wanadhihirisha dhahiri shayiri kwamba nao ni wale wale.

Nimeliona andiko moja la mwalimu wa kutegemeeka sana katika Karismatiki akijadili kwa namna ya kusikitisha mada ya kuwinga pepo. Kiongozi huyo anajidai kujua Kiingereza. Lakini maneno anayojinasibu kuyajua wala hayajui. Anajinasibu kuwa anatofautisha “deriverlance” na “exoticism” vitu ambavyo sijui ni nini. Hii maana yake kama hajui hata kuandika (spell) istilahi anazozijadili hajui maana yake. Maneno unayoyajua lazima ujue yanavyoandikwa. Jiulize katika mfano huu “deriverlance” na “exoticism” ni nini? Natumaini anamaanisha “deliverance” na “exorcism.” Maskini mwalimu, eti hawezi kuona tofauti hapa!

Hadi hapa, naomba uhisi kitu. Kuna kitu. Kuna namna ya mdodoro wa kielimu. Kuna ujinga. Lakini shida si jambo hili tu. Kimaadili, tunastaajabu heshima na adabu vinavyomong’oka. Watoto na vijana wetu wanakazana kuyatoa mambo ya vyumbani hadharani.

Wasanii wetu wengi wakiimba wanaimba matusi na wakicheza wananengua viuno pasipo soni. Kifupi, wasanii wetu wanauziwa propaganda zozote hata zile za kuwadhalilisha wenyewe kijinsia na wanazinunua kwa rejareja. Hii maana yake akili yao imekaa henamu sana hawawezi kujitegemea katika kufikiri. Kwa maneno mengine akili ya kuambiwa hawachanganyi na zao.

Wasanii wengi wamekoma kuwa vioo vya jamii. Kwa kisa hicho, wamekuwa rahisi kupokea hata propaganda za ushoga na usagaji. Katika hili, hali ya kustaajabisha ni hiyo kwamba mtoto wa kiume anaweza kukubali kutumika kama mwanamke na mtoto wa kike kujigeuza kidume. Kwa nini mambo yanakwenda hivi? Zifuatazo ni nadharia zangu tete kuelezea mkasa huo.

Mzee wenu Pd. Titus Amigu.
Copy & Paste.
 
KUFUTA FALSAFA - AFRIKA TUNATENGENEZWA MATAAHIRA
(Sehemu ya Pili)

Kadiri yangu kuna mambo 19 yanayoweza kueleza mkasa wa mdororo wa elimu pamoja na mmomonyoko wa maadili.

1. Kulelewa na dada au kaka wa kazi. Walezi hawa ni watoto hawawezi kuwajengea watoto msingi wa maisha. Lakini ni kutotimiza wajibu kwa wazazi na walezi. Wanabinafsishaje malezi ya watoto wao? Nyumba unayotaka iwe imara huwezi kumwachia fundi saidia akuwekee msingi.

2. Kutonyonyeshwa kwa muda mrefu maziwa wa mama. Watoto wetu wengine wamenyonyeshwa zaidi maziwa ya ng’ombe, na hivyo si ajabu wao kufanana na ng’ombe kwani maziwa ya ng’ombe ni hasa kwa ajili ya kumtengeneza mtoto wa ng’ombe.

3. Kulelewa na mzazi mmoja. Mtoto akilelewa hivi anaelekea tabia za jinsia ya aliyemlea yeye ima ya kiume au ya kike.

4. Matamanio ya mama kutaka mtoto wa aina fulani, mtoto wa kike au mtoto wa kiume. Sayansi inasema matamanio ya mama au baba yanamfanya mtoto asadifu matamanio yake.

5. Kutoshujaishwa. Ulaya na Marekani watoto hurushwa juu na wazazi, walezi na jamaa zao wakiambiwa wao ni makamu ya Mungu, wao ni watoto muhimu waliozaliwa katika mataifa makubwa yanayotawala dunia. Maneno ya namna hii, huwafanya watoto wao wajiamini tofauti na watoto wetu tunaowatisha na kuwaogopesha uchawi, laana, mizimu, majini, nyoka, mijusi, mende n.k.

6. Kupewa mifano mibaya na baba na mama au walezi, mifano ya kulialia kwenye makongamano na kwenye mikesha kwa mfano ile ya Karismatiki. Watoto tunaowalea namna hii hukomaa katika kudhani dawa ya mambo magumu ni rahisi rahisi. Matokeo yake watoto na vijana wetu wengi hawatumii akili na nguvu katika kuamua na kutenda, sana sana wanamsubiri Mungu awatendee miujiza. Lakini mwanadamu alipewa akili na utashi kusudi mambo mengine atatue mwenyewe.

7. Kutofundishwa kazi za mikono isipokuwa kufundishwa nadharia za kutamani kazi za “kola nyeupe” tu, yaani kazi zisizotoa jasho. Tumewasaliti viongozi wetu wazalendo, akina Julius Nyerere, Kenneth Kaunda, Kwame Nkurumah na kadhalika waliojaribu kuingiza elimu ya kujitegemea mashuleni. Wahusika wa mitaala, kwa sababu ya kununulika au kwa umbumbumbu, wakawasikiliza Wazungu waliotutaka tuwe na mitaala ya Kizungu na hivyo tuwalee watoto wetu kana kwamba wataishi London au New York. Tulirufai sana hapo. Ndiyo maana sasa hatuwezi kuwapeleka watoto wetu mashambani na kwenye kuchunga ng’ombe hata kama 80% ya watu wetu ni wakulima na wafugaji. Kwa sababu hii si wengi wanaokuja na mipango kazi ya kilimo kusudi siku moja kilimo kiwe mwajiri mkubwa. Kama sivyo, tutaendelea kulia ukosefu wa ajira bila kuchunguza tulipojikwaa na kuanza kuanguka. Tumeshaingia kwenye mtego wa kujiandaa kuwa mataahira katika miaka 100 ijayo.

8. Kulelewa kwa nepi sana. Watoto wengine wanajisaidia sana kwenye nepi jambo linalowafanya wasijifunze hata kujitegemea katika kujisaidia haja ndogo na kubwa. Ndiyo maana eti Wazungu au Wamerikani wanaweza kuja kutufadhili (kutujengea) vyoo kwenye shule zetu za msingi na sekondari wakati watoto wana baba na mama zao wengi sana. Hata vyoo tufadhiliwe? Aibu!

9. Kuacha dini na kusali au kuswali. Watu wengine hawajali kanuni ya sala na kazi. Lakini kusali ni kumwomba Mungu baraka, msaada na msamaha kwa sababu sisi hatukujiumba wenyewe. Aliyetuhuluku (Mungu) alikuwa na malengo nasi na hivyo si vizuri kutupana naye mikono.

10. Serikali na walimu kuwadanganya raia kwa kuwaonesha wanafaulu sana mitihani, wakati wameshusha alama za kufaulu hadi 75%. Yaani magoli yamepanuliwa kusudi kila mmoja afunge. Inawezekanaje watoto zaidi ya 100 darasani wote wapate “divisheni wani?” Ni kweli watoto wetu wana akili hivyo? Siamini! Kama si kweli tunamdanganya nani? Wenyewe? Watoto? Umoja wa Mataifa? UNESCO? Tukitaka kuwapata watu wenye akili sana (cream) katika jambo fulani au kuwasomesha masomo fulani magumu tutawapataje? Kwa kuwadanganya hivi, raia wanaoneshwa wana akili sana wakati katika mataifa yaliyoendelea alama za kufaulu kuonesha akili ni za juu sana.

Kwa mfano, kwenye vyuo vya kipapa huko Roma, Italia, alama A inaanzia 96% sasa linganisha na 75% yetu. Jambo hili lina hasara kubwa. Mtu aliyeaminishwa kwamba ana akili anajenga kujiamini kwa bure. Alama za kufaulu mitihani zinasaidia kuwapanga raia katika akili na IQ zao halisi. La siyo, anayejiamini kipumbavu anaweza kuziba mianya yote ya kujisomea kwa bidii. Kwa sababu ya kudhani ana akili sana mtu anaweza kuacha kujifunza siku kwa siku akisahau ukweli wa kwamba hajui kila kitu na kwamba “Elimu haina mwisho.”

11. Ulimbukeni wa vifaa vya utandawazi: magari, kompyuta, simu za mkono na mitandao, You tube, Instagram, WhatsApp, Tiktok na kadhalika. Vitu hivi vinatupotezea muda mwingi sana sisi Waafrika, watoto, vijana na watu wazima. Hatujui kwamba vitu hivi vinatudumaza akili, kwa sababu sisi tunatazama, kutumia au kusikiliza tu. Kazi ya kusoma vitabu kutafuta uelewa inaachwa siku kwa siku. Hapo tunajididimiza kwenye ujinga, kwa maana walioandaa vitu hivyo ndio wenye akili na siyo sisi watumiaji. Sisi ni “magolikipa” wa kudka vitu vilivyobuniwa au kuvumbuliwa na wenye akili.

12. Kutofundishwa vizuri. Waalimu wengi siku hiz wanategea maswali ya miitihani iliyopita na hivi kuzipuuza mada zingine wanazojua hazitokei kwenye mitihani, kwa mfano mada ya matumizi ya alama za uandishi na uandishi wa barua. Kwa mfano, vijana hawasomi kwa uhalisia vitabu vya kuhakiki vya fasihi na kadhalika.

13. Kutojifunza kutoa mawazo makamilifu. Mawazo makamilifu huonekana katika kuandika sentensi na alama zake za uandishi, kwa mfano koma, alama ya mshangao, alama ya kuuliza na nukta. Matokeo ya kutofikiri kikamilifu huonekana katika kutokutumia herufi kubwa, mikato, nukta na kadhalika.

Maandishi ya vijana siku hizi hayana alama za kuuliza, mishangao wala nukta. Hii maana yake wanavyosema haiakisiwi kwa alama za uandishi hata kidogo. Hapa kosa ni la waalimu pamoja na vijana wenyewe. Watoto na vijana wetu hawafundishwi uelewa (comprehension) wala utunzi (composition) badala yake wanakaririshwa vitu na kisha kupimwa kwa maswali ya kuchagua (multiple choice) mfumo ambao unaweza kumfaulisha mtu kwa majibu ya kubahatisha tu. Hii maana yake nini? Maana yake ni hatari. Watu wasiojua kuandika na kuelewa hawataweza kuandika wala kuelewa mikataba inayohatarisha nchi na rasilimali zao.

14. Kusikiliza zaidi badala ya kutumia mikono kuandika. Kisayansi, kutikisa mkono kuandika mambo husaidia akili kunasa na kurekodi vitu. Kuandika mambo ni jambo bora kuliko kutazama na kusikiliza. Huko madarasani unawakuta vijana wasio na peni wala daftari kana kwamba ni watu wenye akili sana. Kwa kuwa wana simu za kisasa zenye kamera, wakiona kitu cha maana mara wanapiga picha tu. Hawaandiki, wanapiga picha.

15. Watoto na vijana wengi kuchukia kuandika na kusoma. Watoto na vijana wetu wengi wanapenda zaidi kusikiliza, tena kusikiliza muziki, michapo (stori) na kutazama picha. Hapa ndipo unapolelewa ubumbumbu wa kutokujua maneno yanaandikwaje (spelling). Ndiyo kisa tunaweza kukuta kitu alichoandika kijana anayechukuliwa kama msomi kinaonekana kama kimeandikwa na kijana wa madarasa ya chini kabisa. Unaweza kukuta walimu wenyewe hawakujifunza alama za uandishi na kwa kuwa hawajui kwamba hawajui hawachukui hatua yoyote ya kuwafundisha wanafunzi wao. Hali kadhalika wazazi na walezi.

Kwa upande wao wenyewe vijana hawachukui hatua ya kujiongezea maarifa kwa kujisomea na kujifunza wenyewe. Kujifunza? Ajifunze nani wakati mambo kama hayo hayatokei kwenye mitihani yoyote? Kwa sababu ya kuchukia kusoma, mtu anapomaliza shule anafurahi sana maana kuanzia wakati huo hatashika kitabu wala gazeti lolote kusoma. Siku ya kumaliza shule huandika ukutani kwa haraka kabisa “LY” maana yake “Last Year”, yaani mwaka wa mwisho wa kusoma. Tokea hapo kusoma kitu kirefu, mathalani cha kurasa mbili huumwa kichwa.

Kwa wengi wetu baada ya mitihani tunayofanyizwa kwa lazima tunaposoma, vitabu na magazeti vinakuwa sumu ya kututisha. Tukisafiri hatuchukui kitu chochote cha kujisomea, badala yake kama si kusoma soma meseji za simu na kuangalia mambo ya mitandaoni, tunasafiri tukinunua na kula maandazi, karanga na miwa.

16. Akina mama wa kutosha kuwarithisha watoto wao umbumbumbu tu. Utafiti unasema wanadamu hurithi 80% ya akili zao kutoka kwa mama zao. Sasa akina mama wetu wanaojilegeza na kushughulikia mambo ya urembo tu: kuvaa wigi, kubandika nyusi na kucha bandia wanawarithisha nini watoto wetu? Ndiyo maana nasema mwendo wetu ni wa Afrika kuwa mataahira ndani ya miaka 100.

17. Kufifia somo la hesabu vichwani mwetu. Somo la hesabu linachukiwa mwaka hadi mwaka na sasa vijana wetu hawaoni aibu kuanguka Hisabati. Somo la Hisabati linaitwa majina mengi ya ovyo, likiwamo jina la “somo la mama mkwe.” Vijana wetu hawajisikia aibu kutokujua hesabu. Kutokana na matumizi ya vyombo vya kupigia hesabu, uwezo wa kufanya hesabu kwa kutumia kichwa unatokomea. Hesabu ndogo tu ya kujumlisha mtu anahitaji chombo cha kukokotolea. Si hesabu ya kujumlisha tu, bali za kutoa, kuzidisha na kugawanya pia. Mashine za kupigia hesabu (calculators) zinauzwa kama njugu, na sisi hatujagutuka. Ndani ya miaka mia watoto wetu hawataweza kuhesabu vitu.

18. Kufutwa kwa masomo ya kutuamsha. Historia, uraia, maadili na falsafa. Hapo AI (Artificial Intelligence) tutaianzia wapi? Suala hili ndilo ninaloliweka kama sehemu ya pili ya andiko langu. Nisubirie kidogo.
19. Kuogopa au kukubali kushindwa masomo magumu. Sasa Waafrika wengi, pamoja na wanaoshika ofisi za juu katika elimu, tunaogopa au tunajihisi kutoweza masomo magumu: Fizikia, Kemia, Hisabati, Falsafa na masomo mengine ambayo hata Kiswahili chake ni kigumu kama vile “Space Physics”, “Astronomy”, “Biophyics” “AI - Artificial Intelligence” na kadhalika. Sisi na watoto wetu tumekubali kwamba tu watu wa akili ndogo tu. Tumekubali kushindwa. Tumetupa taulo ulingoni. Kwa kisa hiki, tunakaa chini kuwangojea wenye akili watuvumbulie mambo katika maeneo hayo na sisi tuyapokee kama maskini tu. Elimu ya juu kwetu si yetu ni ya Wamerikani, Wazungu na Waasia si sisi.

Hatima Ndogo
Kama umenipata vizuri, kwa haya yote tunarithishana umbumbumbu na ujinga. Ndipo usistaajabu nililolisema, miaka 100 ijayo Afrika litakuwa bara la mataahira na hivyo tutaendelea kutawaliwa. Kama hali hii inaandaliwa kutoka nje, basi watakuwa wametuweza kweli kweli, lakini ikiwa hali hii tunachangia wenyewe kwa makosa ya maamuzi yetu, utakuwa mwiba wa kutajitakia ambayo mtu huambiwi pole.

Mzee wenu Pd. Titus Amigu
Copy & Paste
 
Kinachoirudisha Africa nyuma ni kuwa na watu wa aina yako ambao mnalalamika tu.

Kizazi bora ni kile kitakachoamini katika ustawi Wa maisha huletwa na kifikiri vyema
 
KUFUTA FALSAFA - AFRIKA TUNATENGENEZWA MATAAHIRA
(Sehemu ya Tatu)

II. MKASA WA KUFUTA MASOMO MBALIMBALI
Mkasa wa kufuta masomo ya kutuamsha Waafrika unazidi kuchafuka. Masomo ya kutuamsha Waafrika yanafutwa moja baada ya jingine. Yanafutwa moja moja mpaka yatamalizika nasi tutatengenezeka mataahira ndani ya miaka 100 ijayo. Mahali pengine wamefuta historia. Wakoloni mambo leo wametufutisha somo la historia. Lakini hiyo maana yake nini? Maana yake Waafrika wasiweze kujua kama waliuzwa kama watumwa na Waarabu na Wazungu kwa miaka 400. Maana yake wasijue kwamba bara lao liligawanywa kama keki miaka ya 1884-1885 huko Berlin, Ujerumani, wakoloni wakajipatia ardhi kirahisi kutoka kwa machifu wetu kama akina Mangungo wa Msovero, wakoloni wakatutawala kwa ukoloni mkongwe na sasa wanatutawala kwa ukoloni mamboleo. Maana yake watu wasijue kwamba kulikuwa na vita vya wazalendo kama Majimaji (Tanganyika) na Maumau (Kenya). Wanataka wasijue kwamba kulikuwa na vita vya ukombozi barani mwetu vilivyopiganwa na watu kama akina Augustino Neto wa Angola na Samora Machel wa Msumbiji. Na tunavyoweza kutengenezeka mataahira, ndani ya miaka 100, vichwa vyetu havitakuwa na rekodi ya kueleweka ya historia yetu.

Mahali pengine wametufutisha somo la Maadili kusudi Waafrika hata tukisoma tuishi pasipo uadilifu. Pamoja na masomo ya historia, mahali pengine wamefutla somo la uraia. Eti hapa napo tunakaa kimya. Kwa hili uzalendo utastawishwaje? Utastawishwa kwa uelewa upi?

Tunamshukuru Mungu kwa nchi ya pekee, Rwanda. Wakati nchi zingine zikifikiria kinyume, Rwanda inajaribu kuingiza somo la Falsafa tangu hatua za mwanzo za masomo kusudi raia wake wajitambue na wajiivishe kifikra na kizalendo. Tufunue macho katika kampeni hii ya kufuta Falsafa kwani inamaanisha mambo mengi. Hebu sasa tuone baadhi ya maana hizo. Kwa muhtasari, tuangalie kwa mizani za faida na hasara.

Faida za Falsafa
Wanadamu wote tunahitaji falsafa kwa sababu ya faida zake nyingi na ndiyo maisha yetu. Jamii na taasisi zote duniani zimenufaika na falsafa kwa miaka mingi. Ndiyo maana kuna falsafa ya magharibi, mashariki, Afrika, Asia na kadhalika. Ndipo kuna wanafalsafa Wazungu, Wamerikani, Waasia, Waafrika na kadhalika. Tanzania na Afrika vitakuwa “maeneo viroja ya kwanza” kwa “wasomi” wake kutoona faida za falsafa. Tunakusudia kuushangaza ulimwengu? Ni kwa sababu ya akili nyingi au kwa sababu ya kukosa akili?

Faida za falsafa zipo katika nyanja zote za kitamaduni, kijamii, kiuchumi, kisayansi, kielimu na kadhalika. Faida zipo tele kabisa. Elimu hukua kwa kustaajabu, kuhoji, kutafiti na kujibu maswali. Elimu Mungu, elimu dunia (sayansi, teknolojia na yote yaliyomo ndanimwe) hayakui ma kuubadili ulimwengu pamoja kuboresha maisha yetu ya kimwili na kiroho pasipo hayo.

Ukiachilia pembeni elimu isiyo rasmi, tangu enzi za akina Socrates, Plato na Aristotle, elimu rasmi hutolewa kwa taratibu na kanuni. Ndiyo maana shahada ya juu, shahada ya uzamivu, huitwa PhD, “Doctor of Philosophy”, yaani ushuhuda kwamba msomi ameiva katika fikra na uchanganuzi wa mambo. “Uzamivu” ndiyo “udaktari wa falsafa”, si kingine.

Falsafa ndiyo mama wa mantiki katika kusoma na kujifunza masomo mengine yote kama sayansi: Hisabati, Fizikia, Kemia, Biolojia, Kosmolojia, Epistemolojia, Maadili na kadhalika. Sayansi na falsafa ni pacha na damu moja. Narudia. Ndiyo kisa msomi anayezamia katika masomo ya namna hii hutunukiwa PhD.

Kifupi, faida za falsafa zipo katika maisha yote, ya kimwili na kiroho. Jiulize, maadili, uzalendo na uadilifu vinakwendaje pasipo falsafa? Ndiyo kisa basi, maadili ni tawi la falsafa. Tena, falsafa imeungana na dini zote kwa sababu wanadini wanapoelezea imani zao hutumia uchanganuzi wa kitaalamu na mpangilio mwanana. Kati ya dini zote, dini za Ukonfusio, Uyahudi, Ukristo na Uislamu zinatumia sana falsafa. Kwa namna ya pekee, Ukristo na Uislamu vimejidumisha kwa miaka nenda rudi kwa sababu wasomi wake wamekuwa wakiunganisha falsafa na teolojia. Je, wengi wetu si Wakristo na Waislamu? Hata uwe mkana Mungu, ukanaji Mungu wako unajitahidi kuuweka kifalsafa, labda hujui tu. Ndipo ukana Mungu wako unaangukia kwenye tawi la “Falsafa ya Mungu” (philosophy of God au theodicy).

Hasara za Kufuta Falsafa
Nayaweka mawazo juu ya hasara za kufuta falsafa katika vipengele kadhaa kama ifuatavyo:

i. Kufuta Falsafa ni Kujiua Wenyewe
Mkasa wa kufuta Falsafa ni mkasa wa kusikitisha sana. Sijui wazo hili limetoka nje au ndani ya Afrika. Kama ni nje, basi nadhani watu wasiotutakia mema Waafrika wanakazana somo la Falsafa lifutwe kwenye vyuo vyetu vikuu ili tufe kifikra. Kama ndivyo kinachosikitisha ni kwamba wenyewe tumekaa kihasara hasara tukikosa kujua tunakotupelekwa. Kama ndivyo nadhani hao wanatuona sisi ng’ombe tu.

Tuvute fikra hivi, kufuta somo la Falsafa kwenye vyuo vyetu maana yake nini? Tuendelee kusema. Kuna maana nyingi sana. Kwa kuwa falsafa ina matawi mama sita, kufuta falsafa maana yake ni kuzikosa faida za matawi hayo yote na kuwa maskini katika: mantiki, kosmolojia, metafizikia, epistemolojia, falsafa ya Mungu na aestetiki. Aidha ina maana ya kujikosesha mifano yote ya siasa na tawala duniani. Maana yake pia ni kujikosesha maelezo, misingi na michango yote katika nyanja za sayansi, historia na maadili.

Maana mojawapo ni kufuta mustakabali wa Waafrika wenye kufikiri kitaalamu. Ni uzuiaji mimba za Waafrika wenye kuelewa. Wanaotutakia mabaya wanazuia wenye fikra tunduizi wasizaliwe popote katika bara hili. Maana yake wasiwepo watu wa kufikiri na kusema vizuri nchini mwetu na barani mwetu. Maana yake wasichipukie popote pale wazalendo au watu wenye kujitambua na kufikiri kama akina Kwame Nkurumah, Patrick Lumumba, Leopold Sengho, Julius Nyerere, Kenneth Kaunda na Nelson Mandela. Hawa walikuwa wanafalsafa wa Kiafrika. Kama wanafalsafa walikuwa na upeo mkubwa katika maamuzi ya kiuongozi. Ukiwasoma vizuri utagundua walipata mawazo yao ya kifalsafa na kimapinduzi walipokuwa vyuoni.

Kwa maneno mengine, kufuta Falsafa kama somo maana yake ni kuzuia wasichipukie wanasiasa wa maana kati yetu. Ni mauaji. Ni kuzuia uzazi wa kielimu. Uanafalsafa wa viongozi waliotuletea uhuru ulianzia vyuoni walikokuwa wanasoma. Lakini hata sasa tukitaka viongozi watakaotutoa kwenye makucha ya ukoloni mambo leo na unyonyaji unaoendelea lazima tuwapate wanafalsafa. Tufute falsafa tuwakose?

Lakini tena tujiulize wote kwa sauti. Hivi ni katika bara gani lingine ambako Falsafa si somo la watoto na vijana wao? Wapi walikozuia watu wao wasijihabarishe na fikra tunduizi za akina Socrates, Plato, Aristotle, Karl Marx na wengineo? Halafu tujiulize tena. Tusiwe kama tumelewa. Kama tukifuta Falsafa, “PhD” itakuwa inamaanisha nini nchini mwetu na barani Afrika wakati maana yake ni “Doctor of Philosophy?” Je, hapo mnaona mwendo wa kufanyika kwetu mataahira? Ndani ya miaka 100 watakuwa wengi mataahira kama wasomi wenyewe wameshaanza kutokujua maana ya vyeo vyao vya kitaaluma?

ii. Kufuta Falsafa ni Kujitukana
Ndugu zanguni, tutakuwa wajinga kweli tukikubali kufuta Falsafa katika vyuo vyetu vikuu na kishapo kuwa tunapokea “PhD.” Huko ndiko kufanyika mataahira. Wenye “PhD” sasa watakuwa wana hadhi gani ya kitaaluma? Basi, iwe ajabu zaidi watu wenye “PhD” sasa za kusomea sawa na za heshima kukubali kujifutia hiyo “Ph.” Waliosimama nyuma ya kampeni hii wanatuona wajinga tusioelewa chochote. Yaani wanaamini sisi ni wajinga wenye kufanana na watu wanaoweza kukata tawi la mti walilolikalia wenyewe. Hii ni dharau na sisi tusikubali kujitukana hivyo. Sisi ni watu wazima, “Fumbo mfumbe mjinga mwerevu atafumbua.”

Mzee wenu Pd. Titus Amigu
 
KUFUTA FALSAFA - AFRIKA TUNATENGENEZWA MATAAHIRA
(Sehemu ya Nne)

iii. Kufuta Falsafa ni Kukubali Ubaguzi wa Rangi
Kama suala la kufuta falsafa linachochewa na watu wa nje basi msingi wake ni ubaguzi wa rangi. Ni kutukanwa kwetu. Ni kuturudishia kinyemela matusi ya Wazungu wanafalsafa wanne: David Hume (1711-1776), Emmanuel Kant (1724-1804), Georg Wilhelm Friedrich Hegel (1770-1831) na Lucien Levy-Bruhl (1857-1939). Hawa walikuwa na mawazo hasi sana dhidi yetu watu weusi. Waliponda IQ (Hisa ya Akili) yetu na uwezo wa akili yetu kumudu mambo ya dhana. Tukisoma Falsafa tunaweza kukutana na mawazo yao hasi. Kifupi walitutukana Waafrika kama watu tusio kamili tusioweza kuwa na falsafa na vile vile wenye kushindwa kujifunza Falsafa.

David Hume alisema sisi watu weusi ni dhalili tukilinganishwa na watu weupe kwa sababu hatuna viwanda, sanaa na sayansi. Emmanuel Kant alisema utu wetu sisi watu weusi si mkamilifu. Badala yake utu wenye ukamilifu wa juu upo kwenye tabaka la watu weupe. Alisema sisi watu weusi sawa na wenyeji wa Marekani hatuwezi kuelimishwa. Alisema hata hivyo sisi, watu weusi, tunaweza kupatiwa mafunzo tukawa watumwa. Akaongeza kusema Wamerikani wenyeji na sisi watu weusi hatuwezi kujitawala isipokuwa tunaweza kutumika kama watumwa tu.

Georg Hegel alisema sisi watu weusi ni watu duni kwa sababu hatuna mataifa, historia, dini ya viwango vya juu wala Falsafa. Hatimaye, kwa upande wake, Levy- Bruhl alisema tofauti na Wazungu, akili yetu na lugha zetu sisi watu tusiostaarabika haviwezi kutufaa kuelewa au kushughulikia dhana. Sasa jiulize, tutakapoacha kusoma Falsafa hata habari za watu hawa waliotutukana hatutakuwa nazo. Kumbe, kwa kututaka tufute somo la falsafa wanaoshadidia jambo hilo kwa ama kujua au kutokujua, wanataka tukiri wenyewe kinyemela, kwa vitendo, jambo hilo la ubaguzi wa rangi yaani kukubali kwamba falsafa ni somo “tuliloliona wenyewe kuwa la kipuuzi kwenye vyuo vikuu vyetu.” Inasikitisha. Kama jambo hili tutashindwa kuliona kwenye vyuo vikuu, taasisi za juu na za mwisho katika taaluma, wataliona nani na wapi tena?

Kifupi, kama ni wageni wanaotushauri hivyo, basi wanataka tukubali kwamba sisi ni masokwe ambao tunaona masomo ya maana na tunayoweza ni yale rahisi kama kucheza, kula na kulala tu. Narudia. Kifupi, hao wanataka tukirishwe kwamba sisi ni wanyama tusioweza kufikiri kifalsafa tofauti na watu weupe. Maana yake tunatakiwa kuungishwa mkono kubaguliwa kwetu wenyewe. Hapa tugutuke hima!

iv. Kufuta Falsafa ni Dalili ya Mdodoro wa Elimu
Nasisitiza kusema kufuta Falsafa ni dalili ya kutoelewa michezo ya dunia. Kama kampeni ya kufuta falsafa imetoka ndani ya bara letu au kwetu wenyewe basi ni dalili mbaya ya kitu ninachokijadili. Ni kitu kinachosema jambo hilo hilo ninalolianza nalo kujadili katika andiko hili: kuongezeka kwa umbumbumbu barani mwetu kiasi cha kwamba katika miaka 100 ijayo bara hili litakuwa limejaa mataahira. Kifupi, ni dalili ya mdodoro wa kitaaluma unaoendelea kuota mizizi. Ni kushindwa kuchanganua ramani ya mustakabali wetu wenyewe.

Ni ishara ya kuburuziwa mbele kiupofu. Kama mtu ana PhD na anakazana kusema falsafa haina mashiko kwa vijana kama haikutoka kwenye mnyororo wa kusomea tangu shule ya msingi na sekondari aliiba au alihonga akaipata? Naomba radhi! Ashakum si matusi! Huo ni utaahira maana taahira ni mtu pekee anayeweza kuchoma moto nguo yake aliyoivaa maana hajui maana yake nini ingawa i maungoni mwake mwenyewe. Au wasomi wetu wanaopendekeza kufuta falsafa vyuoni kwa sababu si somo lililosomwa tangu shule za msingi na sekondari hawajui kwamba shahada za uzamivu walizonazo zinaitwa PhD na PhD maana yake ni “Doctor of Philosophy?” Huu ni umbumbumbu au nini ? Ni ulevi? Kama ni mojawapo ya hivi, basi si ajabu mtu mwenye PhD katika Kemia kutokuona muunganiko wa Kemia na Falsafa. Hii ni hasara kweli!

v. Hoja Inayotolewa ni Uongo wenye Kukera
Imesikika hoja kwamba tunapoingia vyuo vikuu tusome masomo yaliyokaa kwenye mnyororo wa kuanzia shule ya msingi hadi kwenye sekondari na siyo kama Falsafa inayokosekana katika hatua hizo za mwanzo. Na vivyo hivyo eti hata wahadhiri wawe waliosomea kwa mnyororo wa namna hiyo hiyo. Kama hoja ni hii ni hoja ya kujitukana wenyewe. Hivi tunamaanisha akili yetu haina nguvu ya kusoma masomo yasiyo katika mnyororo? Hapa pokeeni maswali yangu ya kuwafikrisheni kidogo. Ina maana tusisome udereva kwa sababu somo hilo halianzi katika shule za msingi na sekondari? Yaani tusisome umakanika kwa sababu somo hilo halianzi katika shule za msingi na sekondari?

Yaani tusisome udaktari wa madawa kwa sababu somo hilo halianzi katika shule za msingi na sekondari? Yaani tusisome fikizia ya anga kwa sababu somo hilo halianzi katika shule za msingi na sekondari? Yaani tusisome unajimu kwa sababu somo hilo halianzi katika shule za msingi na sekondari? Yaani tusisome AI (Artificial Intelligence) kwa sababu somo hilo halianzi katika shule za msingi na sekondari? Ina maana akili yetu ni dhaifiu kiasi hicho? Wapi pengine duniani watu wake walipo dhaifu hivyo? Ikiwa tu dhaifu hivyo, basi, tusomee kulala, kutembea, kukaa na kula tu, vitu ambavyo tuna uzoefu navyo toka utotoni. Maskini wa fikra siye! Tuanzishe basi programu zenye kuhusisha hayo, kula, kulala, kutembea! Mwendo wa kufikiri kwetu ukiwa ni huu, sisi kweli masokwe au la, wanaotudhania kuwa hivyo hawako mbali sana na ukweli.

Basi haya ni matusi; angelisema mtu mweupe tungelalamika kwamba anatuona sisi “machimpanzee” tusio na nguvu ya akili, yaani kwamba huyo anatuona sisi tunajua na kuweza kula, kulala na kuzaa tu. Lakini sasa kwa kuwa haya wanasema weusi wenzetu tunapokea kama hoja zenye mashiko! Lakini kwa kweli ni matusi kwa sababu ni kama kusema vijana wetu wana akili fupi ambayo kwayo hawawezi kujifunza chochote kama hawakuanzishiwa kwenye shule ya msingi na kuendelezewa katika sekondari. Ha! Matusi kweli kweli!

vi. Je, Tunakubali Kutukanwa na Kujitukana?
Nisikilizeni. Tutafute hoja yoyote ile kufutia Falsafa vyuoni, tutakuwa tunakubali kutukanwa na kujitukana wenyewe. Kukubali kutukanwa kwa maana kwamba tunaunga mkono kinyemela matusi ya kibaguzi ya akina Hume, Kant, Hegel na Levy-Bruhl kwamba sisi watu weusi hatuna akili yenye nguvu ya kusomea Falsafa na hivyo kifupi kuwa na akili fupi inayoweza kusomea mambo rahisi tu tena tuliyoandaliwa tangu shule ya msingi na sekondari tu. Na kukiri hivyo ni kama kukiri wenyewe kwamba sisi ni manyani watupu, ni nusu watu tu. Halafu kukubali hili ndiko kujitukana sana wenyewe. Lakini kwa kisa hicho hicho ndiyo tunahitaji falsafa.

vii. Kuwatukana Wengine
Papo hapo, tunapojitukana wenyewe tutakuwa tunatangaza pia kwamba hata kama tunatunukiana “PhD” hatujui maana yake hata kama shahada zinatamkika na “Ph” ndani yake. Na kama huko ni kujitukana wenyewe basi ni kuwatukana watu wengine wote wenye PhD yaani pamoja na marais wetu na wengineo wenye PhD za kusomea na za heshima. He! Kama ndivyo tupime maneno yetu tujiulize kama hayo kweli ndiyo tunayotaka kusema. Kifupi nakualikeni tupime maneno yetu na tunachotaka kukifanya kwa kufuta somo la Falsafa. Tumekubali kutukanwa, kujitukana na kuwatukana wote wenye PhD?.

Tunapowatukana wenye PhD wote ni sawa na kuwaambia ni wajinga na malala bongo tu. Kifupi, kama PhD maana yake ni “Daktari wa Falsafa”, kukubali kwamba Falsafa ni somo lisilo na mashiko kwa vijana wetu, ni kusema kwamba viongozi wetu wengi ni “makanyaboya” kwa sababu ndio wenye PhD za kusomea pamoja na za heshima. Marais wastaafu wana PhD za heshima, tunawatukana sasa kama “makanyaboya?” Marais walio madarakani sana wana PhD za heshima tena wengine mbili ni “makanyaboya” pia? Je, haya ndiyo mapana ya maamuzi ya kuachana na masomo ya falsafa? Kukubali kujitukana na kuwatukana wasomi wengine? Kama ndivyo huko si kujiandaa kuwa mataahira? Si kwamba kwa andiko hili nataka kuwachonganisha wanadamu, ila nawaomba wanaotukanwa iwaume nao waingilie kati matusi haya.

HATIMA YA MWISHO
Kama suala la kufuta masomo yenye kutuamsha, hususani Falsafa, limetoka kwa Wazungu wana maana mbili: ima wanatudharau kuwa sisi si watu kamili tunaolingana na wengine tukaweza kusoma hata masomo ya dhana au wanaendeleza mkakati wa siri wa kututengeneza mataahira kusudi watutawale milele. Kwa namna hiyo wanajihakikishia hatuwi na kitu cha kutuamsha wasije wakalala wao.

Hatimaye, kama jambo hili limetoka kwetu sisi wenyewe Waafrika lina maana mbili pia: ima watu wetu wamebambwa na umbumbumbu mkubwa kiasi hawajui wala hawaoni maana ya PhD zao au wamenunulika na wale wanaoishi wakitudharau kuwa sisi tu manyani yasiyoweza kufikiri.

Nchi nyingi za Afrika zina miaka zaidi ya 50 ya uhuru, tutajitegemea lini katika kufikiri na kuratibisha mitaala yetu? Mbona inaonekana tunajaribia kila kitu? Tutakoma lini kuanza kitu, kuacha, kuanza kingine na kuacha? Afrika! Afrika! Tanzania! Tanzania! Mbona tunakubali kufanya majaribio taaluma yetu? Miaka yote hii falsafa imekuwa kitu cha maana, watu wenye akili mpya ya kuona falsafa haina maana wanatokea wapi humu nchini na barani mwetu? Wametumwa au ni akili yao wenyewe? Je, tunataka kujaribu ujinga baada ya kuona elimu ghali? Tunaogopa falsafa au hatujui faida zake? PhD zetu maana yake nini?

Huu ni mkasa unaochochea simanzi kubwa. Afrika ilikuwa kama inataka kutoka katika udhalili wake, lakini inaonekana spidi ya kurudi kule kule nyuma imeongezeka, na wanaoiongeza ni wale tuliowapa dhamana ya kututoa huko. Kweli ng’ombe wa maskini hazai, akizaa anazaa dume! Hakika wa moja havai mbili!
Tufanye Nini?

Tuna jambo moja tu la kufanya ima kufikiri upya au akili ya kuambiwa kuchanganya na yetu. Kama hamkubali kwamba ndani ya miaka 100 Afrika itajaa mataahira, basi ni nadharia tete. Kama ni nadharia tete, nawaalikeni mtafiti. Kati ya kazi za falsafa ni kustaajabu, kuhoji, kutafiti na kujibu maswali ya maisha haya. Leo nimewapeni maswali ya kuyafanyia kazi. Tuyajibu.

Mzee wenu Pd. Titus Amigu
(Mwisho wa andiko)
 
(Sehemu ya Kwanza)
UTANGULIZI

Andiko langu hili limelipanga katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza inahusu nadharia tete zangu kuhusiana na mdororo wa elimu na mmomonyoko wa maadili katika nchi za Kiafrika na kati ya watu weusi tuishio barani Afrika kwa ujumla. Sehemu ya pili inahusu mkasa unaotazamiwa wa kufutwa kwa somo la Falsafa katika taasisi zetu za elimu.

Kama nitakayosema si kweli basi ni nadharia zangu tete. Kama mambo hayo hayapo sasa basi labda yanakuja. Bila shaka, kila mzazi na mwanadamu anayejali na anayetazama vizuri maendeleo ya dunia, anafuatilia maendeleo ya watoto, vijana na Waafrika kwa ujumla.

Swali lake la maana ni “Kuna nini?” Kuna nini kwani kuna nini? Hili ni swali linaloendesha mbio mioyo ya wazazi na walezi wengi wenye kujali. Wasiojali wanatazama mambo haya kama watazamaji waliojihudhurisha kushuhudia mechi fulani ya mpira wa miguu. Kifupi, kuna ishara nyingi za kuporomoka viwango vya elimu barani mwetu.

I. KUTENGENEZEKA MATAAHIRA
Sikilizeni king’ora changu. Tunatengenezeka mataahira. Miaka 100 ijayo Afrika itajaa mazombi, mataahira wasioweza kujua jema/zuri wala ubaya. Natoa mifano mine kushadidia neno hilo. Mifano yangu nimeichapua kutoka sehemu nne nyeti: ofisi ya maamuzi, darasani, kwenye umma na kanisani. Ofisi ya Maamuzi
Vyombo vya juu vya elimu vinashinikiza kuondoa somo la Falsafa katika mfumo wa elimu. Kuna shida. Yaani watu wenye PhD wanataka somo la Falsafa liondolewe vyuoni sijui likishaondolewa “PhD” itamaanisha nini tena. Hisia zangu ni kwamba watu hao wenye vyeti vilivyoandikwa “PhD” hawajui hata maana ya “Ph” katika “PhD” walizopata. Inatisha. Je, si ishara ya mdororo wa elimu huo?

Darasani Kuna wanafunzi hata wa shahada wasiojua mambo ya msingi. Inasikitisha maana elimu ya Chuo Kikuu ndiyo elimu ya juu kuliko ya sekondari. Kama juu kunavuja, chini kumelowaje? Wanasema Waswahili, “Ukiona kilemba kimechafuka, usiulize makubasi!” Nina ushahidi. Nimeshuhudia mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya ualimu katika historia asiyejua historia ya nchi yake, Tanzania. Aliombwa azitaje tawala tatu zilizotokana na utawala wa Mbwambo wa Upare akaandika eti ni Afrika ya Kusini, Burkina Faso na Palestina. Hii maana yake hata Jiografia ya Tanzania hajui. Sasa mtu kama huyu atawafundisha nini watoto? Mwalimu wa historia asiyejua historia ya nchi yake mwenyewe atafundisha nini?

Kwenye Umma Nina ushahidi watoto wetu kuzidi kuwa wazito madarasani zaidi na zaidi. Lakini kusudi eti waonekane wamefaulu ufaulu wa juu, alama A imeshushwa ianzie 75%. Pamoja na kushushwa hivyo “maksi”, baadhi ya wanafunzi wanamaliza masomo pasipo kujua kuandika wala kuhesabu.

Hapa usiseme wanaomaliza masomo pasipo kujua kuandika vizuri pamoja na kushindwa kushika masomo wanayofundishwa. Hali ni mbaya mintarafu matumizi ya alama za uandishi, uandikaji maneno na matumizi ya aina za maneno, hususani nomino, vivumishi na vitenzi. Kwa mtu anayejua kanuni za lugha inakera sana vijana wanapoamua kujionesha kuwamo katika lugha za kigeni kama Kiingereza wakisema “Kiswanglish.” Hapo utasikia au utasoma vitu kama “kudefence”, “kuperfomance”, “kuleft” n.k. Yaani wanachukua nomino au vitenzi vilivyo katika muda uliopita kutengenezea vitenzi vya wakati uliopo jambo ambalo ni sawa na kujenga maneno kama “kumlo”, “kuchakula”, “kumasomo”, “kulikwenda” n.k.

Si haya tu, mdororo wa elimu unaakisiwa kwa nguvu mitandaoni kwa vijana wengi kushindwa kujibu hoja na badala yake kujibu kwa litania za matusi. Mtu anaandika kitu, anakuja mtu anamtukana tu.
Kanisani Baadhi ya viongozi na walimu wa dini waliotarajiwa kuwa wajuzi kusudi wafundishe kweli wanadhihirisha dhahiri shayiri kwamba nao ni wale wale.

Nimeliona andiko moja la mwalimu wa kutegemeeka sana katika Karismatiki akijadili kwa namna ya kusikitisha mada ya kuwinga pepo. Kiongozi huyo anajidai kujua Kiingereza. Lakini maneno anayojinasibu kuyajua wala hayajui. Anajinasibu kuwa anatofautisha “deriverlance” na “exoticism” vitu ambavyo sijui ni nini. Hii maana yake kama hajui hata kuandika (spell) istilahi anazozijadili hajui maana yake. Maneno unayoyajua lazima ujue yanavyoandikwa. Jiulize katika mfano huu “deriverlance” na “exoticism” ni nini? Natumaini anamaanisha “deliverance” na “exorcism.” Maskini mwalimu, eti hawezi kuona tofauti hapa!

Hadi hapa, naomba uhisi kitu. Kuna kitu. Kuna namna ya mdodoro wa kielimu. Kuna ujinga. Lakini shida si jambo hili tu. Kimaadili, tunastaajabu heshima na adabu vinavyomong’oka. Watoto na vijana wetu wanakazana kuyatoa mambo ya vyumbani hadharani.

Wasanii wetu wengi wakiimba wanaimba matusi na wakicheza wananengua viuno pasipo soni. Kifupi, wasanii wetu wanauziwa propaganda zozote hata zile za kuwadhalilisha wenyewe kijinsia na wanazinunua kwa rejareja. Hii maana yake akili yao imekaa henamu sana hawawezi kujitegemea katika kufikiri. Kwa maneno mengine akili ya kuambiwa hawachanganyi na zao.

Wasanii wengi wamekoma kuwa vioo vya jamii. Kwa kisa hicho, wamekuwa rahisi kupokea hata propaganda za ushoga na usagaji. Katika hili, hali ya kustaajabisha ni hiyo kwamba mtoto wa kiume anaweza kukubali kutumika kama mwanamke na mtoto wa kike kujigeuza kidume. Kwa nini mambo yanakwenda hivi? Zifuatazo ni nadharia zangu tete kuelezea mkasa huo.

Mzee wenu Pd. Titus Amigu.
Copy & Paste.

Halafu tukiletewa msaada wa fortified rice tunasema nchi inachafulliwa, inachafuliwaje wakati ni chafu miaka na miaka, unawezaje kuchafua dumpster?. Kuna kitu gani tunafanya kutumia hata robo ya akili ya kibinadamu? Kila kitu sisi wa mwisho hamna cha kujivunia hata kimoja, hata kulisha familia tu mazao yetu duni hatuwezi, sembuse mambo mazito kama falsafa?

MaPhd hawana hata hiyo personal philosophy wanarukaruka tu kujiita wa majalalani kulamba tupu za wanasiasa weupe kbs vichwani! Tufanye maombi labda tutasolve matatizo ya nchi kwa miujiza tu toka juu mbinguni! Sisi tulipewa akili ya kula, kulala na kunywa ndio maana sio ajabu mwanasiasa akipata kiti tu anajioverfeed na ndani ya mwaka utakuta ana likitambi hata kupumua vyema hawezi tena, tunaiba mali ya umma kupitiliza ili kujihakikishia tutaendelea kula tu miaka na miaka hatuna plan ya kuleta mabadiliko yoyote ya maana kwenye jamii zetu zaidi ya kujilisha.
 
Back
Top Bottom