Kitabu cha ''wanawake wa nguvu'' kimezinduliwa

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,903
30,243
KITABU CHA ''WANAWAKE WA NGUVU'' KIMEZINDULIWA

''KATIKA kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, wakurugenzi mbalimbali wanawake nchini wameungana na kuzindua Jukwaa la Pamoja la Wakurugenzi Wanawake wa Asasi za Kiraia.

Jukwaa hilo linalenga kuwa na sauti za pamoja katika kusimamia haki za wanawake na jamii kwa ujumla.

Pia wakurugenzi hao wanawake wamezindua kitabu maalumu cha wanawake 15 wenye historia kubwa nchini.

Kati ya wanawake hao 15, wapo waliokuwa wakurugenzi katika taasisi mbalimbali na kuleta mapinduzi ya wanawake katika nyanja mbalimbali za kijinsia...''

Kutoka: habarileo.co.tz
------------------------------------
Hili jukwaa na hawa akina mama, ''Wanawake wa Nguvu,'' wanaijua historia ya wanawake wenzao, watangulizi wao, waliowafagilia njia na kuokota mbigili kwa vidole vyao kuwawezesha wao kufika hapo?

Hili Jukwaa wanaijua histori ya wanawake waliopigania uhuru wa Tanganyika?

Wanawake hawa wa ''nguvu,'' wamepatapo kukaa kitako uani kwenye mkeka na kujiuliza kuwa kabla ya wao je hapakuwa na wanawake wenzao waliofanya makubwa kupita yao?

Naamini hawajapata kukaa kitako wakajiuliza maswali haya kwa kuwa katika historia walizosomeshwa vyuo vikuu na shule walizosoma hawakupata kusoma historia ya kweli ya uhuru wa Tanganyika.

Laiti kama wangelisoma basi wasingejitanguliza wao mbele kutambuliwa na kujiita, ''Wanawake wa Nguvu.''

Hakika walikuwapo wanawake hasa, wanawake wa shoka bahati mbaya hakuna aliyetaka kuwatambua lakini walikuwapo na historia zao sisi waliotuhusu tunazijua vizuri.

Ikiwa wataona kwao inafaa watuulize na In Shaa Allah tutawaeleza historia zao na waliyofanya mama zetu hawa katika kupigania uhuru wa Tanganyika wakiwa wanachama wa TANU ingawa leo hawatambuliwi.

Lakini mama zetu hawa walikuwapo sana na historia zao zinaishi ndani ya nyoyo za wale wanaojua mchango wao.

PICHA: Chini ya picha ya Getrude Mongela ni picha ya Bi. Mwamtoro bint Chuma akipiga kura Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 1970.

Nyumba ya Bi. Mwamtoro ilikuwa imepakana ua na ofisi ya TANU.

Ofisi ya TANU mlango wake ulikuwa unatazama New Street na mlango wa Bi. Mwamtoro nyumba yake mlango wa mbele ulikuwa umeelekea Mtaa wa Kariakoo.

Ilikuwa TANU wakiwa na mkutano wa ndani Bi. Mwamtoro anavunja ua wake wa makuti kuunganisha na ua wa ofisi ya TANU ili pawe na nafasi ya kutosha kwa wanachama wake kwa wanaume.

Hizi ziliuwa siku za mwanzo za TANU.

Wanaume walikuwa wanakaa katika ua wa nyumba ya TANU mpaka watakapoishia na wanawake wanaanzia hapo hadi mwisho wa ua wa Bi. Mwamtoro bint Chuma.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage kafanya mikutano mingi katika nyumba hizo mbili hadi pale TANU ilipokuwa na nguvu ya kuweza kujitegemea yenyewe.

Mkutano ukimalizika wanawake wote wanatokea mlango wa uani wa nyumba ya Bi. Mwamtoro uliokuwa unatazama Mtaa wa Udoe au mlango wa mbele unaotazama Mtaa wa Kariakoo.

Wanaume wao wanatokea mlango wa mbele wa nyumba ya TANU.

BI. Mwamtoro ni mama yake Sheikh Haydar Mwinyimvua mmoja wa wanachama shupavu wa TANU na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama.

Screenshot_20220306-233603_WhatsApp.jpg
 
Back
Top Bottom