Kitendawili kimetegwa - Kikwete Tegua...

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,475
39,991
Na. M. M. Mwanakijiji

Ndugu zangu Kitendawili kimetegwa nani atakitegua. Chama cha Mapinduzi kimetaka kutumia madaraka na wingi wake kufanya kile ambacho hakikuwa na hakijawahi kuwa ndani ya ahadi zake. Kimetaka kufanya kitu ambacho hakikupewa ridhaa ya wananchi kukifanya. Sote tunakumbuka vizuri kuwa kampeni nzima ya uchaguzi wa mwaka jana kwa upande wa CCM haikuhusiana KABISA na suala la Katiba Mpya. Katiba Mpya haijawahi kuwa sehemu ya Ilani, ahadi au mipango ya Chama cha Mapinduzi kabla ya Disemba 31, 2010.

Ni uamuzi wa kudandia tena siyo kudandia tu bali kudandia na kushupalia. Leo wanadai kuwa ajenda ya Katiba Mpya ni yao. Lakini wanafanya hivyo wakikataa kabisa kukiri wala kutambua kuwa ajenda hiyo ilikuwa ni ya upinzani kwa miaka ishirini sasa tangu lile kongamano lilillozaa vyama vya upinzani nchini.

Ajenda ya Katiba Mpya imekuwa ni moyo udundao katika mioyo ya wapinzani nchini. Tangu mwanzo ilitambulikana kabisa kuwa mabadiliko ya kweli ya kitaifa hayawezi kutokea kwa kubadili watu tu, kubadili sera tu hata kubadili vyama ilitambulikana kabisa kuwa ni lazima kugusa Kitabu chetu Kitakatifu cha watu wa dini zote ambacho watunzi wake ni sisi wenyewe! Hatuwezi kubadilisha Biblia au Qurani lakini Katiba ni kitu pekee kitukufu ambacho kinatoka kwetu na hicho pekee kinatufunga sote sawa na hivyo kinaweza kubadilishwa na sisi wenyewe tu. Ajenda hii ya Katiba Mpya haiwezi leo kuwa ni ajenda ya CCM na wengine wanakaribishwa kama watoto wasio na kwao! Leo hii tumewaona wabunge wa CCM wakizungumza kwa jazba kana kwamba waliahidi hata mmoja wao kuwa wanataka Katiba Mpya.

Siyo Komba kwa kuimba wala Wasira kwa hasira aliyesimama mwaka jana kutaka Katiba Mpya ndani ya CCM. NONE. Leo wana ujasiri wa kubeza, kukebehi na hata kupiga mkwara wale wanaotaka katiba mpya kwa mfumo ulio wazi, wenye kuweka msingi juu ya wananchi siyo wabunge au Ikulu peke yake! Leo hii watu hawa wana ujasiri wa ulevi wa madaraka kwamba wako tayari kuamuru moto unye kama vile ulivyoteremka kule Sodoma na Gomora kisa tu tumewamua kuwageukia na kuwatazama! Na wapo watu wanaomini kabisa ati ajenda hii inaweza kuongozwa na CCM kwa vile tu CCM iko madarakani! Yaani, watu ambao juzi tu hawakuwa na wazo la Katiba mpya tena wakatubeza, na kutukebehi huku wakishindana kugongana wenyewe kwa maneno wanaweza kuandika mswada wa kusimamia uandishi wa Katiba tukaubali tu kwa vigelegele, ngoma na chereko chereko za vifijo.

Ngoja niliseme hili vizuri tu na kwa uwazi Ee Mungu nisaidie - maana tunazunguka mno - CCM haina uhalali wa madaraka ya kusimamia mchakato wa Katiba Mpya. Inaweza kushirikiana na wengine, inaweza kuzungumza na wengine, lakini yenywe peke yake haina hoja, uwezo, wala mandate (ridhaa) ya kufanya hivyo. Haimo kwenye ajenda yao, na Kikwete alipoamua kufanya hivyo mwishoni mwaka jana hakukuwa na kikao chochote cha Chama cha Mapinduzi ambacho kina madaraka ya kubadilisha sera za CCM. Hakukuwepo na kikao cha Halmashauri Kuu wala Mkutano Mkuu kilichofikia uamuzi wa kuandika Katiba Mpya. Huu ulikuwa ni uamuzi wa Ikulu na Ikulu peke na matokeo yake mswada mzima umezunguka Ikulu!

Wabunge wake hawakutakiwa hata kutoa maoni juu ya Katiba Mpya. Wangeweza kufanya hivyo tu kwanza kwa kukubali kuwa hoja hii ilikuwa inatoka nje yao (kwa wapenzi na wanaharakati) na kuwa kutokana na kutambua huko mchakato mzima kuanzia Alfa yake hadi Omega yake ungehakikisha kuwa watu wote wanashirikishwa siyo wanaburuzwa kwa mikwara ya kitoto na kejeli zisizo na kichwa wala miguu.

Kikwete sasa ametegwa. Kitendawili hiki ni yeye peke yake anatakiwa kukitegua. Alikipiga mwenyewe kwenye hotuba yake ya Disemba 31, 2010 alipotangaza na kutushtua kuwa hatimaye ameona mwanga na nuru ya ajabu ikimzukia na kuwa sasa serikali yake imekubali hoja ya Katiba Mpya . Jambo hili wengine tulilipokea kwa tahadhari tukihofia kile kinachotokea sasa. Tulihofia kuwa kwa vile hoja hii imechukuliwa na Ikulu (Kikwete) basi mchakato mzima utazunguka Ikulu na hivyo ndivyo ilivyokuwa na hapa ndipo kiini cha mgogoro wa sasa kilipo.

Wanaharakati na wanamageuzi nchini, wanayo haki ya kupinga, kukataa na kudhihaki mfumo ambao unapendekezwa na CCM na serikali yake ambao umepuuzia kwa makusudi au kwa sababu ya vimulimuli vya madaraka hoja zote tulizozitoa mwezi Machi. Watanzania ambao wamekuwa wakipigania mabadiliko ya Katiba kuanzia 1992 wanayo haki kabisa siyo tu ya kutoka ukumbini hata kusimama na kuanzisha mwamko wa kupinga kubambikiziwa Katiba Mpya kwa sababu tu watu wana madaraka. Kikwete asaidie kukitegua kitendawili hiki vinginevyo ni yeye ambaye atajiikuta anabeba lawama.

Ndugu zangu, kama sisi sote tutaweka miguu chini na kusema hatusogei na kuamua kugoma tulipo tutalazimishwa kuzungumza na kukaa pamoja wakati damu imemwagika. Hivi kwanini leo Kenya hawapigani mapanga? kwanini leo Zanzibar kuna muafaka, kwanini Zimbabwe kumetulia zaidi kuliko ilivyokuwa miaka michache iliyopita? Ni kwa sababu walifikia kwenye kilele cha kushindwa kuvumiliana. Pande mbili za hizo sehemu zote ziliweka miguu chini na kila mmoja aking'ang'ania upande wake na kukataa kuzungumza na mwingine wala kukubali kwamba yule mwingine yupo. Tangu uchaguzi mkuu wa mwaka jana nimetoa ombi wazi la kusema viongozi wetu wa kisiasa nchini wakae pamoja kuzungumza na siyo kuzungumza tu lakini pia kuwa tayari kukubali upande wa yule mwingine.

Kinachonisikitisha ni kuwa hadi hivi sasa inaonekana watu hawataki kukubali upande wa yule mwingine isipokuwa kwa lazima. "Kubalini msipokubali dola itumike!" wanasema waliolewa ugimbi ule wenye povu la madaraka. Wengine wanasema "msipokubali tutaandamana hadi msitawale" na wengine wanasema "mkiandamana tutawatia pingu hadi mkome" na wengine wanajibu "hamna pingu za kutosha wala magereza ya kufunga fikra". Matokeo yake - watalazimishwa kukaa chini na kuzungumza siku ile tutakapoamka na kusikia watu 50 wameuawa katika siasa! Mtasema tunachuria lakini ndivyo ilivyo mahali pote duniani!

Kikwete tegua kitendawili.

1. Usikubali mswada huu kama ulivyo. Hata wabunge wako waupitishe kwa mbwembwe. Upande wapili hautakubali. Na hamna namna ya kuwalazimisha watu milioni mbili kuukabali. Assadi hadi leo kashindwa anaua watu wake kila siku na bado wanasimama kumpinga. Risasi hazipo za kutosha. Bahati mbaya machozi hayana kikomo... Mkisema kuwa mtaendelea na mchakato na yeyote atakayepinga "atakiona cha moto" well.. mtakuwa mmetengeneza kundi kubwa la wanaowapinga na uzoefu unaonesha kuwa Watanzania nao ni wanadamu wakivuka mstari wa 'sina cha kupoteza isipokuwa utu wangu' tutalia na kusaga meno.

2. Pande mbili zikae chini kuzungumza na katika hili ni utayari wa Rais unasubiriwa. Pamoja na matokeo yale ya uchaguzi mwaka jana nilisema kaa chini na Dr. Slaa mzungumze. Nilimuuliza Dr. Slaa swali hili katika mahojiano na alisema yuko tayari wakati wowote kufanya hivyo. Lakini inaonekana kuna watu hawataki. Na hawa wasiotaka wanafanya hivyo labda kwa hofu kuwa ukikubali kuzungumza na Slaa (nyinyi wawili) basi utakuwa umempa ujiko au Kamati Kuu ya CCM na ile ya CDM vikikaa pamoja itakuwa mmeinua CDM. Well, je ni baya kiasi hicho? Kwamba mje kulazimishwa kukaa pamoja wakati miji inaungua, watu wanakimbiana na kukimbizana na polisi wametanda kila sehemu?

Kikwete tegua. Kitendawili hiki ni cha kwako, hakuna wa kukusaidia. Ulikianzisha mwenyewe na kwa namna nakuonea huruma kwa sababu historia inaweza ikakusamehe kwa mengi sana lakini hili la Katiba Mpya likivurundwa sidhani kama jina lako katika historia litakumbukwa kwa haiba nzuri hivyo. Lincoln anakumbukwa kwa mengi lakini la kutangaza emancipation ya watumwa kumemuweka kwenye level nyingine kabisa. Naamini jinsi utakavyosimamia mchakato wa Katiba Mpya bila kuonekana umeulazimisha ndivyo historia itakavyokukumbuka. Kwanini tufike huko kama tunaweza kuepuka kwa kukaa pamoja katika hali ya amani?

Kitendawili...
MMM
 
Mkuu huwa napenda maelezo yako lakini tatizo huwa unatumia maneno meeeengi yanayojirudiarudia. Yaani hadi mtu unafika katikati hata huelewi paragraph ya kwanza inaongelea nini. Kifupi insha zako hazina muendelezo.
 
signature yangu inaeleza jinsi nkwele alivyo.......hawezi kutegua subiri jioni hiyo si anaongea na wale wazee wacheza bao leo!!!
 
Mkuu huwa napenda maelezo yako lakini tatizo huwa unatumia maneno meeeengi yanayojirudiarudia. Yaani hadi mtu unafika katikati hata huelewi paragraph ya kwanza inaongelea nini. Kifupi insha zako hazina muendelezo.

kwa hiyo hukumaliza kusoma .......
 
Tatizo ya magamba hata huwa hwapokei ushauri wa wananhi wake zaidi ya kuleta udikteta tuu!
 
kwa hiyo hukumaliza kusoma .......

Mbona huwa anaweka mambo very systematically ndugu. mi nadhani tatizo la uelewa wako na akili pia. Kuna watu wengi ni wavivu wa kusoma, na mara nyingi huwa kusoma zaidi ya paragraph moja, ukiongeza zaidi ya hapo akili zao huanza kunyaa kabisa
 
Wazo jema ndugu,wenye hekima uchukua hatua madhubuti ktk wakati muafaka. Tusubiri tuone jinsi kitakavyo teguliwa hicho kitendawili, je jibu litakuwa sahihi? Au la! Muda utaeleza.
 
Mpelekee hii rai kabla hajalikoroga leo atakapokutana na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam.

Najua Salva na Kibanga huwa wanapitia JF lakini kwa unafiki wao hawawezi kumpataa hii kitu.
 
Mkuu huwa napenda maelezo yako lakini tatizo huwa unatumia maneno meeeengi yanayojirudiarudia. Yaani hadi mtu unafika katikati hata huelewi paragraph ya kwanza inaongelea nini. Kifupi insha zako hazina muendelezo.
Mhhhh ndugu yangu, ndio maana wa Bongo ni wavivu wa kusoma. Hii taarifa aloiandika Mwanakijiji ina urefu gani huo wa kumfanya mtu ashindwe kusoma au hadi achanganye paragraph?

Ndio maana tunaambiwa ukitakaficha pesa kwa M-TZ wewe weka noti katikati ya kitabu cha japo page 200 tu. Kama hii presentation tu waona ni ndefu inakuchanganya, je huu mswada tunaoupigia kelele leo hii ukiwekwa hapa mtandaoni kweli utaweza usoma na kuuelewa???
 
Asante MMM naunga mkono hoja. CCM na seikali yake hawana uhalali wa kusimamia katiba mpya. Siyo wazo lao, wala hawaipendi
 
Siasa mkuu ahitaji ubabe kama yanayofanyika sasa. Ubabe wa Rais Mgabe huko wapi kabaki kuwa Rais hasiyekuwa na tija kwa maisha ya wazimbabwe. Nini hasa serkali inataka kufanya.

Swali langu Je ninani ajuaye Rais anayekuja 2015.

Nakumbuka aliyekua Rais wa Zambia Ndg Kennedy Kaunda alifanya kama haya kwa lengo mazuri ya chama chake. Rais Chiluba alimsweka ndani licha ya kumfanyia kampeni kama sikosei.?
 
Mkuu huwa napenda maelezo yako lakini tatizo huwa unatumia maneno meeeengi yanayojirudiarudia. Yaani hadi mtu unafika katikati hata huelewi paragraph ya kwanza inaongelea nini. Kifupi insha zako hazina muendelezo.

Anzisha ya kwako tuone itakuwaje mkuu,hii ni ya MMM.
 
Mwita25,I always wonder! You are so in love to your people kiasi cha kutoruhusu independent thinking!!! Gosh!!! Au ni effect ya shule za kata, ambako hakuna reading practice at early stages!!!Duh!!!
 
Tatizo CCM Wanadhani CHADEMA ni kina mbowe na slaa,kumbe chadema ni sehemu ya kusemea ya watanzania wa ukweli,wale wa hali ya chini kabisa ambao ni wengi zaidi.Wanajiaminisha kuwa watanzania wa sasa hivi ni wale walioambiwa mkichagua upinzani mmechagua vita.Mbona Ghana hakukua na vita? Mbona zambia hakukua na vita? Kwa nini Ivory Cost kumekuwa na vita? Utapata jibu kwamba pale ambao watawala watang'ang'ania madaraka ndipo machafuko hutokea.I swear and that is what i believe,watakaoleta machafuko nchi hii ni CCM.
 
Mkuu huwa napenda maelezo yako lakini tatizo huwa unatumia maneno meeeengi yanayojirudiarudia. Yaani hadi mtu unafika katikati hata huelewi paragraph ya kwanza inaongelea nini. Kifupi insha zako hazina muendelezo.

We acha uvivu...

Kama unaona bandiko hilo lina paragraph nyingi ninaamini mambo yafuatayo...

1. Maswada wa katiba haujausoma
2. Hotuba ya Lisu hujasoma
3. Riport ya Mwakyembe kuhusu Richmond uliangalia tu kichwa cha habari
4. ......
 
Back
Top Bottom