Kuasi kwa jeshi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kuasi kwa jeshi

Discussion in 'Jukwaa la Historia' started by Mudathru, Sep 8, 2012.

 1. M

  Mudathru Member

  #1
  Sep 8, 2012
  Joined: Apr 24, 2011
  Messages: 68
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 15
  Ni sababu gani zilizopelekea kuasi kwa jeshi 1964?Kwa anaefahamu anisaidie
   
 2. J

  JokaKuu Platinum Member

  #2
  Sep 8, 2012
  Joined: Jul 31, 2006
  Messages: 12,734
  Likes Received: 4,955
  Trophy Points: 280
  ..africanization ilichelewa jeshini.

  ..polisi, na sehemu nyingine nyeti zilikuwa tayari zimeshikwa na wazawa, kupitia zoezi la africanization.

  ..jeshini wao waliendelea kuongozwa na mkuu wa majeshi mzungu, pamoja na maofisa wengi wengine wakizungu.
   
 3. U

  Udaa JF-Expert Member

  #3
  Sep 9, 2012
  Joined: Jun 8, 2012
  Messages: 727
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  Endeleeni kufunguka zaidi wakuu.
   
 4. hovyohovyo

  hovyohovyo JF-Expert Member

  #4
  Sep 9, 2012
  Joined: Jul 8, 2012
  Messages: 540
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 35
  Tafuta John Illiffe A Modern History of Tanganyika, utapata uelewa kamili juu ya what happened, why and how it happenned na jinsi serikali ya Nyerere ilivyosgughulika nalo.
   
 5. cement

  cement JF-Expert Member

  #5
  Sep 9, 2012
  Joined: May 5, 2012
  Messages: 583
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 35
  SOMA HAPA KILICHOTOKEA

  LINK Raia Mwema - Nani alichochea jeshi kuasi mwaka 1964


  USIKU wa kuamkia Januari 21, 1964, Jeshi la Tanzania liliasi na kushikilia serikali kwa muda, tukio ambalo Baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alilielezea kuwa ni "siku ya aibu sana kwa Taifa" .
  Wakati jeshi hilo likiasi; siku hiyo hiyo, na saa hiyo hiyo, majeshi ya Kenya na Uganda nayo yaliasi kwa staili hiyo hiyo. Maasi yote ya nchi tatu hizo yalizimwa na majeshi ya Uingereza siku moja na wakati huo huo.
  Kwa Tanzania, maasi haya yalitokea wiki moja tu baada ya mapinduzi ya umwagaji damu ya Zanzibar, Januari 12, 1964; na usiku huo wa maasi hayo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar "Field Marshal" John Gidion Okello, alikuwa na mazungumzo na Mwalimu Nyerere Ikulu, Dar es Salaam, katika hali ya kubadilishana mawazo juu ya hali ya Zanzibar ambapo Mwalimu, alimshauri Okello afanye kazi kwa imani na Rais Abeid Amani Karume.
  Karume aliteuliwa na Okello, Januari 13, 1964 kuwa Rais asiye Mtendaji kutokana na mapinduzi hayo; na yeye Okello akajiteua Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
  Maasi hayo yalitulizwa kwa juhudi kubwa za Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi, Oscar Satiel Kambona, kabla ya kudhibitiwa na hatimaye kuzimwa kabisa na wanajeshi wa Kiingereza siku moja baadaye.
  Mpaka leo, haijafahamika vizuri aliyepanga na kutekeleza maasi hayo; lakini swali kuu linaloulizwa bila kupata jibu ni je, ilikuwaje majeshi ya nchi tatu za Afrika Mashariki kuasi siku na wakati ule ule, juma moja tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar?
  Dhana moja inajitokeza kwamba, kwa kuwa John Okello, mzaliwa wa Lang'o, Uganda, ndiye aliyeongoza Mapinduzi ya Zanzibar, na pia kwamba aliwahi kuishi nchini Kenya kabla ya kwenda Zanzibar miezi michache kabla ya Mapinduzi; huenda alikuwa na mkono wake katika maasi hayo. Okello alijitapa pia kushiriki vita vya Mau Mau nchini Kenya, miaka ya 1950.
  Lakini, kwa vipi maasi hayo nchini yaanze usiku huo huo Okello alipokuwa mgeni wa Mwalimu, Ikulu? Alitorokaje yalipoanza?
  Ipo dhana nyingine kwamba, huenda Oscar Kambona alikuwa na mkono wake. Kwa nini wanajeshi walimsikiliza yeye, wakati huo huo askari hao wakimtafuta Mwalimu hadi viwanja vya Ikulu, kwa shari au vinginevyo?
  Kupata majibu ya maswali haya, hatuna budi kuangalia kwa ufupi matukio kadhaa yaliyotangulia maasi ya nchi hizo tatu, kuona kama yana uhusiano wowote.
  Tanzania bara ilirithi Jeshi kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza baada ya uhuru, Desemba 9, 1961, likijulikana kama "Kings African Rifles" – (K. A. R) na baadaye kuitwa "Tanganyika Rifles" (TR) na kutokana na maasi hayo ya Januari, 1964 likaitwa "Jeshi la Wananchi wa Tanzania" (JWTZ).
  Katika kipindi kufuatia uhuru, ili kukidhi matarajio ya Watanganyika, zilitakiwa hatua za haraka kuhakikisha nafasi zote za juu serikalini na taasisi zake, zinashikwa na Wazalendo. Huu ni utamaduni uliokuwa umejengeka kwa nchi zote za Kiafrika zilizokuwa zikipata uhuru
  Nyerere hakuwa na ujasiri wa kuchukua hatua haraka hivyo, kama pia ambavyo Waziri wake wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Clement George Kahama, hakuwa na ujasiri wa kuwatimua Waingereza katika nafasi za juu ndani ya Jeshi la Polisi.
  Yakaanza malumbano ndani ya Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Tawala, Tanganyika African National Union (TANU), kwamba Nyerere alikuwa anairudisha Tanganyika katika enzi za Ukoloni, na hivyo kwamba "uhuru" haukuwa na maana kwa Watanganyika kwa kushindwa kwake kuwapa vyeo Waafrika.
  Ili kuepusha shari, na ili Chama kisifarakane, Mwalimu akaachia ngazi Januari 16, 1962 na kurejea kijijini kuimarisha Chama kama Mwenyekiti wa Taifa wa TANU; na Rashid Kawawa akachukua Uwaziri Mkuu. Naye Oscar Kambona, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Elimu, akawa Waziri wa Mambo ya Ndani badala ya George Kahama. Wote wawili hao wakaachiwa kazi ya kuwaondoa Wazungu katika vyeo walivyokuwa bado wanashikilia haraka bila visingizio.
  Kazi ya kwanza ya Kambona ilikuwa ni kumtimua Kamishna wa Polisi Mwingereza, na kumteua Elangwa Shaidi kuchukua nafasi hiyo, lakini hakufanya mabadiliko kwa Jeshi (T. R.). Zoezi hili la "Africanisation" lilifanywa kwa kasi ya kutisha kiasi cha kuishitua jamii ya Kimataifa.
  Desemba 1962, ulifanyika Uchaguzi Mkuu ambapo Mwalimu Nyerere alichaguliwa kuwa Rais Mtendaji wa kwanza. Kwa hiyo, Januari 1963, Mwalimu alirejea madarakani kama Rais wa kwanza wa Tanganyika na kusitisha mara moja zoezi la "Africanisation" na kuchochea hasira ya viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi nchini, ambao waliapa kutolala usingizi, wala kuupa nafasi uamuzi wa Mwalimu wa kusisitiza zoezi la kuwapa madaraka Watanganyika.
  Kwa wiki nzima baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mwalimu alijishughulisha zaidi na mambo ya hali ya kisiasa nchini Zanzibar, ambapo Jumapili ya Januari 13, 1964; alikutana na Karume (aliyeondoka Zanzibar usiku saa chache kabla ya Mapinduzi kuanza), akamshauri arudi Zanzibar mara moja isije kutafsiriwa kwamba alikimbia mapinduzi kwa woga.
  Siku hiyo ndiyo Okello alitangaza Serikali yake mpya, ambapo alijiteua kuwa Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi na akamteua Karume Rais asiye Mtendaji; kisha akamwita arudi haraka kutoka popote alikokuwa (amejificha?) ili ashike nafasi yake.
  Jumatatu, Januari 14, Kambona, wakati huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi, akiwa Nairobi, alimpigia simu Nyerere kumtaarifu kwamba Kenya na Uganda tayari zilikuwa zimeitambua Serikali mpya ya mapinduzi Zanzibar na kumwomba naye aitambue. Nyerere alikataa akisema hakuwa na hakika kama kweli Karume alikuwa ameshika madaraka.
  Jumanne, Januari 15; Mwalimu alikwenda Nairobi kukutana na Waziri Mkuu wa Kenya, Jomo Kenyatta, kuzungumzia Shirikisho la Afrika Mashariki, ambako alibaini kuwa Kenyatta na Milton Obote (Uganda) walikuwa wamefuta kabisa wazo hilo, baada ya kubaini kuwa shirikisho hilo lilikuwa mbinu za mkoloni kuzitia nchi hizo ndani ya kikapu kimoja ziweze kudhibitiwa kwa urahisi chini ya "uhuru wa bendera".
  Jumatano, Januari 16, Sultani wa Zanzibar, aliyetimuliwa na Okello Zanzibar, alitia nanga Dar s Salaam, baada ya kukataliwa kutia nanga wala kupewa hifadhi na Serikali ya Kenya. Mwalimu alimpokea na kumpa hifadhi hadi aweze kukamilisha mipango ya kukimbilia uhamishoni nchini Uingereza.
  Alhamis, Januari 17, Mabwana Karume, Abdulrahman Babu na Kassim Hanga, walikutana na Mwalimu, Ikulu, kuelezea hali ya kisiasa ilivyokuwa Visiwani, na kuomba wapelekwe askari Dar es Salaam wa kutuliza Ghasia (FFU) ili kurejesha hali ya utulivu na amani. Siku hiyo, Okello akafuta uteuzi wa Karume, wa nafasi ya Rais, badala yake akampa Umakamu wa Rais kwa kile alichodai kuwa "hakushiriki hata kidogo katika mapambano wakati wa mapindizu" kasha akajiteua yeye mwenyewe kuwa Rais na Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar.
  Ijumaa, Januari 18 na Jumamosi, Januari 19, zilikuwa tulivu kwa Mwalimu, ambapo Jumamosi hiyo, askari wa FFU 300 waliwasili Zanzibar kuitika ombi la Karume. Hata hivyo, kwa kupeleka askari hao 300, Mwalimu hakujua kwamba alikuwa anajipunguzia nguvu ya ulinzi wa nchi yake kwa siku ya maasi ambayo hakuitarajia.
  Matata yalianza usiku wa Januari 20, kuamkia 21 usiku huo, siku ambayo Okello alikuwa na mazungumzo na Mwalimu, Ikulu usiku. Lakini ilipofika saa 7:50 alfajiri, Januari 21, Mkuu wa Kikosi cha kwanza cha TR, Brigedia Patrick Sholto Douglas, aliamshwa nyumbani kwake na sauti ya baruji (buggle) na ving'ora, karibu na kambi ya Jeshi ya Colito (sasa Lugalo Barracks).
  Alipotoka nje, aliona askari wake 12 wakikamatwa na wenzao wenye silaha na kutiwa mahabusu. Ndipo alipofahamu kwamba, nusu ya askari 800 wa Kikosi hicho walikuwa wameasi. Aliweza kutoroka yeye na familia yake hadi katikati ya jiji, akaiacha familia kwa Balozi wa Australia, kisha akakakimbilia kwa Afisa mwenzake, eneo la Oyster Bay.
  Akiwa huko, akampigia simu Oscar Kambona, akamwomba, naye akakubali, kupeleka ndege tatu Kikosi cha Pili huko Tabora, kuleta askari waliokuwa bado waaminifu kwa Serikali.
  Douglas na Kambona hawakujua kwamba, tayari waasi walikuwa wamefunga barabara iendayo uwanja wa ndege; kwa hiyo, marubani walirudi mbio; naye Douglas akakimbilia kwenye Ubalozi wa Uingereza, akajificha kwa siku tano hadi Januari 25.
  Douglas alikuwa amempigia simu Mkuu wa Polisi, ambaye alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa Makamu wa Rais, Rashidi Kawawa, eneo la Ikulu na kumwamsha, kisha hao wawili kwa pamoja, wakaenda kumpa habari Mwalimu.
  Mwalimu alipoelezwa juu ya maasi hayo, alilipuka kwa hasira na ghadhabu kubwa papo hapo; akataka kwenda yeye mwenyewe kukutana na Waasi hao ili wamweleze sababu za kitendo hicho cha aibu. Mama Maria Nyerere, kwa machozi na kwa kupiga magoti, alimsihi mumewe asitoke kwenda kukutana na watu wenye silaha, lakini hakufanikiwa kumgeuza nia.
  Ndipo watu wa Usalama walipojenga hoja nzito kumzuia, na hoja hiyo ikamwingia; akakubali kuteremka dari ya chini, kisha yeye, Kawawa na Mama Maria Nyerere, wakatorokea mahali kusikojulikana. Wakati huo, tayari waasi walikuwa kwenye lango kuu la Ikulu wakimtafuta.
  Bado ni kitendawili kuhusu mahali Mwalimu na wenzake walikokuwa wamejificha. Wapo wanaodai alijificha Misheni au Kanisani; wapo pia wanaosema alijificha kwenye nyumba ya Balozi mmojawapo Jijini.
  Wengine wanasema alijificha kwenye kibanda kidogo sana (Kigamboni?) karibu na Pwani; na baadhi wanadai alikwenda Arusha au Nairobi. Lakini wapo pia wanaosema alijificha kwenye meli. Wala haielezwi kama John Okello aliondokaje Ikulu usiku huo baada ya mazungumzo au kama maasi yalimkuta Ikulu usiku huo.
  Kufikia saa 9:00 alfajiri, waasi walikuwa wamekamata kambi ya Colito, kisha wakajigawa vikundi vitatu na kuingia mjini. Kikundi kimoja kilibakia kulinda kambi ya Colito, kikundi cha pili, kikiongozwa na Sajini Francis Higo Ilogi, ndicho kilichokwenda Ikulu kumtafuta Rais; wakati kikundi cha tatu kililinda barabara kuu zote mjini.
  Kikundi cha Sajini Ilogi kilipofika Ikulu, kilishauriwa na mmoja wa Maafisa Usalama wa Taifa, wamwone kwanza Waziri wao wa Ulinzi, Oscar Kambona; nao wakakubali kufanya hivyo. Wakaenda hadi kwa Kambona na kumleta Ikulu, na kumweleza kwamba walikuwa wamewakamata na kuwaweka mahabusu maafisa wake (Wanajeshi) 16; na kwamba, kama (Kambona) alikuwa tayari kusikiliza malalamiko yao, afuatane nao hadi Colito. Kambona alikubali.
  Ni ujasiri gani huo; ni kujiamini vipi kwa Kambona, kwamba bila ulinzi wala woga, tena akiwa amepanda gari la Mkuu wa Polisi tu, aliweza kukubali kuandamana na askari wenye silaha, na hasira kali, kwenda Colito Barracks?
  Ukimwondoa Nyerere na Kawawa, ambao walikuwa na kila sababu ya kujificha, kulikuwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Job Malecela Lusinde; kwa nini Kambona hakumshirikisha, kama aliona mambo yalikuwa salama kiasi hicho? Hapo ndipo baadhi ya watu wanakwenda mbali zaidi kusema kwamba, huenda Kambona alihusika na maasi hayo.
  Huko Colito Barracks, walimweka Kambona "kiti moto", wakimtaka aamue papo hapo, pamoja na mambo mengine, kuondolewa mara moja kwa Maafisa wa Kiingereza Jeshini, na nafasi zao zishikwe na Wazalendo. Walitaka pia mishahara iongezwe, kutoka 105/= hadi 260/= kwa mwezi.
  Bila kuonyesha kwamba ameyakubali au kuyakataa madai yao, Kambona aliomba wateue wawakilishi wachache ili wafuatane naye hadi Ikulu kwa mashauriano na Mwalimu Nyerere. Ndipo Kiongozi wa waasi, Francis Higo Ilogi, alipokataa na kusema, "Tunataka kila kitu leo hii", Yowe zikasikika, "Apigwe risasi, apigwe" (Kambona) huyo!".
  Pengine kwa kuingiwa na hofu, kwamba lolote lingeweza kumtokea, Kambona akauliza: "Mnataka nani awaongoze?" Lilitajwa jina la Alex Nyirenda; lakini likakataliwa kwamba alikuwa na majivuno. Akatajwa Luteni Elisha Kavana, akapitishwa kwa kauli moja na kuvishwa kofia ya Brigedia Douglas.
  Kambona alikataa kutia sahihi makubaliano, kwa madai kwamba mpaka ashauriane kwanza na Rais. Ndipo kikundi chote cha Ilogi kikafuatana naye kwenda Ikulu.
  Walipofika huko, askari hao walijipanga barabara yote iingiayo Ikulu, lakini Sgt Ilogi aliwakataza wasiingie ndani, wakamruhusu Kambona pekee. Wakati huo Nyerere alikuwa ametoroka zaidi ya saa mbili zilizopita.
  Baada ya mashauriano kwa muda na wasaidizi wa Rais pamoja na mama mzazi wa Mwalimu, Kambona alitoka nje na kuwatangazia waasi hao kuwa Rais ameyakubali madai yao. Lakini askari hao wakapiga kelele "mwongo huyo! Rais hayumo ndani; mpige risasi, mwongo huyo!"
  Hata hivyo, waliondoka wameridhika, wakarejea kambini siku hiyo. Hima, Kambona aliwaondoa maafisa wa Kiingereza na kuwasafirisha kwao kupitia Nairobi.
  Akiwatangazia wananchi kupitia Redio "Tanganyika Broadcasting Corporation" (TCB), Kambona alisema: "Huyu ni Waziri wenu wa Mambo ya Nje na Ulinzi; Serikali ingalipo… Kumekuwa na kutoelewana baina ya askari Waafrika na maafisa wa Kiingereza katika Jeshi. Baada ya kuingilia kati shauri hili, sasa askari wamerudi kambini". Hata hivyo, hakusema lolote juu ya Nyerere, wala mahali alikokuwa.
  Je, ni kweli mambo yalikuwa yamekwisha? Kwa nini Nyerere hakutokea hadi siku mbili baada ya askari kurejea kambini? Kwa nini askari hao waliasi tena siku nne baadaye na Nyerere kulazimika kuita majeshi ya Uingereza kuja kuzima maasi?.


  KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya wiki iliyopita, tuliona jinsi Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa wakati huo, Oscar Kambona, alivyoweza kuwashawishi wanajeshi walioasi Januari 21, 1964, kurejea kambini, kwa ahadi ya kushughulikia malalamiko yao.
  Tuliona pia jinsi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere, alivyoweza kutoroka Ikulu kukwepa shari ya waasi waliokwenda kumtafuta, akaenda kujificha mahali pasipojulikana.
  Mwalimu alijitokeza ghafla siku mbili baadaye, akashika madaraka tena. Hata hivyo, siku nne baadaye, askari hao waliasi tena. Kwa nini? Sasa tuendelee na sehemu ya pili na ya mwisho kupata majibu.
  Siku ya pili, baada ya kurejea kambini, askari waasi walionekana kufurahi kuona maafisa wa Kiingereza wakiondoka, kama walivyoahidiwa na Kambona. Lakini mtu mmoja kati yao hakuwa na furaha kama wengine: naye alikuwa Sajini Francis Higo Ilogi.
  Wakati wa mazishi ya askari wawili siku hiyo, waliouawa mtaani na Mwarabu mmoja wakati wa maasi, Sajini Ilogi aliacha kukwepa kuzumgumza na Oscar Kambona, wala kumtazama usoni. Je, ni kwa sababu Kambona hakuweza kutekeleza yote aliyoahidi? Je, ni kwa sababu yeye hakupandishwa cheo baada ya kuongoza maasi?
  Siku hiyo ilipokelewa taarifa kwamba, Kikosi cha Pili cha Jeshi kilichokuwa Tabora nacho kilikuwa kimeasi, baada ya kupata habari kwamba wenzao wa Collito walikuwa wameasi.
  Inawezekana, ama walikuwa hawajapata taarifa kwamba wenzao wa kambi ya Colito walikuwa wamerejea kambini; au walifahamu, lakini wakataka nao watekelezewe mambo kadhaa kwenye Kikosi chao.
  Wakati Kikosi cha Tabora kikiendelea na maasi, ilipokelewa hapo Tabora, simu ya maandishi (telegraph) kutoka kwa Kambona, kwamba alikuwa amemteua Kapteni Mirisho Sam Hagai Sarakikya, kuwa Mkuu wa Kikosi cha Tabora. Wakati huo Sarakikya na maafisa wengine walikuwa wamekamatwa na kuwekwa mahabusu na askari walioasi hapo Tabora.
  Sarakikya akatolewa mahabusu, akaomba simu hiyo isomwe kwa sauti; kisha akatoa amri wasimame "Mguu sawa", wafungue beneti na kutoa risasi. Nao wakamtii. Usiku huo, Sarakikya alifanya mipango ya kuwasafirisha maafisa wa Kiingereza kutoka Tabora kwenda Dar es Salaam na hatimaye makwao.
  Tukio la Januari 21, na lile la Tabora pamoja na hali ya hatari ilivyokuwa huko Kenya, Uganda na Zanzibar, lilifanya Serikali ya Uingereza ichukue tahadhari ya ziada kwa kupeleka askari 2,000 zaidi ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa hiyo, manowari iliyoitwa Rhy, ikawa imetia nanga hima Pwani ya Dar es Salaam, na nyingine Centaur; iliyobeba ndege, iliwasili na askari 600.
  Siku ya tatu baada ya maasi ya kikosi cha kwanza, Jumatano, Januari 23 asubuhi, ghafla Nyerere akatokea hadharani amepanda gari la wazi akiwa na Mama Nyerere na Waziri wa Mambo ya Ndani, Job Lusinde, akatembelea kila sehemu ya mji iliyoathiriwa na maasi.
  Alhamis ya Januari 24, ilikuwa shwari; lakini Ijumaa, Januari 25, mazungumzo kati ya Serikali na waasi yalionekana kuanza kuvunjika, wakaasi tena. Ni nani alikuwa kiongozi wa maasi haya awamu ya pili? Sajini Higo Ilogi tena?
  Tofauti na maasi ya Januari 21, ambayo hayakushirikisha wanasiasa, wala kugubikwa na hisia au shabaha ya kisiasa, maasi haya mapya yaliingiliwa na wapiga filimbi wa kisiasa.
  Taarifa za kiusalama zilionyesha kwamba, viongozi wa vyama vya wafanyakazi, kupitia Chama Kikuu (Shirikisho) cha Wafanyakazi (TFL), walikuwa wakikutana kwa siri na askari walioasi kwenye kambi ya Colito; na kwamba vyama hivyo vilikuwa vimeandaa mgomo nchi nzima mwishoni mwa wiki kuungana na askari hao.
  Maasi haya ya pili yaliweza kuambukiza majeshi ya Kenya na Uganda, nayo yakaasi vivyo hivyo, siku hiyo hiyo, wakati huo huo, na kwa mtindo huo huo. Marais Kenyatta na Obote walizisoma alama za nyakati ukutani; nao wakajiandaa kuita Jeshi la Uingereza kuzima maasi. Nyerere hakutaka; hakuamini kwamba Jeshi lake mwenyewe lingeweza kumhujumu, yeye na Serikali yake.
  Alianza kuhisi hatari mbele pale maofisa usalama walipomuonesha orodha ya mawaziri wanaotarajiwa iwapo Serikali yake ingepinduliwa, iliyoandaliwa na waasi. Mmoja wa watu wake wa karibu alikwenda mbali zaidi kumwambia kwamba, alikuwa ameombwa na waasi akubali kuwa Makamu wa Rais baada ya Mapinduzi. Mwalimu akalowa; akayaamini maneno hayo, kwamba Serikali yake ilikuwa hatarini.
  Ndipo, yapata saa 11:30 jioni siku hiyo, Mwalimu akamwita Ikulu Naibu Balozi wa Uingereza, Bwana F. Stephen Mills; akamwomba msaada wa Kijeshi wa nchi yake naye Mills, bila kuchelewa, akapeleka taarifa London na kujibiwa kwamba maombi ya Nyerere yalikuwa yamekubaliwa bila masharti yoyote.
  Naye Oscar Kambona akaenda mbio kwenye Ubalozi wa Uingereza, kumtafuta Brigedia Douglas ambaye alikuwa amejificha humo kwa wiki nzima, kumwomba msaada wa kuratibu mipango. Usiku wa siku hiyo, Douglas na ofisa mwingine, walinyatia hadi kwenye manowari Centaur iliyokuwa imefichwa Pwani.
  Jumamosi, Januari 26; saa 12:20 asubuhi, helikopta sita kutoka manowari Centaur zilichukua askari 60 (akiwamo Brigedia Douglas) hadi eneo karibu na kambi ya Colito. Dakika kumi baadaye, saa 12:30, manowari hiyo, na meli nyingine ya vita, Cambrian, iliyokuwa ikisubiri Pwani; zilianza mashambulizi kwa kupiga mizinga kuwatisha waasi.
  Kutoka umbali wa mita 20 hivi, na kwa ujasiri mkubwa, Douglas akatangaza kwa kipaza sauti, kwamba alikuwa ameshika madaraka yake tena; akatoa amri askari wote watoke nje kambini "mikono juu" na kukaa chini barabarani.
  Baada ya dakika 10 bila kuona kitu, Brigedia Douglas akaanza kuhesabu, "moja, mbili….. kumi", askari wa Kiingereza wakafyatua roketi hadi kambini. Waasi wakaanza kujisalimisha.
  Dakika 10 zingine zilizofuata askari 150 walijisalimisha, na wengine 150 baada ya saa moja. Kufikia saa 1:30 asubuhi, wote walikuwa wamesalimu amri; maasi yakawa yamezimwa katika zoezi ambalo askari walioasi, watano waliuawa na wengine watano kujeruhiwa. Hakuna askari wa Kiingereza kati ya 60 walioongoza mapambano, aliyedhurika. Na kwa juma lote la maasi, raia wasiopungua 17 waliuawa.
  Wakati wanajeshi wa Jeshi la Uingereza wakiwadhibiti askari waasi wa Tanganyika, huko Uganda na Kenya nako, Jeshi lilikuwa linachukua hatua kama hiyo, muda, saa hiyo hiyo na kwa staili hiyo hiyo kwa askari walioasi Jinja (Uganda), na katika kikosi cha 11 cha Bark-Lanet (Kenya).
  Haielezwi ni jinsi gani Sajini Higo Ilogi aliweza kuponyoka, akaonekana mjini asubuhi hiyo kwenye jumba la Simu za Nje za Kimataifa (Extelcoms), akituma simu ya mandishi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) U Thant, kuomba msaada. Simu hiyo ilisomeka hivi: "Majeshi ya Tanganyika yametekwa na askari wasiojulikana saidia haraka kuleta Majeshi ya Umoja wa Mataifa LUTENI KANALI ILOGI, MKUU WA JESHI".
  Turejee kwenye swali letu la msingi: Nani alichochea maasi ya jeshi letu mwaka 1964? Oscar Kambona? John Okello?
  Kambona alikuwa Waziri mwenye dhamana ya ulinzi wakati huo, ambapo Jeshi lilikuwa chini ya wizara yake. Kwa sababu hii, kushiriki kwake katika kutuliza maasi ya awamu ya kwanza, hakuwezi kuchukuliwa kwamba alikuwa na hisa au kwamba alijua mpango huo wa maasi hayo.
  Ni ujasiri wake tu uliomtuma kukabiliana na hali hiyo. Kama kweli angekuwa na nia mbaya kwa Serikali; na kwa kuzingatia pia jinsi alivyodhibiti hali hadi askari wakamkubali, angeshindwaje kupindua nchi ambayo ilikuwa mikononi mwa Jeshi kwa siku mbili mfululizo kama alikuwa na nia hiyo?
  Je, ni Field Marshal John Okello? Hapa tena jibu ni HAPANA. Yeye hakuwa na muda huo, kwa sababu kwa kipindi chote tangu Mapinduzi ya Zanzibar, alikuwa katika hati hati za kulinda na kuimarisha utawala wake visiwani kutokana na tishio la kuenguliwa na wahasimu wake ambao alidai hawakushiriki katika Mapinduzi. Okello aliongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa miezi miwili mfulilizo kabla ya kuenguliwa na Karume kwa kushirikiana na Mwalimu Nyerere.
  Wala haishangazi kwamba, maasi ya askari hawa yaliweza kuambukizwa kwa wenzao wa Kenya na Uganda, ikizingatiwa kuwa majeshi ya nchi hizi tatu yamezaliwa na Jeshi la Wakoloni wa Kiingereza waliotawala nchi hizo. Kwa hiyo, kwa kipindi hicho, na kwa mazingira ya kazi ya wakati huo, malalamiko yao yalifanana kuwafanya wadai haki zao kwa njia na kwa mtindo unaofanana.
  Nakubaliana na maoni ya Balozi Abbas Kleist Sykes (akinukuliwa mahali fulani mwaka 2001), kwamba, "Maasi ya Jeshi la Tanganyika Rifles (TR) mwaka 1964, yalitokana kwa sehemu kubwa na kuchelewa kuwaondoa makamanda wa kizungu na kuwapandisha vyeo waafrika", kama ilivyofanyika kwa Jeshi la Polisi na watumishi wengine serikalini. Na ndivyo ilivyokuwa kwa maasi ya Kenya na Uganda.
  Wala haishangazi kwamba, viongozi wa vyama vya wafanyakazi waliungana na waasi awamu hii ya pili kutaka kuiangusha Serikali, kutokana na ukweli kwamba, tangu Mwalimu alipositisha zoezi la "Africanisation" Januari 1963, wao walikwishaapa mapema kutolala usingizi "mpaka kieleweke".
  Kutokana na maasi hayo, Mwalimu alikifuta Kikosi chote cha Kwanza (Colito Barracks) na kuwafukuza kazi askari 100 wa kikosi cha pili, Tabora. Alifukuza pia asilimia 10 ya askari polisi 5,000 waliokuwapo, kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kudhibiti maasi.
  Watu zaidi ya 400 walikamatwa na kuhojiwa, wakiwamo viongozi wa vyama vya wafanyakazi; na wengine 500 walitiwa nguvuni chini ya Sheria ya kuzuia hali ya hatari, lakini wengi waliachiwa.
  Nalo lililokuwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TFL) lilifutwa, badala yake kikaundwa Chama cha National Union of Tanganyika Workers (NUTA) kama Jumuiya ya Chama tawala – TANU. Mwalimu alimteua Mirisho Sam Hagai Sarakikya kuwa Mkuu mpya wa Jeshi na kumpandisha cheo kuwa Brigedia.
  Mwanzoni mwa Aprili 1964, Majeshi ya Uingereza yaliondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Kikosi cha Tatu cha Jeshi la Nigeria, chini ya Luteni Kanali James Pam. Sajini Francis Higo Ilogi alipatikana na hatia ya uasi wa Jeshi na kufungwa miaka 15, ambapo washirika wake wakuu 13 wakafungwa kifungo kati ya miaka mitano hadi 10.
  Waswahili walisema, "Kila ovu lina baraka zake". Mwalimu aliongeza kima cha chini cha mishahara kwa wanajeshi kutoka shilingi 105 hadi 240/= kwa mwezi. Lakini la muhimu kuliko yote ni kwamba, maasi hayo yalitusaidia kujihoji na kufahamu aina ya Jeshi lililotakiwa kwa nchi kama yetu. Yalituwezesha kujenga Jeshi upya, tukapata "Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania" (JWT), kwa maana halisi ya Jeshi la Wananchi na kwa ajili ya Wananchi.
   
 6. i

  ishengom Senior Member

  #6
  Sep 14, 2012
  Joined: Jul 23, 2012
  Messages: 151
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 45
  daaaah kumbe mengi sna yametokea kwenye nchi hii safi sna cement kwa kutujuza ss tusiofahamu haya!!
   
 7. Ngongoseke

  Ngongoseke JF-Expert Member

  #7
  Sep 14, 2012
  Joined: Jan 1, 2012
  Messages: 3,212
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 135
  Dah story nzuri sna mkuu' mimi ningependa utujuze sababu ya mwalimu na karume iliyowafanya mpaka wamuondoe john okello madarakani sababu ilikuwa nini?
   
 8. chumvichumvi

  chumvichumvi JF-Expert Member

  #8
  Sep 14, 2012
  Joined: May 6, 2010
  Messages: 1,050
  Likes Received: 108
  Trophy Points: 160
  kaka asante sana kwa elimu uliyonipatia hapo juu cjui nikushukuru vipi
   
 9. t

  tizo1 JF-Expert Member

  #9
  Sep 21, 2012
  Joined: Mar 9, 2011
  Messages: 857
  Likes Received: 47
  Trophy Points: 45
  DAH KWENYE Kahawa HUWA WANAADITHIA HII KITU KWA MAPUNGUFU MAKUBWA
   
 10. Davie S.M

  Davie S.M JF-Expert Member

  #10
  Sep 21, 2012
  Joined: Jan 6, 2011
  Messages: 720
  Likes Received: 19
  Trophy Points: 35
  Kuna Usiri Bado upo Kwa History ya kule ZanzibAr nA Hata Apo Tanganyika..

  Sent from my BlackBerry 9900 using JamiiForums
   
 11. toghocho

  toghocho JF-Expert Member

  #11
  Sep 23, 2012
  Joined: Mar 16, 2011
  Messages: 1,177
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 135
  nashukuru kupata picha, dah...nasikia nyerere alivaa hijabu eti...
   
 12. s

  sevelina Member

  #12
  Oct 9, 2012
  Joined: Apr 2, 2012
  Messages: 7
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 3
  Asante mkuu.
   
 13. Facilitator

  Facilitator JF-Expert Member

  #13
  Oct 26, 2012
  Joined: Oct 30, 2010
  Messages: 2,288
  Likes Received: 802
  Trophy Points: 280
  Mim niliskia Mwalimu alitoroka na gari la takataka akakimbilia kigamboni
   
 14. Nelson nely

  Nelson nely JF-Expert Member

  #14
  Nov 26, 2015
  Joined: Jan 25, 2014
  Messages: 2,727
  Likes Received: 974
  Trophy Points: 280
  kuna nondo humu aisee
   
Loading...