Kobe

Mlenge

R I P
Oct 31, 2006
2,125
2,291
Hata ingekuwa wewe, kwa yule mwenye nyumba ungelianzisha valangati la nguvu. Sijui hata nianzae wapi kukuambia siku uzalendo uliponishinda, lakini niliamua "kumnywea" mpaka "nilipopendeza" kisawasawa kumpa makavu laivu.

Siku hiyo nilichelewa kama siku nyingine, na kuingia nyumbani mida karibu mlango wa nje utafungwa. Mida kama hiyo mwenye nyumba mwenyewe huwa yupo. Alipenda sana kila wakati kutukumbusha kwamba sisi ni wapangaji wake, na yeye ndiye mwenye nyumba. Kwa hiyo tukambandika jina la "Kobe", kiumbe mwenye kustahili sifa ya kuitwa "mwenye nyumba" kwa vile huwa na nyumba yake kila aendako.

Kuwako kwa Kobe nyumbani kungemaanisha fursa ya kumpa 'mapande yake' niliyosubiri kwa hamu siku nyingi. Na 'nilivyoutwika', nilijua sitarudisha nyuma majeshi kama siku zingine nilizompania. Kufikiria hatua ambazo angechukua baada ya 'kumrarua', nilimuweka kiporo kwa kuzingatia pana maisha ya kupanga kwake baada ya kumpa ' maneno mbofumbofu'. Lakini hii ya sasa, haina kufeli wahenga wa siku hizi husema.


INAENDELEA sehemu ya 2
 
Kobe - 2

Nilimpa 'vipande vyake'. Siku hiyo sikurudisha nyuma majeshi. Yangu ya moyoni yote yalikuwa peupe. Hadharani.

Kobe hakuamini macho yake. Alinitizama kama vile nimetoka sayari ya
Mars. Macho yamemtoka pima mithili ya mjusi aliyebanwa na mlango. Akatulia tuli mithili ya mteja aliye kwa kinyozi.

Wapangaji wenzangu wakajaa pale kibarazani. Nahisi kimoyokimoyo walikuwa pamoja nami, ila wote walifunga kinywa, wakitulia kimyaaa. Kila mmoja alikuwa kwa upande mmoja anachekelea Kobe kakutana na sungura leo. Lakini kwa upande mwingine, walinisikitikia wakitafakuri atakayoyafanya Kobe dhidi yangu, mintarafu kuendelea kuwa mpangaji kwake.

Na kweli, hata mimi hilo la kulipiziwa kisasi nilijua lazima ndilo litafuata. Ima fa ima. Panga, pangua. Mkataba wangu utakapoisha, nitapandishiwa kodi, au nitatimuliwa moja kwa moja. Ubaya zaidi, sikuwa nimejiandaa kuhama, kwa vile kuanza kutafuta nyumba nzuri, iliyo mahala pazuri kama nyumba ya Kobe, lilikuwa si jambo jepesi mtaani kwetu. Na kama hiyo haitoshi, hali ya mfuko ilikuwa tete, isiyo himilivu kwa masharti ya makobe wengine mtaani waliokuwa wakitaka kodi ya mwaka mzima kwa mtu anayetaka kupanga.

Jambo moja nililokuwa naliegemea, ni fununu toka kwa vyanzo vya kuaminika kwamba Kobe alikuwa mbioni kuuza nyumba yake hivi karibuni, kabla ya mkataba wangu kuisha. Hilo ndilo lililonipa kibri. Ni hapo sasa fununu hizo ziwe za urongo! Hata zikiwa za kweli, wanunuzi wenyewe wako wapi, usawa huu? Kwa jinsi Kobe alivyo, hata bei atakayoweka itakuwa kali. Mzee mzima naweza kujikuta naadhirika hivihivi...

ITAENDELEA
 
Back
Top Bottom