Konstebo Nguzu

Konstebo Nguzu

RIWAYA: KONSTEBO NGUZU
MAANDISHI YA: George Iron Mosenya

"Zungumza machache kati ya mengi uyajuayo..... ONYESHA vichache kati ya vingi unavyovimiliki. Katika maisha si vyema kila mtu kukujua kwa asilimia 100"

Hii ni SEHEMU YA KUMI NA MBILI.

GIZA lilikuwa ndani ya giza kwa mara nyingine, Konstebo Martin Nguzu alikuwa amempokea mama yake ambaye alikuwa mmoja kati ya wahanga wa ile kamatakamata iliyofanywa kwa masilahi ya watu wachache waliokuwa wamekerwa baada ya mwenzao mmoja kuuwawa kifedhuli.
Ghafla bin vuu mambo yakabadilika, kota zikatishiwa kuchomwa. Wakagwaya na kuwaachia huru wale waliokuwa wamekamatwa katika namna ya uonevu.
Ni giza hilihili sasa lipo ndani ya giza tena, ana kwa ana na mama yake mzazi.
Martin Nguzu alimpa pole mama yake huku akiwa na haraka sana ya kujua ni wapi hasa anapoweza kumpata Majenga waweze kuzungumza na kutambua ama kujitambua upya yeye ni nani na kwa nini haya yote yanatokea.
Hasira zake bado zilikuwa dhidi ya inspekta Kobo aliyeamini kuwa alimchomea ndani ya nyumba kisa mapenzi.
Alipona vipi na nini kinaendelea katika maisha yake haya nd'o makuu aliyojiuliza.
Kuhusu kutafutwa kwa Majenga na watu asiowajua kukapunguza ile hisi yake kuwa chanzo cha kila kitu ni mapenzi.
Akabaini kuwa lipo la nyongeza.
Mama Martin ambaye hakuwa ameimarika sana kiafya safari hii alionyesha ushirikiano wa hali ya juu, usiku uleule alimpeleka Martin hadi nyumba aliyowahi kuishi mzee Majenga ambapo baadaye alipangisha na kuondoka zake kuelekea Shinyanga.
"Ila Shinyanga sijamuona kabisa..." Nguzu alizungumza wakati wanaelekea katika nyumba ile.
"Bado haujabadilika mwanangu, yaani Shinyanga kubwa vile wewe umtafute mtu usiyemjua na ukampata kabisa. Labda muujiza ama maigizo." Mama alimkata juu kwa juu Nguzu, haikuwa mara ya kwanza hali ile. Tangu utoto wake.
Mtoto hakui kwa mama!
Walipewa ushirikiano mkubwa sana walipowasili eneo lile, uzuri mtoto wa mzee Majenga alikuwa anaishi katika chumba kimojawapo, na alikuwa pale kama msimamizi wa nyumba ile.
"Kumpata kwa leo itakuwa ngumu sana, maana leo watu wametoa kodi. Na yule akipata kodi anamalizia katika ulevi wake.” Mtu aliyekuwa anawapa maelekezo alisema kwa masikitiko.
“Unaweza kujua baa ambazo hupenda kuzitembelea?” Nguzu aliuliza kwa udadisi.
“Bora angekuwa anaenda baa, huyu anaingia vilabuni, ana usemi wake unaosema kwamba mia mbili ya baa ni elfu kumi ya kilabuni”
Martin akajikuta anatokwa na tabasamu hafifu kwa kusikia haya.
Ghafla wakamwona yule mwenyeji akiwafanyia ishara ya kusikiliza kwa makini zaidi, wakasikia sauti ya mtu akiimba.
“Ni yeye... looh! leo amewahi kurudi hivi?” alishangaa na kuwashawishi Nguzu na mama yake washangae pia.
“Halafu..... halafu..... mama huyu kamfanana.... aahm! eeeh!” akaanza kujiuma uma. Alikuwa amemtazama Nguzu vizuri.
“Ninafanana naye sana alikuwa binamu yangu....” Nguzu akaiwahi hii kesi na kuisawazisha.
Mtarajiwa akawasili akiwa anaendelea kuimba nyimbo zake, nyimbo zilizomburudisha yeye pekee.
Hakuwa peke yake.....
Alikuwa na chupa kadhaa za pombe.
“Mnataka kuhama.... mnahama hama na hamjalipa kodi yangu.” Alizungumza huku akiwa hana hata uwezo wa kuona mbele vizuri, sembuse kung’amua kuwa kuna mtu anataka kuhama.
Akasogea kwa kunesanesa bila kuvunja chupa hata moja akawafikia.
“Shkamoo mama..... eeeh! mama nawe umehadimika kweli.” Alisalimia baada ya kumtambua mama Martin.
Salamu ilijibiwa, yule mwenyeji akajitoa katika mkutano huu akawaacha watatu hawa wakizungumza.
Walijitahidi hivyohivyo kuelewana japokuwa ilikuwa ngumu kwani yule mlevi kila mara alikuwa anasahau alichozungumza dakika kumi nyuma.
Mlevi huyu hakujua ni kiasi gani alikuwa faida kwa Martin Nguzu.
______
ASKARI aliyetegemewa na kuaminiwa zaidi alikuwa makini na silaha yake, alikuwa amejinyoosha chini na kunyanyuka kidogo sana usawa wa kifua na kuendelea. Bunduki yake kubwa ilikuwa imelazwa vyema katika muinuko huku akiona kila kitu kilichokuwa kikikatiza mbele yake.
Alitulia katika lindo lile kwa dakika nyingi akingoja walilotarajia litokee waimalize vyema siku yao.
Kilikuwa ni kikosi cha watu saba tu cha siri kilichokuwa kikitambua nini kinaendelea katika giza hili.
Majira ya saa nane usiku mchakacho ulisikika kutoka katika kichaka kimojawapo, mlengaji akatulia tuli bila kufanya shambulizi.
Alihitaji kupata uhakika wa kile alichokuwa anakwenda kukishambulia.
Barua kutoka kwa IGP ilielezea kuwa jambazi aliyekuwa anasakwa miaka mingi alikuwa mjini Shinyanga na huko alitarajia kuanzisha kampeni ya kuvamia na kuiba katika taasisi mbalimbali za kifedha.
Huu ukawa wakati wa askari kujitafutia nyongeza ya nyota kwa kumtia mikononi jangili huyo aliyekuwa anasifika kwa hatari yake na roho mbaya.
Simu ya upepo ilikuwa imeshikiliwa na askari mwingine, kazi yake ilikuwa moja tu kumweleza mlengaji nini cha kufanya ikiwa patakuwa na mabadiliko. Mlengaji hakupaswa kutikisika ama kujihusisha na mawasiliano mengine kwa sababu angeweza kuipoteza shabaha yake.
Mchakacho ule ukaongezeka tena, mlengaji akaendelea kutulia.
Na hapo redio ya upepo ikakoroma ikitoa taarifa kutoka upande wa pili.
“ANGUSHA MBUYU KUNA NYOKA! ANGUSHA HUO MBUYU...”
Sauti ile ikamfikia mlengaji, akaanza kutetemeka mikono yake. Ile sauti haikuwa ngeni na lile neno hakuwa akilisikia kwa mara ya kwanza. Ni siku kadhaa nyuma alilisikia katika simu ya upepo kutoka kwa kijana wake wa kazi aliyeuwawa kwa kupigwa risasi.
Mikono ikazidi kutetemeka, sauti ile nayo ikazidi kusisitiza neno lilelile.
‘angusha mbuyu’
Mapigo ya moyo yakaongezeka kasi yake.
Adui akajitokeza kutoka katika kichaka, mlengaji akatakiwa kufyatua na kumwangusha adui.
“Afande Kobo, fyatua!!” mshika simu alimwamrisha Kobo aliyekuwa anatetemeka na silaha yake.
Inspekta Kobo akaachia risasi ya kwanza, ikaenda malikiti.
Haikumkaribia adui badala yake ilimpa taarifa kuwa kuna hatari inawazunguka.
Kobo akamuona adui akirudi mbio kichakani, na baada ya sekunde chache hakutoka peke yake, lilikuwa jopo la maana lenye silaha za maangamizi.
Mpambano ukaanza.
Kobo akajaribu kutupa risasi nyingine, akakosa!
Ile kauli ya angusha mbuyu ilikuwa ikimsumbua kichwa chake.
Anayeitoa sauti ile ni nani? na kwanini alimuua kijana wake? na ni kipi kinamfanya amfuatilie Juma Kihwele kama yeye alivyokuwa anamfuatilia.
Mlolongo huu wa maswali ukazidi kumpoteza, kwa mara ya kwanza katika maisha yake anafyatua risasi tatu na hakuna hata moja iliyomlenga muhusika.
Kitimtimu kikaanza.
Askari saba ambao umri umewatupa mkono dhidi ya jopo la vijana majangili kumi na watano.
Risasi ziliruka hewani kwa fujo, huyu anarusha yule anajibu.
Inspekta Kobo alikuwa kama mpira wa kona, anakimbia huku na kule angali silaha anayo, badala ya kumkabili adui yeye anajiuliza ni nani mwenye ile sauti inayosema ‘angusha mbuyu’
Wasiwasi mara mbili, kwanza dhidi ya hao vijana majangili na pili juu ya adui ambaye wapo naye katika mpango huu kamambe.
Kobo akatamani kumuuliza askari mwenzake ambaye alikuwa anashikilia simu, amuulize yule ni naji alitoa ile amri.
Lakini, licha ya kuamini kuwa ule wakati haukuwa wa kuuliza maswali bali kila mmoja kuutetea uhai wake. Hata nafasi hiyo pia hakuipata kabla ya kukiona kichwa cha yule askari kikisambaratishwa vibaya mno na risasi iliyotoka inapotokea.
Madonge mazito ya damu yakamrukia wakati akijirusha pembeni zaidi asijekukumbwa na balaa la kusambaratishwa.
Inspekta Kobo alikuwa anahema juu juu huku akiomba dua Mungu amtunze asife usiku huo.
Taswira ya mkewe ambaye yu katika kuzimia ilimvamia. Akahisi kuwa kifo chake kitasababisha mkewe akirejewa na fahamu zake naye apoteze maisha kwa mshtuko wa kupoteza mume.
Sasa hofu ya kifo ilimtawala waziwazi......
Akaiweka sawa silaha yake na kujipa maneno ya ujasiri kupindukia ambayo yangeweza kumrejeshea ari yake ya upambanaji.
Aliiweka vyema silaha mkononi, ikawa inateleza.
Kwa mara ya kwanza bunduki yake ikawa inamsaliti. Akairudisha katika bega lake na kujipapasa kiunoni, akaichukua ile bastola yake anayoiamini kupindukia akaiweka sawa mkononi, hii yenyewe ilimuheshimu ikakaa sawa.
“Serenaserena afande Kobo.... Kobo...” Sauti ikamuita kutokea gizani. Ilianza na utambulisho wao wa siri waliokuwa wamepeana.
Inspekta Kobo akabonyea chini kisha akatoka ‘mkuku’ hadi alipoisikia sauti ile.
Alimkuta mwenzake akiwa katika dimbwi la damu akiogelea bila kupenda.
Hali yake ilikuwa mbaya sana, na alionekana muda si mrefu ataikimbia dunia kuelekea popote anapoamini kwa imani yake.
“Kimbia, hatari.... viumbe hawa hatari. Tunateketea wote....” Alizungumza kwa sauti ya chini sana. Akaweka kituo na kuhema kwa nguvu zote.
“Hakikisha unaishi ili kuwa shuhuda.... viumbe hatari sana wana siri zote. Usimuamini mtu jiamini wewe mwenyewe kuanzia sasa..... kuna wasaliti kati yetu.” alizidi kusihi.
“Na... naku.. nakuf... nakufa afande.” Alizungumza huku akizidi kukauka koo lake na sauti kufifia.
Ikawa kama alivyojitabiria!
Inspekta akazidisha umakini, akabaki na maswali lukuki, ni kwanini bwana yule anamweleza kuhusu wasaliti ndani yao, kwanini amemchagua yeye na amemuamini vipi kuwa yeye sio msaliti?
Mwenzao huyu!! alijisemea huku akiondoka kutoka eneo lile.
Sasa kila upande ulikuwa umetulia, ilikuwa ni vita ya kuviziana baina ya pande hizi mbili. Inspekta hakutaka kumuamini mtu yeyote zaidi.
Alitilia maanani uhai wake pekee.
Akakimbia hadi alipolifikia shimo asilojua matumizi yake, akatumbukia na kutulia ndani yake.
Alikuwa macho kabisa kisije kumdhuru chochote kitu.
Aliendelea kutulia hadi palipokucha akauona mwanga.
Lakini mwanga huu ulikuwa ukingojewa na watu wengi.
Ile Inspekta anatoa kichwa chake nje akakutana na sauti kali zikimkaripia asithubutu kufanya jambo lolote lile atue silaha zake chini na kisha kunyanyua mikono yake juu.
Alijitahidi kujitambulisha lakini hakuna ambaye alimsikiliza.
Akatii, kwa umakini wa hali ya juu askari wenye sare wakamkaribia na kumtia pingu mikononi na miguuni.
Ajabu!
Alistaajabu ni kipi kimejiri hadi kujikuta katika balaa kubwa kiasi kile tena ghafla.
Alionywa asithubutu kusema jambo lolote lile. Akaingizwa katika gari lenye ulinzi mkali kupindukia.
Hawakutaka kulala tena Shinyanga.
Amri ikatolewa kuwa iwe isiwe lazima inspekta Kobo afikishwe jijini Dar es salaam, na hiyo ilikuwa ni amri na sio ombi.
Inspekta Kobo hakuamini, vijana walio chini yake ki-cheo walikuwa wanamlinda huku wakimkaripia mara kwa mara.
Alifedheheka ila hakuwa na la kufanya.
Huu ukawa mwanzo wa safari mbaya na ya kutisha.
Wakati anaiacha ardhi ya Shinyanga, katika ardhi hiyohiyo harakati mpya ilianza kusukwa.
______
 
RIWAYA: KONSTEBO NGUZU
MAANDISHI YA: George Iron Mosenya
SEHEMU YA KUMI NA TATU

FLORIAN NGENGEKUZENZA NGUZU.

USHINDANI wa nani kwao matajiri nilishindwa mapema sana, kila walichokuwanacho sisi tuliishia kukiona tu. Hatukuwanacho wala hatukukaribia kukipata.
Miaka ya elfu tisa mia na arobaini (1940), ni wale watoto ambao baba zao walikuwa wakijipendeza kwa wakoloni pekee ndo wangeweza kuwa na maisha yenye unafuu.
Katika hapa sikuwa mshindani wake.
Tulipata nafasi mara chache sana kucheza michezo ya kitoto, hatukuwa tukishindana sana.
Miaka ikazidi kwenda hatimaye ikafika wakati wa kwenda shule, huku napo hapakuwa na ule ushindani wowote. Alisoma katika shule ambazo walivaa viatu na sare nzuri angali sisi miguu yetu iliunda urafiki wa kinafiki na miba pamoja na matope.
Kitu pekee tulichopata katika maisha yetu duni ni aibu za wazazi wetu pindi waliponyanyaswa na mkoloni. Kisha baada ya hapo wanatusimulia simulizi za mashujaa wao ambao na wao walikuwa wakikiri kuwaogopa hawa watu wenye ngozi nyeupe.
Simulizi hizo zilinijenga barabara, katika akili yangu. Nikajikuta ni kijana ambaye uzalendo ulikuwa katika moyo wangu.
Baba yangu mzazi ambaye alipigana vita ya Majimaji huko Songea alikuwa akiniongezea ujasiri, ni kweli alikuwa akinyanyaswa na wazungu na aliwaogopa kweli lakini alikuwa akinieleza kuwa katika vita ile kwa mkono wake wa kuume akiwa na rungu kubwa aliwauawa wazungu watano.
Kwake ulikuwa ni ushindi mkubwa sana kumtandika mkoloni na bunduki yake mkononi.
Ni kweli watanganyika wengi walipoteza maisha lakini hii ilikuwa alama kubwa sana kuwa waliutaka uhuru kwa namna yoyote.
Baba alinieleza kuwa baba yake ambaye ni babu yangu alipoteza maisha kwa kunyongwa, na ni yeye ndiye alikuwa mmiliki wa jina la Nguzu ambalo maana yake ni NGUVU.
Jina Florian nilipewa na hawa ngozi nyeupe waliojifanya miungu katika ardhi yetu, silipendi jina hilo.
Naitwa Ngengekuzenza Nguzu. Yaani ‘Aliyerithi Nguvu’.
Baba yangu alinipatia jina lile kwa sababu aliniamini sana, nami nikajikuta najiamini mno.
Maisha magumu hayakuiathiri akili yangu, sijui mnaitaje kwa kizazi chenu hiki cha Tanzania, lakini wakati wa Tanganyika tulisema akili zinachaji, akili zangu zilikuwa zinachaji mno.
Nilifanikiwa kulimaliza darasa la nne la mkoloni.
Wakoloni bwana licha ya unyanyasaji wao lakini walikuwa makini sana, wakiona mtu ana akili sana wanamuwahi ili baadaye aje kuwa upande wao na aseme mazuri tu juu yao. Mkoloni akupatie elimu utaanzaje kumsema kwa mabaya angali tayari unaweza kusema’yes no’ kwa sababu yake!!
Hata mimi waliniwahi na hapa ndipo nilikutana na Joseph Kazeze.
Na upinzani ukaanza rasmi.
Wakatupeleka shule ya upili ambayo kwa sasa mnaiita Tabora boys lakini wakati ule iliitwa Tabora Central school. Ilikuwa shule ya vipaji maalumu haswa. Wanafunzi wengi walikuwa ni watoto wa machifu, ni baadaye sana walianza kuchukua wanafunzi wa kawaida.
Kwa wakati ule nadhani ni mimi na wengine wachache sana tuliokuwa tunasoma pale lakini si watoto wa machifu.
Mitihani ya hapa ilikuwa ni kutoka vyuo vya uingereza. Hawakutufundisha kuhusu yetu bali walitaka tuyajue yao.
Hata hayo yao bado nilipata alama za juu.
Urafiki kati yangu na Joseph Kazeze ukaanza kuyeyuka, hakutaka kupitwa alama na mtoto wa kimasikini kama mimi.
Tulipoenda jeshini mwisho wa kidato cha tatu kama ilivyokuwa ada nilikuwa bora zaidi yake katika kila kitu.
Hakupenda kabisa, ila mimi sikujua kama ni kwa kiasi kikubwa vile.
Tukarejea tena kumalizia kidato.
Katika uchaguzi nikateuliwa kuwania uongozi, Joseph naye akawania.
NIkamwangusha na kuwa kiongozi wake!
Wakati ananipa mkono wa hongera ndipo niliiona chuki katika macho yake.
Nikapuuzia.
Nikasema ikiwa wote tunatoka Mwanza, ya nini kuchukiana sasa. Nikadhani yale yataisha...
Kutingwa na uongozi nikasahau kabisa kuketi na Joseph tuzungumze.
Chuki ikakomaa!
Baadaye yakaibuka mapenzi, nadhani hapa ndipo chuki ilibalehe na kuota mapembe!
Joseph alimpenda binti ambaye alikuwa akinipenda mimi. Kuzidiwa huku kete Joseph akaleta ubabe na kunivimbishia kifua.
Mara ya kwanza nilimwacha, ya pili akanifuata tena akinitaka ugomvi, nikamweleza bayana kuwa sisi ni ndugu wa mji mmoja asiwe vile.
Akanipuuzia na siku hii akanisukuma nikaanguka.
Nilipoinuka nilimfundisha kuhesabu moja mpaka kumi kwa lugha ya kirusi.
Somo lilikuwa gumu na kila mara alianguka chini, kila akijaribu kunyanyuka namtandika ngumi ya uso. Akapasuka juu ya jicho lake, nami nikawa napiga palepale.
Siku hii nikatambua kuwa majina yana maana yake.
Ngengekuzenza Nguzu (Aliyerithi Nguvu)
Nilikuwa nimerithi haswa.
Ugomvi huu ulitikisa shule.
Ajabu yake ilikuja katika maamuzi, tulipigana na mgomvi alikuwa Jose lakini katika adhabu nikachukuliwa mimi.
Tabora Central School ilikuwa shule ya kijeshi wakati wetu, hata sare zetu zilikuwa za kijeshijeshi, tulivalia kombati za kaki kama wanazovaa wanamgambo, kila kitu kiliendeshwa kikakamavu, hapakuwa na adhabu za viboko.
Nilivyoadhibiwa nikikusimulia unaweza ukahisi huyu bwana kachanganyikiwa na sasa ananidanganya.
Niliingizwa katika chumba chenye giza nene na hapo nikaanza kulazimishwa kwenda mbele, kadri ninavyokwenda mbele ninazidi kuinama chini kutokana na muundo wa kile chumba, hatimaye paji la uso likayakaribia magoti.
Chumba kikabanwa nikawa siwezi kusogea mbele wala kurudi nyuma.
Niliumia mno, nikaamini kuwa sasa ninakufa.
Waliniacha kwa masaa mengi sikumbuki hata.
Waliponitoa nilikuwa nyang’anyang’a.
Wakanipeleka msituni, huko sasa niliadhibiwa na wazungu. Walimwachia mbwa wao anikimbize na nilipewa ruhusa ya kukimbia kumzidi.
Nilivyochoka vile ningeweza vipi, si waliutaka uhai wangu tu wapuuzi wale.
Basi kama ni mchezo basi mbwa alipata wa kucheza naye, nakimbia hatua kadhaa naanguka mbwa anafika na kuning'ata wanamfukuza.
Wananiambia nisimame tena ninakimbia wanamwamuru mbwa anikimbize, ananifikia na kuniangusha ananing'ata.
Niliteseka mno!
Baada ya hapo nikapokea viboko kumi na viwili vya mkoloni.
Nilinyooka.
Joseph hakuadhibiwa nilipotoka kule kwenye adhabu nyinginyingi za kutisha nikaelezwa kuwa nimefukuzwa shule na wakati huohuo aliyechukua nafasi yangu katika uongozi ni Joseph Kazeze.
Nililia! Nililia sana.
Nikapakiwa katika gari moshi, elimu yangu ikaishia pale nikarejea kuwa mtumwa.
Nilipambana hivyohivyo hadi siku ile mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyokabidhiwa nchi huru.
Walau hali ikaanza kuwa ya heri, sikutamani kusoma tena.
Tayari nilikuwa nina familia ya mtoto mmoja niliyempa nikiwa Mwanza baada ya kufukuzwa shuleni.
Sikupata mtoto huyu na yule mwanamke aliyetuletea uhasama baina yangu na Jose. Nilizaa na maskini mwenzangu tukalea kimaskini hivyohivyo.
Niliamua kuanzisha familia kwa sababu sikuwa na familia tena, baba yangu alifariki na mama vilevile.
Halikuwa jambo la ajabu kwa wakati ile kupoteza familia yako.
Nikamsahau Joseph Kazeze katika kichwa changu. Niliamini yote yaliyotokea Tabora Central School ni mambo ya ujana tu.
Nilikuja kulisikia jina hili katika siasa.
Eti Joseph Kazeze ni mjumbe sijui wa kamati gani katika chama tawala. Hii ilikuwa mnamo mwaka 1977. Niliamua nisijihusishe na habari zozote kuhusu Jose kwa sababu kwa kufanya hivyo nilikuwa nakumbuka chanzo cha mimi kuishia kati katika masomo yangu na sasa sina thamani yoyote katika jamii.
Miaka mitatu baadaye yule mwanaharamu akaanza kunizongazonga tena.
Alinibomolea nyumba yangu. Japokuwa hakuja yeye moja kwa moja lakini nilijua kupitia waliokuja, akanibambikiza kesi kadhaa bahati nzuri ilikuwa upande wangu nikawa natoka salama.
Huwezi kuamini, akavuka mipaka baada ya kuona kila analofanya si kitu kwangu.
Hivi unaweza ukaamini Jose Kazeze akaamua kumposa upya mke wangu!
Andika kila ninachokueleza usiache walau neno moja, yote yana maana sana.
Nd’o hivyo bwana Joseph akamlaghai mke wangu ajuavyo yeye, alikuwa na gari lake aina ya Land Rover ya chama tawala basi aliitumia hii kuishika akili ya mke wangu.
Yule mwanamke naye alikuwa mjinga kweli, ujue nilishamweleza kinagaubaga kuhusu uhuni wa Jose lakini akashawishika akaniacha eti.
Hivi kama sio kuumizana nafsi ni nini hiki, kweli Joseph ambaye alikuwa ana pesa tayari anaamua kuniingilia anga zangu, tena bora ingekuwa kwa mwanamke ambaye ni kigoli, mwanamke huyu alikuwa amecharazwa bakora za mkoloni haswa hatamaniki, alikuwa amechanjwa mwili mzima chanjo za kinga ambazo ziliaminiwa na makabila mbalimbali. Haya yote akajifanya hayaoni.... akaamua kuniadhibu.
Alifanikiwa!
Nilimwambia mwanangu juu ya alichonifanyia mama yake. Nilimweleza huku ninalia.
Akatangaza kumchukia milele!
Basi rafiki yangu akabaki kuwa huyo mwanangu wa pekee, niliyemuita jina Salama.
Mama Salama akahamia katika maisha ya Joseph Kazeze.Iliniuma mno, huyu bwana katumia cheo chake kulipiza kisasi angali mimi sikufanya lolote enzi zile Tabora kwa kumkomesha.
Sasa mwanamke nikamuachia, sifa zote nikamuachia lakini yule bwana kumbe hajaridhika.
Hapo sasa zile jazba za enzi za shule zikarejea nikajisema kuwa nchi hii ni huru kabisa, tena sio uhuru wa bendera. Hakuna utumwa tena labda ukusudie mwenyewe. Ajabu anajitokeza mjinga mmoja mwenye ngozi kama yangu ananirudisha utumwani.
Siku ya tukio sikumuaga Salama!
“Naomba kwa leo tuishie hapo mzee wangu Majenga..... sitaki kusikia kilichotokea. Nakuomba sana alfajiri tutaendelea na mkasa huu. Nimefurahi sana kukukuta ukiwa hai mzee. Na bado nashangaa uliweza vipi kutunza karatasi hizi kila ulipoenda na kutarajia siko moja utamsomea mtu” Martin Nguzu alizungumza kwa hisia kali, sauti yake ilikuwa baridi mno. Alikuwa ameguswa mno na maandishi yale.
“Niliwahi kumsomea mama yako, sijui hata kama alinisikiliza kwa makini maana alikuwa analia kila akisikia lolote kuhusu hayati Ngengekuzenza Nguzu ambaye ni baba yake mzazi.” Alijibu Majenga kwa utulivu.
Na hapo akaitoa miwani yake usoni.
Akajifuta machozi.
“Babu yako alikuwa mtu wa aina yake sana. Namuona hai ndani ya macho yako...” Akaongezea huku akimshika begani Martin Nguzu.
Nguzu akamsaidia kuinuka, akamkokota mpaka ndani akamsaidia kukiandaa kitanda chake akamwacha akilala. Naye akaenda katika chumba kingine akalala.
 
RIWAYA: KONSTEBO NGUZU
MAANDISHI YA: George Iron Mosenya
SEHEMU YA KUMI NA NNE
Wakati Martin Nguzu na mzee Majenga wanakubaliana kulala ili siku inayofuata waendelee kusoma maandishi yale ambayo Nguzu aliamini kuwa si haba yatampa mwanga kidogo juu ya matukio yote yanayotokea. Upande mwingine palikuwa panapambazuka.
Inspekta Kobo akiwa na pingu miguuni na mikononi mwake alikuwa katika mahojiano mazito sana.
Mdomo wake ulikuwa umeanguka na na kubaki wazi kutokana na kipigo kikali alichopokea, midomo hii iliyokosa ushirikiano ilisababisha udenda ulioambatana na damu umwagike katika namna ya kusikitisha sana.
Mguu wake uliokuwa umeunganishwa kwa vyuma ulikuwa umepigwa na sasa baadhi ya vyuma vilikuwa vinachungulia nje.
Damu nzito iliyoganda katika chuma kile ilisaidia kuficha ukweli wa mambo.
Inspekta hakuwa na uwezo wa kutembea na hakulazimishwa kutembea badala yake aliburuzwa hadi akafika mahali alipohitajika.
Macho yake mekundu yalikuwa makubwa sana, na yalikuwa yakiviringika huku na kule katika namna ya kuomba huruma ya yeyote yule mwenye mamlaka ya juu yake.
Hakutokea japo mmoja wa kumtetea.
Maelezo aliyokuwa ameyatoa waliosikiliza hayakuwakuna kabisa na hivyo wakaona suluhu ni kumbana vyema kwa kumuumiza ili aweze kutapika siri zote alizomeza.
"Inspekta Kobo, hili ni agizo la mwisho kabisa la kukubembeleza wewe kusema ukweli wote ili ubaki kuwa salama ama la tutatumia nguvu. Na hatushindwi!" Sauti ya kusihi iliyojaa madaraka iliunguruma.
Inspekta akastaajabu, hawa mabwana tayari walikuwa wameitengua taya yake, wakaupoteza njia mguu wake na sasa yungali mahututi katika bahari ya maumivu, sasa anaelezwa kuwa asiposema ukweli watatumia nguvu.
Nguvu! alistaajabu...
Nguvu gani zaidi ama watamkaliza katika kiti chenye shoti ya umeme, au watampiga risasi?
Hizi nd'o nguvu ambazo walikuwa hawajatumia.
"Mkuu nilichokiandika katika maelezo yangu ni hicho hicho sijaongopa hata nikishtuliwa usiku wa manane siwezi kupindisha ukweli huo." Alijibu kwa shida sana.
"Kama uliweza kupindisha shabaha yako maksudi na kumwacha hai jambazi mkorofi ambaye tumehangaika miaka nenda miaka rudi kumsaka unashindwa vipi kuupindisha ukweli?" Alihoji kisha akasimama wima na kuendelea kuzungumza.
"Kobo, katika maisha yako ya kulenga shabaha umeangusha mibuyu mingapi iliyoleta ukorofi?"
"Mingi sana afande." alijibu kwa sauti ya chini.
"Umetunukiwa shani ngapi kutokana na kulenga kwako shabaha?"
"Tano afande."
"Unaikumbuka shabaha yako ngumu kupita zote?"
"Ahh! mmh! ndio afande, ni ile ya kutoka ghorofa moja kwenda nyingine." aliendelea kujibu upesiupesi. Bila kujua nini hatma ya maswali yale.
"Unaukumbuka umbali kimakadirio?"
"Mita mia tano...." alijibu kwa utulivu. Na safari hii sauti ilikuwa chini zaidi kwa sababu aliijua nia ya maswali yale.
"Yaani nusu kilometa sivyo? Na haukuwa katika utulivu wowote, na uliweza kuipata ile shabaha bila kukosa. Na ilikuwa ni usiku..... halafu leo hii unapiga risasi tatu maksudi unamkosa adui anayetikisa taifa. Kobo! Kwa kitendo chako hicho cha kumuacha adui wa taifa unadhani watanzania wapo radhi kukusamehe? Mimi kama mtanzania siwezi kukusamehe... nastaajabu wanakuchelewesha nini kukutia kitanzi bazazi wewe.... uliyechagua kumlinda mwanaharamu mwenzako!" Sasa alikuwa amewaka yule bwana aliyekuwa anamuhoji Inspekta Kobo. Na alikuwa anatetemeka mno.
Inspekta alikuwa amekamatwa pabaya.
"Ok! unalipwa shilingi ngapi kila anapofanya uhalifu wake.... tuzungumze kama wanaume na haya mambo yaishe. Maana Tanzania mambo ya kitanzi tulishayafuta, na hata ukifungwa maisha huyo mwanaharamu atakuja kukutoa tu utakuwa huru. Haya nieleze tu, unapewa kiasi gani kulisaliti jeshi la polisi katika oparesheni kabambe namna ile." Swali likatupwa.
Inspekta Kobo akafadhaika mno, kwa sababu hakuwa kama walivyodhania.
Alipojaribu kupinga, hasira za yule bwana zikamuangukia.
Akapokea teke kali katika shingo yake, akarushwa na kutua pembeni akabaki kukoroma huku damu ikimtoka puani.
Akatamani kuelezea ukweli wa kila jambo lakini hakuona kama ataeleweka maana katika maandishi yake hakuandika kuhusu mashaka yake juu ya ile sauti inayotamka 'ANGUSHA MBUYU'. Hakuandika kuhusiana na kifo cha utata cha Martin Nguzu na hakugusia hata kidogo juu ya mahusiano baina yake na koplo Zubeda.
Angeanza kuelezea hayo angeonekana ni muongo mara mia zaidi ya alivyochukuliwa awali.
Inspekta akachagua kubaki kimya.
"Inspekta Kobo hivi unajua kuwa hii kesi yako inaweza kuhesabiwa kama kesi ya uhaini na itakuweka pabaya wewe na familia yako, ama unajitazama wewe na masilahi yako pekee hauitazamani familia yako. Haumtazami mkeo ambaye hadi sasa hajui kinachoendelea ulimwenguni, hujali kuhusu watoto wako unajitazama wewe pekee. Sasa mimi nimekusihi sana imetosha naandika ripoti tusilaumiane katika hili." Alizungumza kwa sauti tulivu kabisa huku akiwa anamtazama Inspekta Kobo.
Maneno yale juu ya familia yake yalimvuruga Kobo aliyejitambua wazi kuwa hana kosa lolote lile, lakini la kufanya nd'o hakuwa nalo.
Akarejeshwa katika chumba alichokuwa anafungiwa mle akiwa peke yake.
Tofauti na siku nyingine ambapo chumba hiki kilikuwa kinazimwa mwanga wa taa na kubaki katika giza siku hii kilikuwa kina mwanga na zaidi kiliongezeka kiti.
Nanyongwa!!
Hisia zikakipiga kichwa cha inspekta Kobo, tumbo likaanza kuunguruma kwa hofu ya kuupoteza uhai wake.
Akaingizwa pale chumbani.
Kimya kikatanda kwa dakika zisizopungua tatu. Kisha zikasikika hatua zikijongea katika kile chumba.
Mlango ukafunguliwa na askari wawili, kisha kwa mwendo wa taratibu akaingia Inspekta jenerali wa polisi (IGP).
Mwili wa inspekta Kobo ukaingiwa na ubaridi mkali sana, akaunyanyua uso wake na kumtazama bwana yule nadhifu kabisa aliyekuwa katika mavazi yake ya kazi.
"Funga mlango!" akawaamuru wale askari.
Wakatii! kisha wakaondoka na kuliacha eneo lile likiwa na watu wawili pekee.
Mwili wa Kobo ulikuwa umesulubika sana, lakini kwa kumtazama bwana huyu mwili ukajiona kuwa inayokuja nd'o suluba taslimu.
Kobo alitambua kuwa IGP aliisubiri hii nafasi kwa hamu sana ili aweze kumnyoosha na sasa alikuwa ameipata. Iwe isiwe atamwadabisha.
"K" IGP akaita kwa upole.
Inspekta akamtazama kisha akaitika kwa shida sana.
"Pole sana rafiki yangu. Pole!" IGP aliketi vyema.
Unafiki! Kobo akajisemea.
"Kabla sijazungumza mengi na wewe ninapenda kukueleza kuwa ninakupenda sana rafiki yangu, huwezi kuamini haya lakini elewa kuwa nimejaribu zaidi ya mara tano kuonana na wewe lakini nimeshindwa kwa sababu sikuwa tayari kukuona katika hali hii. Umeteseka sana K" alizungumza kwa hisia IGP.
Hali hii ilimtisha Kobo, akajiuliza anachokisikia ni sahihi ama kuna namna ya ulaghai.
Yaani huyu bwana ajisikie vibaya kwa yeye kuwa katika wakati ule mgumu.
Haiwezekani.
Inspekta Kobo akakumbuka vitisho vyote alivyowahi kupewa na IGP wakati huo akiwa hajapewa dhamana hii ya juu katika jeshi la polisi. Alikuwa kamishna wa kanda maalumu
"K, yale yote yalikwisha kwa upande wangu. Nimetafiti sana na nikagundua kuwa wewe haukuwa chanzo cha mke wangu kuwa mlemavu. Niliumia sana awali na kujikuta nikikuchukia lakini nimeikubali hiyo hali na nipo hapa kwa ajili ya kukusaidia tu! Tafadhali sema nami"
"Niliyoyasema ni hayohayo." Akajibu kwa ukaidi Kobo, bado alikuwa na hisia za chuki dhidi ya IGP bado hakuamini kuwa wao ni marafiki tena.
"K, sikiliza ndugu yangu. Ukaidi hautasaidia kitu chochote kwa wakati huu. Laiti kama ningekuwa juu ya sheria ningeamuru uachiwe huru na ubaki kujuta na nafsi yako ikiwa ni kweli umefanya yote hayo ama la. Lakini kwa hili mimi sina ninalazimika kuiheshimu sheria ya nchi, sio kuivunja kisa ninakuonea huruma. K, tafadhali nieleze ni nini kilitokea...." IGP alizungumza kiukarimu kabisa.
Inspekta Kobo akaamua kurusha karata yake ya kwanza. Akaelezea kwa ufupi sakata la Nguzu, hakulitaja jina la mwanamke ambaye alikuwa anahusika.
Akaitaja ile sauti ambayo aliisikia usiku wa tukio la Nguzu kuchomewa ndani na kisha akaitaja tena sauti ileile ilisikika siku ambayo alikuwa ameishika bunduki yake tayari kwa kufanya shambulizi.
"Nikapagawa sana kugundua kuwa licha ya kwamba nimelenga shabaha kwa ajili ya kummaliza adui ila ndani yetu pia kuna adui. Tena adui asiyekuwa na huruma aliyeiteketeza kwa moto nyumba ya askari mwenzetu pasi na huruma kabisa. Nilitetemeka sana, hata lile agizo alilonipa la kuushusha mbuyu lilinikwaza badala ya kunihamasisha. Hakika nilikuwa natetemeka..."Alimalizia.
Palepale IGP akamsogelea na kumnong'oneza jambo kwa kusihi.
"Usiyaseme maneno haya popote pale. Umeniamini mimi imetosha sana na ninakuahidi italeta manufaa. Nimeupata mwanga."
IGP akatulia kidogo kisha akarusha suala jipya kabisa ambalo lilikuwa jipya kwa inspekta Kobo.
"Umesema juu ya Nguzu kuchomewa ndani ya nyumba yake, unadai ulienda kuzungumza naye usiku ule. Sawa kabisa.... na je Majenga unamfahamu vipi?"
"Ma nani?"
"Majenga" Akajibu IGP huku akimtazama kwa ukaribu kabisa inspekta Kobo.
"Sijawahi kulisikia jina hili katika maisha yangu."
"K, mbona hutaki kuamini kuwa ningali upande wako? nieleze nijue ni wapi nakusaidia rafiki yangu. Ujue kuna watu watatu wameuwawa huko Shinyanga na huu mlolongo wote unakuangukia wewe. Ndugu zao wamechachamaa si kidogo, huyo Majenga ni nani Kobo! Tell me..." alianza kupandwa na ghadhabu IGP.
"Simjui na sijawahi kulisikia jina hilo Gervas, mbona unanilazimisha kutema maneno ambayo akili yangu haijawahi kuyameza. Simjui huyo Majenga for God's sake!!" Aling'aka inspekta Kobo huku akimtaja IGP kwa jina lake.
IGP akaanza kufura kwa hasira, akajitahidi kujiweka katika hali ya kawaida. Akauliza tena na tena bila majibu kubadilika.
Inspekta Kobo akasimamia analoliamini!
IGP akamtazama kwa sekunde kadhaa, akatoa kitambaa chake mfukoni na kujipangusa matone ya jasho na mwisho akamtupia Kobo neno la mwisho.
"Pambazuko hili litakuwa baya sana kwako na sitakuwa na namna ya kukusaidia. Nimejaribu sana Kobo nawe umeona. Umekataa kumtaja Majenga na unamjua waziwazi...."
Akasubiri kidogo, Kobo akamtazama kisha akalazimisha tabasamu na kisha akazungumza.
"Nimekuwa na mapambazuko mabaya sana tangu mke wangu apate janga lile, nimekuwa na mapambazuko mengine mabaya tangu vijana wako, vijana niliowafundisha ukakamavu jeshini walipougawana mwili wangu na kufanya kwa vitendo yale niliyowafundisha, mapambazuko mabaya hayataanza leo ama kesho yalianza tangu uliponituhumu kuwa nimeshiriki kumfanya mkeo awe mlemavu wa miguu angali nilijaribu kadri ya uwezo kuokoa maisha yake, niliokoa maisha yako pia Gervas kwa kukusukuma ili usipigwe risasi, nikawa na mapambazuko mabaya ulipozisahau fadhila zangu, ni pambazuko gani baya zaidi unaloniahidi sasa... eeh! pambazuko gani unalolisema, pambazuko la kupoteza uhai? Kuteswa? Kufungwa gerezani maisha yangu yote? Hakuna pambazuko la ajabu hata moja kati ya hayo, ni wewe utayaishi mapambazuko ya ajabu siku utakapoujua ukweli angali nimenyamaza katika kile kimya cha milele, Attaccati a sto cazzo."
akaweka kituo huku akimalizia kwa kutokwa na lile tusi lake murua katika lugha ya kiitaliano.
IGP akabaki kuganda, midomo ikimchezacheza asijue ni maamuzi gani ayachukue.
Akatoweka pale na kwenda nyuma ya mlango. Akajibanza pale na machozi yakaijua njia yake, yakayalowanisha mashavu, kamasi nyepesi zikatoka kuchungulia nini kinaendelea katika uso wa IGP.
IGP alikuwa analia kiume!
_________________

Majira ya saa sita usiku aligutuka kutoka usingizi huku jasho likimtoka sana.
Majenga! jina hili likakivamia kichwa chake, akaketi kitako na kuanza kukumbuka juu ya maneno yale aliyokuwa akiyasoma yule mzee. Akatamani asubuhi ifike upesi aweze kuendelea kusikiliza ni kipi ambacho kitakuwa na faida kubwa sana kwake.
Akamaizi kuwa licha ya kushtuka vile na kuandamwa na jina hilo lakini pia alikuwa pia amebanwa na haja ndogo.
Na choo kilikuwa mita nyingi kutoka chumba alichokuwa amelala.
Akapatwa na uvivu sana huku akijilaumu kwa kukataa kunywa maji mengi baada ya chakula cha ili asije kupata shida kama hizi usiku na sasa amezipata shida zilezile.
Akajivuta taratibu kuelekea choo kilipokuwa. Nje palikuwa kimya sana, walisikika wale viumbe wanaopenda kulala mchana kisha usiku wanazurura kusumbua viumbe wengine.
Popo!
Umbali wa choo ulimtatiza sana, akajiona mpuuzi sana giza lote lile kuna vichaka vya hapa na pale ni kwanini ahangaike na choo.
Akakiendea kichaka kidogo alichokiona karibu yake.
Akakidhi haja yake lakini hakuweza kugeuka kabla ya kusikia sauti ikimuamuru asimame.
Akasimama tuli!
"Kwanini unakojoa vichakani we tahira?" sauti ikakaripia.
Martin Nguzu akastaajabu, tangu afike pale Shinyanga sauti karibia zote zilikuwa zinaambatana vyema kabisa na lafudhi ya kisukuma, iweje hii sauti inakuwa na miporomoko ya pwani ama Zanzibar?
Hakujibu kitu!
"Nakuuliza weye mwanaharamu..."
"Nisamehe tafadhali..." Hatimaye akazungumza.
"Mzee Majenga analala chumba kipi hapa? na ni nani ako...." Swali likatupwa.
"Analala nyumba kubwa!"
"Geuka utupeleke upesi.."
Nguzu akageuka na kukutana na mambo aliyoyazoea.
Mitutu ya bunduki.
Walioibeba waliishika kizembe sana. Ni vile hawakujua kuwa ile hatari inayodhaniwa kuzikwa katika tanuru la moto, iliishia kung'arishwa na kuwa dhahabu yenye thamani kali huku ikiwa na makali ya kisu kipya.
Walisimama wanaume wawili, mmoja akiwa na bastola mkononi mwake. Huyu aliielekeza kwa Nguzu.
Nguzu akajitia kutetemeka huku akiwasihi wasimuue. Kutetemeka kule kukawazidishia uzembe.
Mmoja aliyebaki akasikika akizungumza kwenye simu kuwataarifu wenzake kuwa wamefika eneo la tukio na muda si mrefu watauchukua mzigo wao.
Walitembea hatua kumi kuelekea ilipokuwa nyumba ya mzee Majenga na familia yake.
Nguzu alizihesabu zile hatua vyema huku macho yake yakiwa makini sana kutazama kitu.
Hatimaye akakifikia, kilikuwa ni kigogo kilichokuwa njiani. Akakikanyaga na kujikwaa maksudi.
Akaanguka chini huku akitokwa na yowe la hofu.
"Inuka hanithi wewe..."
Kauli hii aliisubiri Nguzu kwa hamu, mkono wake ulikuwa tayari na jiwe, akatumia sekunde chache kubaini kuwa mshika bastola yule hakuwa anakaribia kufyatua, kidole chake kilikuwa mbali kabisa na kifyatulio.
Safi sana! akajisemea na hapo akajitutumua ainuke.
Alipoinuka akaliachia lile jiwe likampata bwana mwenye lafudhi ya kipemba usoni, kapiga yowe huku bunduki ikimtoka.
Yule mwenzake akajiweka sawa kufanya shambulizi kwa kutumia bunduki.
Nguzu akajirusha huku goti lake likitangulia mbele hadi katika kifuani kwa adui.
Akambwaga chini.
Nguzu akaitwaa ile bunduki.
"Acha ujinga dogo, vita sio kama kunywa urojo unakunywa hata kama ni kibogoyo. Vita inahitaji watu majasiri wenye meno makali." Alimwonya alipomuona akitafuta bastola.
Yule bwana akatulia asiamini kuwa kibao kimewageukia wao.
Mwenzake alikuwa amekodoa macho.
"Mwambie jamaa aje moja kwa moja eneo la tukio, ukiongeza neno nakuua muda huu, na usipoongeza nitakuua baadaye." Nguzu akaamrisha.
Simu ikapigwa jamaa akazungumza aliyopaswa kuzungumza. Kisha simu ikakatwa.
"Nilikueleza ukiongeza neno nakufanyaje?"
"Unaniua!"
"Na usipoongeza?"
"Utaniua baadaye. Nisamehe tafadhali sisi tunatumwa tu" alijibu huku akitetemeka.
Nguzu akamgeukia yule mpemba.
"Shehe! mwenzako kaongeza neno tayari, anasema nimsamehe na sikusema hivyo." Hakusubiri jibu, akaigeuza bunduki, hakutaka kupoteza risasi akaizamisha bunduki katika kifua cha yule bwana singe ikaingia nzima nzima.
Akagalagala kuusaka uhai wake.
Mpemba akakurupuka akairukia bastola. Lakini hakuweza kufyatua kabla Nguzu naye hajamrukia na kumkanyaga mkono.
"Swahiba, nakukumbusha tena huu sio urojo kila mtu anakunywa." akamtia ngumi kali katika paji la uso wake.
Ilikuwa ni vita ya kistarabu sana, mtu akianguka chini waliolala wanajua ni maembe yanaanguka, wanajigeuza upande wa pili na kuendelea kuota ndoto zao.
Hawakujua kuwa roho zilikuwa zinatoka na uwanja ule ulikuwa umegeuka kuwa wa kivita.
Nguzu akambana maswali yule mpemba, akajibu kuwa huyo anayekuja ndiye kiongozi wao, wenyewe hawajui kiundani juu ya tukio lile.
"Kwa maana hiyo unamaanisha wewe hauna umuhimu wowote kwangu sivyo."
"Walah! naapa mie wanionea bure tu sina nijualo." Jibu lile likawa la mwisho.
Kama hauna maana unabaki na Nguzu kufanya nini.
Akaunganishwa katika safari ya mwenzake aliyekuwa ametulia tayari.
Nguzu akaweka windo lake kumngojea huyo aliyeitwa mjua mengi.
Windo hili likazua safari mpya ya Konstebo Martin Nguzu kurejea jijini Dar es salaam.
Jiji ambalo linaamini kuwa yu kwa muumba akijibu tuhuma zinazomkabili. Huku wengine wakiamini bado anahangaika na adhabu ya kaburi.
 
RIWAYA: KONSTEBO NGUZU
MAANDISHI YA: George Iron Mosenya

SEHEMU YA KUMI NA TANO

ILIKUWA safari iliyojaa katika kichwa chake ghafla baada ya vita ile ya usiku iliyoondoka na uhai wa watu watatu ambapo mmoja kati yao alikuwa ni kiongozi wao kwa mujibu wa maelezo yao.
Martin Nguzu ambaye sasa hakuwa akiushangaa uwezo wake wa kukabiliana na maadui alikuwa amewaangusha wengine watatu huku akifanikiwa kuwapokonya bunduki tatu pamoja na risasi za kutosha kabisa.
Hakutaka kulala baada ya kuhakikisha ameitelekeza ile miili mbali na ngome ya mzee Majenga. Alimwamsha mzee Majenga na kumweleza kwa ufupi juu ya kilichotokea.
Tofauti na matarajio yake kuwa taarifa ile itamtisha sana Majenga, hii ilikuwa kinyume. Mzee Majenga akatokwa na kicheko kidogo kisha akampigapiga kifuani Martin Nguzu na kumwita kwa jina la babu yake.
"Ngengekuzenza Nguzu umezaliwa upya..." Kauli ile ilimtoka na kumwacha Martin Nguzu katika pumbazo asielewe ni kitu gani bwana yule alimaanisha.
"Mimi nimezeeka kijana wangu, niliisubiri sana hii vita kwa muda mrefu lakini imekuja nikiwa mzee tayari. Nenda ukapambane hii ni vita yako na inakuhusu. Nakuachia haya maandishi niliyoyaandika bila kuongeza wala kupunguza neno kutoka katika kinywa cha hayati babu yako anayeishi sasa katika nafsi yako. Hakikisha unayamaliza yote kabla haujaivaa hiyo vita...... mimi nitakuwa salama kabisa na tutakutana nikiwa hai, na hata nikifariki ni kwa sababu ya uzee tu..." Aliongea kwa ujasiri mkuu. Kisha akachechemea hadi ndani na kuchukua makaratasi yaliyoandikwa kwa kalamu akamkabidhi Martin.
"Nilikuwa napenda sana kuandika na babu yako alikuwa anapenda sana kunisimulia, nadhani ni maneno hayo kwa ufupi yatakupa jawabu nilikutana vipi na babu yako." Majenga alitoa kauli ile na Martin akaipokea lakini alikuwa na swali la ziada.
"Niliokoka vipi katika ule moto jijini Dar es salaam?"
"Mzee wako asingeweza kukuacha uangamie. Wazee wa zamani hawakuwa wa kawaida, akinuia jambo linakuwa kama lilivyo, nadhani ni kutokana na kutenda dhambi chache nd'o maana Mungu alikuwa akiwasikiliza." Alifafanua na kuzidi kumvuruga Martin.
Akagundua mvurugano ule, akaongezea "Kasome haya yote kabla hujaamua wapi pa kuanzia"
Maongezi yakaishia hapo.
MAANDISHI YA NGENGEKUZENZA.
Ubaya ni kwamba wakati wa ukoloni, sisi watu wa rangi nyeusi hatukuishia tu kunyanyaswa na ngozi nyeupe katika uhai wetu, hata ulipokuja ustaarabu wa kuhifadhi maiti zetu sisi tuliwekwa katika kundi la mbwa koko aliyefia jaani baada ya kukabwa na mfupa aliodhani ni mnofu.
Ukipata bahati sana unafukiwa, ila ni waafrika wachache waliokuwa na bahati, wengi tulitunukiwa nuksi.
Ukiwa na nuksi unaachwa hapohapo ulipofia ama unasogezwa kidogo porini, ukawe chakula kwa wanyama wenye tabia ya uvivu katika suala la kuwinda na ndege wanaoona sifa kudonoa donoa.
Hata babu yangu alikuwa na nuksi vilevile baada ya kufariki alitupwa, akaipata bahati akiwa maiti tayari waafrika kadhaa wakamfukia.
Baada ya kuupata uhuru wetu nikawa naitembelea ile sehemu niliyoaminishwa kuwa babu yangu alifukiwa pale, pakawekwa alama nami nikawa naenda kumsalimia na kuzungumza naye bila kujali ananisikia ama la!
Sasa yule mwanahizaya baada ya kuona haitoshi kumchukua kiharamia mke wangu na kuniacha katika jitimai, akaona hata! hii haitoshi huyu bwege bado anapata raha. Akaanza kuniandama kivingine, najua aliwatuma mashushu wake waliokiamini na kukiabudu chama chao kuliko Mungu wa mbinguni na miungu ya porini.
Hawa wakamfikishia habari kuwa ninayo furaha nyingine, furaha ya kuzungumza na babu yangu makaburini.
Ikapita ajenda katika siku nisiyoijua na baadaye ikawa ni amri bila kutahadhalishwa.
Eneo lile lilipaswa kupandwa miti, mara lilitakiwa kupita barabara.
Sikuelewa hata kidogo, na hakuna aliyesubiri nielewe.
Kwani Ngengekuzenza nani mpaka aelewe?
Lile nililoamini kuwa ni kaburi likavunjwa na huyu mkoloni mshenzi mwenye rangi kama yangu huku akiiga miondoko ya wazungu na afro yake kichwani akiipaka kalikiti na kuwa laini kama nywele za mkoloni.
Lugha yake pia ilifanana na yao.
Poor Joseph Kazeze!
Kama ni kunipiga, hapa alinipiga na mjeledi wa chuma nikaangukia pua huku mikono yangu ikishika makaa ya moto.
Huyu mjinga aliniweza hakika!
Uchungu wangu ule nikamshirikisha mwanangu Salama nikamweleza kuwa Jose anataka kuvuka mipaka ambayo ameivuka tayari, yaani sielewi anachotaka.
Salama alinisihi niachane naye, nikaona hajui uchungu ninaoupitia kwa kupokonywa mke na kisha hapohapo nikapokonywa furaha yangu.
Babu yangu!
"Salama, nikiachana naye akagundua nina furaha kuwa na wewe atakuchukua na wewe pia...." nilimwambia Salama. Wazo hili likamkuna na kuiona hatari ya waziwazi.
"Sasa utamfanya nini?"
"Yule ni mjinga tu kwangu, nataka nimfanyie yale mambo ambayo wajanja huwafanyia wajinga wanaodhani pesa nd'o ujanja." nilimweleza huku nikiona wazi kuwa hanielewi.
"Unataka upigane naye?" aliniuliza.
"Nikipigana naye wote tutakuwa levo ileile ya ujinga, nataka nimpige ili tuunde daraja kati ya nani mjinga na nani mjanja."
"Lakini baba, huyu ana pesa na cheo atakusumbua sana. Yaani nina uhakika hautafikia hata nusu ya azma yako."
"Kwanini unasema una uhakika." nilimuuliza salama.
"Si kila kitu kipo wazi, ana pesa na vyeo na zaidi ana kundi kubwa la watu linalomzunguka."
“Nd’o maana unasema ni hakika?”
“Ndio baba”
"Sikiliza mwanangu Salama na uliweke hili milele katika maisha yako, hapa duniani kuna kitu kimoja tu nd'o cha uhakika vingine vyote si vya uhakika. KIFO pekee ndo jambo la uhakika, kila mtu atakufa hii haina mjadala. Ujiue, unyweshwe sumu, ugongwe na gari ama hata ukilala usiamke. Vyote vina maana moja tu ya uhakika.... asije akakudanganya mtu kuwa jambo hili ni uhakika... anakulaghai na wewe unayemsikiliza na kumkubalia unakuwa upande wa mjinga. Sipendi uwe mjinga siku moja...." Nilimsomea mambo yale. Yakamuingia na kumpa ujasiri naye akanibariki katika uamuzi wangu na hiyo ilikuwa ni mnamo mwaka elfu tisa mia themanini na tatu ama nne kama sijasahau.
Sijui itakuwaje miaka ya huko mbele lakini enzi zetu hizi hapakuwa na ulinzi wa kutosha kwa viongozi, ulinzi huo tuliusikia tu na kuuona walipokuja viongozi kutoa nje, Mwalimu Julius Nyerere alihamasisha sera za kuishi kijamaa, nasi tukaamua kuishi kama ndugu.
Hapakuwa na wa kumpinga kirahisi mwalimu. Ukitaka kumpinga sisi tunakwambia nenda ukapambane kuileta Tanganyika huru ndipo ujilinganishe na mtaalamu huyu.
Hivyo tuliishi kijamaa sana, halikuwa jambo la ajabu kukutana na mwalimu Nyerere barabarani na kusalimiana naye kwa kushikana mikono. Sasa vipi kuhusu mjinga huyu anayeitwa Joseph Kazeze?
Sidhani kama kwa miaka yenu huko mbeleni itakuwa hivi. Nahisi hata balozi naye atatafuta ulinzi...
Nilikueleza awali kuwa tangu nilipokuwa mtoto nilikuwa nina uwezo mkubwa sana darasani, hata akili yangu haikuwa ndogo katika kufikiri.
Nikaamua kuitumia akili yangu kumwonyesha yule bwana nini maana ya mwanaume kutoa machozi.
Kwakweli nilimkosesha amani!
Kwanza nilifurahia kile kitendo cha mwalimu Nyerere kutowafukuza wazungu baada ya kutupatia uhuru, hivyo upatikanaji wa silaha hadi miaka ya themanini bado ulikuwa ni mwepesi sana, unaweza kuipata bunduki hata kwa kubadilishana na gunia la mahindi pekee.
Zilikuwa zimezagaa.
Nami nikajipatia bunduki yangu, uzuri nilipitia jeshini hivyo sikuhitaji kufundishwa lolote.
Nikamuaga mwanangu kuwa naanzisha mapambano rasmi.
Sikuwahi kuua ila nilijeruhi sana.
Nilianza na baba yake mzazi, akiwa katika mizunguko yake. Nikamteka na kumpiga kipigo cha mbwa mwizi, akavunjika mkono.
Sikumtumia salamu Jose Kazeze kama ni mimi ili aendelee kuhadaika.
Akafuata mdogo wake, huyu nilimfungia safari hadi Morogoro, nikamkamata na kumfunza adabu asiweze hata kuiona sura yangu.
Jose Kazeze kitu alichosahau ni kwamba sisi tulikuwa marafiki na nilimfahamu vyema yeye na familia yake.
Niliendelea kumpa presha bwana yule kwa kufikia hatua ya kuvamia kwake nikarusha risasi zikavunja vioo vya nyumba aliyokuwa akiishi lakini sikumdhuru mtu na sikutaka kumdhuru.
Uwezo wangu katika kupanga matukio ulianza kunishangaza hata mimi, kila nikilala na kuamka nawaza pigo jingine.
Jose akaanza kukonda!
Mara akaachana na yule mwanamke aliyenipokonya.
Nami sikurudiana naye mjinga yule aliyekosa hata nukta ya akili.
Nilikuwa nina hasira kali.
Baadaye baba yake alifariki, kwa magonjwa mengine sijui kama na kile kipigo kilichangia.
Sikujali!
Siku mbili baada ya kuzikwa nikaenda makaburini, huku nikaweka bomu nililolipata kwa bei nzuri tu.
Likafanya mlipuko uliotikisa nchi.
Hakuna kilichobaki zaidi ya jeneza kusambaratika huku na kule.
Hili lilikuwa pigo kubwa zaidi, wanandugu wakalundikana nyumbani kwa Jose Kazeze kujadiliana nini kinaendelea.
Nikavamia na huko na kurusha bomu jingine katika choo kilichokuwa mbali kidogo na nyumba na hii ni baada ya kuhakikisha hapakuwa na mtu ndani yake.
Mparangano uliojitokeza nilijikuta nacheka mwenyewe.
Amakweli mtenda akitendwa....
Jose akazidi kuzorota kiafya.
Ni hapa ndipo nikaamua kumweleza bayana ili kama ni kufa kwa mshtuko afe tu, who cares?
Hakufa!
Ila alipagawa vibaya mno, na hapo ndipo ikaanzishwa oparesheni ya Ngengekuzenza Nguzu anasakwa auwawe.
Kisa ni jambazi, yakaundwa matukio ya kushangaza kunihusu mimi na hapo nikaanza kusakwa rasmi.
Nilijua kuwa hali ni mbaya, nikaraejea kwa mwanangu... usiku wa mwisho kumwona mwanangu.
Akanieleza kuwa yu mjamzito, nikamweleza kuhusu kinachoandikwa na magazeti ya serikali huku nikimweleza kuwa moyo wangu u radhi kuwa nimemuweza yule bwana.
Zaidi ya hayo nikamsihi kuwa iwapo atazaa mtoto wa kiume basi amwite Nguzu!
Tulikumbatiana huku sote tukishindwa kuyazuia machozi.
Nikaondoka na kuja kwako Majenga unihifadhi nikusimulie ya kuandika kama ulivyohitaji wewe kijana wangu.
Na nimejitahidi sana kukusimulia.
Maandishi yale yaliacha nafasi kubwa kisha ikafuata aya ambayo mwandishi wake alikuwa ni Majenga.

Mnamo mwaka 1988 mwezi wa kumi na moja mzee Ngengekuzenza mwenye msongo wa mawazo kwa kuishi maisha ya mashaka kila kukicha aliniaga kuwa anakwenda msalani, ilikuwa majira ya usiku. Hakurejea mapema nikalazimika kutoka pamoja na mbwa kwenda kumtafuta.
Nilimtafuta sana hadi pambazuko likanikuta nikiwa namtafuta, mbwa asiyechoka ndiye alinihimiza kumsaka mzee wangu nimpendaye.
Hatimaye nikaufikia mti ambao alikuwa amejitia kitanzi.
Nasikitika kuwa sikuwahi kukiri kuwa ninamfahamu mzee yule kwa sababu za kiusalama, alikuwa anasakwa sana na jeshi la polisi kama jambazi sugu.
Niliporejea ndani nikakutana na karatasi katika kitanda alichokuwa akilalia. Haikuwa na maneno mengi sana aliniandikia kama nilivyokuwa nimefanya tayari.
"Umenihifadhi kwa moyo wote wa upendo, wewe ni kijana wangu nikupendaye. Ninaomba uendelee kunitunzia maneno yangu..... utawapatia wajukuu zangu ili wajifunze kuwa babu yao hakuwahi kuwa mtu dhaifu hata kama nilionewa, babu yao sikuwahi kuwa jambazi hata kama watayaona maandishi hayo, pia kwa imani yangu kuu naamini kuwa sijafa kirahisi rahisi. Mizimu ya mababu zangu waliouwawa kifedhuli utumwani imeniambia kuwa najipumzisha ila ipo siku nitazaliwa na nitazaliwa katika damu yangu mwenyewe. Ninapumzika Majenga ila nikizaliwa tena usishangae. Naamini mizimu hii kulikoni dini walizotuletea wakoloni, dini zilizotuongopea kuwa Mungu ni mzungu, zikaenda mbali na kusema kuwa Mungu anaishi katika majengo yao waliyoyajenga.
Dini za kishenzi zilizonipatia jina la kishenzi, Frolian na kunipokonya jina la kishujaa kutoka kwa babu yangu.
Dini zilizotulaghai kuwa kila asemacho yule mzee mweupe anayesimama mbele yetu basi ni sawa, anatuona tunateseka na anasema tumwachie Mungu, nasi tukijaribu kupambana anasema tena sisi ni watu wabaya sana na hatufai kuwekwa kundi la wanadamu.
Dini zao hazijaniambia kuwa siku moja nitarejea, lakini wazee wangu ambao tuliwalilia njaa wakatusikia katika miti, tuliwaomba kila kitu na walikuwa wakweli.
Wazee hawahawa wamesema nami, acha nipumzike ila ipo siku nitarejea na sitakuwa wa kujificha tena.
Kwaheri mjukuu wangu!"
Kisha akwakeka hitimisho Majenga kwa wino mzito.
"MNAMO MWAKA 1988 BABU YETU Ngengekuzenza aliaga dunia na ni mwaka huohuo mwanaye Salama alipata kujifungua... yule mtoto akaitwa NGUZU"
_________________

NGUZU alibaini kuwa alikuwa anatetemeka baada ya kuimaliza sentensi ile ya mwisho.
Akaituliza akili yake na kutaka kumaizi ni kitu gani kimempa majibu katika maandishi yake.
Kwanza, aliamini katika mizimu na kimyakimya akakiri kuwa mzimu wa babu yake ungali ndani yake.
Pili, Jose kazeze yawezekana aliweka kisasi cha kudumu, baada ya familia yake kunyanyaswa akaisambaza ile chuki kwa wajukuu na vitukuu kama wapo.
Hivyo yawezekana mmoja kati ya kitukuu ama mjukuu alikuwa akilishambulia jina la Nguzu popote atakapokutana nalo hivyo naye alikuwa ameshambuliwa.
Mambo haya mawili yakamwacha katika sintyofahamu nyingine mpya.
Akajaribu kulitaja jina la Inspekta Kobo...... akatazama kisa chake hadi kuja kumchomea ndani ya nyumba yake.
Hili akaliweka katika mabano, yawezekana kuna watu wengine walihusika katika hili jambo.
Akayakumbuka maneno ya yule kiongozi wa waliotumwa kumkamata Majenga.
Akakumbuka kuwa yule bwana ndiye aliyemueleza juu ya Inspekta Kobo kuwa yungali rumande akituhumiwa kwa kesi mbaya kabisa inayoweza kumtokomeza uraiani, lakini alimtajia jina la kiongozi wao mkuu ambaye hata wao hawakuwahi kumwona hapo kabla.
Zumbe!
Nguzu akafuatilia katika mitandao mbalimbali kutazama huyu mtu ni nani katika serikali ili ajue je? ana uhusiano na ukoo wa Kazeze? na kama hana uhusiano ni kitu gani anataka?
Kichwa kikamuuma alipojikuta anayo orodha kubwa sana katika kichwa chake.
Na kadri basi lilivyoikaribia ardhi ya jijini Dar es salaam,mara moyo wa Nguzu ukapiga kwa nguvu sana.
Kuna kitu alikuwa amekisahau kwa muda mrefu.
Koplo Zubeda!
Mungu wangu! Akahamanika kutokana na hali ile ambayo ilimtokea naye asijue ni kwanini imekuwa hivyo ghafla wakati analikaribia jiji na si wakati yupo mbali?
 
RIWAYA: KONSTEBO NGUZU (Mzimu wa babu)
MAANDISHI YA: George Iron Mosenya

SEHEMU YA KUMI NA SITA

MAJIRA YA saa saba usiku Martin Nguzu alikuwa akirandaranda katika kona mbalimbali za jiji la Dar es salaam kusaka hoteli ambayo angeweza kulala kama si kupumzika mpaka patakapokucha na kuutazama uelekeo ambao anapaswa kuanza nao.
Hakuwa na mashaka yoyote ya kuufichaficha uso wake, habari zake zilikuwa zimesambaa lakini si picha yake.
Wasambaze picha yake kwa cheo chake cha u-konstebo kwani hawana mambo mengine ya kuandika?
Alifanikiwa kupata hoteli ya bei ya wastani, akafanya malipo na kujiandikisha kwa jina batili.
Akakabidhiwa chumba.
Alipoingia na kuufunga mlango akaiwasha taa, akakiona kioo kikubwa jirani na mlango.
Akajitazama jinsi alivyokuwa, kimaumbile alijiona yungali vilevile lakini ndani ya mwili wake alijihisi yupo ngangali sana tofauti na awali.
Bila kutarajia akajikuta akimuwaza tena Zubeda.
Akiwa palepale mkabala na kioo alifikiria ule ukaribu wao jinsi ulivyokuwa ukimpa raha ya kipekee, raha iliyomfanya ajikute akimwonea wivu inspekta ambaye alisemekana kummiliki Zubeda, kuna kipindi alikuwa akitamani hata kumdhuru yule inspekta ambaye ndiye kikwazo pekee kilichokuwa kati yake na penzi la uhuru baina yake na Zubeda.
Nguzu alikuwa akitamani kumtambulisha Zubeda kwa marafiki zake kama shemeji yao, ukiachana na kuufurahisha moyo wake na pia kuuweka wazi udhibiti wake dhidi ya Zubeda, Sifa pia kilikuwa ni kigezo cha kutamani uhuru ule.
Nani ambaye angeacha kumsifia kuwa anamiliki 'mtoto mkali'
Zubeda alikuwa mzuri, urembo wake haukufichika hata alipojitundika katika gwanda zake za kazini.
Askari wengi walikiri kuwa binti huyu alikuwa wa aina yake, na hii ni sifa waliyoitoa huku akiwa katika gwanda zake.
Nguzu alikuwa amepata fursa ya kuziondoa zile gwanda kisha akamvesha kanga moja nyepesi mwanadada huyu na kisha kuambatana naye maliwatoni.
Macho yake mawili yenye nguvu yakifanikiwa kutazamana ana kwa ana na mzigo wa matiti ambayo yalikuwa yamevuka kidogo ule muda maarufu wa 'saa sita' lakini hayakuwa mbali sana kufananishwa na muda huo hasahasa yakipewa msaada mdogo wa sidiria.
Macho ya Zubeda yangeuamuru mwili wa mwanaume yeyote atakayemtilia maanani kujikuta ukisisimka na donge la hamu kumshika.
Macho yake makali angali akiwa kazini yalikuwa yanatepeta wakiwa wawili na Nguzu na kumfanya Nguzu ashangazwe na hali hii.
"Huyu mtu aliupata vipi ukoplo wa polisi? Kwa macho haya tepevu?" Haya ni baadhi ya maswali aliyojiuliza kabla hajachoshwa na mikono laini ya Zubeda. Mikono ambayo hakuamini hata kama inao uwezo wa kuzishika pingu na kumlazimisha mtuhumiwa azivae.
Ajabu Zubeda alisifika kwa kuwahenyesha watuhumiwa.
Kuhenyesha watuhumiwa??
Ilishangaza!
Lakini Nguzu naye akajikuta anahenya kupambana na msisimko uliokuwa ukimkumba kila mara mikono ile ilipomgusa.
Na hapo akakiri kuwa hata yeye ni mtuhumiwa pia na alikuwa anahenyeshwa wawapo chumbani wawili.
Kweli Zubeda ni kiboko!
Kumbukumbu hizi zikajirejesha nyuma kwa kasi ya ajabu, Nguzu akakumbuka jinsi alivyokutana na Zubeda jijini Mwanza.
Akaukumbuka utambulisho wake wa kijivuni dhidi ya Zubeda ambaye hakuwa na cheo chochote wakati ule na hata jeshini alikuwa hapajui.
"Naitwa Martin, Konstebo Martin Nguzu!"
Tabasamu likamponyoka na kujikuta akipiga saluti ya kihuni kwa mkono wa kushoto.
Akakiendea kitanda na kujirusha hapo kwa fujo zote.
Kitanda kikahimili kishindo!
Na hapo kikaanza kuufyonza ule uchovu wote na kuugeuza kuwa raha ya kipekee.
Usingizi ukampitia.....
_____________

MAHAKAMA kuu ya Tanzania ilikuwa imesheheni haswa, maaskari walikuwa wanafanya kazi ya ziada kuwazuia watu waliozidi kumiminika pale mahakamani.
Punde ikasikika amri ya kumaanisha kuwa jaji na baraza zima la wazee lilikuwa linaingia pale mahakamani.
Kimya kikuu kikatanda ikiwa ni ishara ya kuheshimu mahakama.
Akiwa na pingu miguuni na mikononi kisha pingu hizo za miguu na mikono zikaunganishwa na mnyororo mgumu aliongozwa hadi katika kizimba.
Alipofikishwa kizimbani akafunguliwa zile pingu, akaingia akiwa huru kizimba kikafungwa.
Macho yake yaliyozama ndani na kuzidi kuonekana kuwa ni makubwa yaligeuka huku na kule, safari hii hakuwa na uoga tena alikuwa ameikubali hali halisi.
Macho yake yakatua katika kiti alichokuwa ameketi mama yake aliyepooza upande mmoja.
Licha ya kwamba alikuwa amelia sana hadi machozi kumkauka aliweza kuhisi machozi ya moyoni yakimlowanisha.
Wakagonganisha macho yao, akamwona mama yake akizungumza maneno yasiyoweza kusikika hata kidogo huku machozi yakimtoka kwa wingi.
Aliamini kuwa mama yake alikuwa akimwombea kwa Mungu ili kesi ile ipate muujiza wa yeye kushinda.
Uchungu uliomshika alitamani angepewa walau nafasi moja tu ya upendeleo aweze kuzungumza na mama yake, amkumbatie na kumfariji.
Jicho lile likaendelea kubarizi pale ndani ili aweze kuwaona watu wengine ambao huenda anawajua.
"Marafiki hawana maana!" Alijisemea baada ya kuhakikisha kuwa hakuna rafiki yake hata mmoja aliyefika mahakamani hapo.
"Kwa hiyo wameogopa kuwa nitawachoma ama?" alijiuliza.
Hakupata muda wa kujiuliza zaidi wakati jicho lake likitua katika kiti kingine upande wa kushoto.
Macho yakagongana tena na huyu mkaaji wa kiti hicho.
Zubeda!
Walitazamana kwa sekunde kadhaa kabla Martin Nguzu hajakwepesha macho yake.
Hakutaka kumwangalia binti huyu aliyekonda sana na kuonekana wazi alikuwa akitawaliwa na uchungu mkubwa.
Alipomaliza kuzungusha macho yake akamwona jaji akitoa ruhusa ya mwendesha mashtaka kumuuliza maswali mshtakiwa.
Maswali yalikuwa magumu sana, akayajibu kadri alivyoweza. Mengi alikuwa ameyasahau kabisa.
Miaka sita mahabusu bila kesi kusikilizwa, angekumbuka nini sasa.
Wakati wote huu alikuwa akishangaa kumwona wakili kwa ajili ya kumtetea.
"Lakini nilimkataza mama kuhangaika kuweka wakili." Martin Nguzu alijiuliza huku akitikisa kichwa chake kama namna ya kusikitika.
Akakiri kuwa katika ulimwengu huu mzazi ni mzazi lakini mama ni bora zaidi kuliko baba. Mama anaumia sana akimwona mwanaye katika wakati mgumu wakati baba huhesabu ugumu ule kama changamoto na kusema 'kijana wangu amekua na atatatua changamoto hizo' mama huinama chini na kusema 'mtoto wangu anateseka'
Ni hii tofauti aliikiri katika kesi yake hii. Mama mzazi aliyepooza mwili alikuwa mahakamani kushuhudia kile kiumbe alichokileta duniani baada ya suluba ya miezi tisa, kisha kuhangaika katika malezi.
Hakujali kupooza kwake, hakujali kuwa yawezekana mwanaye akahukumiwa kifungo cha maisha gerezani ama kunyongwa kabisa kwa jinsi kesi ilivyokuwa.
Alichokifuata pale ni kumwona mwanaye kwa jicho lake mwenyewe. Kama alivyomuona wakati amemzaa, alihitaji kumwona tena katika ugumu huu, ugumu wa kukondeana kwa sababu ya mateso na lishe duni, ugumu wa kuwaza kufia jela.
Mama alibaki kuwa shuhuda wa mwisho!
Ni nani kama mama kwani?
Wakili alisimama na kutema vifungu vya sheria ili kumnusuru Martin Nguzu kutoka katika janga lile.
Alionekana kuijua vyema sheria lakini upande wa mashtaka ulionekana kuwa imara zaidi, sura nyingi zilitawaliwa na hasira kali. Hasira hii iliboreshwa zaidi na mavazi yao, walifanania na kundi la mafia ambalo limemshukia mwenzao baada ya kuwasaliti na sasa wanataka kumpa adhabu ya kumzika huku akiwa hai akaupiganie uhai wake akiwa chini ya ardhi.
Nguzu akamgeukia jaji ambaye alionekana mwingi wa chuki kuliko haki.
Jaji alipounyanyua uso wake Nguzu akajikuta anagundua kitu kipya kabisa. Ile sura ya jaji haikuwa ngeni machoni mwake hata kidogo.
Hofu ikamjaa ya kutotendewa haki juu ya kesi ile ambayo alitambua wazi kuwa ni vile tu amekosa mashahidi lakini haikuwa ikimuhusu kabisa na alitakiwa kuwa mtu huru.
Jaji yule akaanza kusoma vipengele kimoja baada ya kingine kwa utulivu sana.
Ni kama aliyeelekea kutoa hukumu, hii ilimshangaza sana Martin.
Hukumu inatoka vipi kirejereja hivi bila kesi ile kupewa muda wa baraza la wazee kuipitia na kutoa mitazamo yao.
Jaji alisoma taratibu huku kila mahali akijaribu kumbana Nguzu.
Na hatimaye kauli ikamtoka.
"UTANYONGWA MPAKA UFE"
Mungu wangu! Nguzu akamwona mama yake mzazi akitua chini kama mzigo, watu wakakimbilia alipokuwa ili kumwokoa.
Palepale akawaona askari wanne wenye ghadhabu wakisogea katika kile kizimba na pingu kwa ajiri ya kumchukua na kumpeleka katika mahabusu ya mahakama kabla hawajampeleka gereza la Ukonga.
Gereza pekee ambalo washtakiwa waliohukumiwa kunyongwa mpaka wafe huhifadhiwa huko mpaka siku ya hukumu yao.
Kuwaona watu wale kukamchanganya Nguzu, na jaji alikuwa amefunga mjadala tayari.
Nguzu akaona haiwezekani, akawahi kujirusha akaidaka silaha ya askari mmoja na mara moja akaielekeza alipokuwa yule jaji.
Jaji akakodoa macho yake alipojikuta anatazama ana kwa ana na bunduki iliyoshikwa na mtu asiyekuwa na masihara hata chembe.
Akafyatua risasi kiufundi lakini yule jaji akawahi kujificha chini ya meza.
Na hapohapo Nguzu akaisikia sauti ya kike ikimpigia kelele kumtahadhalisha.
Ilikuwa sauti ya Zubeda!
Akageuka na kukuta amechelewa tayari, bunduki nyingine ilikuwa inaelekea kufyatuliwa ili yeye adhurike.
Ilielekezwa kifuani pake.
Akajikuta anapiga mayowe ya hofu huku akikiziba kifua chake kwa mikono yake.
Bunduki ikacheua.
"Mamaaaa nakufaaa!" alipiga kelele kubwa sana na hapo akajikuta akibiringita kama chaguo lake la mwisho.
Akashangaa kujikuta anaelea hewani. Akaanza kutapatapa akirusha miguu huku na kule.
Hatimaye akasimama wima tena.
Hakuwa mahakamani! alikuwa amesimama katika kitanda huku akiwa amejifumbata mikono yake katika kifua chake.
Mwili wote ukitetemeka na jasho likimwagika kwa chati.
Ndoto!
Jasho lilikuwa linamwagika vibaya mno, bado moyo ulikuwa unapiga kama unaotaka kutoka nje ya kifua chake.
Alikuja kutulia baada ya dakika kumi na hapo ndipo akakiri kuwa ile ilikuwa ni ndoto lakini ndoto ya ajabu sana.
"Yule jaji yule! Yule jaji ni nani!? Jaji, jaji...." Nguzu alibaki kusema kama ambaye anajaribu kulazimisha kung'amua vitu kutoka katika ile ndoto ya ajabu ambayo hakutaka kuamini eti ilikuwa ndoto ya kawaida.
Alihisi yule ni babu yake anasema naye. Hofu ikatanda alipokumbuka kuwa alihukumiwa kunyongwa katika ndoto yake.
Hofu ya kifo ikamjaa, akaanza kuhofia uwepo wake katika jiji la Dar es salaam.
Jiji ambalo ipo ile mahakama ya ndotoni na pia lile gereza wanalohifadhiwa wafungwa wa adhabu ya kunyongwa mpaka kufa.
Hiki nini? alijiuliza.
Bado hofu iliishi naye, akamkumbuka mama yake alivyokuwa akimlilia na hata alivyoanguka baada ya hukumu ile kutolewa.
Hofu ya kifo ikiwa haijaisha ikapanda hofu nyingine.
Hofu ya kumpoteza mama yake mzazi pindi atakaposhuhudia matatizo yakimpata.
Nguzu akakiri kuwa huu mpambano ulikuwa maji ya shingo kwake naye alikuwa hajui kuogelea vyema. Akaamini kuwa alikuwa anahitaji watu watakaosimama pamoja naye.
Kwa mara nyingine tena jina Zubeda likakiandama kichwa chake.
"Kwanini Zubeda?" alijikuta katika swali hili.
Hisia mbili zikaanza kupambana, mojawapo ilikuwa hisia za mapenzi. Nguzu akakiri kuwa alikuwa akihangaishwa na jina Zubeda kwa sababu tu aliwahi kumpa burudani ambayo ilikatishwa ghafla bila kufika ukingoni.
Pili alihisi kuwa anahitaji kupata msaidizi na msaidizi wa kweli katika vita hii ni koplo Zubeda.
Kujua hisia ipi ni ya kweli nd'o ukawa mtihani mzito.
"Ngoswe penzi kitovu cha uzembe" Usingizi ulimkuta Nguzu akiwa katika uchambuzi hafifu wa kitabu hiki maarufu , alianza kwa kumpa kongole mwandishi Edwin Semzaba kwa kuandika kitabu hiki, kisha akahamia kwa Ngoswe na Mazoea na hadi anasinzia alikuwa amefikia mahali ambapo Mazoea ameanza kuzoeana na Ngoswe! Hii ni baada ya Ngoswe kumuhadaa binti yule wa kijijini kuwa atamtorosha waende wote mjini......
Alisinzia akiwa anatabasamu, bila shaka ni vile visa vya Ngoswe vilimpa tabasamu.
 
RIWAYA: KONSTEBO NGUZU
MAANDISHI YA: George Iron Mosenya

SEHEMU YA KUMI NA SABA

ASUBUHI ilimkuta konstebo Martin Nguzu katika ofisi ya gazeti mojawapo kati ya yale yaliyoandika habari ya kifo chake na kisha kusemekana aliyeandika ni 'mwandishi wetu.
Kama ilivyomkera inspekta Kobo na kujikuta akiponyokwa na matusi ya kiitaliano, kwa Nguzu ilikuwa vilevile lakini hakuwahi hata siku moja kuota ndoto za kiitaliano.
Yeye aliponyokwa na matusi mfululizo ya kisukuma.
Lakini hakuishia kutukana tu, aliamua kupiga hatua na aliamini hatua hii inaweza kuwa ya muhimu zaidi kumfikisha katika hatua nyingine.
Akalisoma gazeti lile na kuyapata mawasiliano ya muhariri mkuu wa gazeti hilo.
"Huyu jamaa lazima anawajua waandishi wake wote, wenye majina na wasiokuwa na majina wanaojiita 'mwandishi wetu'. Atawataja ama atakula maumivu yao..." Alizungumza konstebo wakati akizungusha macho yake huku na kule kabla hajazama ndani ya ile ofisi.
Awali alipanga kwanza kumjua sura huyu bwana na kisha ajiweke katika lindo zuri aweze kuijua gari yake.
Baada ya kujua hayo angeachana naye na kisha kumpangia siku ya shambulizi.
Alijua kuwa amezisahau taarifa zile tayari, na hata hao akina'mwandishi wetu' walikuwa wanaendelea na maisha yao mengine.
Mambo yakaenda tofauti, Nguzu akiwa amejivesha miwani ya jua katika uso wake huku akiziachia nywele zake wazi kwa maksudi kabisa.
Hazikufanania na nywele za askari, hasahasa wa cheo cha konstebo.
Nguzu alikuwa katika hali ya utofauti.
Alianzia mapokezi na kuulizia ni wapi atampa muhariri, katibu muhtasi akauliza ikiwa ana shida binafsi ama ya kiofisi.
Maswali yao yaleyale kila siku! Nguzu alijisemea kabla hajajibu, "Shida ya kiofisi dada."
"Ok! nyoosha moja kwa moja hadi katika ile korido kisha pinda kushoto utaiona ofisi, keti katika foleni subiri huduma."
Nguzu akainama chini kidogo huku akijishika kifua chake kama ishara ya kushukuru.
Akatoweka!
Alimkuta bwana mmoja mwenye mvi akiwa anangoja kuingia, akaketi pembeni yake.
Bwana mwenye mvi akaanzisha soga kuhusu siasa mara ahamie katika mpira wa miguu, huku ndipo alizidi kumpoteza Nguzu.
Ushirikiano wake pekee ukawa 'ndio' ama kujichekesha.
Hatimaye mzee akaingia na kutoka baada ya muda mfupi.
Bila shaka muhariri hakuwa tayari kusikiliza soga nyingi kutoka kwa yule bwana.
Ikawa zamu ya Nguzu.
Hofu ikamwingia hakutambua kama yupo sahihi katika hatua ile ama ameitupa karata yake vibaya.
Akaufungua mlango na kuingia ndani huku akitambua kuwa yeyote yule anaweza kustaajabu kuhusu ile miwani lakini alifurahi kwa sababu ni watanzania wachache sana anaweza kukuona haupo sawa katika jambo fulani naye akawa kimya asikwambie badala yake anamweleza rafiki yake kisha wanacheka!
Hee! Watanzania?! Tusaidiane kujishangaa.
Kweli! hakuna aliyemuuliza.
"Karibu!" Sauti nyembamba lakini ya kiume ilimkaribisha huku mikono ikimwonyesha mahali pa kuketi.
Martin akaketi.
"Naitwa Sebastian! natokea Temeke Dar es salaam." Alianza kujitambulisha.
Muhariri hakuonyesha kujali juu ya lile jina, Nguzu akaendelea.
Sasa akayafungua magazeti kadhaa aliyokuwa ameyashika mkononi akayatua mezani.
"Nakusikiliza bro.." Sauti ile iliyotawaliwa na kiburi cha kuwa muhariri ilizungumza.
"Nilikuwa nataka kuuliza..."
"Ulikuwa unataka ama nd'o unataka kuuliza mkuu?!" Muhariri akamuwahi Nguzu.
Nguzu akafadhaika na kuamua kutuliza akili yake, tayari alishagundua kuwa alikuwa anakosa kujiamini.
Akajipa sekunde kadhaa akaingia tena kushambulia.
"Nauliza, hizi habari ambazo anaandika mwandishi wetu, ni nani anaziandika na kwa nini asijitambulishe kwa majina yake." Akaweka kituo.
"Samahani umeuliza ama umetoa lalamiko!" Muhariri mwenye nyodo akazungumza, sasa aliachana na kazi alizokuwa anafanya akamtazama Nguzu huku akiyabetua mabega yake.
"Nimeuliza."
"Ni utaratibu wa kiofisi. Ukihitaji ubadilishwe utapaswa kuandika barua na kuiweka kuleee kwenye sanduku la maoni. Sijui kuna la ziada lililokutoa Temeke bwana.... bwana..." Akalisahau jina lake na kulipuuzia.
Konstebo Martin Nguzu akanywea na kujiona anazidiwa karata hivihivi mchana kweupe.
Akapaniki!
Akasimama wima, akawa anayetafuta neno la kuzungumza linakikataa kinywa linarudi kichwani.
Akaona haifai kuendelea kusimama hivyohivyo.
"Huyu aliyeandika hii habari ni nani?" Akafoka. Bado alikuwa wima.
Muhariri hakuligusa lile gazeti badala yake akainyoosha shingo yake na kuona nini anaonyeshwa.
Akakutanisha macho yake na habari juu ya kifo cha Nguzu na kuhusishwa sababu za kimapenzi na mengineyo.
Akajikuta anarudi nyuma kwa kasi, uso wake ukiitangaza wasiwasi yake.
Akaishika simu na kutaka kubofya nambari kadhaa, palepale Nguzu akauwahi ule mkono na kuugandamiza.
Kisha ili kuimarisha usalama akachomoa kisu kikubwa kutoka katika ficho lake.
"Huwa ninaua bila taarifa maalumu, sipendelei ufe hivyo. Jibu swali langu." Hakuonekana kuonyesha mzaha.
Muhariri akalitambua hilo.
"Sijaandika mimi."
"Mwandishi wetu ni nani?"
"Mwandishi wetu... sim... simj.."
Ngumi kali ikatua katika shingo ya muhariri.
Ilikuwa ngumi maalumu kwa ajili ya kumzuia yule mwanadamu anayependa kuongea kwa sauti ya juu, kumpunguza uwezo wa kupiga kelele na kujikuta akinong'ona.
Nguzu alimwacha akihangaika pale akauendea mlango na kuufunga!
"Simu yako ya mkononi..." Alisema kisha akautega mkono wake. Muhariri akaikabidhi huku akilia kwa sauti yake ile nyembamba ambayo ngumi kali ilizidisha ule wembamba na kujikuta akigumia kama mtoto wa kike.
Nguzu aliipekua ile simu upesi upesi katika sehemu za jumbe mbalimbali, hakupata ujumbe wa kumvutia.
"Unapendelea kufia ofisini ama nyumbani kwako?"
"Si... aahm! nisamehe si... nitasema lolote utakalo."
"Unanijua mimi?"
"Sikujui."
"Ni nani huyu mwandishi wetu na anapatikana wapi?"
"Niliandika mimi... lakini hata mimi nilipewa."
"Nisikilize we fala.... ndoto yangu moja ambayo nahitaji kuitimiza ni siku moja nimuue mtu akiwa ofisini nimkatekate nimtie kwenye mfuko wa rambo, kisha nitoke na ule mfuko niingie nao katika daladala niutelekeze huko. Vyombo vya habari vishindwe kuelewa vitaandika nini kuhusu kifo hicho...... Nina hasira ya kutimiza ndoto zangu. Nakupa nafasi ya mwisho kujieleza ukitetereka natimiza ndoto yangu. Nakuhakikishia kuwa sitaacha walau tone la damu humu ndani kwa ajili ya wapelelezi." Nguzu alizungumza huku akiwa amemkazia macho muhariri.
Kijasho kikamwagika...
Akatapika kila alichokuwa anakijua katika ile habari iliyoandikwa na 'mwandishi wetu'.
_____

JAMBO la kwanza lililokituliza kichwa cha Martin Nguzu ni juu ya inspekta Kobo.
Nguzu alistaajabu asimini hata kidogo kuwa aliachoelezwa kipo kama kilivyo. Licha ya kukiri kuwa yule muhariri alikuwa 'chamtoto' sana na asingeweza kuficha lolote kwa kitisho alichompatia lakini bado hakutaka kumpatiliza na kumwamini kwa asilimia zote.
Nguzu alitoka pale moja kwa moja akisimamia wazo lake kuwa kwa namna yoyote ile ni lazima afike nyumbani kwa Koplo Zubeda, aliamini kuwa ni huku ambapo angeweza kuupata mwanga zaidi katika hatua zake.
Alikiri kuwa kuonekana kwake mbele ya Zubeda kutazua kizaazaa cha aina yake ambacho kinaweza kusababisha majirani wakajazana kutaka kujua nini kinatokea.
Nguzu akajipa tahadhari kubwa sana kuwa ni lazima umakini utangulie mbele kuliko kiherehere cha kutaka kukutana na Zubeda ambaye kichwani anaamini Nguzu ameuwawa.
Ili kuondoa macho mengi kumfuatilia juu ya alichokuwa anahitaji kufanya Nguzu akaamua kufanya uvamizi wake mchana kweupe. Alilipenda giza lakini alijua linavutia wengi sana....
Akauchagua mchana kwenda nyumbani kwa Zubeda.
Akajiapiza kuwa Zubeda akionyesha dalili zozote za kuwa upande usiokuwa wake basi hatasita kumshukia kama mwewe anavyomshukia kifaranga na kumwacha mamaye akipiga kelele asiweze kutoa msaada.
Majira ya saa nane mchana alikuwa analitazama geti la kuingilia nyumbani kwa Zubeda.
Hali ya ukimya ilitawala sana, akategea mpaka alipowaona wanaume wawili wakipita kuelekea njia ile naye akaunga tela ili asionekane kama anajihusisha kwa lolote na nyumba ile.
Akapita na kuangaza huku akiulazimisha ule ukimya umwingie akilini na kumpatia jawabu la ni kitu gani kinaendelea.
Kimya kilimtatanisha!
Si kwamba hapajawahi kuwa kimya ama huwa ni sehemu yenye kelele za kutisha, ila ni mwili uligoma kuupokea ukimya ule katika namna ya kawaida.
Alilipita geti lile kwa mara ya kwanza huku akifanikiwa kujifunza kuhusu mazingira yale upesiupesi, mara ya pili aliporudi alilifikia geti na kubisha hodi.
Mlinzi akajitokeza na kufungua.
Hakusema kitu akabaki kumsikiliza Nguzu mwenye miwani nyeusi.
"Ni mgeni wa Zubeda! Koplo Zubeda.." Nguzu akajitambulisha huku akigundua kuwa huyu mlinzi ni mpya sio yule wa awali.
Akasaili eneo lililomzunguka yule mlinzi na kugundua kuwa hata silaha imebadilika.
Sub Machine gun!
Akaduwaa, kunani mpaka Zubeda aamue kuajiri mlinzi ambaye ana utaalamu wa kutumia silaha hii tena mchana kweupe.
"Sub machine gun!" akajikuta anajisemea kichwani kwake, kana kwamba ni mashairi ya wimbo anaotaka kuukariri.
"Wewe ni nani?" Mlinzi akauliza.
Polisi! Machale yakamcheza Nguzu kwa jinsi mtu yule alivyouliza lile swali, hakuwa mlinzi wa kawaida huyu alikuwa polisi.
"Naitwa Sebastian Madeko. Ni jirani..." alijitambulisha.
"Nisubiri hapa!" mlinzi alimwamrisha kisha akapiga hatua kwenda katika mlango wa nyumba ya Zubeda.
Nguzu akamwacha hadi alipoufikia mlango akawa makini kumtazama atazungumza na nani.....
Alishatambua kuwa hali haikuwa shwari, ni aidha Zubeda alikuwa matatani ama la alikuwa analeta matata.
Mlinzi akarejea baada ya dakika mbili.
"Twende!" akamwambia huku akimkazia macho.
Nguzu hakutaka kuionyesha hofu yake badala yake alijiandaa kwa mapambano.
Mlinzi akalifunga geti vyema kabisa kabla ya kumwongoza Nguzu kuelekea katika mlango wa kuingilia nyumba ya Zubeda.
Wakaufikia mlango, Nguzu hakuendelea kuwa kondoo.
Katika mlango ule wa kioo, aliweza kumsoma yule mlinzi, kuna shambulizi alijiandaa kumkumba nalo kabla hawajaingia ndani ama kuishia palepale.
Nguzu akawa sekunde moja mbele, akatokwa na teke maarufu kwa jina la 'Shukrani ya punda'.
Lilikuwa teke la nyuma!
Mlinzi ambaye hakutarajia pigo lile akapepesuka mpaka chini, alimanusura bunduki yake imuue yeye mwenyewe kwa kumchoma kooni.
Macho yakamtoka pima!
Nguzu akawahi kukitoa kisu chake na kujitoa mpaka pale chini kisha akadidimiza katika mkono wa mlinzi.
Akatokwa na yowe kubwa kwa muda mfupi, Nguzu akachomoa ile ngumi yake ya kupunguza sauti.
Ikamwingia yule bwana na palepale akaiondoa miwani yake.
"Naitwa Martin, Konstebo Martin Nguzu. Sikijui kifo bado, ukifanya mfano wa kunidanganya utakijua kifo kabla yangu." Alifoka Nguzu huku midomo yake ikitetemeka.
Mlinzi hakuamini alichokuwa anakiona, alijiona akiwa anatazamana na mzimu wa Nguzu ambaye anasadikika kuwa ni mfu.
"Ni nani amekuagiza kulinda eneo hili na ni nani yupo ndani ya nyumba hii zaidi yako?"
Mlinzi akajifanya hajasikia.
Nguzu akatokwa na ngumi kali hii ikatua katika sikio la kuume la mlinzi.
Hakuweza kutokwa na yowe kubwa, damu ikaanza kumtoka.
Nguzu akatokwa na tabasamu wakati akimuuliza kuwa ni kipi chepesi kusikia swali ama ngumi?
Mlinzi yule ngangari akaanza kutokwa na kamasi.
Bwege alikuwa amepatikana!
"Nipo mwenyewe.... nipo mwenyewe usiniue."
"Amekuagiza nani?"
"Inspekta.... Inspekta Kobo." Alijibu kwa utulivu.
Nguzu akaishiwa hamu! hakutarajia jibu lile.
Huu ukawa ni mkanganyiko mpya kutoka katika majibu ya muhariri na huyu bwana mlinzi.
____
 
RIWAYA: KONSTEBO NGUZU
MAANDISHI YA: George Iron Mosenya
SEHEMU YA KUMI NA NANE
Akamtazama kwa jicho lililotangaza chuki ya waziwazi kabla hajamtundika swali jingine katika namna ya kisharishari.
"Muonekano wake upoje huyo bwana wa kuitwa Kobo.
Huku akikumbuka kuwa akijifanya hajasikia swali lile basi kifuatacho ni kubamizwa ngumi na kuulizwa swali la kukera safari hii aliwahi kujibu.
Akauelezea wajihi wa inspekta Kobo.
Nywele ndefu nyeupe zinazojaribu kuuficha uwalaza wake, ndevu fupi zenye uwiano sawia na nywele zake katika rangi.
Umri wake ukichezea miaka sitini hadi sitini na nane.
Konstebo Nguzu akachoka upya!
Huyu hakuwa inspekta Kobo aliyekuwa akimfahamu yeye.
Lakini kilichomjaza nguvu upya ni ule utambulisho ulikaribiana na ule ambao alielezwa na muhariri wa gazeti baada ya kumbana vizuri.
Konstebo akiwa anajiandaa kumuuliza tena yule bwana swali jingine, akafanya kosa kuitazama anga kama anayefikiria aulize kwa namna gani nyingine ili apate mwanga mkali anaouhitaji katika giza lile nene.
Yule muhanga alitokwa na teke kali likatua vyema katikati ya mapaja ya Nguzu, teke lile likamfanya Nguzu ainame.
Naam! adui alihitaji hivyo.
Uso ukawa jirani naye, akatokwa na teke kali sana lililoongezewa uzito na kiatu kigumu alichokuwa amevaa.
Uzito huu ukatua barabara katika uso wa Nguzu.
Ilikuwa mchana ghafla ukawa usiku kwa Nguzu pekee. Pigo lile lilimsukuma mpaka mlangoni.
Akaingia na ule mlango, kiuno kikapokea maumivu stahiki.
Konstebo Nguzu akajaribu kurejea katika mapambano lakini giza lilikuwa linamuharibia, hakumwona adui yake. Sanjari na hilo alikuwa akipambana kuilamba damu iliyokuwa inamtoka puani.
Adui alikuwa amechachamaa.
Alijaribu kutapatapa lakini adui hakumwachia nafasi, ni kama alimaanisha kutaka kuondoka na roho ya Nguzu na hakuhitaji kumuuliza swali lolote lile.
Nguzu alibaki kuikumbatia sakafu wakati mateke yasiyokuja kimpangilio yakimwandama.
Pumzi zikaanza kumsaliti, na hapa akajaribu kwa mara ya mwisho kuusaka uhai wake ambao yule bwana alitaka kumpokonya angali hajamaliza shughuli yake.
Akaituliza akili katika maumivu. Kitu ambacho wanadamu wachache sana wanaweza.
Kasumba ya mwanadamu akisikia mlio wa risasi anaanza kukimbia asijue kama anaikimbia ama anaikimbilia risasi.
Nguzu akautafuta uelekeo wa yale mateke makali yaliyomaanisha kuua. Akaupata uelekeo wa mpigaji, na jinsia livyokuwa anapiga hovyo akatambua bayana kuwa anatumia zaidi hasira na hapohapo anapoteza muhimili wa umakini.
Teke lilipomwingia akajitutumua na kusimama wima, na kujirusha kulekule katika uelekeo wa adui yake.
Karata sahihi!
Akamsomba yule bwana na kutua naye chini.
Majogoo mawili yaliyochoka haswa yalikuwa yamelaliana.
Na heri tele ziwe kwa kwa jogoo lililomlalia mwenzake.
Martin Nguzu alikuwa juu.
Hakuweza kurusha ngumi, kuchimba mikwara wala lolote lililoonyesha umwamba. Wote walikuwa wanahema juu juu.
Martin akapambana na kufanikiwa kuyafumbua macho yake.
Likafumbuka jicho moja kwa shida sana.
Akamwona adui yake akiwa mdomo wazi, anahema juu juu!
Akaiona shingo ikiwa wazi.
Akajitutumua akaifikia na kuikaba, anayekabwa akaanza kurusha mikono kuzuia kitendo kile.
Hakika walikuwa wamechoka!
Vishindo vilisikika kwa mbali, Nguzu akahisi hatari kubwa inakuja mbele yake.....
Uwezo wa kupambana kwa wakati ule hakuwanao, kama huyu aliyechoka anashindwa hata kummalizia vipi hao wanaokuja huku wakiwa na nguvu mpya.
Akajigeuza na kutua chini kisha ukaanza mpambano mpya wa kila mmoja kujaribu kusimama.
Nguzu akajaribu akaanguka, mwenzake naye yakamkuta yaleyale.
Nguzu akakerwa na hali hii ya kujikuta mnyonge angali oparesheni ikiwa mwanzo kabisa.
Hali ikazidi kuwa mbaya alipomwona yule mlinzi akifanikiwa kusimama wima, akayafuatilia macho yake yakiwa yanaangaza huku na kule hatimaye kwa pamoja wakajikuta wakiitazama bastola iliyokuwa imetulia sakafuni ikisubiri yeyote ajuaye kuitumia na aitumie.
Nguzu alitamani nguvu zimjae na akimbilie kule kuiwahi lakini hakuwa na nguvu za kutosha na alikuwa katika maumivu bado.
Kifo kikanukia katika namna ya kukera. Yule mlinzi akaanza kujivuta kwa kasi kuifuata bastola ile, Nguzu akaanza kujiona yu mjinga kukisubiri kifo chake bila dalili zozote za kupambana.
Akapitiwa na fikra za harakaharaka juu ya hayati babu yake, aliyemrithisha jina hilo lenye maana kubwa.
Nguzu 'chikichia' hapa hapafai tena! alijionya huku akiangaza lilipo kimbilio.
Hakuliona kimbilio kabla hajamwona yule mlinzi akigeuka huku akiwa na bastola mkononi.
Akafyatua hovyo kwa mara ya kwanza, bastola isiyokuwa katika kiwambo cha kuzuia sauti ikatoa mlio mkubwa.
Mlio huu ukamuhamasisha Nguzu kujitutumua na kukimbia.
Alikimbia ndani ya ile nyumba huku akiamini kuwa ataukuta wazi ule mlango aliokuwa anaufahamu ili aweze kutokea upande mwingine.
Hofu ya kifo ilizidi kujenganaye urafiki, alijitutumua akaufikia mlango.
Mungu wangu!! ulikuwa umefungwa kwa kutumia mnyororo.
Hakuwahi kuiona hali kama hii hapo kabla. Huku nyuma akawa anamsikia yule mlinzi akitoa matusi yote huku kila mara akimaanisha kuwa iwe isiwe lazima amuue.
Nakufa! Hatimaye Nguzu akakiri, lakini hakubaki kibwegebwege afe bila kupambana.
Akausukuma mlango wa chumba cha Zubeda ambacho enzi zile alikuwa akiingia huku amebebwa mgongoni na koplo yule mwenye asili ya Tanga lakini akiishi zaidi Mwanza.
Sasa aliingia katika chumba hiki huku akiwa anasota, jicho moja likiwa linaona kwa tabu huku lile jingine likiwa limefumba kabisa.
Hamadi! mlango ulikuwa umezuiwa na kitu kwa ndani.
Hofu ya kichwa chake kusambaratishwa na risasi ikamfanya Nguzu ajitupe mzima mzima na kufanikiwa kukisogeza kizingiti.
Akajikuta ndani ya chumba.
Sauti ya yule mlinzi nayo ikazidi kutapatapa ikitishia kuua.
Chumba kilimkaribisha Nguzu katika hali ya utulivu, utulivu ule ulimtisha zaidi, akajaribu kufikiri ni wapi atajificha ili kumkwepa mshika bunduki.
Uvunguni! hili lilikuwa wazo la kizembe lakini walau naye aliwaza.
Akaanza kujitutumua aingie uvunguni, akaanza kujivuta kwa kutumia tumbo.
Hakuzama sana kabla hajabamizwa ghafla na kitu kigumu katika paji la uso wake.
Ile anajaribu kujiweka sawa akatandikwa teke kali usoni, akajikuta yungali nje ya ule uvungu huku akiwa nusu hai nusu mfu.
Alikuwa amepiga magoti damu zikimvuja.
Hazikupita sekunde nyingi kiumbe akauona mdomo wa bunduki ukitangulia kutoka katika ule uvungu.
Nipokee baba nakufa mimi Nguzu! alijifanyia dua upesiupesi.
Na hapo mlango ukasukumwa akamsikia yule mlinzi akiendelea kuropoka.
Nguzu akatambua kuwa nyuma yake palikuwa na mtutu na pia mbele yake alijionea waziwazi.
Swali likabaki juu ya nani atakayekuwa wa kwanza kufyatua ili auondoe uhai wake.
Yule wa uvunguni akawa wa kwanza kufyatua.
Risasi ikapenya jirani kabisa na sikio la Nguzu, ikafanya mlio kama wa nyuki mwenye hasira.
Kisha kishindo kikafuatia, Nguzu akatua chini akiangukia tumbo.
Kichwa chake kikawa jirani kabisa na ule mdomo wa bunduki iliyotokea uvunguni.
Na hapo akaviringika na kutoa uvunguni mshambuliaji yule aliyemkosa Nguzu maksudi na kumlipua aliyekuwa nyuma yake.
"Nilijua kuwa umekufa duniani, lakini si katika moyo wangu. Nikaamini tutakutana mbele ya haki, sijui kama ni mahali sahihi tulipokutana Martin, konstebo Martin Nguzu." Sauti imara ya kike ilizungumza.
Nguzu hakuhitaji macho yake katika hili, masikio pekee yalitosha kutambua kila kitu. Hatimaye kinywa kizito kikajitutumua na kuzungumza.
"Koplo Zuu!"
"Nihakikishie kuwa sitakiwi kukulipua kwa sababu u mmoja kati yao..."
"Si..sijui kitu hapa. Usilipue koplo." Alisihi Nguzu.
Zubeda akamdaka na kumsimamisha. Nguzu akakosa muhimili akataka kuanguka, Zubeda akatega mgongo wake kama alivyokuwa akiutega zama zao za furaha.
Nguzu akatua juu yake.
Zubeda akaanza kupiga hatua kutafuta uelekeo, Nguzu akiwa anakoroma.
Hali yake ilikuwa mbaya sana. Zubeda naye alikuwa anajitutumua, mguu wake mmoja ulikuwa haujaimarika..
Zubeda akiwa ndiye anayetegemewa alijaribu kufikiria juu ya uwepo wao pale ndani. Hapo kabla alikuwa amefanikiwa kuua na kisha kumpokonya bunduki mtu aliyewekwa kwa ajiri ya kumlinda asiweze kuleta bughudha yoyote.
Walimpatiliza kwa sababu ya miguu yake kuwa na mushkeli.
Dharau zao zikawafanya wapunguze ulinzi na kumwacha mbabe mmoja.
Yakamtokea puani!
Wakati Zubeda akiendelea kufikiria ni nini kilitokea hadi akabadilishiwa ulinzi ghafla, kutokea ule ulinzi aliowekewa na inspekta Kobo hadi ulinzi huu wa ajabuajabu. Akalishuhudia geti likifunguliwa na gari ikaingia huku askari watano waliovalia sare wakitangulia mbele.
Balaa!
Akajaribu kumshirikisha Nguzu aliyekuwa bado hoi. Nguzu hakuwa na la kuchangia.
Askari yule imara ndani kwa ndani na legelege kwa umbo la nje alitoweka mpaka chooni. Huku aliweza kuona kila kitu kilivyokuwa kinaendelea nje.
Alimtua Nguzu na kumsihi anywe maji yanayotoka katika bomba ili aweze walau kupata nguvu kiasi. Wakati huo akiendelea kuilazimisha akili yake ifanye kazi kwa kasi zaidi kuhusu tukio linalokuja mbele yao, alifahamu fika kuwa hakuna namna ya kuwa salama angali mle ndani kuna maiti mbili.
Kwa namna yoyote yeye na Nguzu watayamalizia maisha yao gerezani.
Maji yalikuwa msaada mkubwa sana kwa Martin Nguzu. Hayakumfanya kuwa imara sana lakini walau macho yake yaliweza kuona na aliweza kupumua vyema kwa sababu aliweza kuyaondoa mabonge ya damu yaliyounda uzio mbele ya pua zake na kumsababisha apumue kwa mdomo badala ya kutumia pua.
"Martin, Martin!" Zubeda aliita kwa kunong'ona.
Konstebo Martin akaupokea wito ule kwa kutulia akimsikiliza.
"Askari wote wanatuzingira." alimweleza kana kwamba Nguzu alikuwa anafahamu tayari juu ya uwepo wa ugeni ule..
"Akina nani? wako wapi?"
Zubeda hakumjibu badala yake alimsaidia kunyanyuka na kisha akamwelekeza kila alichokuwa akikiona kwa nje.
Walichoka!
__________________

BAADA ya kukataa kata kata kubadili maelezo yake, amri ilitolewa ya kwenda kupekua nyumba ya inspekta Kobo ili iweze kubainika kama anayo mawasiliano yoyote aliyowahi kufanya na kikosi cha majambazi kilichoinyanyasa Shinyanga kwa wakati ule huku askari kadhaa wakiangushwa na kupoteza maisha.
Msako wa kwanza haukuzaa matunda yoyote waliyoyatarajia.
Walikata tamaa huku wakianza kuamini yawezekana kuwa inspekta Kobo aidha hajuani na lile kundi ama la ni mafia aliyefuzu mafunzo yote stahiki.
Yaani hata umkate mguu akisema sijui ni sijui. Anameza maneno yake na kuingia nayo kaburini...
Wakiwa wanakaribia kuondoka, askari mmoja akafika na kitu kipya.
Akamtupia swali Kobo.
"Hii nyumba unayoishi ni mali ya nani?"
"Binafsi." Alijibu kwa sauti iliyokata tamaa.
"Umeijenga mwaka gani na umeanza kuishi humu lini?"
"Huu ni mwaka wa kumi sasa naishi humu."
Jibu lile likamfanya askari yule afanye tabasamu hafifu kabla hajamtundika pagumu bila yeye kujua.
"Umejenga nyumba nyingine tofauti na hii?"
"Hapana!"
"Mtu akifika hapa kukutafuta na asikupate je? ni wapi zaidi anaweza kukupata?"
"Kazini kwangu."
Jibu la sasa likayafanya meno ya yule askari yaonekane kwa sababu ya kicheko kidogo.
Na hapo akayabwaga makaratasi kadhaa mbele ya maaskari wenzake na Kobo akayashuhudia.
Alikuwa ni mnyonge lakini haya yalimtia unyonge zaidi.
Mikataba!
Mikataba baina yake na mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi hawara yake.
Koplo Zubeda!
Alitamani ardhi ifunguke atumbukie humo, alijiona waziwazi kuwa alikuwa anaelekea pabaya.
Kwanza alidanganya kuwa hana makazi mengine zaidi ya hayo, pili mikataba yote aliiandikisha kwa majina yake na si ya Zubeda.
Mkataba wa mwisho aliuandikisha miezi miwili tu iliyopita.
Anakwepa vipi rungu la sheria?
Watamuhesabu kama mnyang'anyi ambaye analo eneo la siri kwa ajiri ya kufanyia shughuli zake haramu.
Inspekta Kobo akaumia zaidi kwa sababu alikuwa anakwenda kumweka Koplo Zubeda na maaskari aliowaweka kumlinda matatani.
Wote hawa watahesabika kuwa ni chama kimoja cha kimafia na wataminywa kama alivyominywa yeye hadi kufikia hapo alipo.
Akaunganisha meno yake kwa uchungu mkubwa.
"Tunaenda moja kwa moja hadi katika nyumba hii. Ukithubutu kutudanganya utajutia uongo wako" Akachimbwa mkwara, akamtazama yule bwana kwa jicho kali, akajilaumu sana kwa sababu alikuwa na pingu, vinginevyo angefanya shambulizi kwake.
Hakupendelea masuala ya kuchimbwa mkwara!
Inspekta Kobo akawaelekeza nyumba ile inapopatikana, na hata asingewaelekeza bado kuna namba ya nyumba iliorodheshwa katika ile mikataba.
Bila kusahau kiherehere cha mmiliki wa nyumba ile kuweka nambari yake sahihi kabisa ya simu ya mkononi na ile ya ofisi.
Wakatoweka kuelekea nyumbani kwa Zubeda
 
RIWAYA: KONSTEBO NGUZU
MAANDISHI YA: George Iron Mosenya
SEHEMU YA KUMI NA TISA

ZUBEDA hakuamini macho yake pindi alipomshuhudia inspekta Kobo akishushwa garini huku akiwa hajiwezi walau kutembea, nguo yake kwa mbali kabisa ilionekana kumpwaya, na ilikuwa imefubaa huku mabakamabaka yaliyoashiria kugandiana kwa damu yalionekana.
Donge la uchungu likamkaba kooni, akajikuta yungali katika mfadhaiko mkubwa sana.
Hakujua ni kwanini Kobo yu katika hali ile lakini kichwani aliitabiri kuwa haikuwa ya heri hata kidogo.
"Martin...... Inspekta Kobo..." Alimwita kutoka pale alipokuwa ameinama bafuni.
Martin akajikuta akisimama wima na hapo akawa amejitonesha mbavu zilizokuwa katika maumivu makali.
Hakujikunja tena, akanyoosha shingo akakiona kile ambacho Zubeda alikuwa anakiona.
Mpango huu ulikuwa maridhawa kabisa.
"Hatuchomoki!" Zubeda alijikuta akitokwa na kauli ile ya kukata tamaa.
Kauli ile haikuelea sana hewani kabla mlipuko mkubwa haujasikika na palepale askari wawili walio katika sare wakaanguka chini.
Mmoja aliyekuwa amemshika Kobo ili aweze kutembea alimwachia na Kobo akatua chini mzimamzima.
Akatulia!
Hapoikazuka vita mpya, Nguzu na Zubeda wakashindwa kuelewa hii vita inahusisha pande ngapi.
Wakati wanaamini kuwa ni pande mbili pekee sasa wanashangaa kuwa wao hawahusishwi na wakati huohuo vita inaendelea.
Milio ya risasi za kuviziana ikaendelea huku askari wakipokea amri kalikali kutoka kwa kiongozi wao.
Mambo yalikuwa magumu haswa!
Asakari walikuwa wamepagawa, ni kama walikuwa hawajatarajia upinzani wa aina ile kutoka katika nyumba ile aliyokuwa akiishi Zubeda.
_______
HAKUWA katika mavazi yake yaliyowatisha wengi pindi walipomuona, hakuwa katika kiti chake cha kuzunguka huku akipokea taarifa zilizopaswa kumfikia yeye na kisha kutoa maamuzi.
Hakuwa katika nafasi yake ya kuwasiliana na raisi wa jamuhuri wa muungano.
Alikuwa katika fulana yake pamoja na bukta laini, na alikuwa chumbani kwake.
Vyeo vyote aliamua kuviweka kando.
Alichoingia nacho pale chumbani ni thamani ya urafiki.
Hakuwa na roho mbaya, na hilo alilitambua vyema bali alikuwa ni mtu anayesimamia haki na usawa.
Ukimwona ana roho mbaya kwa sababu tu amekushinda kwa kuusema ukweli basi alikuwa tayari kuonekana hivyo.
Aliijua mipaka yake vyema, hakuwa shabiki wa mateso wala vifo vya hovyohovyo.
Alikuwa na weledi wa kutosha na hii haikuwashangaza wenzake baada ya kusikia jina lake likitajwa kuwa atakuwa mkuu wa majeshi ya polisi.
Hata yeye hakushangaa, maana hakupewa cheo kile kwa bahati mbaya.
Alistahili!
Sasa alikuwa hayafikirii yote haya, alikuwa akimfikiria Kobo, ambaye alitokea kuwa rafiki yake sana mpaka mtafaruku ulivyokuja kuwaweka mbali kidogo kisha madaraka yakahakikisha wapo mbali kabisa.
Kwa kufumba ama kufumbua macho IGP hakuacha kuiona sura ya Kobo ikiitaka huruma yake, akayakumbuka maneno ya Kobo juu ya mkewe ambaye yu katika kuzimia.
"Nampenda sana mke wangu, ninapaswa kumuomba msamaha. Kama haitafaa mimi kubaki huru nakusihi rafiki yangu na mkuu wangu nifanyie upendeleo nisining'inie katika kitanzi kabla mke wangu hajazinduka."
Maneno haya yalimuumiza mno, akajaribu kuelekeza macho huku na kule ili asahau kuhusu Kobo lakini akajikuta akilitazama tukio la Kobo kujitoa muhanga na kumsukuma kando ili asipatwe na risasi iliyomkusudia.
Akajikaza hisia zisimwendeshe lakini chozi likamsaliti.
Akajikuta analia!
Akayakumbuka maneno makali ya Kobo juu yake alipomwambia kuhusu pambazuko baya kupindukia.
"Jitazame yawezekana pambazuko hili likakuandama wewe pindi utakapogundua kuwa sikuwa nyuma ya maovu haya."
IGP akasimama na kujifuta machozi pamoja na jasho lililoanza kumtoka.
Akachukua simu yake na kumpigia msaidizi wake, ambaye pia alikuwa ni rafikii yake nje ya madaraka hayo.
Akajaribu kumweleza kwa kifupi, akaeleweka na hatimaye wakachukua maamuzi ya kutuma watu watatu wa ziada katika tukio hili kutazama jinsi linavyokwenda.
Walikuwa ni vijana wanaoaminika sana kiuwezo katika mapambano na pia katika umakini.
Walau IGP aliweza kulala vyema baada ya kufanya hatua za mwisho kabisa za kutambua ikiwa Kobo anastahili jela ama la?
Majira ya saa kumi jioni alishtuliwa na simu yake ya mkononi.
Ni nambari aliyompatia msaidizi wake ili lolote litakalotokea waweze kupeana taarifa.
Akaipokea upesi ile simu.
"KIjana mmoja ameuwawa na mwingine amejeruhiwa begani." Taarifa ile ilimtisha mno IGP.
Alitambua kuwa jambo hili lina uzito lakini hakukadiria uzito ule kufikia huku kwa vijana ngangari kama wale kutetemeshwa.
Akamsihi aongeze vijana na amri iwe moja tu, warejee na majibu.
"Kiongozi kuna kitu kingine cha ziada." Alisema kisha akamwacha IGP apumue kidogo.
"Ile sauti uliyoniambia imesikika tena. 'SHUSHA MBUYU KUNA NYOKA..."
"Ni sauti ya nani?" Aliuliza kwa utulivu wa hali ya juu.
"Aliyeisikia ni marehemu tayari. Lakini ni mmoja kati ya timu uliyoipa dhamana ya kwenda kuikagua nyumba ya Kobo."
"Na ni nani anayeshambulia ikiwa sio hao wapekuzi?"
"Kuna safu nyingine kutoka katika kona za nyumba waliyoenda kuipekua. Kuna vita ya pande zaidi ya mbili mkuu."
"Ongeza vijana, fanya wanane. Wahakikishe wanaleta majibu."
"Sawa. Afande..." Alijibu na kukata simu.
Hali ilikuwa mbaya tayari.
_____
INSPEKTA KOBO alianguka mwili wote lakini hakuzimika macho yake. Alitulia kama aliyekwishapoteza uhai tayari.
Aliendelea kutazama mashambulizi yalivyokuwa ya kutisha, kuna jambo alikuwa akilisoma.
Wapinzani waliokuwa wamejificha katika kuta na dari walikuwa wakifanya mashambulizi ya akili sana huku hawa waliomsindikiza kukagua nyumba walikuwa wengi lakini bure kabisa.
Walikuwa ni watu wanaotii sheria tu, wakiambiwa waachie risasi wanamimimina hovyo bila kumaanisha kudhuru!
Akiwa palepale alizungusha macho yake huku na kule, na mara akatua katika madirisha ya nyumba ile.
Akaona kama kivuli kikivuka upesi kwa kuinama chini.
Kivuli kile alikuwa amekizoea sana, kama kisingekuwa chenyewe basi kingekuwa ni pacha ya kile alichokizoea.
Zubeda! Inspekta akatokwa na jina lile huku akiwa bado amenasa pale chini, kulia kwake pakiwa na mwili wa askari aliyetokwa na uhai tayari.
Kwa umakini wa hali ya juu akajisogeza mita kadhaa taratibu hadi akawa jirani kabisa na yule askari. Muda wote macho yake yaliwatazama wale washambuliaji waliojificha.
Alishagundua tayari kuwa washambuliaji walikuwa wanaye mdunguaji wao na alijua vyema kazi ya kudungua maana alikuwa hakosi kila akishambulia.
Faida kuu kwa Kobo ni kwamba huo ulikuwa moja kati ya mchezo wake uliompandisha cheo upesi na mchezo huohuo ulikuwa umemuingiza matatani.
Shabaha!
Kobo akainyakua silaha ya askari mfu pale chini.
Akatabasamu baada ya kuitambua kuwa ni silaha aipendayo.
Akatulia tena kama mfu huku akiangalia ni wapi anapoweza kuanza kushambulia. Alitambuwa wazi kuwa hawezi kushambulia kwa muda mrefu kabla nguvu hazijamwisha na pia kuchabangwa risasi na kupoteza maisha hivyo alihitaji akifanya shambulizi liwe kubwa na lenye maana kubwa.
Akiwa bado katika kuliandaa shambulizi aliisikia simu ya upepo jirani na lile gari waliloingia nalo pale ikiunguruma maneno kadhaa ya kusihi.
Hakuwa na uhakika kama msikilizaji wa ile simu aliamua tu asiijibu ama simu ilikuwa haina msikilizaji.
"Shusha mbuyu kuna nyoka. Shusha sasa hivi ova!"
Sauti ile ilitokea nyuma ya gari ambalo lilikuwa limeharibika vibaya kutokana na milipuko ya risasi.
Mapigo ya moyo yakaongeza kasi, umakini ukatoweka akataka kukurupuka lakini alipokumbuka kuhusu 'sniper' aliyejificha mahali fulani aliendelea kutulia.
Punde baada ya amri ile kutoka mita kadhaa hadi kuufikia ukuta mrefu kiasi ulioizunguka nyumba ile akasikia kishindo kikali, na kisha kikasikika kilio.
Kuna mwanaume alikuwa amemezeshwa risasi tayari. Alikisia
Huyu ni nani? alijiuliza kisha akajigeuza na kuilalia ile bunduki na kuendelea kubaki kana kwamba hana uhai.
Alikuwa na uhakika wote kuwa alichokisikia katika simu ni sauti ileile iliyomkosesha shabaha na utulivu mjini Shinyanga na kisha kumletea majanga.
Lakini safari hii ilisikika katika simu ya upepo. Hakufahamu fika ni nani mzungumzaji na alikuwa upande upi.
Na punde baada ya kauli ile shambulizi likafanyika.
Ni nani huyu? likabaki kuwa swali zito kwa Kobo.
Tukio la Kobo kuichukua bunduki hadi kuilalia lilikuwa likifuatiliwa vyema na mdomo wa bunduki iliyokuwa tayari kukohoa risasi.
Kobo hakujua, aliamini kuwa umakini wake ulikuwa wa kiwango cha juu zaidi.
Baada ya shambulizi lile akazisikia hatua zikisogea kwa kujiamini kuja mahali alipokuwa.
Akazivuta pumzi zake kisha akaanza kuzitoa nje taratibu kabisa.
Akakisikia kiatu kigumu kikimkanyaga mguuni.
"Huyu tayari... hamna kitu humu." bwana aliyekuwa anamkanyaga akatoa jibu lile.
"Chapa risasi kabisa kujihakikishia, hakawii kuwa hai akatuharibia." Iliamrisha sauti nyingine kwa ukali iliyotawaliwa na madaraka.
Kobo akaanza kuweweseka pale chini, alijilazimisha kuendelea kutulia kana kwamba ni mfu lakini kitendo cha kusikia kuwa anapaswa kuchapawa risasi ili kuhakikisha juu ya uzima ama kifo chake, hii ilikuwa ni sahihihi mbaya kabisa.
Kobo hakumsikia yule aliyeamriwa akijibu kitu chochote, alishindwa kuelewa nini maana ya kimya kile.
Hakutaka kucheza bahati nasibu ya 'nitakufa ama wataniacha'
Akaamua kutumia nguvu zake za mwisho na njia pekee iliyosalia katika kujitetea.
Akageuka upesi mtutu wa bunduki katika mikono yake tayari kwa kufyatua.
Lakini hakuwa na mwendokasi wake wa zamani, Kobo huyu alikuwa mgonjwa, mzito, asiyeweza kuona vyema.
Hakuwa Kobo anayetisha tena.
Inspekta Kobo alikuwa amechelewa tayari....
 
RIWAYA: KONSTEBO NGUZU
MAANDISHI YA George Iron Mosenya

"Nayaweza yote kwa Imani na jitihada"

SEHEMU YA ISHIRINI

ILIPOISHIA

Inspekta Kobo yu matatani, ana kwa ana na mtutu wa bunduki. Hesabu zake zimeenda ndivyo sivyo na sasa kivumbi kimemgeukia.

ENDELEA!!

Kama alivyoona ndivyo ilivyotokea, yule bwana akafyatua risasi.
Kobo hakutarajia kama angepata nafasi ya kusikia risasi ile ikivuma pembezoni mwa sikio lake.
Lakini hivyo ndivyo ilivyokuwa.
Shabaha iliyumba malikiti.
Kobo akapata muda wa kufumbua ili atazame kama ataweza kubiringita tena ili akwepe kwa mara nyingine tena.
Akayahimiza macho yake kutazama....
Macho yakakutana na kitu cha kutisha, haikuwa risasi ya kawaida... hii ya sasa asingeweza kuikwepa asilani.
Ilikuwa pana sana, hata kama angebiringita kwa kasi kuu bado asingeweza kujinasua.
Inspekta Kobo akasalimu amri kwa kuitanguliza mikono yake kukabiliana na kitu kile kikubwa.
Kilipomkaribia zaidi akayafumba macho yake.
Kikatua juu yake, upepo ukakata!
Kobo akarejea katika ulimwengu wa waliopoteza fahamu wasijue namna ya kuzitafuta.

__________

MIILI miwili ilikuwa imebebana bila kukusudia, yote isiyojiweza na bila budi kujibweteka mwili mmoja juu ya mwingine.
Miili hii ilitazamwa kutokea mbali na vikundi viwili visivyokuwa na majina rasmi ya kuvitambulisha.
Kukosa majina hakukumaanisha ule uwepo ni batili.
"Unahisi bado anapumua yule?" Sauti dadisi ya Zubeda ilimuuliza Nguzu.
"Uhakika pekee ninaoweza kuuthibitisha ni kwamba yule bazazi nimemfyatua barabara katika chembe ya moyo wake..." Alijibu huku akiwa bado na umakini wa hali ya juu.

Kundi la pili lilikuwa katika mfadhaiko, wakati likiamini kuwa limeunyakua ushindi na kilichosalia ni kuvikwa taji mara shambulizi linatoka wasipopajua na kumsambaratisha mwenzao aliyekuwa anangojewa waweze kuondoka eneo lile.

Makundi yote mawili yalibaki katika tahadhari hakuna aliyekuwa tayari kwenda kuwatenganisha wawili wale waliolaliana.
Mmoja akiwa ni mwili na mwenza wake akiwa ni mwili na roho pamoja na fahamu zilizokwenda likizo isiyokuwa na muda maalumu.

"Martin.... bila kujalisha kama mzee Kobo atainuka ama la, bila kujali kama tutabaki hai ama la. Naomba unisamehe mimi kwa yote yaliyotokea" Sauti tulivu ya Zubeda ilipenya katika masikio ya Martin Nguzu.
Hakuitoa silaha yake katika lindo lake katika watu wale wawili waliolaliana mmoja akiwa ni Inspekta Kobo.
"Unavyozungumzia kuwa hai ama la kana kwamba ni pipi ambayo unaweza ukaamua kuimung'unga ama la na isikupunguzie lolote. Uhai unayo thamani kubwa sana usiuongelee kijuu juu hivyo" Akamjibu kwa kumnanga.
Koplo Zubeda akabaki kimya huku hatia ikimsulubu na kujiona yu mkosaji mkubwa sana.
Hakukumbuka kujiuliza ni lipi basi kosa lake?

KUTOKEA upande wa pili, tumaini la ghafla katika pori la mfadhaiko liliibuka, aliyeshuhudia akawasihi na wenzake nao waone.
"Oya...yupo hai aisee... namuona anatikisika" Alisema na kuwavuta wenzake kutazama kwa makini, kweli mwenzao alikuwa anajitikisa.
Ile hulka ya wanadamu waonapo jambo wasilolitarajia hujikuta wakiisahau misingi yao yote na kujikuta katika mkumbo wa liwalo na liwe, haikuwa upande huu badala yake ilikuwa upande wa pili.
Zubeda anayesukumwa na hatia ya kupendwa kwa dhati kisha kuja kumsaliti Inspekta Kobo na hatimaye kumweka katika kitanzi kile ilikuwa inamponza.
Konstebo Nguzu naye alihitaji sana kujua ni nini hatma ya Kobo pamoja na makundi yanayoshambulia yana nia gani.
Hakuamini hata kidogo kuwa yawezekana kabisa kuwa eti chanzo ni yeye tu hadi haya yote yanatokea.
Kama ni yeye kwanini wahukumiwe hata wasiokuwa watu wa ukoo wake?
Wakati akiwaza na kuwazua akaikumbuka sura tulivu ya Kobo iliyojaa hekima na busara siku aliyomuita na kumsihi aachane na Zubeda wake!
Huruma kuu ikamvamia.
Hali hizi ziliwafanya wasisimke walipoona ile miili pale chini ikijitikisa.
Nguzu akamuhakikishia Zubeda kuwa aliyejitikisa ni Kobo si yule hayawani aliyejaribu kumfyatua.
Zubeda hakuamini upesi, Nguzu akajitoa muhanga kwenda kumwokoa Kobo, huku nyuma shughuli ya kulinda usalama wake akaiacha mikononi mwa Zubeda.
"Kiumbe yeyote atakayejaribu kunidhuru, fyatua usifikirie mara mbilimbili. Ule muda utakaotumia kufikiri nd'o muda ambao macho yako yatakishuhudia kifo changu. Hiki cha sasa kitakuwa kifo taslimu." Nguzu alimweleza Zubeda.
Kisha akamkumbatia kwa nguvu sana, akamtazama machoni na kuzungumza kwa sauti tulivu.
"Naitwa Martin Ngengekuzenza Nguzu. Jina langu lina maana kubwa kulikoni uhai wangu... kwa lolote lile nikianguka naomba nifukiwe kwa jina hilo." Akamaliza na kumbusu Zubeda katika papi za midomo yake.
Akaondoka akimwacha Zubeda akipambana machozi yasiyazibe macho yake.
Alihisi lile ni busu na kumbatizi la mwisho kutoka kwa kijana yule machachari.
Umakini ukarejea baada ya Konstebo Nguzu kuingia ukumbi wa vita, Zubeda askari mkakamavu akaishikilia vyema silaha yake, akavuta pumzi na kushusha akajiandaa kukabili kwa lolote kama alivyoelekezwa.
Umbali wa kutoka mlangoni hadi ulipokuwa mwili wa Kobo haukuwa mita nyingi sana, lakini ilikuwa ni zaidi ya kilometa kadhaa kwa Nguzu kutokana na kutokuwa na uhakika ni wapi anaweza kuwepo adui awezaye kuitoa roho yake mara moja.
Akapiga hatua huku uoga ukishamiri katika moyo wake, alijitia ujasiri kwa maneno aliyoelezwa na mzee Majenga kuwa hatakufa kwa sababu mzimu wa babu yake unaishi naye mpaka atakapoitimiza azma yake.
Hatua takribani kama tano kabla hajaufikia ule mzoga juu ya mwili. Kilio kikubwa kikasikika kutokea katika dirisha ambalo alibaki Zubeda kama mlinzi wake wakati akielekea kumkomboa Kobo.
Upesi Nguzu akaiweka vyema silaha yake lakini hakujua ni wapi afyatue kabla hajaisikia sauti kali nyuma yake ikimwamuru kutulia kama alivyo.
Nguzu alikuwa mikononi mwa watu wabaya!
Nini kimejiri kwa Zubeda?? alibaki akijiuliza wakati huu ambapo alimuhitaji sana mwanamama yule ili kuweza kumkomboa.
Kimya! hapakuwa na shambulizi lolote la kumkomboa.
"Taratibu kabisa angusha silaha yako chini, bila kuinama walau sentimita moja" Sauti ikachimba mkwara zaidi.
Nguzu hakusubiri onyo la pili akaiachia bastola yake itue chini naye abaki na Mungu pekee kama mlinzi wake wa haja.
"Wananiua wapuuzi!" alijisemea
"Sogea mbele kwa hatua za taratibu kabisa. Bila shaka sina haja ya kukumbusha kuwa ukifanya upuuzi wowote ule hautakumbuka chanzo cha kifo chako...." sauti ile tulivu inayojiamini iloiendelea kumwongoza Nguzu.
Nguzu akatii!
Alikuwa kama hayawani ama zuzu asiyejua 'a' wala 'ba'. Kifo pekee nd'o kitu ambacho aliwaza kwa wakati huo.
"Shusha mbuyu mwamba...." Sauti tofauti na ile iliyokuwa inamwongoza ilizungumza kwa kukaripia na kuonyesha uharaka.
Mbuyu? Nguzu akajiuliza asijue ni kitu gani kimemaanishwa katika kauli ile tata.
Hakuwa tayari kuuwawa namna ile bila kuimaliza kazi yake, lakini pia hakuwa walau na akili ya ziada ya kujiokoa.
Utajiokoa vipi ungali jirani na mdomo wa bunduki usiokuwa na huruma ukifunguliwa?
"Mpigie tajiri..." Sauti iliyokuwa ya kwanza kumtetemesha Nguzu ilizungumza.
Baada ya sekunde chache, mazungumzo yalisikika upande uliosikika zaidi ulikuwa upande wa kwanza huku aliyepigiwa simu akisikika kwa mbali sana.
Simu haikukatwa iliachwa hewani na hapo Nguzu akarushiwa swali.
"Unaitwa nani? na upo hapa kwa shughuli gani?"
Nguzu akafikiria kuhusu kuongopa kuhusu jina lake, lakini akachagua kucheza karata nyingine.
"Naitwa Martin, nipo hapa kwa ...."
"Martin nani?" Swali lilitupwa, hadi sasa alikuwa hajaziona nyuso za maadui zake.
"Martin Nguzu!" Akamalizia.
"Acha upuuzi, hatuna muda wa kupoteza," alijibu kwa hasira kisha akarejea katika simu yake, "Tajiri... huyu mjinga anasema anaitwa Martin Nguzu. Hana faida kwetu..."
"Naitwa Martin, Konstebo Martin Nguzu. Sijawahi kufa lakini nakijua kifo. Jaribuni kuniua mara ya pili huenda nikakijua kifo" Nguzu akapigilia hofu na utata mwingine. Alikuwa ameupata ujasiri wa hali ya juu sana.
Wale mabwana wawili hawakuelewa ni kipi anachojiamini angali hana silaha na wakiamua ni sekunde moja tu wanammaliza.
Mazungumzo katika simu yakaendelea huku akibaini sasa kuwa mpiga simu alimuhitaji akiwa hai. Lakini hilo si pekee lililomjengea ujasiri.
Kuna jambo la ziada ambalo lilihesabika kwa sekunde kadhaa kabla halijabadilika na kuwa kindumbwendumbwe!
Ilikuwa ghafla sana, Nguzu akaruka upande wa kushoto bila wale watu kumtarajia kama atafanya hivyo.
Palepale milipuko miwili ya risasi ikasikika.
Mayowe ya hofu na maumivu yakasikika.

"Usithubutu walau kujitikisa, maana nitafyatua jicho lako badala ya bega!" Sauti iliyoongea kwa tabu kabisa ilitoa maelekezo.
Bwana aliyekuwa anazungumza na simu akabaki kutulia tuli asiamini kilichokuwa kinatokea.
Inspekta Kobo kutoka katika usingizi wa kifo alikuwa amechota medali zake za ushujaa palepale chini.
Nguzu pekee ndiye aliyeutambua uhai wake, na aliamua kumuamini walipozungumza kwa ishara za macho.
Ishara ambazo ni wao pekee wangeweza kuelewana kwa sababu wamepitia mafunzo ya kijeshi.
Nguzu akajitokeza na kuiwahi ile silaha ambayo ilimponyoka yule aliyesambaratishwa na Kobo kwa shabaha moja iliyojikita katika kifua chake moja kwa moja.

"Nahitaji ujibu swali uliloniuliza hapo kabla. Ni nini unafanya hapa na unafanya kwa manufaa ya nani? Niko tofauti kidogo na wewe... sichimbi mkwara huwa natenda. Ukichelewa kunijibu nakuvunja miguu....." Nguzu akiwa anatazama na bwana yule aliyepagawa alizungumza.
Yule bwana akapagawa asiamini anaonana ana kwa ana na Kontebo Martin Nguzu ambaye wanaamini kuwa walimteketeza ndani ya nyumba.
Hakuwa na budi kujieleza vyema kabisa.
Nguzu akashtuka jina la muhusika wa haya lilipotajwa.
Lilikuwa jina refu lakini ubini wa 'KAZEZE' ukamwacha katika namna ya kupigwa butwaa.
Jina ambalo lipo katika kitabu cha babu yake, mzee Florian Ngengekuzenza Nguzu, jina lililosheheni chuki, visasi na unyanyasaji.
Jina hili linasikika tena katika maisha yake.
"Ina maana Joseph Kazeze alikiacha kisasi chake kirithiwe na watoto wake ama?" Nguzu alijikuta akiuliza kwa sauti, lakini asipate mtu sahihi wa kumjibu.
"Zu...Zubeda yupo wapi" Inspekta Kobo akiwa ameketi chini aliuliza kwa sauti ya chini sana, bila shaka alikuwa katika maumivu bado.
Swali lile likamshtua sana Nguzu, alikuwa amesahau kabisa kuwa kuna mlipuko ulikuwa umesikika kabla hajadhibitiwa na mabwana wale waliodai kuwa walikuwa wameagizwa na mkuu wa majeshi mstaafu, Jeremiah Stamford Kazeze.
Kukosa kule utulivu kukaondoka na umakini wake.
Yule mtumwa akamvamia Nguzu upesi na teke kali ambalo liliiondoa silaha yake mkononi.
Akarusha teke la pili ambalo lilielekea kupasua fuvu la kichwa cha Nguzu. Nguzu akawahi kuinama.
Wakati anajiandaa kumkabili akajikuta akikabiliana na madonge ya damu.
Kobo alikuwa amejipima tena umakini wake kama upo sawa.
"Usingemuua Inspekta..."
"Angekuua wewe.... amepitia mafunzo ambayo wewe hujawahi hata kuyaona kwenye luninga.... hata hivyo sijamuua labda aamue kufa mwenyewe tu..."
Hatimaye Inspekta alisimama kwa tabu, wakati huo Nguzu alikuwa ametangulia kwenda kuitambua hali ya afya ya Zubeda ambaye bila shaka alishambuliwa.
Hakika alikuwa amepoteza fahamu, risasi ilikuwa imemkwangua begani na kumtupa ukutani.
Halikuwa jeraha kubwa sana, hata alivyoshtuliwa kwa kumwagiwa maji ilikuwa rahisi kwake kusimama na kutambua kila kilichokuwa kinaendelea.
Kigiza kilikuwa kinaanza kuingia wakati watatu hawa wakiwa wamepata fursa ya kuwa mbali na ile nyumba na walikuwa wameweza kujadili kwa ufupi sana juu ya kisa hiki.
Hakuna aliyegusia suala la mapenzi ya kuchangia, walitazama zaidi uhai na amani yao.
Inspekta akashauri wafanye mchakato wa kuwasiliana na IGP waweze kuupata msaada wa upesi sana dhidi ya Kazeze IGP mstaafu waliyeamini fika kuwa yupo nyuma ya yote haya.
Wakati wao wanafikiria namna ya kuwasiliana na IGP.... ni wakati huohuo IGP mstaafu Kazeze alikuwa yu njiani kuelekea nyumbani kwa IGP.
 
RIWAYA: KONSTEBO NGUZU
MAANDISHI YA: George Iron Mosenya

SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA

JOTORIDI lilikuwa la wastani lakini hiyo ilikuwa kwa wale wenye amani pekee.
Mashaka ya mwandishi wa habari, Juma Kihwele 'kimbelembele' yalisababisha mwili wake utokwe jasho mara zote zlizokuwa akifikiria ni mbinu gani za ziada atazitumia kuweza kuipata tena amani yake na uhuru.
Hapo kabla shuleni alikuwa nguli wa kusaliti wenzake linapokuja suala la mgomo. Hakuwa mtu anayeweza kupigana, kila penye shari yeye alijiweka kando na alikuwa shahidi wa kwanza ulipohitajika ushahidi wa nani ameanzisha ugomvi.
Hali hii ilifanya walimu wampende lakini alichukiwa na wanafunzi.
Mbaya zaidi darasani alikuwa anaongoza, chukia usichukie nd'o ilibaki hivyo.
Baadhi ya wanafunzi ambao walijikuta matatani kutokana na ushahidi wa Juma Kihwele waliishia kumwekea viapo ambavyo kwa macho ya kibinadamu ilionekana wazi kuwa ni maneno ya mkosaji.
Walimweleza kuwa ipo siku atajutia uoga wake, kiherehere chake na hapohapo akili zake za darasani hazitamwokoa.
Aliishia kucheka na kuendelea kuhsika namba za juu darasani.
Baada ya miaka mingi kupita Juma amejichanganya na kujiingiza katika 'dili' alilolichukulia kuwa ni pesa nyepesi, sasa yu mikononi mwa watu ambao ili uone jino lake moja ni pale tu atakapokuwaanapiga mwayo. Kinyume na hapo zilikuwa ni ndita na lugha za ukali kila mara.
Juma Kihwele analazimishwa aelezee ana ubini gani na Martin Nguzu ambaye aliendelea kutambulika kama hayati Konstebo Martin Nguzu.
Juma alikuwa ametema kila alichokuwa anakitambua lakini bado hakuonekana kama amesema lolote, hakuwa amepigwa sana, vibao kadhaa na mateke yasiyodhamiria kuvunja lakini kipigo hicho kwa Juma alijihisi anapaswa kuorodheshwa katika kitabu cha rekodi za dunia kama mwanadamu aliyewahi kupigwa kupita wote duniani na bado anapumua.
Juma hakujua maana halisi ya kipigo.
Maelezo ya Juma Kihwele yakalileta mezani jina la Inspekta Kobo na Koplo Zubeda.
Juma akamtaja Zubeda kuwa anajihusisha kimapenzi na Inspekta Kobo na hapohapo alikuwa anajihusisha na Konstebo Nguzu.
Jibu hili likaongeza umakini kwa waliotumwa kumuhoji, majibu yakatumwa na kufika sehemu husika.
IGP Mstaafu Jeremia Kazeze akayatazama majina yale kama maadui zake, yeyote aliye karibu na Nguzu kwake alikuwa ni adui asiyefaa kuishi.
Sumu aliyomezeshwa na babu yake na kisha baba yake ilikuwa imekolea na ilikuwa muda wa kuitema.
lakini urithi si kwa magonjwa tu, hata nidhamu ya akili unaweza ukarithi.
Hayati Florian Ngengekuzenza Nguzu wakati anamsimulia Majenga kwa ajili ya kuandika kumbukumbu ya kizazi chake alimuhesabu Joseph kazeze (babu wa Jeremiah) kama mshamba anayetumia cheo chake kijinga. Ngengekuzenza alijihesabu kama mshindi kwa vita vyote dhidi ya Joseph Kazeze, na kweli alimtandika ipasavyo kwa mbinu chache tu ambazo kwa Joseph Kazeze zilikuwa ngeni na zilizosheheni suluba kubwa.
Sasa wawili hawa walikuwa wamepumzika tayari katika nyumba zao za milele.
Ngengekuzenza Nguzu akijitoa uhai kwa kujinyonga huku Joseph Kazeze akikamilisha safari yake kwa shinikizo la damu. Shinikizo lililosababishwa na mapigo kutoka kwa Ngengekuzenza Nguzu.
Chuki haikuishi katika moyo wa Konstebo Martin Nguzu na hakujua hapo kabla kuwa kuna vita mbayo haikuwahi kukamilika, lakini Jeremiah Kazeze yeye alibaki na chuki kuu.
Akafuata misingi aliyorithishwa ikiwa pamoja na mbinu za 'kikuda'za kukabiliana na adui zake.
Akavishwa cheo cha IGP na kukitumia kusulubu wowote aliodhani ni maadui.
Akamaliza muda wake huku akiwa hajakutana na jina Nguzu.
Akiwa hana cheo jina lile linamjia ghafla mezani kwake.
Vita mpya inaanza, vita mbayo haikuonekana kama inatisha.
Jeremia Kazeze anatuliza akili yake na kufikiria ni kifo gani kitamfaa zaidi Konstebo Martin Nguzu, kifo ambacho kitakuwa ni kisasi sahihi kwa yale yaliyomtokea babu yake miaka ya nyuma.
Hatimaye anamchagulia adhabu ya kuchomwa moto dunia kisha akakutane na mwingine katika safari yake nje ya dunia.
Mpango mdogo unasukwa kwa akili ileile ndogo, Nguzu anachomewa ndani ya nyumba yake.
Wakati wa utafiti wa kuzifuatilia nyendo za konstebo Nguzu. Wanapata jambo jipya, mahusiano kati ya Nguzu, Zubeda na Inspekta Kobo.
Jeremiah anachekelea na kuamua kumuuzia kesi ile Inspekta Kobo.
Oparesheni inafanyika na jalada linakaribia kufungwa.
Mwishoni mwa mchezo anatokea Juma Kimbelembele akijaribu kuandika makala juu ya yaliyotokea.
Anakuwa amenunua kesi pasi na kujua kuwa ni kesi kubwa.
Upande wa Jeremia Kazeze ukaamini fika kuwa yule bwana kuna uwezekano anafahamu ni wao wanahusika katika kuiteketeza nyumba ya Nguzu.
Upesi akaamuru kundi jingine linalomtii limfuatilie kwa ukaribu kila hatua ambayo atakuwa anapita.
Ni katika kufuatilia huku yanazuka mengine makubwa.
Sasa Juma Kimbelembele yu katika mikono yao.

Anatamani walau kupambana lakini uwezo huo hana. Amelia kama mtoto lakini haijatosha kulainisha sauti za watu wale wanaozungumza kama wauguzi wa wodi ya vichaa walioshindikana.
Kila mara wanafoka!

Ilikuwa siku nyingine tena katika mazingira yaleyale, lakini sura ngeni ilimjia.
Ilikuwa ni ngeni kwa pale ndani na sura hii ilimpa tumaini jipya kwa sababu alikuwa akiifahamu vyema.
Alikuwa ni mkuu wa jeshi la polisi mstaafu.
Jeremia Kazeze.
Juma Kihwele akajihesabia kuwa amekutana hatimaye na mtu ambaye atamuelewa na kumwokoa.
Hakujua kuwa amekutana na anayewatuma wale aliowaona kama mashetani yanayoishi.
"Haujambo?" Jeremiah aliuliza kifedhuli.
"Sija... shkamoo... sijambo.." alijiumauma katika kujibu.
"Martin Nguzu alikufa ama hakufa? na kama hakufa nataka kujua ni nani aliyehusika katika kumwokoa..." Sauti kavu ya Jeremia ilihoji.
"Sijui lolote muheshimi..." kabla hajamaliza kumjaza cheo alipokea kofi kali katika shingo yake.
Yowe la hofu likamponyoka.
"Nahitaji jibu tofauti na sijui."
"Muheshimiwa mi naapa haki ya..." Hata hii kauli pia haikumalizika kabla hajapokea kofi jingine, hili la sasa liliuchana mdomo wake.
"Umeona biblia ama msaafu humu ndani? Sihitaji viapo nahitaji majibu..."
Juma Kimbelembele sasa alikuwa amepatikana.
Alijaribu kutuliza akili yake na kuchagua jibu la kutoa lakini alihofia kuwa linaweza lisiwe na ushawishi.. Lakini ni heri kuzungumza kuliko kuwa kimya dhidi ya mtu yule aliyekuwa mbele yake.
"Nyumba iliungua mkuu, sikumuona akitoka hai. Alikufa na wanahabari waliandika..."
"Wanahabari ni akina nani hadi unawataja kama utetezi wa hayo unayosema?"
"
Kimya! hakuwa na la kujibu.
"Una uhakika alikufa?"
"Nyumba iliteketea..." alijibu kinyonge lakini unyonge wake haukumzuia Jeremia kumbutua tena, safari hii kwa kutumia mguu wake.
Juma akajikaza hakupiga kelele kubwa licha ya kuumia.
Jeremia Kazeze akatoa picha kadhaa akamtupia Juma Kihwele akawa anatazama nazo.
"Unafahamu hicho ni nini?"
"Ndio mkuu, nyumba ya hayati Nguzu baada ya kuteketea"
"Ooh! Kila mtu anajua nyumba iliteketea, sijafunga safari kutoka huko mbali kuja kupata uthibitisho kuwa nyumba iliungua..... najua kusoma na ninaona pia... nahitaji kujua wewe na Nguzu ni washirika katika ngazi ipi?"
"Wallah! naapa sina ushirika wowote na marehemu..."
"Unavyosema marehemu kama vile uliuzika mwili wake... sikiliza wewe mtoto. Kama unayaficha unayojua kuhusu Nguzu, hautajificha kuizika miili ya wapendwa wako. Kwa mkeo nitajitahidi ubaki uso pekee ili usije kugoma kuuzika mwili ukisema sio mkeo, ila hutapata hamu ya kukiuona kiwiliwili chake, na ukijitia shujaa kukiona utakuwa unakiota ndotoni kila siku na itakuwa ndoto ya kutisha..."
Akaweka kituo na kutoka nje.
Juma alipojaribu kuzungumza akaishia kujikaza asijikojolee zaidi wakati tayari keshajimwagia kojo muda mrefu tu.

______

JEREMIA KAZEZE mwenye akili kiwango cha babu yake aliona njia pekee ni kuwahi kwa IGP kwa ajili ya kujisafisha na kuyaweka sawa mazingira ikiwa tu jambo lolote litaharibika zaidi.
Aliziona dalili za kuangushwa kama alivyoangushwa babu yake zikimnyemelea....
Ilikuwa yapata majira ya saa mbili usiku.
Haukuwa utaratibu wa Kazeze kumtembelea mara kwa mara IGP, ni yeye aliyependa kutembelewa kwa sababu ya kumzidi kiumri na urithi wa tabia ya kupenda sifa za kijinga alioupata kwa babu yake.
Siku hii ilikuwa tofauti zaidi, tena saa mbili usiku.
Mbaya zaidi hakupiga simu kutoa taarifa.
Alipokelewa bila mashaka, taarifa za walinzi zikapitishwa ndani na ruhusa ikatolewa.
Kazeze akaingia kuonana na IGP.

Tofauti na nyakati nyingine walizowahi kuonana, hii ilikuwa tofauti sana. Kila mmoja alikuwa katika ulimwengu wake.
Licha ya kujilazimisha kuonenekana kuwa wapo sawa ila nafsini hali ilikuwa wazi.
Mgeni alianza kuelezea juu ya ujio wake usiku ule, akaanza kuulizia hatma ya Inspekta Kobo na sakata la kujihusisha na majambazi sugu mkoani Shinyanga.
IGP akamweleza juu juu kuwa hadi wakati huo Kobo alikuwa amekataa kukiri kuwa aliikosa shabaha ile maksudi na anaapa kuwa hajihusishi na kundi lile.
"Nawe umeamini?" Aliuliza kwa mshangao..
IGP akaduwazwa na swali lile, japokuwa haikuwa mara ya kwanza kukerwa na maswali ya yule aliyemtangulia.
Kwanini ananichimba huyu?! Alijiuliza kisha akatabasamu na kujibu, "vijana wangu wanaendelea kumuhoji. Watanipatia majibu ninawaamini sana..."
"Na unafahamu lolote kuhusu mauaji ya askari wetu mtiifu, konstebo Nguzu aliyechomewa ndani ya nyumba?"
"Naam! na nilifika eneo la tukio, vipi kuna jipya?"
"Inspekta Kobo anahusika kumteketeza, inasemekana Nguzu anajua kuhusu Inspekta Kobo kujihusisha na kundi lile, na alikuwa anakaribia kuvujisha siri.."
"Unasema Nguzu anajua kama yupo hai mkuu...."
"Aam! Nguzu alikuwa anajua..." Akarekebisha huku akijaribu kujichekesha.
"Upo ushahidi wowote wa kumweka hatiani Kobo?"
"Kuna mwandishi wa habari alishuhudia kila kitu, kuanzia muda wa kuwasili hadi muda wa tukio?"
"Aisee! aliarifiwa na nani hadi kuweza kuzijua nyendo za askari makini kama Kobo!" Alijibu IGP.
Kitendo cga Kobo kuitwa askari makini kikamkwaza Jeremia Kazeze.
"Unamuita makini na kwa maksudi kabisa ameacha kumsambaratisha jambazi sugu, jana watu nane wameuwawa huko Shinyanga, wawili kati ya hao ni askari wetu na pasi na shaka muhusika ni huyohuyo aliyeachwa apumue na Kobo. Leo hii unaendelea kumvesha nishani ya umakini? Are you damn serious brother?" Alilalama.
"Nimvishe jina gani ambalo litakuridhisha na kuyanyoosha mazungumzo yetu?" IGP akahoji, Jeremia akatambua kuwa kile ni kijembe.
hakujibu.
"Anyway, nina taarifa njema sana zinaweza kusaidia katika kuboresha hizo tuhuma" IGP akazungumza kisha akaiacha kauli ile hewani ili imuingie vyema bwana Jeremia.
Jeremia akahoji kwa kimuhemuhe.
"Ni taarifa gani mkuu..."
"Nimepigiwa simu na mtu anayedai kuwa yeye ni konstebo Martin Nguzu. Na tayari nimeagiza vijana wangu wafuatilie alipo na kumtia nguvuni, bila shaka atatusaidia sana katika kukamilisha upelelezi... tukimuunganisha na huyo mwanahabari wako, sioni Kobo anachomokea wapi...." Alimalizia huku akiwa anamtazama kwa macho ya kuibia Askari mwenzake.
Moyo wa Jeremia ulipiga kwa nguvu sana, hakuamini kile alichokuwa anakisikia, alijiona kile kikombe anachomwandalia Kobo kikigeukia upande wake ndani yake kikiwa na uji wa mto ambao anapaswa kuunywa bila kupooza.
Mbaya zaidi kile kikombe kilikuwa cha bati.
Akatamani kutoa kauli yoyote lakini kauli yenyewe ikagoma kuunganika.
Koo lilikuwa limekauka.
"Nisaidie maji ya kunywa!" Jeremia akamwomba IGP.
IGP akatabasamu kisha akaitazama meza, Jeremia alikua ana kikombe cha maji mbele yake.
Ajabu alikuwa hakioni!
"Kwani Nguzu yupo hai au?" Akatokwa na swali la kizembe.
"Kitu pekee ninachofahamu ni kwamba nyumba yake iliteketezwa, kuhusu uhai nitakuongopea,Vipi kwani?" IGP akazidi kuzungumza kwa utulivu kabisa na hapohapo akiifurahia hali ya kupagawa ya Jeremia Kazeze.
 
RIWAYA: KONSTEBO NGUZU
MAANDISHI YA: George Iron Mosenya

SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI
______
"Kwani Nguzu yupo hai au?" Akatokwa na swali la kizembe.
"Kitu pekee ninachofahamu ni kwamba nyumba yake iliteketezwa, kuhusu uhai nitakuongopea,Vipi kwani?" IGP akazidi kuzungumza kwa utulivu kabisa na hapohapo akiifurahia hali ya kupagawa ya Jeremia Kazeze.
Na hapo IGP akashuhudia tembe za jasho zikiumuka katika mgongo wa pua ya Jeremia.
Uoga!
Anaogopa nini sasa? Ina maana jamaa ana 'kamisheni' katika kutekeleza mauaji ya Nguzu?
Kwanini mtu aliyewahi kuwa na cheo cha juu kama huyu ahusike katika mpango mdogo kama ule.
Haya yalipita katika kichwa cha IGP kwa kasi kubwa.
Kwa upande wa IGP mstaafu Jeremia Kazeze alikuwa anajaribu kuutuliza muhimili wake wa kufikiri, alijiona yu katika kupagawa tayari na alihisi IGP ameanza kumgundua kuwa anapagawa.
Akajivika ukakamavu huku akijizuia asitazamane ana kwa ana na IGP kwani aliogopa kupepesda macho yake.
"Nadhani sasa mimi niende" Jeremia alizungtumza kwa kuridhika.
"Mkuu, kwa hiyo huyu Nguzu tunamfanyaje ikiwa kweli anapatikana angali hai wakati sote tunajua amepoteza maisha?" IGP akamtundika swali lililojaa maswali ndani yake.
"Nani? Nguzu...aah!" Jeremia akatetereka. Kichwani mwake akajiona yu katika kumi na nane za IGP na sasa alikuwa anajaribu kucheza naye atakavyo na ikiwa ataghafirika na kumkwatua basi uamuzi ulikuwa ni 'penati.
"Akikamatwa inabidi hapo sheria tu ichukue mkondo wake... no way out! Lazima Nguzu aadabishwe. Period!" Jeremia akajikaza kishupavu akajibu kama mtu aliyeshtuliwa toka usingizini akaulizwa moja jumlisha moja akajibu nne kwa sauti ya juu, akiamini yu sahihi
IGP akaponyokwa na tabasamu jepesi kabla hajamdhihirishia Jeremia kuwa mojawapo kati ya watu wanaoitwa mabwege basi yeye kama si kiongozi wao basi ni msaidizi.
"Sheria ya kumshtaki kwa kuchomewa nyumba ama tutamuadabisha katika 'engo' ipi afande" IGP akatupa bomu jingine dogo lenye mlipuko mkali.
Jeremia akajiona jinsi anavyodhihirisha kuwa yungali fala katika ubora wake. Na kupitia maswali yale ni namna ya kuitwa fala bila tusi hilo kutajwa.
Ilimuuma!
Hakutaka kuendelea kulithibitisha hilo mbele ya bwana yule ambaye alikuwa mdogo kwake kimri.
"Kwa hiyo unataka akikamatwa aachwe tu bila hata kusaidia upelelezi?" Akauliza kwa ghadhabu.
"Hapana mkuu, yule kukamatwa muhimu tena muhimu sana...." IGP akajibu kichangamfu kisha akamalizia, "Ishu hapa ni tunamshtaki kwa lipi? Kudanganya uma kuwa amekufa kumbe hajafa? kujichomea ndani ya nyumba au tunamshtaki kwa kuwa hai?"
Jeremia akagundua anachezewa ngoma iitwayo shere.
Ngoma wanayochezewa wajinga bila kujua wanadhihakiwa.
Akaaga na kuondoka kwa mara nyingine.

______

SAFARI ya kulifikia gari lake ilikuwa ndefu sana, Jeremiah alijiona katika akili yake anatembea kama kitoto kinachojifunza kutembea, kikijiona kinao uwezo wa kumkimbia mama yake, angali mama anapunguza mwendo maksudi ili kichukue ushindi kitoto kile.
Miguu yake ilikuwa kama inayopambana kutangulia kupiga hatua, wa kulia unataka utangulie na wa kushoto unahitaji nafasi hiyo.
Ikafikia hatua akili yake ikawqa haiwazi kitu kingine zaidi ya kuwaza namna ya kuiamuru miguu yake ipeane heshima stahiki japo kwa dakika hizo chache tu za kulifikia gari lake.
Miguu ikatii!
Akalifikia gari.
Walinzi wakamkabidhi silaha yake ambayo waliichukua kabla hajaingia ndani kwenda kuonana na IGP, akaziona saluti alizopigiwa zikiwa ni kama ishara inayochukiwa na vijana wengi wafanyiwapo.
Macho yake hayakuona saluti ya heshima bali aliwaona vijana kadhaa wakiwa wanamzomea na kumwonyeshea ishara ya kidole cha katikatika katika mpangilio wa vidole kiganjani.
Hasira zikazidi kumchemka, akapanda garini.
Akatoweka huku akikiri kuwqa katika maisha yake yote, hii ilikuwa mara yake ya kwanza kujikuta amewekwa mtu kati na siweze kujing'atua.
Aliendesha kwa mwendo wa wastani, hakuelekea nyumbani kwake na hakujali kuhusu hilo na hakufikiria walau kumpa taarifa mkewe.
Alizoea kumwendesha kama alivyokuwa na tabia ya kuendesha askari waliokuwa chini yake wakati wa cheo chake.
Kitu kama mwiba mdogo kikaichoma akili yake wakati akiendelea kuendesha gari, akawakumbuka haohao askari wenye vyeo vya chini walivyo na hatari wakipewa amri.
Akajiona jinsi watakavyomfunga pingu huku mara kwa mara wakimfokea badala ya kumwelekeza nini cha kufanya.
Wakati huo akiitwa mtuhumiwa.
Na baadaye akaziona kero za kulishwa chakula kibovu, kuhesabiwa kwa kupigwa bila sababu pamoja na kulala sehemu moja na chawa kunguni na kadhalika pindi atakapokuwa mahabusu rasmi.
Mapigo yake ya moyo yakapiga kwa nguvu zaidi, hakutaka haya yamtokee.
Lakini katika yote haya hakusita kutabasamu na kisha kutoa sauti ya chini.
"Ukoo wa Nguzu ni kiboko!"
Pongezi hizi zikamkera na kujikuta akipiga honi bila sababu zozote za msingi.
Safari yake ikaishia nyumbani kwa Veto!
Kiongozi wa kikundi cha vijana waliokuwa wakimtii, wakati na baada ya utawala wake.
Muunganiko huu ni pamoja na wale waliopewa vyema hovyohovyo bila kuwa na sifa, ama ambao watoto wao waliingizwa jeshini kwa kauli moja tu ya aliyekuwa IGP.
Jeremia Kazeze!
Wangemlipa nini zaidi ya kuwa vibaraka, wenzetu waliwaita 'puppets'.
Hakumpigia simu Veto hapo kabla, tabia ya ujivuni ilimtawala na kujiona kuwa anaweza kwenda kwa IGP bila kupiga simu, ya nini kumpigia simu Veto ambaye nd'o kwanza anapambana aweze kuupata u'inspekta?
Hakupiga!
Alifika bila kujali kuwa ule ni usiku sana, akagonga hodi mara kadhaa, hatimaye akaufungua mlango mkewe ambaye bila shaka alikuwa amelala sebuleni kwa kupitiwa na usingizi ama akimngoja mwenzi wake.
"Shkamoo shem!" Mwanadada yule alitoa salamu.
"Vipi yupo huyu?" Jeremia akaipuuza ile salamu akahoji yaliyomleta.
"Hajarudi hadi muda huu lakini niliwasiliana naye akanieleza kuwa iwe isiwe atakuja nyumbani shem" alijibu kwa nidhamu, bila shaka alikuwa akijua nguvu ya mtu aliyekuwa mbele yake.
"Alisema atakuja saa ngapi na wakati anakupigia alikuwa ameanza kuja ama?"
"Hakusema lolote shemeji... ila alini..."
"Sawa.. nitampigia simu." Akamkatisha.
"Labda ujaribu wewe, maana nimejaribu sana hapatikani, hadi nimeanza kupata mawazo. vipi kwani mbona sielewi."
"Ambacho huelewi ni kipi na ni wewe umeongea naye kwenye simu?" Akang'aka.
Mke wa Veto akawa mpole!

Wakabaki kutazamana kama kuku, kuku mmoja akiwa amechoka mwingine akiwa muoga sana.
Ukimya uliotanda kati yao ukasababisha chochote chenye kutoa sauti kiweze kusikika.
Jeremia akasikia mchakacho ndani ya nyumba.
"Upo na nani ndani?" Alihoji kama anayesuta
"Niko.. mwe.. aah! nipo na binamu yangu.."
"Binamu yako yupi?" Akahoji tena sasa akiwa amemkazia macho makali.
tayari alihisi kudanganywa.
Na hapo ikasikika sauti ya kike yenye kila dalili za kuongea kwa shida ya kukabiliwa na usingizi mkali sana.
"Nani kwani... eeh!"
Kabla sauti ile haijamalizika, Jeremia Kazeze ambaye alikuwa amerithi tabia ya kukurupuka kutoka kwa babu yake alimsukuma mke wa Veto na kuingia naye ndani kwa fujo.
Bila kutarajia akaitoa bastola yake asijue ni kwa nini alikuwa ameamua kufanya vile.
Wazo la kuwa yule mwanamke anamwongopea na Veto alikuwa yu ndani lilimfikisha hapo, akaamini kuwa Veto amenunuliwa tayari na upande mwingine.
Hivyo ilikuwa ni vita tayari.
Vita dhidi ya kijana wake mtiifu.
Giza lilikuwa limekikabili chumba, alivyoingia Jeremia mara ghafla taa ikawashwa, akababaika na kutamani angekuwa na macho memngi aweze kuona kila upande.
Mbele yake alikuwa Veto aliye hoi kabisa, kushoto alikuwa anatazamana na Inspekta Kobo ambaye alikuwa anaonyesha hali ya uchovu sana lakini anayetabasamu.
Wakati anajifikiria ni kipi anapaswa kusema akayaona macho makali ya Veto yakimulika kumaanisha kuna kitu nyuma yake, upesi akageuka na silaha yake.
Na pale akakutana na teke kali lililopiga silaha yake ikatua chini, kisha mpiga teke yule akafanya ujuzi wa ziada akazunguka na mguu uleule kisha akambamiza Jeremia katika kichwa chake.
Jeremia kazeze aliyesahau masuala ya mazoezi na kuruhusu mwili wake kuwa legevu wenye manyama uzembe alikuwa amepatikana. Lakini alijaribu naye kurusha ngumi ya hovyo, ikamkosa aliyekusudia, akayumba na kuliacha tumbo lake lililochomoza kitambi kama walivyo askari wengi wa Tanzania.
Tumbo lile likapokea tiba mbadala ya kuzuia kitambi.
Mateke mawili ya upesiupesi yakadunda katika tumbo lile.
Jeremia akatapika maji aliyokunywa nyumbani kwa IGP.
Kinywa kile kikawa kimefanya kosa la jinai kutema maji katika zulia lililokuwa na thamani ya juu, mpigaji akatokwa na ngumi nyoofu lakini ya kushtukiza ikakibamiza kile kinywa, kikaacha kutema maji kikatapika damu nzito.
Jeremia Kazeze akaanguka chini na kutulia magoti.
"Naitwa Martin, konstebo Martin Nguzu! Sikijui cheo kingine zaidi ya ukonstebo nilionao" Utambulisho ukatoka hatimaye. Huku anayejitambulisha akiwa amekunja ngumi za mikono yote miwili na mwili wake ukitetemeka sana.
Jeremia akaamini hiyo ilikuwa siku yake ya kushuhudia muujiza, anazungumza na maiti.
"Sikurithi cheo chochote kutoka kwa babu yangu nisiyermjua kwa sura wala sauti, nilirithi hiki unachokiona mbele yako mheshimiwa, sikurithi kupigiwa saluti wala kupiga saluti kinyonge.
Sikurithi roho ya kuua bila sababu na sikurithi udhaifu wa kufa kizembe.
Ninaishi katika misingi ya Florian Ngengekuzenza Nguzu, unaishi katika misingi ya Joseph Kazeze.
Babu yangu alishinda, aliniachia huu ushindi na katu hautakuja kupotea kirahisi, mliweza kuuteketeza mwili wangu lakini sio rahisi kuupoteza mzimu wa babu yangu.
Unapambana na mzimu, kama upo tayari unaweza kusimama tena ujaribu kuurushia ngumi mzimu!"
Alifoka kwa ghadhabu zote Martin Nguzu.
Jeremia Kazeze akabeua damu.
Angesema nini zaidi ya kuendelea kutema tu damu.

Baada ya Nguzu kumaliza aliyotaka kusema, akasimama Inspekta Kobo.
Pamoja na udhaifu wake uleule, hakuna aliyetarajia kuwa angeweza kuwa imara tena mpaka ambapo angepata tiba ya kutosha.
Naye akambana Jeremia Kazeze kadri alivyoweza, na hapo akataja alipo muandishi Juma Kihwele na familia yake, akalazimishwa kupiga simu na watu wale waachiwe huru mara moja.
Jeremia hakuamini hata kidogo kuwa alikuwa anachezeshwa ngoma ya namna ile na vijana wale.
Hakuwa na la kufanya akatii.
Maelezo ya ziada yakatolewa, simu ikapigwa kwa IGP kuhusu ujio wa Juma Kihwele katika himaya yake.
IGP wakati anapigiwa simu ile alikuwa tayari katika sare zake na alijisikia faraja kwenda kuimaliza vita ile angali ana nyota tele katika bega lake.

Vita ilikuwa inaelekea ukingoni kabisa, Konstebo Martin Nguzu akaingia katika chumba kimojawapo na kumkuta Koplo Zubeda akiwa katika usingizi mzito.
Akamwinamia na kuzungumza naye maneno kadhaa ambayo aliamini fika kuwa hataweza kuyasikia.
Kisha akambusu katika paji lake la uso.
Akaliendea dirisha kubwa la kioo, akaruka na kutoweka akipishana na gari kadhaa za polisi zikiwa zinalikaribia eneo lile.

Wazo la kwanza lililomuondoa ni Zubeda. Asingeweza kuendelkea kuwa naye katika mahusiano mwanamke ambaye ni usingizi wa inspekta Kobo, pia asingekuwa na amani kumwona binti yule katika mahusiano mengine hata kama ataachana na Inspektra.
Pili ni upindishaji wa sheria katika ardhi aliyokuwa ameikanyaga, masuala ya kubebana kwa sababu ya kujulikana aliyafahamu wazi kabisa.
Akakihesabu cheo nchake cha ukonstebo, cheo cha Zubeda ukoplo na Inspekta Kobo. Akajaribu kufananisha na kile cha Jeremiah aliyewahi kuwa mkuu wa majershi ya polisi IGP.
Akaamini fika kuwa lolote linaweza kutokea, aidha kuzimishwa hapohapo na kisha taarifa kubadilishwa kuwa waliuwawa wakikabiliana na polisi, ama la kubadilishiwa kesi kabisa na kuonekana walimteka Jeremia na kumtesa kesi ambayo katu isingeweza kuwaacha bila hatia.
Miaka thelathini ingewahusu pamoja na mateso makali.

Konstebo Martin Nguzu, akayaweka mapenzi kando, akautazama usalama wake.
Kubwa zaidi alikiri kuwa hakuwa yeye yule konstebo mnyonge, huyu alikuwa imara na alikuwa na kazi kubwa zaidi za kufanya kuliko kuendelea kuwapigia saluti watu kama Jeremia Kazeze.
Konstebo Martin Nguzu akazidi kukata mitaa jijini Dar es salaam, hatimaye akaipata nyumba ya kulala wageni.
Akamtazama muhudumu aliyekuwa ana mawenge ya usingizi.
Akaulizia bei ya chumba akatajiwa, akalipia na kushangaa anapewa funguo bila kusajili jina lake.
"Hee! unaniruhusu tu naingia kama unanijua vile."
"Ah! bro we kalale bwana..."
"Hapana lazima niandikishe la si hivyo nilale bure." akatilia mkazo.
Huku akiwa amekereka yule binti wa mapokezi akampatia daftari huku akihangaika kuipata kalamu.
Hatimaye Nguzu akaishika vyema kalamu, akautazama mstari wa kuandika jina, akatokwa na tabasamu la ushindi kisha akaandika kwa herufi kubwa kiasi cha kuingilia hadi mstari wa chini.
"KONSTEBO MARTIN NGUZU"
Hakujaza sehemu nyingine zilizosalia.
Akamkabidhi daftari akiwa amelifunika na kuamini fika kuwa kwa jinsi alivyoelemewa na usingizi hataweza kusoma, na hata akisoma ataambulia patupu.

Alivyokifikia chumba, akaitoa bunduki yake. Akatoa risasi na kisha akauvamia ukuta na kuandika kwa kukwangua rangi. Huku akiifurahia hali hii, alijiona hana namna nyingine ya kufanya sherehe zaidi ya hii.
Akauchubua vyema hadi ukasomea alivyotaka.
"NAITWA MARTIN, KONSTEBO MARTIN NGUZU"
Akapiga saluti na kisha akalala vyema.
Alfajiri akatoweka.
Akaelekea popote watu wanapoelekea lakini mwisho wake akiutambua yeye mwenyewe.

MWISHO
 
Niseme nini juu yako eeh@Madame S?
Sina neno jingine zaidi ya kusema
Asanteh mnoo
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom