Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 23,447
- 34,001
Sheikh Ilunga Hassan Kapungu kaingia katika historia ya Dar es Salaam katika kifo chake.
Bahari ya watu waliojazana Msikiti wa Kichangani kuja kuswalia jeneza lake na kisha kulifata nyuma jeneza hilo hadi Makaburi ya Mwinyimkuu, Magomeni Mapipa haijapatapo kuonekana.
Sheikh Ilunga ni ''mgeni'' katika mji wa Dar es Salaam kwa maana ya kuwa hakuzaliwa Dar es Salaam wala hakuwahi kuishi Dar es Salaam wala hakuweza kujinasibu kwa lolote au chochote katika mji wa Dar es Salaam.
Alikuwa akija na kuondoka zamani akirejea kwao Tabora na baadae baada ya kuhamia Mwanza, akija Dar es Salaam na kurejea Mwanza.
Iweje leo mji mzima wa Dar es Salaam usimame na utoke kuja kumzika Sheikh Ilunga Hassan Kapungu?
Hakika hili ni swali linalotaka majibu ya kuridhisha.
Jibu ni dogo na rahisi sana.
Hivi ndivyo Waislam wanavyofanya dunia nzima kila wanapofiwa na kipenzi chao.
Labda linaweza kuja swali jingine, ''kipenzi?''
Sheikh Ilunga kawaje kuwa kipenzi cha Waislam?
Naam Sheikh Ilunga Hassan Kapungu juu ya udogo wake wa umri alikuwa kipenzi cha Waislam na si Waislam wa Dar es Salaam peke yao.
Sheikh Ilunga alikuwa kipenzi cha Waislam wa Tanzania nzima.
Kibla cha kila msikiti wa Waislam katika Tanzania kilikuwa kinamkaribisha kama si kuwaidhi basi angalau asimame awasalimie nduguze Waislam.
Sheikh Ilunga alipendwa na umma hakuwa katika lile kundi la mesheikh wanaoogopa kuswali katika baadhi ya misikiti au hata kupita nje yake.
Sheikh Ilunga hakuwa katika lile kundi la masheikh wenyeji katika futari za serikali na''misikiti ya wakubwa'' lakini wageni katika misikiti ya ndugu zao Waislam maskini, Manzese au Tandale.
Kubwa Sheikh Ilunga hakukosa usingizi wala kujiona duni kwa kukosa kualikwa futari Ikulu au kualikwa katika dhifa za kitaifa akapigwa picha kavaa kanzu za kupendeza na katupia kashda za marembo kakaa na waheshimiwa na kutokea katika runinga na magazeti siku ya pili ukurasa wa mbele.
Sheikh Ilunga Hassan Kapungu hakushughulishwa na hayo.
Yeye alishughulishwa na kuliweka juu jina la Allah Subhana Wataala.
Hili ndilo lililokuwa likimshughulisha mpaka siku Allah alipomuhitimisha.
Kitabu hiki kinaeleza maisha yake mafupi hapa duniani.
Kitabu kinapatikana Ibn Hazm Media Centre Msikiti wa Mtoro, Manyema na Mtambani kwa bei ya Shs: 2,000.00 tu.