Kosa Kubwa linalowagharimu wengi

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,891
KOSA KUBWA AMBALO HUWAGHARIMU WATU WENGI.

Na, Robert Heriel.

Maisha ni mitego, ili ufanikiwe katika maisha basi sharti uitegue mitego hiyo. Kikawaida kabla ujategua mtego sharti ujue kuwa kwenye maisha kuna mitego, ujue aina za mitego iliyopo katika maisha, kisha baada ya kujua aina zake, uione mitego hiyo, kisha uitegue. Hivyo hapa kuna mambo yafuatayo:

Mosi; Kujua kuwa kuna mtego. Hii mtu yeyote hupaswa kutambua kuwa kwenye maisha ipo mitihani.

Pili, Kujua aina za mitego. Lazima ujue aina zote za mitego.

Tatu, Uione mitego hiyo na kuitambua ikiwa itatokea katika maisha yako.

Nne, Kujua mbinu za kutegua mitego hiyo.

Ipo mitego mikubwa na mitego midogo. Kikawaida mitego katika maisha hutegemeana na aina ya mtu, utashi wake, akili yake, elimu, ujuzi, tamaa na matamanio yake. Kanuni ya utegaji mitego huzingatia umbo, akili, ujanja, tamaa, mahitaji, na muda ambapo mtegwaji hutegwa.

Mtego wa Panya ni tofauti na mtego wa simba. Hii ni kutokana na tofauti ya kimaumbile baina ya viumbe hao. Akili zao na mahitaji yao. Hivyo mtego wa panya utazingatia zaidi umbo la panya, mahitaji yake, akili yake, tamaa yake, na hata muda ambao panya atanaswa.

Kwenye maisha, ipo mitego ya aina tatu kuzingatia na nani aliyeitega. Aina hizo nimezianisha kama ifuatavyo;-
i/ Mtego Uliotegwa na Adui
ii/ Mtego Uliojitega.
iii/ Mtego unaotegwa na mtegwaji mwenyewe.

Mtego uliotegwa na Adui ni ile mitego ambayo adui huzingatia vigezo nilivyovitaja hapo juu. Hii ndio mitego mibaya ambayo mara nyingi hulenga kukuangamiza, kukupoteza, kukurudisha nyuma miongoni mwa madhara mengine. Mitego hii huwa haiishi adui angalipo. Mitego hii hubadilishwa muda hadi muda kulingana na malengo ya adui mpaka atakapokunasa. Mitego hii mara nyingi huisha au kuondoka kabisa pale adui yako anapokufa, unapomkamata na kumuangamiza lakini bila ya hivyo maisha yako hayataisha mitego zaidi ya mitego kubalika badilika. Mfano adui anaweza kukuwekea sumu kwenye chakula, kukufanyia fitina kazini kwako, kukuendea kwa waganga na wachawi kukuloga, kukupa mikataba bandia usaini ili uingie mkenge, hiyo ni mitego iliyotegwa na adui.

Mtego uliojitega; hii ni mitego ambayo haikuwekwa na adui, wala haina dhamira yoyote iwe mbaya au nzuri. Mitego hii ni ile ambayo mtu hujichanganya kwa kutokuwa makini. Mitego hii haizingatii vigezo vya juu, bali hutokana na mtu kujichanganya. Kwa mfano, mtu akitembea njiani akajikwaa kwenye jiwe akataka kuanguka au kuanguka kabisa, au kule vijijini unatembea barabarani lakini kwa bahati mbaya unategwa na nyasi unaanguka. Hiyo ni mitego uliojitega wenyewe na wala hauna dhamira yoyote mbaya wala nzuri na wewe.

Mtego Uliotegwa na mtegwaji, Yaani Kujitegea mtego. Huu ni mtego ambao mtu hujitegea mwenyewe pasipo yeye kujua. Mitego hii hutokana na uzembe, hofu na tamaa iliyopitiliza.
Mitego hii mara nyingi huwa mingi katika maisha ya mtu ikiwa atakuwa mzembe, mwenye hofu na tamaa iliyopitiliza.
Kwenye maisha, adui hutumia mitego ya mtegwaji zaidi kuliko mitego yake mwenyewe. Hutumia tamaa ya mtegwaji kama chambo katika mitego yake.

Ili ufanikiwe kwenye jambo lolote sharti ujue mitego iliyomo katika jambo hilo. Lazima ujue mambo yako binafsi ambayo adui anaweza kuyatumia kama chambo kukuangamiza.

Mtu asiyejua mitego iliyomo katika jambo alifanyalo yupo katika hatari ya kushindwa katika jambo hilo. Ni rahisi kujikuta amenaswa na mitego katika jambo hilo hivyo akajikuta hawezi kutoka iwe kwa muda au daima dawamu adui angalipo.

Ipo mbinu mbili za kutega mitego.
i/ Kutega kwa kuificha
ii/ Kutega kwa kuipamba na kuiremba.

KUTEGA KWA KUIFICHA; Hii ni mitego ambayo huzingatia zaidi uono wa mtu. Kama ni kwenye vita basi huzingatia macho ya mtu. Kama mtu haoni kwa haraka na hana utambuzi wa haraka hujikuta amenaswa na mtego. Mitego hii hufichwa aidha ardhini, majini, hufukiwa na majani au namna yoyote itakayofanya macho ya mtegwaji asione kwa haraka hivyo hujikuta amenaswa na mtego kwa ghafla

Mitego ya namna hii hutegwa kumfanya mtegwaji ajihisi bado yupo salama kumbe yupo katika hatari kubwa bila kujua. Mitego hii hutegwa bila kutofautishwa na mazingira asilia. Yaani mtegwaji atajiona yupo mahali paliposawa kutokana na kutokuwepo na utofauti au viashiria vya mashaka. Ndio maana hata mtego ukiwekwa barabarani hufukiwa na kuwekwa vile vile kama hakuna mtego.

Mitego hii zaidi hutumika vitani, kwenye maofisi makubwa ambapo mtu unakuta unashauri jambo fulani baya kwa namna njema nawe bila kujua unaingizwa mkenge unaliwa. Mitego hii hutumika zaidi kwa habari za kushauriwa. Pia kulogwa, na mambo yote ya ushirikina huingia katika mitego hii ambapo hufanywa kisiri na kwa kificho. Mtegwaji huona yupo salama lakini kumbe yupo katika hatari kubwa.

KUTEGA KWA KUIPAMBA NA KUIREMBA:
Mitego hii huwa dhahiri, haifichwi, huonekana kwa macho kabisa. Mara nyingi huwekwa chambo kinachovutia kulingana na tamaa ya mtegwaji. Lakini pia huzingatia akili na ujanja wa mtegwaji. Mitego hii hurembwa na kupambwa kwa umbo la nje lakini ndani ni mtego. Huvutia kwa mbele lakini nyuma ni mtego mbaya. Mitego hii zaidi hutumiwa na matapeli, wachungaji wa siku hizi ambao hukuahidi maisha mazuri kama kuwa na fedha, kumiliki nyumba nzuri, na mambo mengine kama hayo. Hutumia Fedha, magari na majumba kama chambo cha wewe kuingia mtegoni. Ukiingia umeliwa. Utawanufaisha wao na wewe utaendelea kusota na kuhangaika.

Mitego ya hivi hutumia wanawake wazuri warembo kuwanasa wanaume wenye tamaa mbaya. Mwishowe wanajikuta wameliwa pesa zao bila kubakiwa na kitu. Wanawake wazuri kwa kawaida ni mitego iwe wajitumie wenyewe au watumiwe na adui mwingine. Wengi wamenaswa na maadui zao na wanawake, wengi wamepata magonjwa kwa sababu ya mitego ya wanawake, wengi wamefilisika kwa sababu ya wanawake.

Mitego hii pia hutumika kwenye makampuni ya Mikopo, kampuni za kamari, biashara za network marketing ambapo wategwaji huwekewa mitego yenye vyambo vilivyonona huku wakipewa maneno matamu. Mwishowe hujikuta katika taabu. Kiufundi ipo mitego ambayo hulenga kuwanufaisha wachache na kuwadhuru wengi. Mitego hii utumia wanufaika wachache kama chambo la kuwavutia wategwaji wengi ambao hawa watadhurika moja kwa moja. Mfano mzuri ni biashara za network market na mchezo wa kubet ambao kila siku huwapiga wengi na kuwanufaisha wachache ili kuwarubuni waliopigwa kuwa ipo siku nawe utapata.

Ipo mitego ya mbali na mitego ya karibu. Kwa kawaida mtego hatari ni ule mtego wa karibu. Mtego wa karibu huhusu mzunguko wa watu wa karibu yako. Mke/ mume wako huweza kuwa ndiye mtegaji wa mitego katika maisha yako. Mitego ya mbali huhusu watu wa kazini, majirani, na ngazi za kitaifa na kidunia.

Kikawaida, mitego ya mbali hushirikiana iwe moja kwa moja au isiyomoja kwa moja na mitego ya karibu.

Maisha ya mwanadamu hayatabiriki ikiwa mwanadamu hajui adui yake ni nani, yupo wapi, anaujuzi, nguvu na akili kiasi gani. Ikiwa mtu atamjua adui yake ni nani basi ni rahisi kuyatabiri maisha yake.

Unapomjua adui yako, basi utajua mitego atakayoitumia kukunasa, kukukwamisha na kukuangamiza. Ikiwa hutajua adui yako ni wazi hutajua mitego utakayotegewa kuwa ni mitego ya aina gani, itategwa wapi, saa ngapi, na inateguliwaje.

Nashauri, iwapo utakuwa mmoja ya watu wanaoishi iwe duniani ama mahali popote, basi ni kosa kubwa kuishi bila kumjua adui yako. Kutokujua adui yako ni dalili ya kushindwa kwenye maisha. Ni kushindwa kwenye maisha yako mwenyewe. Huwezi ishi kama mtu aliyekufa. Kufanikiwa kwenye maisha ni kumjua, kupambana na kumshinda adui yako.

Kuishi ni kupambana na adui, kushindwa na kutomtambua adui hali iliyopelekea kupigana na maadui bandia ambao hukutakiwa kupigana nao.

Wakati mwingine watu wengi hufikia hatua huoa na kuolewa na maadui zao bila ya wao kujua. Hapo ndipo kizaazaa hutokea. Kuzaa na adui yako ni kujimaliza mwenyewe. Hapo utapata watoto ambao watakuwa adui zako ambao utakuwa mtego kwako.

Kwa leo niishie hapa.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom