Katika uga wa taaluma ya sayansi ya Siasa moja ya viashiria vya uchaguzi kuwa huru na haki ni kuwepo kwa Wagombea wenye Sifa na Nguvu sawa au zinazokaribiana.
Kinadharia CHADEMA imekuwa ikijipambanua kama Chama chenye Demokrasia kuanzia jina lake, ni katika muktudha huo ilitarajiwa na Watanzania wengi kuona Chama hicho kinatafsiri kwa vitendo dhana hiyo.
Bahati mbaya CHADEMA kimeshindwa kutumia vizuri fursa ya zoezi la uchaguzi wa Ndani kudhibitisha kwa vitendo nadharia hiyo, kwani ni dhahiri kinachofanywa na CHADEMA sio uchaguzi tena bali maigizo na kiini macho ya uchaguzi na Demokrasia kwa ujumla.
Hebu tazama wagombea waliopitishwa kugombea katika nafasi mbalimbali na matokeo yake.
Nafasi ya Mwenyekiti Taifa, Freeman Mbowe vs Cecil Mwambe, ukiangalia wasifu na wajihi wa wagombea hawa ni Mbigu na Ardhi, katika mazingira haya ni wazi MBOWE aliandallwa Mazingira ya ushindi na ni sahihi kabisa kusema hapakuwa na uchaguzi zaidi ya igizo la uchaguzi lililowasilishwa kwa hadhira ya wanachama na Wananchi.
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti bara, wagombea walikuwa TUNDU LISSU vs SOPHIA MWAKAGENDA ukiondoa utofauti mkubwa wa wasifu wa Wagombea hawa, LISSU alipendekezwa kugombea na MBOWE ambae ndio ‘mmiliki wa Chama’ hapa hauhitaji kusubiri matokeo, hata kama ingetokea SOPHIA akashinda bado kamati ya Uchaguzi iliyochini ya MBOWE isingedhubutu kwenda kinyume na bosi wake (MBOWE)
CHADEMA kuanzia hatua za awali za mchakato wa kuchukua fomu kilihakikisha kinawadhibiti wagombea ambao wangetoa ushindani kwa MBOWE, mathalani SUMAYE aliwekewa Zengwe na hujuma na baadae akajitoa.
Ni wazi kuwa MBOWE na CHADEMA hakikuwa tayari kufanya Uchaguzi wa viongozi wa kitaifa kwa hiari licha ya Muda wa kikatiba kufika na kupitiliza, bali kilifanya ili kutii agizo la Msajili.
Ni wakati muafaka kwa wafuasi, wapenzi , mashabiki, wakereketwa na wanachama wa CHADEMA kuanza vuguvugu la kupigania kuwepo kwa Demokrasia hai Ndani ya Chama ili kupata uhali wa kimaadili ‘moral authority‘ wa kukemea na kuhubiri Demokrasia Nje ya Chama.