Kolonia Santita (Dibaji)

Ushimen

JF-Expert Member
Oct 24, 2012
37,160
85,151
Kolonia Santita: Laana Ya Panthera Tigrisi ni hadithi ya kusisimua ya kijasusi na madawa ya kulevya iliyoandikwa na Enock Abiud Maregesi. Inazungumzia vita kati ya Tume ya Dunia ya Umoja wa Mataifa, ya kudhibiti madawa ya kulevya na ugaidi wa kimataifa, World Drugs Enforcement Commission (WODEC) au Tume ya Dunia; na shirika kubwa la madawa ya kulevya la Kolonia Santita (CS-14) la Kolombia na Meksiko. Inaelezea, kwa kinagaubaga, jitihada za pamoja kati ya Tume ya Dunia, Marekani na Meksiko za kuwasaka na hatimaye kuwatia nguvuni viongozi nduli wa CS-14; na kuzuia shehena (kubwa) ya madawa ya kulevya na malighafi ya nyukilia: kwenda Afrika, Asia, Amerika, Ulaya – na kung’oa mizizi ya shirika la CS-14, lote, katika nchi za Hemisifia ya Magharibi – na duniani kwa jumla.

Hiki ni kitabu cha kwanza cha aina yake cha kimataifa katika Tanzania. Lengo lake si tu kukata kiu ya wapenzi wa riwaya za kipelelezi na kufufua mwamko wa usomaji wa vitabu; ni kuleta, hali kadhalika, ufahamu na burudani ya kimataifa kwa Watanzania, Wakenya na Waganda – na jamii nzima ya Afrika ya Mashariki inayozungumza Kiswahili – na walowezi wa jamii yote ya Kiswahili duniani.

Muhtasari wa mauaji ya kinyama ya Meksiko uliotolewa na Kristoffer Balder Sortevik (Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama ya Tume ya Dunia – WODEC Intelligence Services (WIS)) kwa Rais wa Tume ya Dunia Kamishna Boidin Tony Versnick, unachochea hofu na mtafaruku mkubwa katika jamii ya vyombo vya habari na ujasusi duniani. Mauaji ya Tijuana-San Diego, ambayo Kolonia Santita imedai kuyafanya, yanachipua hasira na shinikizo kamambe kwa viongozi wa Tume ya Dunia. Dunia nzima imeghadhibika. Viongozi wa dini, viongozi wa serikali, wananchi kwa jumla – wamekasirika na kupoteza imani na Tume ya Dunia ya Umoja wa Mataifa.

Kolonia Santita si tu shabaha ya Tume ya Dunia kwa sababu ya madawa ya kulevya na maanguko ya kijamii. Ni shabaha ya Tume ya Dunia kwa sababu ya ugaidi na amani ya dunia hali kadhalika. Mauaji ya Meksiko, yaliyotokea katika mpaka wa Tijuana na San Diego kwa sababu ya uhasama wa siku nyingi wa Kolonia Santita na Guanajuato wa himaya ya Sinaloa, hayakusababishwa na husuma au mgogoro wa Sinaloa peke yake. Kilo 400 za kokeini, ambazo Kolonia Santita ilitaka kuziingiza San Diego kupitia San Ysidro lakini ikashindwa, na kilo 78 za bangi na methamphetamine ilizoziingiza San Diego kupitia Mto Tijuana, Baja California, Meksiko; na Ufuko wa Bahari wa Imperial, San Diego, California, Marekani; ndizo zilizosababisha mauaji ya kidhalimu ya Tijuana-San Diego – kwa kutupiana risasi, na silaha zingine, kati ya autodefensa (jeshi binafsi la Kolonia Santita) na polisi wa Tume ya Dunia (WPD) na maafisa wa polisi wa pande zote mbili za mpaka na sicarios (wauaji wa kulipwa) wa Guanajuato.

Ukiachilia mbali uhasama na madawa hayo hata hivyo, ambayo wengi huamini ndiyo pekee yaliyosababisha mauaji ya Meksiko, kuna kitu kingine cha hatari na kibaya zaidi kwa amani ya dunia kilichoyasababisha hali kadhalika, ambacho wengi hawajui na ambacho kwacho Tume ya Dunia 'haitaki' kushirikiana na jumuiya ya kimataifa. Kolonia Santita ina malighafi ya nyukilia, Plutonium-239, katika msitu mkubwa wa Amazoni nchini Kolombia; iliyoibwa na mwanafizikia wa Kolonia Santita (Martin Turner Smith, Ph.D.) kwa kiongozi wa Guanajuato (Roberto Mosquera Portocarrero 'El Padrino') miezi mitatu iliyopita katika jiji la New Mexico nchini Marekani.

Kiongozi wa Tume ya Dunia hajui atajieleza nini kwa Umoja wa Mataifa. Hajui atasema nini kwa wahisani wa Tume kuhusiana na ufisadi wa Kolonia Santita. Rais wa Tume ya Dunia hakuchaguliwa kuwa kitu katika Tume. Alichaguliwa kufanya kitu katika dunia. Lakini Boidin ameuangusha Umoja wa Mataifa. Licha ya kuuangusha Umoja wa Mataifa, kwa kushindwa kuleta mabadiliko katika dunia kama Rais wa Tume ya Dunia, hata hivyo, Boidin anakataa kusalimu amri kwa wahalifu wa kimataifa na kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Watu hawaheshimu wewe ni nani au unatoka wapi. Wanaheshimu nguvu ya matendo yako. New York uvumi umetapakaa kila mahali. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (mmiliki wa Tume ya Dunia) litamtengua Boidin katika wadhifa wake ndani ya siku saba asipomkamata kiongozi wa Kolonia Santita. Lakini Boidin hataruhusu hilo limtokee. Anachohitaji ni nguvu, hasa ya Baraza la Usalama UNSC. Ndoto yake ya utumishi bora na mchango wake wa amani katika dunia kama Rais wa Tume ya Dunia, haitakufa mpaka anaingia kaburini.

Kumkamata kiongozi wa Kolonia Santita ndani ya siku saba kama uvumi wa New York unavyosikika, ambaye Tume ya Dunia imekuwa ikimtafuta – bila kukoma – kwa miaka tisa, ni maajabu ya nane ya dunia! Boidin atahitaji msaada. Yeye peke yake hataweza kufurukuta, hataweza kufua dafu, hata kidogo! Sisi ya umoja si mimi. Hakuna mimi katika umoja. Kuna sisi! Bila kushirikiana na watu wengine, bila kushirikiana na mataifa ya dunia; kilichokamilika kitalazimika kuimarishwa! Kwa ukatili wa Tijuana-San Diego, mashetani ya Kibelgiji ya Boidin Versnick yamechipuka. Atapigana mpaka dakika ya mwisho; mpaka risasi ya mwisho; kutetea wadhifa, na thamani ya utu wake, na kutengeneza nafasi (nzuri) katika historia ya Tume ya Dunia na dunia kwa jumla.

Akiwa ofisini kwake Vesterbrogade Jumatano asubuhi na washauri wake wa usalama akiwayawaya, Rais wa Tume ya Dunia anaongea tena na Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (pamoja na Rais wa Marekani) na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Kisha anaongea na Waziri Mkuu wa Uingereza. Anaongea na marais wa Afrika Kusini, Ginebisau, Urusi, Meksiko na viongozi wengine wengi; hususan wahisani wa Tume ya Dunia, na kuwaahidi kusimama nyuma ya maneno yake! Kama vile wameambizana, viongozi hao wanamtaka Versnick awafanyie msaada wa kitu kimoja: avunje ngome ya Kolonia Santita, kwa gharama yoyote, ndani ya wiki moja kwa manufaa ya uanadamu.

Kujibu mapigo, na kukabiliana kikamilifu na shinikizo la kimataifa, Rais wa Tume ya Dunia analazimika kuunda timu. Anaunda timu ambayo kisheria haruhusiwi kuunda (kutokana na masharti ya WODEC-Intelligence, na mkataba wa kisheria wa kimataifa wa WODEC) lakini imembidi. Kwa kushirikiana na Kamati ya Usalama ya Tume ya Dunia na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Boidin Versnick anaunda Operation Devil Cross! Kikosi cha watu wanne hatari, mahodari wa 'kutupwa' wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Devil Cross (Vijana wa Tume) au DC au VT inakusanywa kutoka Israeli (Daniel 'Yehuda'), Tunisia (Radia 'Hosni'), Denmaki (Frederik 'Mogens') na Tanzania (John 'Murphy'). Mjumbe wa Kamati ya Usalama ya Tume ya Dunia, Balfour McMillan, Mwingereza wa Uskochi na Balozi wa zamani wa Uingereza nchini Tanzania, rafiki mkubwa wa John Murphy, anampendekeza Murphy kuwa kamanda wa Operation DC. DC inapewa jukumu kubwa: Kusimamisha usafirishaji wa tani 600 za madawa ya kulevya, kilo moja ya malighafi ya nyukilia, na silaha maelfu (hatari) ndani ya siku kumi; na kumkamata na kumpeleka nchini Marekani Kiongozi Mkuu wa Kolonia Santita, anayejulikana kwa jina moja tu la El Tigre au The Tiger – jina alilopewa na vyombo vya habari vya Amerika ya Kusini na Kaskazini.

Kwa sababu za kiusalama, DC inaundwa katika mazingira makubwa ya siri. Hakuna mtu nje ya jumuiya ya kijasusi ya Umoja wa Mataifa anajua nini kinaendelea kuhusiana na harakati za kuikabili Kolonia Santita. Versnick, na washauri wake wa usalama, anaunda kikosi cha DC kutoka EAC (Executive Action Corps); kitengo maalumu aula, cha makachero-wanajeshi-makomandoo cha Tume ya Dunia, bora kuliko mashirika mengi ya kijasusi duniani. Hiki si kitengo cha kawaida hata kidogo! Historia yake ni ya kusisimua.

Kwa sababu za kiusalama, DC inaundwa katika mazingira makubwa ya siri. Hakuna mtu nje ya jumuiya ya kijasusi ya Umoja wa Mataifa anajua nini kinaendelea kuhusiana na harakati za kuikabili Kolonia Santita. Versnick, na washauri wake wa usalama, anaunda kikosi cha DC kutoka EAC (Executive Action Corps); kitengo maalumu aula, cha makachero-wanajeshi-makomandoo cha Tume ya Dunia, bora kuliko mashirika mengi ya kijasusi duniani. Hiki si kitengo cha kawaida hata kidogo! Historia yake ni ya kusisimua.

Vijana wa Tume wa EAC: Yehuda, Hosni, Mogens na Murphy (majina bandia kwa sababu za kiusalama na urahisi wa kumbukumbu) ni mabingwa wa mabingwa wa Tume ya Dunia na mahodari wa mahodari wa Executive Action. Uwezo wao wa kijeshi (na kijasusi) ni wa kipekee. Radia Hosni na Frederik Mogens kwa mfano, wamefundishwa na majemadari wa SAS wa Uingereza. John Murphy amefundishwa na makomandoo wa Navy SEALs wa Marekani. Yehuda amefundishwa na Kidon, kitengo cha mauti na utekaji nyara cha Shirika la Kijasusi la Mossad la Israeli. Hawa, Kidon, wakikutaka; hata ujifiche wapi katika uso wa dunia hii, watakupata! Ni watu hatari kabisa, pengine kuliko wote duniani; wenye uwezo wa hali ya juu wa kijasusi, mauaji na kupigana. Hii ni mara ya kwanza wanahusishwa na operesheni za Tume ya Dunia za kiwango cha juu za HVT (High Valued Target) au STKJ (Shabaha ya Tume ya Kiwango cha Juu).

Tume ya Dunia ina kanda sita katika mabara sita ya dunia nzima. Kila kanda inaongozwa na kamishna-kiongozi (kamishna-mlezi) na mkurugenzi mkuu wa sekretarieti ya kanda ya Tume ya Dunia. Saa nane mchana, baada ya majina ya Vijana wa Tume kupendekezwa katika Chumba cha Usalama cha Tume ya Dunia huko Vesterbrogade – Copenhagen; Mkurugenzi wa WODEC-Intelligence Kristoffer Sortevik, anatuma faksi kwa makamishna-walezi – kupitia kwa wakurugenzi wao wa sekretarieti – kuwakaribisha Copenhagen kwa minajili ya kuonana na Rais wa Tume ya Dunia. Lakini kumbe Sortevik anajidanganya. Taarifa za siri za Chumba cha Usalama cha Tume ya Dunia zilishapenya (muda mrefu) 'kuta' za WODEC-Intelligence – na kusafiri mpaka kusini mwa Meksiko katika himaya ya Kolonia Santita!

El Tigre – Kiongozi wa Kolonia Santita – kipindi hicho akiwa mafichoni nchini Meksiko katika Jimbo la Oaxaca akihudhuria kikao cha dharura cha bodi ya wakurugenzi wa shirika lake la kimataifa, anapata taarifa za kuundwa kwa kikosi cha Vijana wa Tume na za wito wa haraka wa Copenhagen wa makamishna wa Tume; na mapendekezo yote ya kumkamata (yeye na wenzake) na harakati zote za Tume ya Dunia – kuzima harakati zote za Kolonia Santita, zote: kuanzia madawa mpaka mafuta ya nyukilia mpaka ukiritimba wa kokeini wa Kolombia!

Kolonia Santita (CS-14) ni shirika kubwa la madawa ya kulevya kuliko yote nchini Meksiko na Kolombia. Kiongozi wake mkuu El Tigre, ambaye Kolonia Santita humwita Panthera Tigrisi kwa sababu ya Chui wa Siberia (na The People's Don kwa sababu ya kusaidia watu ambao serikali imewasahau), ni 'mnyama' mfanyabiashara mkubwa wa madawa ya kulevya mwenye nguvu kuliko wote duniani. Kiongozi wa Kolonia Santita anatafutwa na nchi nyingi. Meksiko inamtafuta kwa sababu ya mauaji ya halaiki na umiliki wa silaha za kijeshi. Kolombia inamtafuta kwa sababu ya kulima kokeini, na kuwafadhili wanajeshi wa msituni wa Kolombia. Marekani inamtafuta kwa sababu ya kulima (na kusafirisha) kokeini, kutoka katika mashamba ya msituni ya Kolombia mpaka katika mishipa ya damu ya watoto wa Amerika. Tume ya Dunia (nchi 143) inamtafuta kwa sababu ya ugaidi na kuzorotesha afya za watu duniani kote.

Kwa sababu za kijiografia, Copenhagen iko mbele kwa masaa 9 (PST) kuilinganisha na Tijuana (kaskazini-magharibi mwa Meksiko) na masaa 7 (CST) kuilinganisha na Salina Cruz (kusini-magharibi mwa Meksiko). Mauaji ya Meksiko yametokea saa 4 usiku wa Jumanne, Copenhagen ikiwa saa 1 asubuhi Jumatano CET. Saa 5 usiku wa Jumanne, El Tigre anahamishwa (na ndege binafsi) kutoka katika milima ya Tijuana (alikokuwa amejificha) mpaka katika jumba la kifahari la Eduardo Chapa de Christopher (Mkurugenzi wa Usafirishaji wa Kolonia Santita) nje ya Salina Cruz – ambako Chui anafika saa 10 alfajiri na kuendesha kikao cha dharura cha Bodi ya Wakurugenzi ya Kolonia Santita.

Kutokana na mbinu za welekevu wa kibinadamu, Human Intelligence, Kiongozi wa CS-Copenhagen (Tawi la Kolonia Santita Skandinavia (Regner Steiner Valkendorff, 'The Storm', au 'Kimbunga')) alipata taarifa za siri za Tume ya Dunia mapema na kuzituma haraka Oaxaca kwa Mkurugenzi wa Usalama wa Kolonia Santita Gortari Manuel – kwa niaba ya El Tigre. El Tigre, katika kikao cha bodi (yeye na wenzake 20, wakiongelea usafirishaji wa madawa na malighafi ya nyukilia – na kutengeneza ajenda za mkutano wao mwingine, wa kesho, na wanasiasa wa msituni wa Kolombia Alhamisi usiku), anafurahi kupata taarifa za WODEC na kuushukuru sana uongozi wa Copenhagen (kupitia kwa tarishi aliyeziwasilisha) na kusitisha shughuli zote za kikao!

Kwa ujasusi wa Copenhagen, majasusi 16 wa kike (wa Kolonia Santita) wanatumwa haraka nchini Denmaki huko Skandinavia. Kazi yao ni kutafuta (kwa kadiri ya uwezo wao wote) taarifa kamili za kijasusi za Tume ya Dunia zinazoihusu Kolonia Santita mahususi – na picha za Vijana wa Tume kupitia kwa makamishna-walezi, watakaofika Alhamisi mjini Copenhagen kuonana na Boidin Versnick. Bila ujasusi wa picha, Gortari Manuel (na watu wake) hawatawatambua Vijana wa Tume watakapothubutu kuingia Mexico City.

Kwa maono ya Regner Steiner, Vijana wa Tume wataingia Meksiko muda wowote kuanzia Alhamisi; na operesheni yao ya kwanza itakuwa Álvaro Obregón, Mexico City, katika Makao Makuu ya Kolonia Santita. Kuilinda Meksiko, El Tigre anaandaa kikosi kingine (kipya) cha hatari cha majambazi wa kulipwa cha sicarios. Makamanda wanne wanaitwa. Wanaamrishwa na Gortari kukusanya haraka sicarios, si chini ya 400 nchi nzima, na kuwasambaza katika kila kona ya Mexico City na Salina Cruz na kuwa tayari muda wowote, kupambana na 'wanyama' wa Tume ya Dunia watakapowavamia kuanzia Alhamisi.

Meksiko ikiwa chini ya ulinzi wa sicarios na autodefensa ya Kolonia Santita Alhamisi asubuhi, makamishna wa kanda (za Tume ya Dunia) wanaingia Copenhagen kufanya kikao na Rais wa Tume ya Dunia Alhamisi jioni. Majasusi wa Kolonia Santita (majasusi 16 wa Gortari) tayari wameshaingia Skandinavia. Sasa wamejikusanya katika kambi ya CS-Copenhagen, Smallegade, Frederiksberg, wakimsubiri Kimbunga (na viongozi wengine wa CS-Copenhagen) awape taarifa za kijasusi – za pilikapilika za viongozi wa Tume na watu gani hasa wawashughulikie.

Kwa mbinu za welekevu wa kibinadamu wa ukusanyaji wa taarifa za kijasusi (HUMINT) Kimbunga anapata tena taarifa za kijasusi za Chumba cha Usalama cha Tume ya Dunia. Isipokuwa za Frederik Mogens! Nje ya kiwanda cha bia cha Carlsberg, katika kituo cha mawasiliano cha Kolonia Santita, karibu na Makao Makuu ya Tume ya Dunia, Kimbunga anachukua teksi na kumwambia dereva amkimbize (upesi) Smallegade (Frederiksberg); kusini-magharibi mwa Copenhagen – kabla makamishna wa Tume hawajatawanyika.

Majasusi 6 kati ya 16 wanakimbizwa haraka katika Uwanja wa Ndege wa Copenhagen, Kastrup, Amager. 10 wanapelekwa (arubii) Makao Makuu ya Tume ya Dunia, Vesterbrogade, kuwachunguza viongozi wa Tume na kuandaa ripoti (ya Tume ya Dunia) kwa ajili ya Kimbunga na mkurugenzi wao wa usalama Gortari Manuel. Wa Kastrup wanapewa viza na tiketi za Bama, Tanzania, Tunisia, Uingereza, Marekani na Bolivia; na picha za makamishna sita, akiwemo Kamishna Profesa Randall Buchanan Ortega (Mshauri wa Madawa wa Gavana wa Massachusetts, na Kiongozi wa Kanda ya Amerika ya Kaskazini ya Tume ya Dunia) ambaye mauaji ya Meksiko yametokea ndani ya kanda yake; na anayekwenda Meksiko kuongea na maafisa wa serikali, juu ya mipango ya Tume, na kuwatayarishia corps wa Tume (hifadhi ya muda) kabla hawajaingia nchini humo kwa 'kishindo' kikubwa.

Vijana wa Tume wa EAC: Yehuda, Hosni na Murphy, bila kujua nini kinaendelea dhidi ya maisha yao katika upande mwingine wa dunia huko Oaxaca na Mexico City nchini Meksiko, wanasafiri mpaka Copenhagen (katika mazingira ya kutatanisha) kama walivyoagizwa na makamishna-walezi wa kanda zao. Huko wanakutana na Mogens, anayekaa Copenhagen, na Rais wa Tume ya Dunia na kamati nzima ya usalama ya Tume ya Dunia – Jumamosi saa 11 alasiri. John Murphy anakabidhiwa rasmi ukamanda wa Operation Devil Cross! Operation Devil Cross inakabidhiwa rasmi majukumu ya Kolonia Santita!

Historia kwa ufupi ya Kolonia Santita haikuandikwa mpaka zaidi ya miaka kumi iliyopita katika Jimbo la Oaxaca nchini Meksiko. Desemba 1980 (miaka mitano na mwezi mmoja baada ya kuanzishwa kwa Tume ya Dunia) El Tigre na viongozi 13, wa mashirika 7 ya madawa ya kulevya ya Americas (Amerika ya Kusini na Kaskazini), waliungana katika Mkutano wa Oaxaca na kuunda La Familia (Familia) – kwa lengo la kujiimarisha kibiashara (ndani ya Americas) na kupanua wigo wa biashara yao mpaka nje ya Hemisifia ya Magharibi.

Kutawala biashara ya madawa ya dunia, La Familia ikabadilika na kuwa La Federación (Shirikisho) iliyosambaa kutoka Meksiko mpaka Australia mpaka India mpaka Afrika ya Kusini – na kuwa na nguvu kuliko Medellín ya Pablo Escobar, na Cali ya Gilberto Orejuela, na mashirika mengine mengi ya kipindi hicho katika Amerika ya Kusini na Kaskazini.

Chini ya utawala wa El Tigre kama kiongozi mkuu msaidizi, La Federación ikafungua matawi makubwa saba dunia nzima – Saldanha, Paris, Mumbai, Moscow, Miami, Bissau na Copenhagen – kwa ajili ya ugaidi, wa kimadawa (narcoterrorism), na usambazaji wa madawa duniani kote kwa niaba ya Federación.

Oktoba 1983, hata hivyo, Tume ya Dunia ilipoanza rasmi kumtafuta El Tigre na baadhi ya makamanda wake, La Federación ilisambaratika. Jeshi la Anga la Meksiko (FAM) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (PGR) vilimuua Kiongozi Mkuu wa Federación (Carlos Pulecio Alcántara) na kuwafunga makamanda wawili wa juu wa muungano wa shirika hilo (Eduardo Chapa de Christopher (Kiongozi wa Diablos de Amazonas [Mashetani wa Amazoni] ambaye baadaye alikuja kuwa Mkurugenzi wa Usafirishaji wa Kolonia Santita akiwa mmojawapo)) katika gereza la Mexico City, Reclusorio Preventivo Oriente, alikowahi kufungwa El Tigre na kutoroka katika miaka ya sabini – hivyo kuathiri (kwa kiasi kikubwa) uongozi na biashara ya Federación, hasa ya kokeini (na heroini) duniani kote.

Kurudisha imani ya wateja (na kutambulisha eksitasi na 'hielo' katika soko la dunia la Federación – na kujipanga upya) La Federación ikabadilika na kuwa jina la sasa La Colonia Santita Cartel (CS-14), Shirika la Madawa ya Kulevya la Kolonia Santita (KS-14), Septemba 1985 katika Mkutano wa Kolombia. El Tigre na wenzake wanne: Ignacio Leonardo de la Fuente, Raymundo Escoto Martinez, José Alberto Araújo na Panceano Nieto (viongozi wanzilishi wa La Familia; waliokuwa wakitafutwa na Tume ya Dunia na Jeshi la Meksiko sawa na El Tigre na Alcántara) hawakuhudhuria Mkutano wa Kolombia. Jefe de Jefes (Bosi wa Mabosi) El Tigre, na wenzake wanne walikuwa mbali kabisa; ng’ambo ya pili ya Pasifiki, wakicheza mariachi (muziki wa asili) na campesinos (wakulima) katika milima ya Sierra Madre Occidental huko Sinaloa – na kulala na wanawake warembo, wenye bikini, wanaokunywa martini, Acapulco nchini Meksiko.

Watu wanaohatarisha maisha yao kwa kudharau sheria wakati mwingine hawatakiwi kudharauliwa. Ni sawa na mtu aliyepoteza kila kitu katika maisha yake. Wanauwezo wa kufanya chochote. Serikali ya Meksiko ilipokataa kukidhi matakwa ya El Tigre ya kubadili katiba ya nchi – kuondoa kipengele cha mkataba wa kubadilishana watuhumiwa na washtakiwa – ili akikamatwa asipelekwe Marekani ambako atafungwa na kufia gerezani, El Tigre aliilaani Serikali ya Meksiko. Kujibu mapigo, ya laana ya maluuni, Serikali ya Meksiko ikawakabidhi makamanda 7 wa Kolonia Santita kwa mamlaka za Marekani, na kuongeza juhudi za kumsaka El Tigre mpaka nje ya Amerika Kusini na Kaskazini. El Tigre, kuikomoa serikali na kuwalipia kisasi makamanda wote waliouwawa na kufungwa na shirikisho, akamuua Mwanasheria Mkuu wa Serikali (PGR) na maafisa 7 wa Jeshi la Polisi la Nchi (PJF) kulinganisha idadi ya makamanda wake waliopelekwa Marekani – halafu 'akapotea', kabisa; baada ya kutangaza vita na Serikali ya Meksiko!

Tume ya Dunia imekuwa ikimtafuta Chui wa Siberia kwa zaidi ya miaka tisa. Bila mafanikio. Ulinzi wa Panthera Tigrisi ni wa kimataifa. Mbali na kulindwa na wananchi wa Oaxaca (kwa sababu ya kuwajengea shule, hospitali, makanisa, na kadhalika), na polisi wa shirikisho (kwa sababu ya vitisho, mauaji na rushwa); El Tigre analindwa na jeshi binafsi la kujihami (autodefensa) la wanajeshi wastaafu zaidi ya 1300! Mbali hali kadhalika na autodefensa; kiongozi wa Kolonia Santita ana walinzi binafsi makomandoo (48) akiwemo A. Narochnitskaya Belinsky, mtaalamu wa kutengeneza nyambizi wa Urusi, na Nicolas Kahima Kankiriho ('Kahima the Warrior') mwanajeshi wa kulipwa wa Uganda – aliyetoroka na El Tigre katika nyambizi ya Jefe de Jefes SPD (the Silent Predator of the Deep), iliyotengenezwa na Belinsky, katika Ghuba ya Meksiko Septemba 16, 1986.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mexico City Benito Juárez, tukiachana na historia ya Kolonia Santita, Kiongozi wa Kanda ya Amerika ya Kaskazini ya Tume ya Dunia Randall Buchanan Ortega; anaingia Mexico City kuonana na maafisa wa Serikali ya Meksiko (na maafisa wa Tume ya Dunia) Ijumaa saa mbili usiku CST. Kamanda wa Idara ya Polisi ya Tume ya Dunia (WPD) Meja-Jenerali Sebastian Alejandro, anamtambulisha Kamishna Ortega kwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (PGR) Virgilio Santo Graciano; Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (PJF) Demetrio Vega del Castilo; Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Marekani (DEA) Baxter Salvatore Sincere, na kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu (CNDH) Daktari Santiago Luis-Fernando.

PGR inakubali kuandaa nyumba za siri (safe houses) nne, katika maeneo tofauti ya Mexico City kwa ajili ya Vijana wa Tume. PJF inaahidi kutoa notisi kwa wahariri wa vyombo vya habari nchi nzima (D-Notice) kutotaja, kabisa, ujio wa Vijana wa Tume katika ardhi ya Mexico City. Kukiuka masharti ya D-Notice ya serikali, kutaathiri vibaya maendeleo ya operesheni ya Tume ya Dunia.

Vijana wa Tume huko Copenhagen, kabla hawajaondoka kuelekea Meksiko kupambana na El Tigre, wanapambana kwanza na CS-Copenhagen Jumapili usiku. Wanabomoa kambi mbili za Copenhagen za Kolonia Santita – Smallegade na Saltholm (Tårnby) – na kuondoka, kuelekea Meksiko (Jumatatu jioni), kwa ndege ya Tume katika Uwanja wa Ndege wa Roskilde.

Majasusi wa Kolonia Santita, wale wa kike waliotumwa kusafiri na makamishna wa Tume kuwapeleleza Vijana wa Tume, hawakukamilisha kazi kama walivyoagizwa na Mkurugenzi wa Usalama Gortari Manuel. Manuel hana habari ya Frederik Mogens! Anajua DC ina vijana watatu. Si wanne! Delfina Moore, jasusi mrembo, aliyemsindikiza Kiongozi wa Kanda ya Afrika ya Kusini ya Tume ya Dunia Kamishna Profesa Justin Mafuru wa Tanzania; alikutana uso kwa uso na mpelelezi maarufu duniani – John Murphy (kwa makosa ya profesa) katika ofisi za Kanda ya Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya huko Dar es Salaam: lakini picha aliyochukua haikutoka Tanzania!

Kolonia Santita ina picha mbili za Vijana wa Tume – Radia na Yehuda. Radia na Yehuda hata hivyo (na Murphy na Mogens), hawajui kama picha zao ziko mikononi mwa wakorofi huko Meksiko. Mexico City (Makao Makuu ya Kolonia Santita) na Salina Cruz (Maabara Kuu za Kolonia Santita), ulinzi umeimarishwa! Kila sehemu (viwanja vya ndege, mabarabara, mahoteli, migahawa, sehemu za wazi, majengo ya serikali, majengo ya Tume na kadhalika) inalindwa barabara! Hali ya hatari imetangazwa rasmi. Picha za Vijana wa Tume (Radia (msichana pekee) na Yehuda) zimesambazwa kila mahali kwa sicarios na autodefensa, wote, wa Salina Cruz na Mexico City! Licha ya silaha za kawaida; kama visu, mapanga, bastola na bunduki za masafa mafupi za shotgun, sicarios na autodefensa wana bunduki hatari (ndani ya makoti na magari yao ya kihuni) za Kalashnikov za Kirusi (AK-74 na AK-47) – cuerno de chivos (au 'mapembe ya mbuzi') kama zinavyojulikana huko Meksiko: na bunduki fupi, nene za Kibelgiji (FNP90) – mata policias (au ‘kiboko cha polisi’) zenye uwezo wa kutoboa kinga ya risasi.

Ndege ya Vijana wa Tume inaingia Meksiko katika mji wa Guadalajara: Jumatatu, usiku wa manane CST. Usiku huohuo, Vijana wa Tume wanaingia Mexico City (kwa mbinu za WODEC-Intelligence na Jeshi la Meksiko – bila sicarios kujua) katika nyumba waliyotayarishiwa na PGR, Calle Gante, Mexico City. Jumanne asubuhi, Murphy na Mogens wanakwenda Zona Rosa (katika ofisi za Tume) kuonana na Meja-Jenerali Sebastian Alejandro. Radia na Yehuda wanakwenda San Ángel, Álvaro Obregón, Makao Makuu ya Kolonia Santita – kutafuta ujasusi mwafaka wa kuanzia kazi. Masponji wa taarifa za kijasusi (majasusi wa Tume ya Dunia) wanasema El Tigre yuko 'mjini' Mexico City (mahali fulani) kwa ajili ya hafla ya mafanikio ya mkutano wake na magorila wa Kolombia.

Kabla hawajafika Zona Rosa hata hivyo, Murphy na Mogens wanaamua kula (kabisa) kutuliza njaa. Hawakupata nafasi ya kustaftahi. Hawatapata nafasi tena, baada ya kuonana na Sebastian Alejandro. Wakipata chakula na vinywaji katika Mgahawa wa Angus (si mbali na Zona Rosa), macho ya Murphy na Mogens yanakutana na macho ya msichana mrembo! Msichana huyo; mrefu, mwembamba, mwenye nguo nyeusi kuanzia chini mpaka juu, watu wanasema ni mtoto wa Rais na wanashangaa kumwona katika baa kama Angus! Sifa kubwa ya Murphy ni udadisi. Anapofanikiwa kuongea naye, kwa mbinu ya ua, binti huyo anasema yeye ni Debbie Patrocinio Abrego. Ana miaka 25. Si mtoto wa Rais! Ni mtoto wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Murphy anapomwuliza kuhusu walinzi wanne alioingia nao na wanaoendelea kumlinda (kuhakikisha hakuna kitu kibaya kinamtokea) Debbie anacheka na kusema hicho ni kitu cha kawaida kwa watoto wa wakubwa.

Kengele ya hatari inalia katika kichwa cha John Murphy. Kuna maswali ya kujibu hapo. Rais wa Meksiko haitwi Patrocinio Abrego. Mwanasheria Mkuu wa Serikali haitwi Patrocinio Abrego! Hata hivyo, baada ya kucheza muziki (huku watu wakishangaa kwa kutokujua Murphy ni nani mpaka acheze muziki na mtoto wa Rais), Debbie anazidi kumshtua Murphy. Anasema angependa kumwona tena, lakini si hapo. Katika baa ya watoto wa wakubwa ya San Ángel, Desierto de Los Leones, kesho yake asubuhi. Ametokea kumpenda na anahisi kuna kitu wanaweza kusaidiana! Kuna cheche za mapenzi hapo. Unaweza kuona kemia. Lakini San Ángel ni Makao Makuu ya Kolonia Santita! Na Debbie haonekani kuwa jambazi! Kwa nini anasema ni mtoto wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakati watu wanasema ni mtoto wa Rais! Kwa nini yeye na walinzi wake (wote) wamevaa nguo nyeusi!

Sifa kubwa ya Murphy ni udadisi, lakini kubwa zaidi ni unyamaume. Haogopi kitu. Anaheshimu sheria. Jumatano saa nne asubuhi, Murphy na Mogens wanakutana na Debbie Patrocinio Abrego (na rafiki yake mpenzi Lisa Madrazo Graciano) katika Baa ya Desierto de Los Leones, San Ángel, kusini-magharibi mwa Mexico City. Miadi kama hiyo John Murphy huwa haichukulii mzaha hata kidogo! Ndani na nje ya baa: Radia, Yehuda na maafisa wengi wa WODEC-Intelligence (wametapakaa kila mahali – kumlinda Murphy na Sajini Mogens). Murphy na Morgens wamefurahi kumwona Debbie (kwa mara nyingine) na wana hamu ya kumjua vizuri yeye na rafiki yake. Muda unakwenda. Kengele ya hatari ndani ya kichwa cha Murphy inazidi kulia. Mogens ameanza kubadilika! Naam. Kutetea afya na amani ya dunia, Operation Devil Cross imeanza kazi rasmi! Kitakachotokea baada ya hapo kitabadilisha historia ya Tume ya Dunia milele!

El Tigre ni nani? Anatoka wapi? Lengo lake na magorila wa Kolombia ni nini? Kwa nini anaitwa Chui wa Siberia? Miezi michache baada ya Panthera Tigrisi kutangaza vita na Serikali ya Meksiko na mashirika-pinzani ya Kolonia Santita; ukulima, utengenezaji na usambazaji wa madawa – na ugaidi wa kimadawa wa kimataifa – viliongezeka maradufu duniani kote! Kukidhi mahitaji ya wateja, na kulinda katiba na kiapo cha tambiko la uanachama wa Kolonia Santita; CS-Saldanha (Tawi la Kolonia Santita Afrika ya Kusini – lenye wajibu wa kusambaza madawa katika nchi 22 za Kusini mwa Afrika – kuanzia Afrika Kusini mpaka Somalia mpaka Kameruni), ikaanzisha magenge kadha wa kadha ya wahuni katika bara la Afrika; Wakombozi (la Masaki) na Magomeni Witches (la Magomeni), ya Dar es Salaam, Tanzania, yakiwemo. Wakombozi ikapewa jukumu la kuyachunga Makao Makuu ya Kanda ya Afrika ya Kusini ya Kudhibiti Madawa ya kulevya – na kusambaza madawa kuanzia Masaki mpaka Madagaska. Magomeni Witches (inayoongozwa na Naga Lubuva 'Bekka' au 'Kichogo') ikapewa jukumu la kusambaza madawa, bunduki na wanawake kuanzia Magomeni mpaka Bujumbura – na kujihusisha na vitisho, ukahaba, shughuli haramu za kibenki na mauaji ya kulipisha, ya kimkataba, kwa niaba ya Kolonia Santita. Nani anaongoza CS-Saldanha? Nani anaongoza Wakombozi? John Murphy ni nani? Murphy ni jina lake la bandia (kwa sababu za kiusalama, kumbukumbu na kukwepa mashabiki). La kwake halisi ni nani?

Kadiri unavyozidi kupanda juu ndivyo utakavyoanguka vibaya.
 
Back
Top Bottom