Mahakama yachomwa, ofisi ya DC yaharibiwa
* Ni baada ya polisi kudaiwa kuua raia
- Risasi, mabomu ya machozi vyarindima
- Biashara, barabara zafungwa kwa muda
Na Solomon Mwansele, Mbeya
VURUGU zilitawala jana eneo lote la Kyela mjini, mkoani Mbeya, kutokana na kifo cha mkazi wa Mbugani, Lucas Mwaipopo, aliyedaiwa kuuawa kwa kipigo kutoka polisi watatu.
Kwa mujibu wa habari kutoka eneo la tukio, Mwaipopo alikamatwa na polisi waliokuwa doria saa mbili usiku, eneo la Mashineni, akiwa na mwenzake ambaye aliachiwa njiani kabla ya kufikishwa kituo cha polisi kwa madai kwamba, alitoa kitu kidogo.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari, baada ya Mwaipopo kufikishwa kituoni alipigwa na kupoteza fahamu, hivyo kupelekwa hospitali ya wilaya ambako alifariki dunia akipatiwa matibabu.
Mamia ya wananchi waliandamana jana asubuhi kuelekea kituo cha polisi kupata ufafanuzi juu ya tukio hilo, ambapo wakiwa njiani waliuona msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile.
Wananchi hao waliamua kuufuata msafara huo ili kwenda kuwasilisha malalamiko yao, ambapo polisi waliwafukuza, hivyo kuamua kuvamia kituo cha polisi wakiwa na mawe mikononi.
Polisi walilazimika kutumia risasi za moto na mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi hao, ambapo watu watatu walipigwa risasi, miongoni mwao akiwamo Jacob Anthony, aliyepigwa risasi tumboni na kutokea kwenye kalio la upande wa kulia.
Anthony alipelekwa kwa matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, ambapo wengine waliojeruhiwa kwa risasi ni Daud Kibona, aliyepigwa mkono wa kulia na Ramadhan Hassan, ambaye risasi imeingia na kutokea upande mwingine wa bega la kulia.
Askari D.9713 Koplo Mbanga na E. 7787 Koplo Robert walijeruhiwa kwa kupigwa na mawe na wananchi na walipelekwa hospitali ya wilaya ya Kyela kwa matibabu.
Vurugu hizo pia zilisababisha ajali, ambapo mwanamke ambaye hajatambuliwa alishindwa kulimudu gari alilokuwa akiendesha na kujikuta akigonga mti kutokana na kuchanganyikiwa. Amelazwa katika hospitali ya wilaya kwa matibabu.
Baada ya wananchi hao kuona wanazidiwa nguvu na polisi waliondoka na kwenda Mahakama ya Mwanzo ya Kyela, ambako waliichoma moto na pia kwenda kufanya uharibifu kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kyela.
Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Harrison Makinda, akizungumzia tukio hilo, alisema ameshangazwa na kitendo cha wananchi kuvamia mahakama na kuichoma, kwani haihusiani na kupigwa na kuuawa kwa Mwaipopo.
Makinda alisema walipofika kazini asubuhi kabla ya tukio hilo, walilazimika kuahirisha kesi zote baada ya nyumba iliyo jirani na mahakama kuwa na msiba, hivyo kuwafanya kushindwa kufanya kazi.