Kitanzi cha Zitto kinavyomtesa Spika, serikali | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kitanzi cha Zitto kinavyomtesa Spika, serikali

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Paschal Matubi, Apr 30, 2012.

 1. P

  Paschal Matubi Member

  #1
  Apr 30, 2012
  Joined: Sep 15, 2008
  Messages: 92
  Likes Received: 31
  Trophy Points: 25
  Source:
  TANZANIA DAIMA (Jumapili)
  {
  www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=35396}

  MWAKA jana ilipozuka hoja ya kupinga nyongeza ya posho za vikao za wabunge kutoka sh 70,000 hadi sh 200,000 kwa kikao cha siku moja, baadhi waliotetea nyongeza hiyo walitumia kauli hii: “Kwanza vikao vyenyewe vya Bunge havizidi kumi kwa Mkutano mmoja”.

  Je, ratiba ya vikao vya Bunge ikoje? Aliyekuwa Spika wa Bunge Pius Msekwa, aliandika kitabu kiitwacho {Reflections on the First Decade of Multi-Party Politics in Tanzania}. Kitabuni, ameonyesha ratiba ya Bunge kwamba lina jumla ya mikutano minne kwa mwaka (uk.184-5).

  Msekwa anasema Bunge lina mikutano “mifupi” mitatu ambayo hufanyika Februari, Aprili na Novemba. Mada ya mikutano hii huwa ni miswada na hutumia wiki mbili hadi tatu.

  Mkutano wa Juni huwa ni “mrefu” huchukua zaidi ya miezi miwili kwasababu unajadili bajeti ya Mwaka (uk.185).
  Msekwa anasema ndani ya mwaka mmoja Bunge huweza kukaa vikao 80. Kanuni za sasa za Bunge zinasema Bunge letu hutumia saa 6: 45 kwa kikao kimoja linapokutana tangu saa 3:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana kisha saa 11:00 jioni hadi saa 01:45.

  Hivyo, kigezo kizuri ni saa kwa mwaka na wala si siku kwani mabunge ya nchi nyingine hufanya vikao vyake kuanzia saa 8:30 mchana hadi saa 1:00 jioni yaani saa 4:30 kwa siku.

  Mikutano hii “mifupi” imeonyesha kwamba kwa miaka ya karibuni imekuwa ikifikisha vikao takriban 10. Mkutano uliomalizika wiki iliyopita ulikuwa na vikao 11.

  Agosti 26,mwaka jana ilikuwa ni siku ya kikao cha 56 cha Bunge la Bajeti. Kama Bajeti imechukua siku 56, wakati mikutano mitatu iliyobaki ina wastani wa siku 9 au 10, basi Bajeti hutumia asilimia 65 ya vikao vyote vya Bunge kwa mwaka.

  Mkutano “mfupi” sana ni ule uliokaa Oktoba 24 hadi 27 mwaka 1967 ambapo miswada 11 ilipitishwa ndani ya hizo siku nne tu, likiwa ni Bunge la kwanza kufanyikia nje ya Dar es Salaam kwani lilifanyikia Mwanza.
  Hii ni moja ya sababu inayofanya mambo mengi yaonekane kutokea na kumalizika kwenye Mikutano ya Bajeti kuliko mikutano “mfupi”.

  Kama tunakubali kwamba posho za wabunge ni gharama, basi wingi wa gharama hizo ni kwenye Bunge la Bajeti yaani asilimia 65, bila kuhesabu vikao vya Kamati mbalimbali.

  Suala lililoibuliwa na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) la kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, linahitaji walau siku 14 ndipo liweze kuingia katika masuala yatakayojadiliwa na Bunge. Siku 14 ni zaidi ya Mkutano mmoja wa Februari , Aprili au Novemba.

  Tunapohesabu siku 14, kwa namna moja tunaambiwa kwamba jambo kama hilo saizi yake ni Mkutano wa Bajeti, vinginevyo halikamiliki ndani ya mkutano mmoja wa Februari , Aprili au Novemba. Je, ndivyo hali ilivyo? Tuzichambue siku 14 kama ifuatavyo tukianza na kazi za mbunge.

  Mbunge ni mwakilishi wa watu wa jimboni kwake. Unapomalizika mkutano wa Bunge, tunamtarajia Mbunge atingwe na ratiba ya kushiriki kutatua kero za kimaendeleo jimboni mwake. Kero zinazozidi uwezo wa jimbo, ndizo baadhi tunatumaini aziwasilishe kwenye mkutano ujao wa Bunge.

  Wabunge ni wengi na kero ni nyingi, hivyo muda na utaratibu wa kufikisha hata swali moja bungeni, ni jambo la kuzingatiwa.

  Mbunge anapopewa nafasi ya kujieleza, hata kama hatujajua ataongelea nini, basi asilimia kubwa ya makisio yetu itakuwa kwamba atagusa zaidi Jimbo lake. Asilimia ndogo tunaiacha kukisia maeneo mengine au sekta yoyote.
  Hiyo ndiyo hali ya mbunge kwa ufupi. Mbunge anapokabidhiwa fungu la mfuko wa jimbo basi ni wazi zimelengwa shughuli za maendeleo ya jimbo lake.

  Kumbe, kipaumbele cha mbunge si kujua ni mbunge gani kasafiri kwenda nchi gani mara wanapotawanyika pale Dodoma. Mfuko ule wa Jimbo si kwa madhumuni ya kukodi ndege inayoweza kuzunguka dunia nzima akitafuta sahihi za wenzake 70 ili kuwahi siku 14 kabla kikao kinachofuata.

  Hivyo, mazingira hata kama hayakidhi, yamewekwa ili mbunge aweze kutimiza uwakilishi jimboni na aweze kusafiri hadi bungeni kwenye mikutano ya Bunge.

  Taratibu, tuendelee kuchambua kigezo cha siku 14 kwa hoja kama hii aliyoleta Zitto ya kutokuwa na imani na waziri mkuu.

  Mjadala kuhusu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, haukuibuka wakati wabunge wako majimboni wakisubiri kikao kinachofuata. Hivyo, haikuwahitaji wabunge waanze kupigiana simu kwamba watakapofika Dodoma wajipange vipi kuhusu hoja ile.

  Suala lile liliibukia pale bungeni, halikumalizika kwa siku moja, hadi ikatugharimu wiki kadhaa baadaye, Spika aunde kamati kwa jambo hilo.

  Jairo hakuwa waziri wala naibu waziri au mbunge. Lakini haya ndiyo matumizi mazuri ya jambo kubwa kushughulikiwa kwa wingi wa wabunge yaani kamati. Ni moja ya sababu kwa mabunge mengi duniani kuendeshwa kwa mtindo wa kamati.

  Msomaji, jiulize kama Bunge zima ililibidi litafakari wiki kadhaa ndipo itokee kuundwa kwa Kamati kwa suala la mtumishi (Jairo) na lisiishe siku ileile lilipoibuka, iweje leo mbunge mmoja akiwa jimboni kwake aweze kuandaa hoja ya kutokuwa na imani na waziri mkuu akiwa hukohuko jimboni.

  Baada ya kuandaa hoja hiyo, ndipo aanze kukodi usafiri wa haraka kama ndege, azunguke kokote duniani waliko wabunge 70 wanaoelekea kuunga mkono hoja yake.

  Hivyo, mazingira kama haya, yanapafanya Dodoma wakati wa mkutano ndipo pawe ni mahala tegemezi ambapo Mbunge anaweza kupata taarifa sahihi za jambo lolote kabla ya yeye au na wenzake hawajaanza hatua ya nyingine hata kama itakuwa ni hatua ya kuiwajibisha Serikali.

  Kanuni zinahitaji hoja kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, ipitie kipengele cha muda usiopungua siku14. Mkutano ulioisha wiki iliyopita kama hoja hii ingetakiwa kujadiliwa katika kikao chochote cha mkutano uliopita basi ilitakiwa kufika kwa Spika kabla ya Machi 28, mwaka huu.

  Hata ingefika ofisini kwa Spika asubuhi na mapema siku ile ya Kikao cha kwanza tena kabla hakijaanza, bado hoja hiyo ingefikiriwa kupelekwa bungeni labda kuanzia Aprili 23 ambayo ilikuwa siku ya kuahirishwa kwa Bunge.

  Hapa tunatahadharishwa nini? Makala imeanza kwa kueleza hali ya Mbunge akiwa hayukoDodoma Bungeni? Nimesema kwamba wakati huo hatujui wabunge wamesambaa vipi duniani baada ya kutoka Dodoma?

  Hivyo, maana yake ni kwamba, ni rahisi kwa mbunge kupata mawasiliano na mwenzake yeyote duniani na kumshawishi kwamba zimebaki siku kadhaa anataka kuwasilisha hoja kama hii.

  Lakini ni vigumu, kumpata hata mbunge mmoja akaweka sahihi kwenye hoja yake kabla Bunge halijaanza huko Dodoma. Utampataje wakati huenda ulipomweleza uzuri wa hoja yako, yeye alikuwa yuko safaraini Toronto, Canada?

  Mazingira haya si tu kwamba yanasababisha ndugu zetu wengine waite kitendo cha Zitto kuwa ni “Political Stunt” bali ukweli ni kwamba kilitakiwa kiitwe “Periodical stunt”. “Stunt” ni neno la Kiingereza kwa maana ya jambo lisilowezekana kirahisi.

  Binafsi ninasema ni “Periodical stunt” kwani si kwamba jambo hili haliwezekani kufanikiwa ndani ya mikutano wowote wa Bunge. Haliwezekani kwa msimu fulani au mikutano fulani linawezekana kabisa ndani ya mkutano wa Bajeti unaofikisha vikao hata zaidi ya 50.

  Tuangalie sasa thamani ya muda yaani “siku”. Je, Katiba yetu ina mambo gani mengine yanaohitaji utekelezaji kwa siku 14. Yapo walau manne huku ibara zake zikiwa kwenye mabano kama ifuatavyo:
  (i) Kumteua Waziri Mkuu baada ya Uchaguzi Mkuu {Ib. 51(2)}, (ii) Kuziba nafasi ya Makamu wa Rais {Ib. 50(4)}, (iii) Kutangazwa kwa hali ya hatari {Ib. 44(2)}, (iv) Kutangazwa kwa hali ya vita {Ib. 32(3)}.

  Kwa nini “siku 14” ziwe na uzito huo? Urais ni nafasi nyeti kuliko nafasi zote nchini, hivyo, muundo wa Katiba yetu hauachi mwanya kwa nafasi ya urais iwe wazi hata kwa dakika moja.

  Je, unyeti huo uko na kwenye nafasi nyingine zaidi ya Urais? Nafasi inayofuata ni ya Makamu wa Rais kisha Waziri Mkuu. Inapotokea uteuzi wa moja ya hizi nafasi mbili, uteuzi huo unagawanyika katika mamlaka mbili. Mamlaka ya kwanza ni ya kutangaza uteuzi ambayo ni kazi ya Rais. Mamlaka ya pili ni ya kuthibitisha uteuzi ili mhusika aanze kazi.
  Rais kama sehemu au mamlaka ya uteuzi amepewa siku 14 awe amekamilisha uteuzi wake, ndipo Bunge liingie katika mamlaka ya uthibitisho kwa kumpigia kura mteule huyo.

  Baada ya Bunge kumthibitisha, mteule ambaye sasa anakuwa mthibitishwa, kama ni waziri mkuu anaapa mbele ya Rais {Ib. 51(1)}, na kama ni Makamu wa Rais anaapa mbele ya Jaji Mkuu {Ib. 49}, ndipo aanze majukumu.
  Tumeona unyeti wa “siku 14” kwa shughuli ya uteuzi wa Wasaidizi hawa wa Rais. Tuje sasa kwenye unyeti wa “siku 14” kwa hali ya nchi. Inapotangazwa hali “hali ya hatari” au “hali ya vita” basi Rais atatuma mara moja nakala ya tangazo hilo kwa Spika wa Bunge ambaye baada ya kushauriana na Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, ataitisha mkutano wa Bunge.

  Hivyo, inapotokea fursa suala ya kujaza nafasi ya Waziri Mkuu au Makamu wa Rais, basi Rais amepewa, azitumie vizuri zile “siku 14” kukamilisha uteuzi wake. Wakati inapotangazwa mara moja hali ya hatari au vita, basi Bunge linatahadharishwa lizitumie vizuri zile “siku 14” kukamilisha uthibitisho wake.

  Hali ya hatari, au ya vita, au hali kubaki uwazi kwa nafasi ya Waziri Mkuu ama Makamu wa Rais, ni mambo manne ambayo hatuyapendi lakini hatuwezi kuyazuia yasitokee ghafla bila kutarajiwa.

  Hivyo, “siku 14” kwa nchi si za mzaha hata kidogo. Linajitokeza jambo jingine kubwa nchini basi lisitufanye tukasahau kwamba Bunge na Rais siku zote wanawaza zile “siku 14” kabla ya hilo jipya, kwa mujibu wa Katiba kama tulivyoona.
  Baada ya kuelewa nini thamani ya “siku 14” tuje kwenye hoja aliyoleta Zitto. Moja ya uzito wa hoja hii si kupata asilimia 20 ya wabunge wote. Uzito upo kwenye Kanuni ya Bunge namba 133(4) inayowafanya wabunge wapige kura ya siri.

  Usiri unaoweza kuleta matokeo yoyote hata kama chama anachotoka Waziri Mkuu kina asilimia 99 ya Wabunge mle Bungeni.

  Kitendo cha kufanikiwa kuwapata asilimia 20 ya wabunge waliosaini hoja hiyo, ni kama kengele ya tahadhari kwamba lolote linaweza kutokea kuhusu hatima ya kiti cha uwaziri mkuu.

  Kitendo cha kuwasilisha hoja hii kwa Spika, na kuifanya isubiri kufikisha umri wa “siku 14”, kinamfanya yeyote anayeijua Katiba ajiandae ki mawazo kama alivyojiandaa kimawazo ulipowahi kuhitajika uteuzi wa waziri mkuu.
  Magazetini, mitandaoni na hata meseji za simu kitakuwa ni kipindi cha tetesi za “mawaziri wapya” na yapo yatakayohiji uwezekano wa “waziri mkuu mwingine”.

  Hiki ndicho kisa cha “siku 14” hata kama kuna sababu nyingine zinazosababisha “siku 14” ziwe kigezo kwa hoja hii ya kutokuwa na imani na waziri mkuu.

  Sijasoma nakala ya Zitto aliyoifikisha kwa Spika kuhusu hoja hii. Lakini ninavyojadili na kubishana na wenzangu nasikia kunatajwa kwamba zikipita “siku 14” bila muitikio wowote basi inabidi liitwe kinachoitwa “Bunge la Dharura”.

  Ndani ya Katiba yetu neno “dharura” limetokea mara nane lakini hakuna linapotanguliwa na maneno “Bunge la...”. Ndivyo pia lilivyotokea mara 22 kwenye Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Mwaka 2007.

  Hivyo, hakuna chombo kinachoitwa “Bunge la Dharura” kiasi kwamba wengine wameamua kuliita “Bunge Maalumu” na kusahau kwamba “Bunge Maalumu” ni lile lililounda Katiba ya sasa Aprili mwaka 1977.

  Bunge ni Bunge tu, yaani Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hata kama litaitwa kwa shughuli maalumu kama “Bunge la Tanganyika”, lilipokutana April 25, 1964, siku moja kabla ya Muungano {Pius Msekwa, uk. 54}

  Badala ya kuzungumza neno “Bunge la Dharura” au “Bunge Maalumu” ni bora tuelimishane kuwa ni nini kitatokea iwapo mazingira kama yalivyo ndani ya siku 14 baada Zitto kukabidhi hoja yake ofisini kwa Spika.

  Ibara ya 53A(3)(b) ya Katiba inasema, hoja ya kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu itajadiliwa na Bunge baada ya Spika kuridhika kuwa masharti ya Katiba kwa ajili ya kuleta hoja hiyo yametimizwa.

  Hadi naaandika makala hii sijasikia lolote kutoka ofisi ya Spika kutoridhika na masharti ya kikatiba kwa hoja ile. Ibara inayofuata {53A(4)} inasema hoja iliyotimiza masharti ya kikatiba itawasilishwa Bungeni “mapema iwezekanavyo” kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.

  Hapa, Katiba inatuambia kwamba, hoja iliyomaliza masharti yote ya kikatiba, basi haina kizuizi tena cha kuendelea kukaa ofisini kwa Spika, bali sasa mahala pake ni bungeni, tena “mapema iwezekanavyo”.

  Tunapaswa kukumbushana kwamba, kama hali itaendelea kuwa ileile sawa na siku Zitto alipowasilisha hoja ile, basi Katiba ndiyo itakayotupeleka huko inakokuita “mapema iwezekanavyo” {53A(4)}.

  Kama Aprili 23, 2012 ndipo hoja imewasilishwa kwa Spika, basi kilichobaki ni hesabu rahisi za kuhesabu siku yaani “countdown”.

  Maneno “mapema iwezekanavyo” yaliyomo ndani ya Katiba, yanatufanya tuseme Jumatatu, Mei 07, 2012, ndiyo siku ya kwanza inayostahili kupelekwa hoja ile bungeni ikaamuliwe kwa kura za siri{Katiba: Ib. 133(4)}.

  Source:
  TANZANIA DAIMA (Jumapili)
  {www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=35396}
   
 2. B

  Bwanamdogo Member

  #2
  Apr 30, 2012
  Joined: Aug 6, 2011
  Messages: 66
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Imetulia
   
 3. m

  maselef JF-Expert Member

  #3
  Apr 30, 2012
  Joined: Oct 31, 2010
  Messages: 255
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Uchambuzi umekaa vizuri sana
   
 4. U

  Uswe JF-Expert Member

  #4
  May 1, 2012
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 2,201
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  mbona inapotoswa maana, sio kwamba hoja inajadiliwa kwa siku 14 la hasha, ila hoja inahitaji kuwa na umri wa siku kumi na nne au zaidi toka ilipowasilishwa kwa speaker ndio iweze kujadiliwa
   
 5. S

  Satanic_Verses Member

  #5
  May 1, 2012
  Joined: Sep 6, 2011
  Messages: 37
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Hakuna mahali ambapo mwandishi amesema hoja inajadiliwa kwa siku 14.

  Labda hapo kwenye red unataka kuanzisha thread yako potofu ukiwa na uhakika kwamba wapo wavivu wa kusoma utakaowapata.

  Ukiona thread kama hii ambayo huwezi kusema kuna mleta mada kwa sababu kaikopi kama ilivyo kwenye makala ya TANZANIA DAIMA, basi ifuate hukohuko kwenye website ya gazeti uisome kama ilivyo.

  Hapo kwenye blue pia unahitaji kutufafanulia. Katiba inasema baada ya siku 14, hoja inapaswa kupelekwa Bungeni kupigiwa kura ya siri.

  Inawezekana itajadiliwa lakini si neno lililotumika kiasi kwamba hata kama mjadala utakuwepo hakuna panaposema kwamba mjadala huo wa wabunge utaweza kuzuia kitendo cha kupigiwa kura ya siri.

  Tujuvye zaidi kama unalo la ziada.
   
Loading...