JE, mtu akipanda mpunga atarajie kuvuna mbaazi badala yake? Je, mtu akipanda viazi atarajie kuvuna mahindi?
Si kweli kwamba kile mtu apandacho ndicho avunacho? Sasa iweje leo tushangae yanayotokea Tanzania na Zimbabwe? Iweje tupigwe tahamaki tulipoyaona yaliyotokea Kenya, Rwanda, Burundi, na wiki chache zilizopita Afrika Kusini na sehemu nyingine za Afrika kana kwamba hatujui tulichopanda ni nini?
Si jambo la wazi kuwa walichopanda Ujerumani ndicho walichovuna chini ya Adolf Hitler, na kile kilichopandwa Serbia ndicho kilichovunwa chini ya Slobodan Milosevic?
Mojawapo ya kanuni za chanzo na matokeo inasema kwamba kila matokeo yana chanzo chake. Kwamba hakuna kitu kinachotokea ambacho hakina chanzo. Hivyo, mara nyingi tunapoona jambo limetokea badala ya kujikuta tunashangaa imekuwaje tunapaswa kujiuliza kwanza kimetokana na nini. Ni katika kujua chanzo cha kitu ndipo hapo basi tunaweza kuanza kutafuta suluhisho lake.
Ni wazi kuna wakati ambao tunatakiwa kushughulikia tatizo kwanza ndipo tuweze kujua chanzo chake ni nini ili kuhakikisha tatizo hilo halirudii tena. Tunapoona bomba linavuja kitu cha kwanza tunachojaribu kufanya ni kuziba ufa au upenyo huo ili tuweze kufanya upembuzi wa kujua ni hatua gani inafaa kuchukuliwa ili kuhakikisha tunakomesha kabisa kuvuja kwa maji.
Endapo tunagundua kuwa tatizo ni sehemu ya bomba iliyochakaa basi suluhisho ni kuleta bomba jipya.
Ni kutokana na mawazo haya leo najikuta nalazimika kuzungumzia hali ya uongozi katika Afrika na kujenga hoja ya kwamba uongozi tulionao katika Tanzania na sehemu nyingi za Afrika (wengine nitawaacha wazungumzie mabara yao) unatokana na kile ambacho tumekipanda katika uongozi.
Tulipopanda viongozi wabovu, tumevuna uongozi mbovu! Haiwezekani mtu aupate uongozi kwa ufisadi halafu baadaye awe kinyume cha ufisadi! Kile tulichopanda, ndicho tunachovuna.
Leo tunashuhudia uonevu mkubwa kabisa katika Afrika ambao umeendelea kumdhalilisha mtu mmoja chini ya mkono wa mtu mwingine. Yaliyotokea Zimbabwe siku chache zilizopita, yanaendelea kuthibitisha jambo moja muhimu kuwa Waafrika bado hatujafikia mahali pa kuhakikisha kile tunachopanda ndicho tunachovuna.
Kwa muda mrefu Robert Mugabe amekuwa kama mbegu nzuri iliyopandwa Zimbabwe na kwa muda watu waliona mazao mazuri yaliyotoka katika nchi ile na hivyo kutoangalia sana mbegu yenyewe iliyopandwa ni mbegu gani.
Baada ya maamuzi ya Robert Mugabe kunyanganya mashamba ya Wazungu na hatimaye kuingiza siasa kwenye maamuzi ya kiuchumi, Zimbabwe imejikuta ikiwa na mfumuko mkubwa wa bei ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia iliyoandikwa ya mataifa.
Kuvurugika kwa hali ya kisiasa Zimbabwe ambako kumeshuhudiwa na dunia nzima ndani ya miaka hii michache iliyopita hakukutiliwa maanani na jamii ya Kiafrika.
Viongozi walikaa pembeni na kuwaacha Wazungu walipigie kelele wakati tunaona Zimbabwe ikitokomea taratibu kwenye shimo la giza.
Tumeshuhudia wananchi wa Zimbabwe kwa maelfu yao wakiikimbia nchi yao. Tumeshuhudia raia wa Zimbabwe wenye asili ya Ulaya wakinyanganya mashamba yao kwa kisingizio cha sera mpya ya kugawanya tena ardhi. Tumeshuhudia katika nchi ya Zimbabwe raia wa kweli wa Zimbabwe ni yule mwenye rangi nyeusi.
Ukimya wetu umethibitisha jambo moja kuwa tulikuwa tunakubaliana na sera hizo za kibaguzi za Zimbabwe chini ya Robert Mugabe. Mara kadhaa tumepata nafasi ya kuchukua msimamo lakini kama watu waliolishwa limbwata viongozi wetu wamekuwa waoga kusema ukweli.
MUGABE akisikiliza kwa makini kwenye kikao cha AU Misri.
Hata juzi wakati Rais Jakaya Kikwete anafungua mkutano wa AU Misri yeye kama wengine alishindwa hata kutaja jina la Mugabe! Huu woga si wa Watanzania. Huu woga wa viongozi wetu kuchukua msimamo katika medani ya kimataifa umeanza lini?
Yawezekana Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na mapungufu yake lakini kwenye suala la msimamo hakuwa na utata. Wengi tulijua jinsi gani Mwalimu alipinga ubaguzi wa rangi au uonevu wa mtu mmoja dhidi ya mwingine.
Ni msimamo ambao Mwalimu alikuwa nao maisha yake yote. Mwalimu aliupinga ubaguzi pasipo utata na hakuwahi kuhalalisha aina yoyote ya ubaguzi kwa maneno yake au kwa ukimya wake.
Watawala wetu wamesahau.
Agosti 1972, Jenerali Idi Amin aliwatimua kutoka Uganda raia wa Uingereza wenye asili ya Asia (Wahindi) na akafuatia na amri ya kuwatimua raia wa Uganda wenye asili ya Asia pia. Na hata alipojaribu kubadilisha sera kidogo wale waliobakia walijikuta wakiishi katika mazingira ya kubaguliwa kwani si raia kamili.
Agosti 21 mwaka huo huo, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere akiwa kwenye shughuli Chuo cha Ualimu Changombe, aliamua kuzungumzia suala hilo lakini kwa mapana yake na kuonyesha ni kwanini Waafrika hawatakiwi kubaguana na kutendeana vibaya kwa misingi ya rangi, au nasaba zao.
Mwalimu akasema kitu kimoja ambacho ni muhimu kukifikiria kwa sekunde; Afrika lazima ikatae kudhalilishwa, kunyonywa, na kusukumwa sukumwa. Na kwa nguvu hiyo hiyo ni lazima tukatae kuwadhalilisha, kuwanyonya na kuwasukuma sukuma wengine. Siyo kwa maneno tu bali pia kwa vitendo.
Hili viongozi wetu wamelisahau. Viongozi wetu walikaa kimya wakati Mugabe anawadhalilisha, kuwanyonya, na kuwasukuma sukuma wananchi wake. Tulimwacha afanye hivyo kwa sababu tukiamini kuwa ni shujaa wa Afrika.
Mugabe akapata kichwa na kitendo cha kumkaribisha kwenye mkutano huu wa Umoja wa Afrika ni kilele cha woga wa viongozi wa bara letu. Hivi ni kweli hakuna kiongozi katika bara letu ambaye angeweza kumwambia Mugabe kwa jina lake kuwa anachokifanya na alichokifanya Zimbabwe ni uovu na ubaguzi mkubwa?
Nyerere katika maelezo yake hayo aliongezea na kuonyesha uzito wa viongozi wenye kusukuma sukuma raia wake. Alisema Fikiria kuwa na sisi Tanzania tunaamua kuwafukuza baadhi ya raia wetu, tufanyeje?
Tuwaswage hadi mpaka na Kenya halafu Kenya wanasema hapana siyo raia wetu, na tunawapeleka Uganda, Malawi, Zambia, Burundi na Rwanda na kote wanasema hivyo hivyo. Tufanyeje sasa? Tuwaue?
Hivyo ndivyo alivyofanya Hitler miaka ile ya 1930 na 1940. Akawaweka kwenye matanuri ya moto na kuwaua Wayahudi milioni sita! Hawa walikuwa watu si sokwe.
Rais Thabo Mbeki mwoga, Rais Hosni Mubaraka mwoga, Mwai Kibaki mwoga, Kikwete mwoga! Wote waoga kwani wameshindwa kusimama mbele ya ukweli na kutetea haki ya wananchi.
Si kwenye suala la Zimbabwe tu, si tumeshuhudia maelfu ya wananchi wa Sudan wakiuawa chini ya mkono wa Janjaweed? Nani kati ya hawa viongozi wetu ameikemea serikali ya Sudan? Si wote wanaendelea kukaribishana kwenye vikao vyao vya utukufu?
Wamembeba na wamemlea Mugabe na sasa analiaibisha bara zima na tunu yetu kama Waafrika. Tumeendelea kuwa kichekesho cha dunia.
Inawezekana vipi kukaa meza moja na mtu ambaye ameiba uchaguzi mbele ya macho yenu halafu mkamkumbatia?
Viongozi wasiokuwa na msimamo wa jambo jema wa nini katika bara letu?
Mwaka 1961 wakati bado tukiwa chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa ulifanyika mkutano wa Jumuiya ya Madola. Katika mkutano huo mada ambayo ilikuwa inawagawa viongozi wa nchi hizo ilikuwa ni kama kuikubalia Afrika Kusini kuingia tena kwenye Jumuiya hiyo.
Mwalimu Nyerere akiendeleza kanuni yake ya kutobembeleza ufisadi wa ubaguzi wa rangi aliandika makala kwenye gazeti la London la The Observer la Machi 7.
Katika makala yake hiyo Mwalimu kwa umahiri wa lugha alionyesha ni kwanini Afrika ya Kusini iliyokuwa na sera ya ubaguzi wa rangi isingeweza kuwa mmoja wa wanachama wa Jumuiya hiyo.
Mwalimu aliandika na kusema kuwa kanuni za haki za binadamu na usawa wa wanadamu wote unalilazimisha Taifa letu kuchukua msimamo dhidi ya mwanachama ambaye ni wa zamani zaidi, mwenye fedha zaidi na ambaye ana watu wengi wenye asili ya Ulaya.
Alisema ni msimamo ambao unatokana na kanuni kuwa binadamu wote ni sawa na haiwezekani kukaa meza moja na Kaburu. Ndipo aliposema maneno yale maarufu kuwa kupiga kura ya kuiingiza Afrika Kusini, itakuwa ni kutupigia sisi kura ya kutoka. Hoja ya Mwalimu ilishinda na Afrika ya Kusini haikuingizwa.
Leo viongozi wetu wanagwaya mbele ya mtu asiye na nguvu zozote, utajiri au mvuto wowote duniani. Sababu pekee ya kushindwa kumkemea ni rangi yake! Kwamba kwa vile ni Mweusi mwenzetu basi tusimkemee kwani tutawapa furaha Wazungu na maadui zetu! Hiyo ni hoja ya kipuuzi.
Nelson Mandela akisimama katika kizimba ya Kaburu Aprili 20, 1964 (siku tano kabla ya Tanganyika na Zanzibar kuungana) alielezea ni kwanini yuko tayari kufa kutetea msimamo wake kuwa anapinga kuonewa na mtu Mweupe, kama vile anavyopinga kuonewa na mtu Mweusi.
Akasema kwa uthabiti kuwa hili ni wazo ambalo nimeishi kwalo, na ikibidi niko tayari kufa kwalo. Huo ndugu zangu ndio msimamo; msimamo ambao hauko ndani ya Kikwete, Mbeki, Kibaki au kiongozi mwingine wa Afrika. Mashujaa wa kweli hawaonekani tena katika bara letu!
Ni kwa sababu hiyo naamini Tanzania inaweza kurudia katika nafasi yake ya kihistoria, nafasi ya kusimama na kusema ukweli mbele ya wenye nguvu, nafasi ya kutetea haki ya binadamu wote.
Tumekaa kimya muda mrefu ndiyo maana kina Mugabe wameshamiri. Tumemungunya mno maneno ndiyo maana leo hii Mugabe na makuwadi wake wanaujasiri wa kuzamia mkutano wa viongozi tena akiwathubutisha wamnyoshee kidole ili aone ni nani kati yao ni msafi.
Lakini tutarajie tofauti kutoka serikali ya Kikwete kuhusu suala hili? Je, tutarajie kuwa Rais Kikwete anaweza akanyoosha mkono na kumuambia mzee Mugabe kuwa Tanzania inamuondoa Balozi wake na hatutambui ushindi wake hadi pale utakapofanyika uchaguzi huru na wa haki?
Hivi kweli Rais Kikwete anaweza kusimama na kusema ubaguzi dhidi ya mtu Mweusi unaofanywa na mtu mwingine Mweusi haukubaliki.
Kweli Kikwete anaweza kusema ipo haja ya Mugabe kukaa meza moja na wapinzani wake ili waone jinsi wataiendesha serikali wakati miaka miwili na nusu sasa yeye mwenyewe ameshindwa kukaa na wapinzani wa Tanzania na ameshindwa kuwakutanisha Seif na Karume Zanzibar?
Ndugu zangu, tulichopanda ni viongozi hawa tulionao, na hawa ndio tunaowavuna! Na kama rafiki yangu mmoja alivyosema kuwa viongozi wetu ni taswira yetu sisi wenyewe. Viongozi wetu wanatoka kwetu na wao ni kama sisi.
Hivyo tutarajie tofauti kwa hawa walioko madarakani sasa? Binafsi sitarajii lolote tofauti kwani kama rafiki yangu mwingine asemavyo (japo kwa kebehi zenye dalili ya ukweli kuwa Waafrika ndivyo tulivyo! Ama tunasingiziwa?