Kisa cha Sindbad baharia na safari saba

Kisa cha Sindbad baharia na safari saba

SEHEMU YA SABA

Siku ya pili baada ya kuoga na kuvaa nguo nadhifu, Hindbad Hamali akaenda tena kwa mkarimu wake, baada ya muda wageni wengine waliwasili na maakuli ya mchana yaliandaliwa, walipo maliza kula Sindbad Baharia alianza tena kuwasimulia yaliompata katika safari yake ya pili.
SAFARI YAKE YA PILI
Baada ya kurejea kutoka katika safari yangu ya kwanza, kama nilivyo wasimulia Jana, akaanza Sindbad Baharia, nilirejea Baghdad ambako niliishi maisha ya raha na mustareh nikiwa katika mazingira ya ndugu, jamaa na marafiki zangu.
Lakini baada ya muda nikaingiwa hamu tena ya kusafiri kibiashara na kuuona tena ulimwengu kwa kuitembelea miji na visiwa vya mbali, basi nikaanza tena kununua bidhaa nyingi na baada ya matayarisho, nikasafiri ktoka Baghdad mpaka basrah.
Huko pamoja na wafanya biashara wengine tukapanda merkebu moja mpya iliokua na mabaharia hodari wenye nguvu. Tukang'oa nanga tukaenda bahari kuu.
Kwa msaada wa upepo mzuri tukasafiri kwa muda wa siku kadhaa kutoka kisiwa kimoja hadi kingine na kutoka bahari moja hadi nyengine. Tukiuza na kununua bidhaa mbali mbali,
Siku moja kwa uwezo wa mwenyezi mungu tukafika kwenye kisiwa kimoja kisichokua na watu lakini kilichojaa matunda, na ambako ndege wa kila aina walijaa wakioga kwenye chemchemi ya maji safi yaliotiririka.
Baada ya nahodha kutoa amri tutie nanga, wasafiri pamoja na mabaharia tukashuka tukaelekea pwani kunyoosha miguu yetu na kupumzika tukifurahia mandhar na kuburudishwa na sauti za milio ya wale ndege.
Mimi nikawaacha wenzangu nyuma nikaenda kutembea mpaka nikafika mahali penye majani laini palipokua na chemchemi ya maji yaliyobubujika
****************
Nikakaa kwenye kivuli cha kichaka kimoja kilichokua karibu huku nikila matunda niliyoyachuma njiani. Baada ya kula nikajinyoosha pale majanini kwa ajili ya zile sauti na mbubujiko wa yale maji ya ile chemchemi,
Na kwa ajili ya zile sauti nyororo za wale ndege waliokua wakiimba imba mle vichakani na usingizi nikalala. Siwezi kusema ni mda gani niliolala pale lakini nilipoamka sikuwaona tena wale wasafiri wenzangu.
Ndipo nikatambua ile merkebu imeshaondoka bila mimi na bila wasafiri wenzangu kujua kuwa wameniacha nyuma! Hapo nikakimbilia upande wa bahari, nilipofika pwani niliona kwa mbali merkebu ikitoweka kwenye upeo wa macho yangu.
Huwezi kukisia jinsi nivyoumia, hapo nikajitupa chini mchangani nikalia: "Sindbad huu ndio mwisho wako! Kwani mtungi uangukao chini Mara mbili hauna budi kuvunjika?"
Niliilaani ile siku niliofunga safari ya pili; nikajuta kuacha raha, furaha na starehe za maisha ya kuridhisha niliokua nikiishi kwetu. Nikajuta kufunga safari hii ya pili ilionitia katika hatari baada ya kuokoka chupuchpu katika safari yangu ya kwanza.
Mwisho nikamshukuru mwenyezi mungu nikijua kuwa huu ndio mwisho wangu. Basi nikanyanyuka na baada ya kuzunguka zunguka huku na huko matumaini yoyote, nilipanda mti mrefu nikatazama pande zote nne lakini sikuona chochote isipokua miti, ndege, mchanga ya bahari ilioshikamana na mbingu kwenye upeo wa macho.
Walakin wakati nilipokua nikiangalia kwa makini kile kisiwa kutoka pale mtini kwa mbali nikaona kitu kikubwa cheupe cha mviringo, Mara ile ile nikashuka upesi nikaelekea kule kulikokua na kile kitu.
Nilipokikaribia, kwa mastaajabu makubwa niliona ni kitu kama kuba kubwa lisilokua na kiingilio. Isitioshe kuba hili lilikua laini la kuteleza ambalo lisingewezekana kwa urahisi kulipanda
Baada ya kuweka alama mchangani nililizunguka; nikagundua kua kulizunguka ilikua ni zaid ya hatua hamsini duara.

ITAENDELEA
 
SEHEMU 8

Wakati nilipokua nikistaajabia mara jua lilitoweka likafunikwa na wingu nene ulimwengu mzima ukaanza kua Giza totoro, hapo nikanyanyua macho juu; nikastaajabu na kuona dege kubwa ajabu ambalo wakati lilipokua angani lililiziba jua kwa mbawa zake kubwa.

Hapo nikakumbuka hadithi nilizozisikia ujanani mwangu kwa mabujaji na wasafiri kuwa, kwenye kisiwa kimoja mbali sana kunaishi dege kubwa sana liitwalo Rok lilishalo vifaranga vyake tembo. Hapo nikatambua kua bila shaka lile kuba jeupe ni yai lake!

Mara lile dege lilishuka likakalia kwa hadhari lile yai lake likilifunika kwa mbawa zake likalala, mara ile ile nikatoka pale nilipo jificha nikafumua kilemba changu kichwani nikakikunja mara dufu, nikajifunganacho vizuri kwenye guy la lile dege.

"Labda hili dege litanibeba mpaka kuliko binadamu, kokote litakako nifikisha bila shaka kutakua ni bora kuliko kisiwa hiki kisichokua na mtu."

Basi usiku kucha nikawa sikufumba macho niliogopa kua nikilala lile dege litaruka nami wakati nimo usingizini! Kulipo pambazuka lile dege lilinyanyuka likanyoosha mbawa zake kubwa, likaruka nami angani bila kuhisi kuwa kuna kitu limebeba huku mimi nikilishikilia vizuri.

Baada ya muda lile dege lilishuka kwa kasi ya ajabu mpaka likatua kwenye kilima, kabla halijaniona nilijifungua upesi mguuni pake huku huku nikitetemeka, mama ileile lile dege lilielekea kwenye kitu cheusi kilichokua karibu nilichofikiri ni gogo.

Lililishika kwa makucha yake makubwa likaruka nalo ndipo nilitambua kuwa lile sio gogo bali joka kubwa ajabu! Like dege lilitoweka angani na windo lake, baada ya kutazama huku na huko nikagundua kuwa nipo kwenye bonde la ufa lisilopandika juu.

Kwa kila upande ilikua ni vigumu kuona kilele cha lile bonde kwa jinsi lilivyonyooka wima. Kuona vile nikaingiwa na khofu kubwa nikajuta kujifunga kwenye guu la lile dege, "ningejua litanileta hapa ningebaki kule kule kisiwani kulikokua na matunda na maji safi"

Kwani pale nilipoletwa na lile dege palikua pakame kabisa pasipokua na dalili yoyote ya uhai, nikatambua kuwa nimeokoka kutoka katika hatari moja na kuingia katika hatari nyengine kubwa zaidi.

Nilipoteremka kutoka pale lile dege lilipotua na nilipofika bondeni, nilistaajabu kuona ardhi nzima imejaa almasi safi ya aina ya pekee iliolifanya bonde zima kumeremeta kwa Nuru ya kupofoa macho.

Nikaona kuwa kila sehemu ya lile bonde palika pana joka kubwa ajabu lililojikunja lenye unene na urefu wa shina la mtende ambalo lingeweza kummeza hata tembo mzima. Majoka haya mchana yalijificha mapangoni kusipokua na mwangaza kuepukana na madege yale yaliyo wawinda, kwa hiyo yalitoka usiku tu kuwinda.

Kwa ajili ya uchovu mwingi, njaa na woga wa yale majoka nikaanza kutembea mchana kutwa pale bondeni nikitafuta pahali pa kujistiri na kuupitisha usiku, jioni niliona kiingilio kimoja chembamba cha pango moja ambako niliingia kwa kujibanza banza.

Itaendelea....
 
SEHEMU 9
Nilipoingia ndani nilikiziba kile kiingilio kwa jiwe kubwa nikifikiri labda humo nitasalimika usiku ule na kwamba, kukicha mwenyezimungu anajua yatakayo tokea.
Lakini kabla sijachukua hatua chache baada ya kuingia mle pangoni nikaona, mbali na pale nilipokua kwenye ukingo wa pili wa lile pango joka kubwa limejikunja linatamia mayai yake! Kuona vile nywele zikanisimama wima, na kwa woga mkubwa niliokua nao nikashindwa kujongea popote,
Kwa kukosa njia nyengine yoyote ya kujisalimisha, walakin nilimwamini mungu kwani mwamini mungu si mtovu, nikabaki pale pale nilipokua; nikiwa macho usiku kucha, kulipokucha nililisukuma lile jiwe nikatoka mle pangoni nikipepesuka kama mlevi kwa uchovu na usingizi.
Wakati nilipokua nikipepesuka vile pale bondeni mara niliona mzoga mkubwa wa mnyama mbichi limeporomoka kutoka juu, nilipolikagua niligundua kuwa alikua ni kondoo mkubwa aliyechunwa ngozi, nilizidi kushangaa kwa kioja kile kwani hapakuwa na binadamu yeyote pale.
Ndipo nikakumbuka hadithi niliyoisikia zamani kutoka kwa wasafiri waliofika kwenye mlima almasi na jinsi watu wanavyojipatia almasi kutoka katika bonde hilo lisilofikika kwa kutupa mizoga ya kondoo kutoka juu ili almasi zinate kwenye mizoga hiyo inapoiangukia.
Ifikapo mchana madege makubwa kama vile Rok au tai wakubwa hushuka kwa kasi na kuinyakua mizoga na kuruka nayo mlimani kwenye viota vyao. Hapo ndipo wafanyabiashara walioitupa ile mizoga hutokea na kuyapigia makeleke, na madege huiacha mizoga hiyo na kuruka.
Hapo wafanya biashara huikagua na kugoboa almasi zilizo nata na kuyaachia madege mizoga yao. Nilipokumbuka hadhithi hiyo fikira zilinijia. Lakini kwanza nilikusanya almasi nyingi nzuri, safi tena zathamani.
Nikazitia kibindoni nyingine nikazijaza mifukoni na kila palipokua na nafasi ya kuzihifadhi, halafu nikachukua kilemba changu nikakijaza almasi pia halafu nikakikunja vizuri, nikajilaza chini yamzoga mmoja mkubwa, muda si mrefu mara nikanyakuliwa kwa makucha makubwa ya ndege yalioushika imara ule mzoga.
Lile dege lilipaa nami juu kwa juu mpaka baada ya muda likatua juu ya kilele cha mlima. Lilipotua tu lilianza kuurarua ule mzoga. Mara palisikika sauti za makelele ya watu kutoka nyuma ya jabali lililokua karibu.
Lile dege lilishtuka likaruka likauacha ule mzoga, hapo bila kuchelewa nilijifungua nikasimama nikiwa nimejaa damu. Mara akatokea mwanamume mmoja akakimbilia pale palipokua na ule mzoga.
Lakini aliponiona alisimama ghfla bila kutamka neno lolote aliinama. Akaanza kuukagua ule mzoga huku mara kwa mara akinitupia macho kwa was wasi.
Alipoona hakuna almasi yoyote akanyoosha mikono juu akapiga kelele: "O mwenyez mungu wangu menye uwezo na rehema tuepushe na balaa la masheitwaan na majinni yaliyotapakaa note!"
Kabla sijamweleza jinsi nilivyofika pake, yule bwana huku akitetemeka kwa khofu akanigeukia akaniuliza: "wewe ni nani na imekuaje uko hapa?"
Itaendelea...
 
KISA CHA SINDBAD BAHARIA

SEHEMU 10

"Bwana wangu" nikamjibu "usiwe na khofu mimi si sheitwaan wala si jinni, wala si pepo mbaya, bali ni mwanadamu kama wewe tena mfanyabiashara, kisa changu kilichonifanya nifike hapa ni cha ajabu kishindacho kisa chengine chochote kilichowahi kumpata mtu, kwanza tafadhali hebu pokea almasi hizi ambazo mimi mwenyewe nimezikusanya kutoka katika lile bonde la kutisha.

Hapo nikachagua almasi chache nzuri kutoka mfukoni mwangu nikamkabidhi yule mtu, nikisema: "almasi hizi zitakuletea utajiri wowote unaoutaka."

Yule bwana alipozipokea na alipoona uzuri wake alifurahi sana; akanishukuru na kuniombea dua njema.

Wakati tulipokua tukiongea vile wakatokea wafanya biashara wengine kutoka pande nyengine za ule mlima. Wakatuzunguka wakisikiliza kwa mastaajabu makubwa yale yalionipata. Wakanipongeza wakisema, "hakika kuokoka kwako ni kwa ajabu sana, kwani hakuna mtu yeyote aliewahi kukanyaga bonde lile akarejea hai, mwenyezi mungu ashukuriwe kwa kuokoka"

Basi wale wafanya biashara wakanichukua mpaka kwenye kambi yao wakanipa chakula na kinywaji, halafu nikalala kama mfu, mapema asubuhi ya pili tukang'oa kambi na baada ya kusafiri kwa muda mrefu kupitia milima mirefu, tukafika kwenye ukingo wa bahari, huko tukapanda merkebu tukasafiri mpaka tukafika kwenye kisiwa kimoja kilichojaa miti yenye mashina manene.

Watu mia wangeweza kukaa kwenye kivuli cha mti mmoja, ni kutoka katika mashina ya miti hii ndiko kafuri inayotoa harufu nzuri baada ya watu kichimba mashina ya miti hiyo. Utomvu utokao huangukia kwenye vyombo maalum vilivyotegwa chini yake. Utomvu huo unapoganda hua kafuri.

Kwenye kisiwa hicho niliona pia wanyama wakubwa waitwao karkadan waliofanana na vifaru, wanyama hawa wamefanana na ng'ombe au nyati lakini warefu kuliko hata twiga, karkadan wanapembe katikati ya paji la uso na huwashambulia tembo kwa pembe yao hio na kuwakita nayo na kuwabeba kila waendako mpaka tembo hufa.

Baada ya muda mafuta ya tembo humyenyukia machoni na kumpofoa nakumuuwa yule karkadan. Hapo madege Rok kushuka kwa kasi na kuwabeba wote wawili tembo na karkadan mpaka kwenye vilele vya mlima kwenye viota vyao.

Basi hapo kisiwani nikawauzia wafanya biashara sehemu ya almasi zangu na nyengine nilibadilishana nao kwa bidhaa nyengine nyingi. Baada ya muda tulitweka matanga tukaendelea kufanya biashara kutoka bandari hadi bandari, na kutoka kisiwa kimoja hadi kingine mpaka tukawasili basrah, baada ya kupumzika basrah kwa muda wa siku chache nilielekea Baghdad jiji la amani, huku nimejaa kila namna ya vitu vya tunu na almasi nyungi.

Bila kukawia nilielekea nyumbani kwangu nilipokelewa mikono miwili na ndugu, jamaa na marafiki zangu na majirani. Wote nikawapa zawadi halafu nikatoa sadaka kwa maskini, yatima na wajane.

Baada ya muda nilisahau kabisa yale masaibu yote yalionipata katika safari yangu ya pili, nikaishi kwa raha, furaha na starehe zisizo na kifani nikawa nawaalika ndugu na marafiki kuja kwangu kila siku kushiriki maakuli mbali Mali.

Ikiwa navaa lebasi ghali za thamani mpaka sifa zangu zikaenea kote. Watu wakawa waja kusikiliza visa vya safari zangu zilizonifikisha nchi za mbali. Wote wakawa wanastaajabu kwa hatari nilizozikabili na kuokoka kwangu.

"Na hiyo waungwana ndio ilikua safari yangu ya pili" alimalizia kusimulia Sindbad Baharia. "Kesho in sha Allah nitawasimulia yaliyonipata safari yangu ya tatu."

Itaendelea...
 
Back
Top Bottom